Dominika ya VIII ya Kipindi Cha Mwaka C: Huruma na Upendo
Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.
Amani na Salama! Sehemu ya Injili ya Dominika ya VIII ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Lk 6:39-45 ni hitimisho la sura ya 6 ya Injili ya Luka, yaani mafundisho ya Yesu akiwa sehemu ya tambarare, maarufu kama “Mafundisho ya Heri na Ole.” Ni mafundisho yanayotualika nasi kufanana na Mungu mwenyewe kwa kuwa wenye UPENDO na HURUMA kwa wengine. Ni muhtasari wa mafundisho na mwaliko wa Yesu wa kubadili vichwa vyetu kwa maana ya kutofikiri na kuenenda kadiri ya mantiki ya ulimwengu huu bali tuongozwe na ile mantiki ya Kimungu yaani wongofu wa ndani (Metanoia), yaani kupenda na kuwa na wenye huruma kwa watu wote bila masharti. Kupenda hata adui zetu na wale wanaotutakia au kutunenea mabaya dhidi yetu. Ndio kupenda kama Mungu anavyotupenda, kusamehe na kuwahurumia wengine kama vile Mungu anavyotusamehe nasi makosa na madhambi yetu kila tunapoomba msamaha na kufanya toba ya kweli. Injili ya leo inaanza na msemo uliokuwa maarufu sana katika nyakati na hasa mazingira ya Kiyahudi, yaani “kipofu hawezi kumuongoza kipofu." la sivyo wote watatumbukia shimoni. Hata Yesu alipoambiwa na wanafunzi wake kuwa mafarisayo wamekwazika kwa mafundisho yake, basi akawaita mafarisayo kuwa ni vipofu. (Mathayo 15:14). Ila Wayahudi waliamini kuwa wao sio vipofu, na badala yake walikuwa na uwezo wa kuwaongoza vipofu, yaani watu wa mataifa au wapagani wasiomjua Mungu.
Leo Yesu Kristo anatugeukia wanafunzi na wafuasi wake na kututahadharisha na hatari ya upofu. Katika Kanisa la mwanzo Wabatizwa waliitwa au kujulikana watu wa mwanga, kwa kuwa mwanga wa Kristo uliwafunua macho na kuishi katika iliyo kweli. Wabatizwa ni wale walioangaziwa mwanga wa Kristo na hivyo kuwa na uwezo wa kujua lipi lililo jema na kuenenda kadiri ya huo mwanga na hata kuwaongoza wengine ili nao waweze kuenenda katika mwanga na nuru ya kweli. Lakini, Yesu leo anatutahadharisha nasi kuwa macho na hatari ya kuwa vipofu, kukosa mwanga wa Injili yaani Neno lake kama taa ya kutuongoza. Ni Yeye anayepaswa kuongoza maisha yetu kama Nuru na Mwanga wetu wa kweli. Ni kwa njia ya Neno lake nasi tunatembea katika mwanga. Yesu leo anatualika kumruhusu aangaze maisha ya kila mmoja wetu, aingie ndani mwetu ili nasi tuweze kutambua kila aina ya uovu unaojificha ndani mwetu. Hakika bila kumruhusu Kristo aliye kweli mwanga na nuru yetu, hatuwezi kamwe kuona udhaifu na uovu unaokuwa umejificha ndani mwetu. Ni mwaliko wa kumruhuru Yesu Kristo amulike nafsi na maisha yak ila mmoja wetu. Kinyume chake tunabaki gizani na kushindwa kuona kwa nafasi ya kwanza yaliyo maovu, mapungufu yetu wenyewe na hivyo kukimbilia kuona na kutaja na hata kusambaza madhaifu na maovu ya wengine, na hapo kuishia kuwa ni wanafiki kwani kweli haimo ndani mwetu, kwani ndani mwetu hatujaruhusu mwanga wa Kristo kuingia na kutuangaza.
Mwanafunzi hawezi kumzidi mwalimu wake, ni mwalimu anayepaswa kuwa ndio kielelezo cha kila mwanafunzi. Ni kwa mwalimu tunapata majibu ya maswali na miongozo ya jinsi ya kujifunza kama wanafunzi. Leo Yesu anapozungumzia juu ya mwalimu, anarejea katika nafsi yake yeye mwenyewe. Ni Yesu anapaswa kubaki kuwa ndio kiongozi wetu na mwalimu wetu wa kweli katika maisha ya kila mfuasi. Ni mwaliko wa kujifunza kwake ili tuweze kuenenda kama yeye. Hivyo ni yeye anabaki kuwa kielelezo cha kweli kwa kila muumini. Kinyume chake kama hatumuweki Yesu kuwa kielelezo cha kila mmoja wetu basi hapo kuna hatari ya kuwa vipofu na hivyo kutumbukia shimoni. Ni Yesu anatualika kumwangalia daima yeye na kumfuasa yeye katika maisha ya ufuasi. Mara nyingi tunasikia kashfa nyingi tena hata za kusikitisha kama tunavyosikia siku hizi katika vyombo vya habari na mitandao kuwa kuna baadhi ya makasisi na hata maaskofu na makardinali waliokutwa na tuhuma za kudhulumu watoto wa kike na kiume kingono. Nikiri ni aibu na fedheha kubwa kwa Kanisa. Lakini ni vema kuangalia kuwa sisi sote tunaalikwa kumfuasa Yesu Kristo aliye mwenye upendo na huruma, ni yeye anabaki kuwa kielelezo cha kila muumini. Kielelezo sio askofu au kasisi au mtawa bali ni Yesu Kristo mwenyewe. Ni kwa kujifunza kwake tu hapo tunakuwa na hakika ya kutembea katika mwanga, Ni Yeye aliye zaidi ya mwalimu kwetu, kwani pia ni njia, ukweli na uzima. Hatuna budi sote kumwangalia yeye aliye mwanga wetu na kufanya toba maana sote tumepungukiwa na neema na rehema katika maisha yetu.
Yesu pia leo anatutaadharisha na hatari na kishawishi cha kuhukumu wengine kwa kuona maovu na ubaya wao kwa nafasi ya kwanza, na badala yake kuanza kujiangalia sisi wenyewe. Na ndio mwaliko katika somo la kwanza la Dominika ya leo kujitafakari maisha yetu, kuingia katika maisha yangu lakini MBELE ANABAKI KAMA KIOO NI YESU MWENYEWE. Ni Yesu anapaswa kumulika maisha yangu na kamwe sio kulinganisha maisha yangu na wengine maana hapo kuna hatari ya kuanza kuhukumu wengine. Ni Yesu anapaswa kuwa kioo cha maisha ya kila mmoja wetu. Ni kumweka Yesu mbele tunapofanya tafakari ya maisha yetu. Kabla ya kumsaidia mwingine hatuna budi kutangulia kuruhusu mwanga wa Kristo umulike na kuangaza nafsi na maisha yetu binafsi, na baada ya kurekebisha maisha yetu, tunaweza kutoka kwa upendo na kuwasaidia wengine. Kwa kuwa hatuna mwanga wa Kristo ndani mwetu, hatuna Kristo katika maisha yetu, tunashindwa kuwasaidia wengine na badala yake tunaishia kuwashuku na kuwahukumu na hata kuwaharibia jina lao katika jumuiya na jamii zetu. Mwingine anapokosa kuonja upendo na nia njema ndani mwetu katika kumsahihisha na kumrekebisha basi tunabaki kuwa wanafiki, kwani hatuna ukweli na upendo ndani mwetu, kwani hatuna Kristo pamoja nasi. Kanisa la Kisinodi leo linatualika kila mara kuishi sio tena kwa akili na mantiki yetu ya kibinadamu bali ile ya Mungu mwenyewe, ndio kuwa wasikilizaji wa Neno la Mungu kwa msaada na mwanga wa Mungu Roho Mtakatifu. Ni kwa msaada wa neema za Mungu hakika tunaweza kuishi imani yetu bila unafiki wowote. Ni kwa kuongozwa na Mungu mwenyewe hapo tunakuwa na hakika ya kutembea katika njia ya kweli na haki, yaani Yesu Kristo mwenyewe.
Yesu anatumia pia lugha ya picha ya kibanzi na boriti. Ni lugha iliyotumika na kueleweka vema katika mazingira yake. Kila mmoja wetu tusiporuhusu kuongozwa na Yesu mwenyewe katika maisha yetu hapo kwa hakika tunabaki vipofu na wenye boriti katika macho yetu. Mwanafalsafa wa Kirumi aliyeitwa Seneca aliwahi kusema kuwa mbele yetu daima kuna maovu ya wengine na yetu yapo nyuma yamejificha. Na ndio Yesu anatualika leo kuanza kuangalia maisha na hasa maovu yetu kwa kumweka Yeye mwenyewe kama kioo na taa ya kuangaza ili kuondoa kila giza linalokuwa ndani mwetu. Kinyume chake ni kuwa wanafiki. Mnafiki kwa Lugha ya Kigiriki ni υποκριτα (hipokrita), likiwa na maana ya muigizaji anayevaa uhusika kinyume na uhalisia wa maisha, ni muigizaji stejini kwa mazingira yetu ya leo na hata nyakati zile. Tunaalikwa leo kuepuka kuwa waigizaji katika maisha bali kuwa watu tunaoongozwa na kweli yaani Yesu Mwenyewe na Neno lake ndio Injili au Habari Njema. Mwigizaji alivaa aina ya barakoa usoni na hivyo kushindwa kutambulika kwani alipaswa kujivisha uhusika mwingine, lakini mimi na wewe tunaalikwa kubaki wenyewe mbele ya Mungu kama kweli tunataka kupiga hatua na kukua katika mahusiano yetu na Mungu na wengine. Mkristo hana budi kutokuvaa uhusika na badala yake kuwa mwenyewe, kumruhusu Mungu aangaze na kuongoza maisha yetu.
Kwa kumalizia Yesu anatumia tena lugha ya picha juu ya mti kujulikana kwa matunda yake. Labda hapa ni vema kuepuka kuchukua tafsiri ile ya Injili ya (Matayo 7:15-20), ambapo matunda inatafsiriwa kuwa ni matendo yetu kuwa mema au mabaya. Kwa kweli mwinjili Luka kwa matunda hamaainishi matendo yetu ila badala yake ni neno au ujumbe utokao ndani mwetu inatemegemea sana kama sisi tunajishikamisha na Yesu Kristo mwenyewe. Je mimi na wewe ni habari njema kwa wengine au ni habari mbaya ? Kama somo la kwanza kutoka kitabu cha Hekima ya Yoshua bin Sira, mzee mwenye hekima na busara anapowaandikia kizazi kipya au vijana kuwaalika kwa kusikiliza kwanza yatokayo kinywani kwa mtu. Je maneno yetu yanabariki na kuwaleta wengine karibu na Mungu au ni makwazo na kinyume na upendo na huruma ya kimungu isiyo na mipaka ? Mwenyezi Mungu halaani wala kutuhukumu na hivyo nasi tunaalikwa kuakisi upendo na huruma ile ya Kimungu, ya kuwa watu wa kuwabariki wengine, kuwanenea na kuwatakia mema wengine kwani kinyume chake tunafanya kazi ya yule anayejulikana kama msingiziaji, ndio Ibilisi, anayetutambua sio kwa majina yetu ya Ubatizo bali kwa madhambi na makosa yetu, ndio hukumu. Hakika tuwatambue wengine sio kwa maovu na mabaya bali kwa majina yao, kwani hawa wote ni watoto wa Mungu, wanabeba na kuakisi sur aya Mungu mwenyewe.
Mtakatifu Yohane XXIII, katika maisha yake anaweza kusimama kama mfano wa kuigwa tukipenda kwani daima aliingia ndani ya nafsi yake kwa kuangalia dhamiri na nafsi yake bila kujionea huruma, na ndio kuruhusu mwanga wa Kristo upenye na kuangaza kila kona ya maisha yetu, kuruhusu mwanga huo kuondoa kila aina ya giza inayojificha katika maisha yetu. Mtakatifu huyu alipenda kusema na kututahadharisha tusiwe wepesi wa kuona madhambi na makosa ya wengine, na anatolea mfano kwa kusema kuwa baadhi yetu labda tungatamani hata wakati wa kusali sala ya nakuungamia, « Confiteor », badala ya kupigapiga kifua changu nigeuke na kwa furaha kupigapiga kifua cha jirani yangu na kusema ni yeye aliyekosa sana tena sana. Hivyo, kila mara hatuna budi kuwa watu wa toba ya kweli, kwa kuruhusu mwanga wa Kristo kwa nafasi ya kwanza uangaze giza la mioyo na maisha yetu na kisha tunaweza kutoka kwa upendo na kuwasaidia wengine ili nao waweze kuonja upendo na huruma ya Mungu katika maisha yao. Nawatakia tafakari njema na pia maandalizi mema ya kuanza safari ya kipindi cha toba cha Kwaresima. Dominika njema!