Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya V ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Mwaliko ni kusikiliza na kutenda kwa ushirika na umoja katika maisha na wito! Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya V ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Mwaliko ni kusikiliza na kutenda kwa ushirika na umoja katika maisha na wito! 

Sikilizeni Na Kutenda Kwa Umoja Katika Wito na Utume Wenu: Sinodi

Ni mwaliko wa kumsikiliza Bwana na kutenda kadiri ya Neno lake, kuwa mashuhuda wa Injili. Hivyo ni ujumbe juu ya utume wa kila Mbatizwa, ndio ujumbe kwa kila mmoja wetu tulio wafuasi na rafiki zake Kristo Mfufuka. Moja tunaloliona waziwazi ni mwitikio wa wale wanaotumwa na Mungu kushiriki katika kazi ya kutangaza na kushuhudia: ukuu, huruma na upendo wa Mungu!

Na Padre Gaston George Mkude, Roma.

Amani na Salama! Masomo ya Dominika ya ya tano ya Mwaka C wa Kanisa kwa namna ya pekee yanatupa wazo kuu juu ya watumishi wa Neno la Mungu, wahubiri wa Habari Njema ya Wokovu, utume wao ndio ule mwendelezo wa kazi ya Mungu mwenyewe kuzidi kujifunua na kujimwilisha kwa njia ya Neno lake. Ni mwaliko kwa kila mmoja wetu kumsikiliza Bwana na kutenda kadiri ya Neno lake, kuwa mashuhuda wa Habari Njema ya Wokovu kwa maneno na maisha yetu. Hivyo ni ujumbe juu ya utume wa kila Mbatizwa, ndio ujumbe kwa kila mmoja wetu tulio wafuasi na rafiki zake Kristo Mfufuka. Moja tunaloliona waziwazi ni mwitikio wa wale wanaotumwa na Mungu mwenyewe kushiriki katika kazi hiyo, yaani kuutakatifuza ulimwengu.  Nabii Isaya anajiona hastahili kwani ni mtu mwenye midomo michafu, Mtume Petro anakiri kuwa yeye ni mdhambi, na hata Mtume Paolo pamoja na kutokewa na Kristo Mfufuka, bado anajiona kama mmoja aliyekataliwa na kuzaliwa nje ya wakati wake. Hivyo wito huo sio matunda ya mastahili yetu, bali ni upendo na huruma ya Mungu kwetu. Ni mwaliko unaotokana na kushiriki fumbo lile la mateso, kifo na ufufuko kwa njia ya Ubatizo wetu.

Tunaweza bado kuwa na msululu mrefu wa wajumbe au watumishi wa Mungu wanaojiona kuwa hawastahili kuwa vyombo vya kupeleka Habari Njema ya Wokovu. Nabii Yeremia anasita kwa kuwa yeye ni mdogo, Musa anaona kuwa yeye hawezi kwani sio mwongeaji mzuri ni mtu mwenye kigugumizi na shida ya kuongea. (Yeremia 1:6 na Kutoka 4:10) Kwa hakika tunaweza kusema sifa moja wapo ya wajumbe wa Mungu, ni kujua kwa hakika mipaka na hata udhaifu wetu wa kibinadamu, na ndipo hapo tunaweza kujinyenyekeza na kuomba neema zake zitutegemeze katika kushuhudia upendo na huruma yake kwa wengine. Mjumbe wa kweli wa Habari Njema hana budi kuongozwa na fadhila ile ya unyenyekevu, ndio ile inayotutaka sio katika kutegemea uwezo wetu wenyewe bali daima kwa kushirikiana na neema za Mungu katika kutimiza utume wetu, kumtegemea pia Mungu Roho Mtakatifu aliye mwalimu na mfariji wetu. Yesu amekuja ulimwenguni ili sisi tujaliwe uzima na tujaliwe uzima tele. (Yohane 10:10). Na ndio Mwinjili Luka anajaribu kutuonesha katika somo la Injili Lk 5: 1-11 ni kwa namna gani tunajaliwa uzima wa kweli.

Toba na Wongofu wa ndani ni muhimu katika kutangaza na kushuhudia Injili
Toba na Wongofu wa ndani ni muhimu katika kutangaza na kushuhudia Injili

Mwinjili anatumia simulizi la wito wa wale Mitume watatu wa kwanza kutuonesha jinsi ya kuupata huo uzima wa kweli, uzima tele na ndio uzima wa milele. Nawaalika sasa tujikite zaidi katika sehemu ya Injili ya Dominika ya V ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa kama tufanyavyo kila mara tupatapo nafasi ya kutafakari pamoja. Katika Injili ya leo tunakutana na makundi makuu mawili, kundi la kwanza ni la makutano waliomfuata Yesu Kristo ili kumsikiliza na la pili ndio wale maarufu kama mitume ila leo wanatambulika kama wavuvi, kazi yao waliyofanya hata kabla ya kukutana na Yesu na hata wataendelea nayo hata baada ya fumbo la ufufuko wake Yesu Kristo. Sehemu ya Injili ya leo inatokea kando ya Ziwa Genesareti, linajulikana pia kama ziwa Galilaya. Yesu akizongwa na umati wa watu na anaona pale mitumbwi miwili ya wavuvi na ndipo anaingia katika ule wa Simoni aliyejulikana baadaye kama Petro na kumuomba kuusogeza kutoka nchi kavu ili aweze kuhutubia makutano. 

Ukiangalia vema unaona mara moja ugumu wa kuhutubia watu wengi kutoka katika mtumbwi, hivyo Mwinjili Luka hapa ana ujumbe wa Kitaalimungu nyuma ya taswira hii anayotumia. Muktadha ni siku ya kawaida ya kazi ambapo wavuvi wale palipopambazuka wakawa kando ya ziwa wakisafisha nyavu zao baada ya kukesha usiku kucha katika kujaribu kuvua samaki bila mafanikio. Ni kazi ngumu na yenye maudhi kwani unaweza kuona jinsi ya harufu kali ya shombo ya samaki na kuweza kuziweka tena katika hali nzuri kwa ajili ya uvuvi siku nyingine. Bila shaka wavuvi wale walijawa na uchovu na usingizi wa kukesha usiku kucha wakivua, na hivyo walitamani wamalize kazi ile haraka iwezekanavyo na kurejea majumbani kwao kwa mapumziko. Hivyo mazingira yake inaonesha wazi haikuwa siku ya Sabato wala katika sehemu ya ibada; Bali ni sehemu ya kazi na maisha ya kila siku baina ya wachuuzi na wanunuzi wa samaki, wavuvi na hata watoza ushuru na wengine wengi wanaoweza kupatikana katika mazingira yale.

Hivyo Yesu anahubiri kila mahali sio tu sehemu zile zilizotengwa kwa ibada na kuabudu bali hata sehemu za kazi na masoko na makutano ya watu mbali mbali ili aongoze kila kona ya maisha ya mwanadamu. Ndio kusema Yesu anataka kutembea nasi sio tu tunapokuwa Kanisani na Ibadani bali katika katika kila nyanja ya maisha yetu. Injili haina budi kupenya na kufika hata sehemu zile tunazojipatia kipato, iwe ni maofisini, masokoni, na popote pale. Anaingia na kuketi, kitendo cha kuketi ni kuchukua jukumu la kuwa mwalimu kama ambavyo walifanya Marabi wa nyakati za Yesu. Yeye ni mwalimu wetu wa daima hivyo anatualika kujifunza kutoka kwake na kumsikiliza. Mtumbwi au chombo anacholezea mwinjili Luka ndio Kanisa, yaani jumuiya ya Waamini Wakristo. Ni kutoka katika Kanisa tunaalikwa kusikiliza na kujifunza Neno la Mungu. Ni ndani ya Kanisa au jumuiya ya waamini Yesu Kristo anaingia na kuketi kama mwalimu wetu ili kutufundisha mapenzi ya Mungu katika maisha yetu. Ni katika Kanisa tunaalikwa kusaka mwanga, faraja ya kweli na matumaini katika maisha yetu. Ni kwa njia ya Kanisa Yesu Kristo anadumu kuwa mwanga wa mataifa na watu wote. (Lumen gentium)

Pamoja na Yesu katika mtumbwi, yaani jumuiya ya waamini tunajikuta bado wanadamu wenye madhaifu na mipaka yetu. Ni Yesu pekee aliye kichwa cha mwili fumbo huo ni mtakatifu, ila sisi wengine sote tunauchuchumilia huo utakatifu kwa kumsikiliza yeye na kuenenda kadiri ya Neno lake. Petro anakiri kuwa ni mdhambi, ila pia ni ungamo kwa ajili ya kila mmoja wetu. Ingawa mtumbwi huu una wadhambi lakini Yesu amechagua kutangaza Habari Njema ya Wokovu kutoka katika mtumbwi huo wa wadhambi. Ni kupitia mimi na wewe tulio wadhambi, Mwenyezi Mungu anatutumia ili kupeleka Habari Njema kwa watu wote. Ni kwa njia ya Kanisa lake, Neno la Mungu linatangazwa ulimwenguni kote, ni mimi na wewe tulio wadhambi na wakosefu tunaalikwa daima kuwa mashahidi wa kweli za Injili, mashahidi wa Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya maneno na matendo yetu. Tunatumwa kuipokea kwanza Habari Njema na kisha tutoke tukawe mashuhuda wa kweli za Injili, yaani, Kerygma.

Na ndio tunaona mara moja Yesu Kristo anawaagiza kuingia tena ziwani katika kina kirefu na kurusha nyavu zao ili waweze kuvua. Kwa kadiri ya simulizi la sehemu ya Injili ya leo, kuvua mchana kama anavyowaagiza Yesu tunaona haiendani na mantiki na utaalamu wa kivuvi. Petro pamoja na kuwa mtaalamu na mzoefu wa uvuvi tunaona anaweka pembeni ujuzi na uzoefu wake na anamsikiliza Yesu wa Nazareti. Anatii agizo la Yesu na kuweka kando ujuzi na uzoefu wake.  Hata kama haikuwa saa muafaka kwa kazi hiyo ila anajiaminisha kwa Yesu wa Nazareti. Simon Petro anajivua majivuno ya utaalamu na weledi wake na kujikabidhi kwa Neno la Yesu, na ndio sifa tunayopaswa kuwa nayo kama wafuasi ni unyenyekevu, kukiri udogo na uduni wetu daima. Simoni Petro haogopi kusikiliza na kutenda kadiri ya maagizo ya Yesu, hajali kuwa atageuka kuwa kihoja na kituko kwa wavuvi wengine, ikiwa hawatapata samaki.  Badala yake anaamini kuwa agizo na Neno la Yesu linaweza kutenda miujiza; Na ikumbukwe Simoni Petro tayari alipokea muujiza nyumbani kwake pale mama mkwe wake alipoponywa homa na Yesu wa Nazareti. (Luka 4:38-39)

Matokeo yake ni ya kustaajabisha kwani wanavua samaki wengi kiasi cha kuomba washirika wao wawasaidie na hata kuhatarisha kuzamisha vyombo vyao vya uvuvi. Hivyo kila mara tunapotenda kadiri ya Neno na mapenzi ya Mungu tuwe na hakika ya kuwa na mafanikio mengi. Ni kwa kumsikiliza tu Mungu hapo tunakuwa na hakika ya mavuno mengi. Kila Mbatizwa tunaalikwa kuwa wasikivu na watiifu kutenda sio kadiri ya mapenzi yetu bali kadiri ya mapenzi yake Kristo anayetutuma na kutupeleka. Mwinjili Luka mara moja anatuonesha mwitikio wa Petro baada ya kuona muujiza huu mkubwa, ndio ule wa kujiona kuwa mdhambi na yupo mbali na mawazo na mpango wa Mungu. Na ndio hali yetu ambayo inatukuta kila mara tunapokutana na Mungu, tunafaulu kujiona undani wetu, kuona ni kwa jinsi gani maisha yetu hayaakisi urafiki na utakatifu wa ndani. Ni hapo tunatambua kuwa tuwadhambi na wakosefu kila tunaporuhusu Mungu aguse maisha yetu na hasa kwa njia ya Neno lake na Masakramenti ya Kanisa.

Na ndio taswira ya Kibiblia kila mara tunapokutana na Mungu: Musa alifunika sura yake (Kutoka 3:6), Eliya naye alifunika sura yake kwa joho lake (1 Wafalme 19:13), kama Isaya katika somo la kwanza la leo, vile vile na Simoni Petro anagundua udhaifu na hali yake ya kuwa mdhambi. Hii ni kuonesha jinsi gani nguvu na uwezo wa Mungu vinazidi kila ujuzi, akili, utaalamu, ujanja na kila sifa unayoweza kuwa nayo. Ni sifa muhimu kwa kila muhubiri wa Injili, ya kukiri na kukubali udogo wetu ili nguvu ya Mungu iweze kuonekana. Ni angalisho muhimu kila mara tutambue ni nguvu ya Mungu, ni Yesu Kristo tunayemuhubiri na kamwe tusiingie katika majivuno ya kujihubiri sisi wenyewe. Sio tu kwa nguvu na uwezo wetu bali daima kwa kushirikiana na neema za Mungu tunaweza kutoka na kuwa mashahidi wa kweli za Injili. Ujumbe wa Injili ya leo ni kututaka kutambua utume wetu kuwa ni ulewa kuwa wavuvi wa watu. Samaki wanakuwa salama wanapokuwa majini na si nje ya maji, nje ya maji wanapoteza uhai wao. Samaki kwake majini! Samaki wakitolewa majini wanakufa ila kinyume chake mwanadamu anayeokolewa kutoka majini anabaki hai na salama! Na mwanadamu habaki salama katika kina kirefu cha maji mengi na hasa maji yaliyotibuka na kuwa yenye dhoruba. Hivyo ndio misheni ya Yesu ya kutualika kuvua watu sio kwa kutumia ndowano bali wavu ili watoke wakiwa hai na wazima bila kujeruhika.

Waamini wanaitwa na kutumwa kuwa ni mashuhuda wa Habari Njema ya Wokovu
Waamini wanaitwa na kutumwa kuwa ni mashuhuda wa Habari Njema ya Wokovu

Zaidi tunaona hata Mwinjili Luka anatumia neno la lugha ya Kigiriki (ζωγρων -Zogron) likimaanisha kuwatoa wakiwa bado wazima, ni kuwaleta katika uzima wale waliokuwa katika kina kirefu na kuhatarisha uzima.  (Hesabu 31:15,18 Kumb. 20:16) Uinjilisha ni kumfanya mwanadamu au kila mmoja wetu kuupata uzima wa kweli. Na ndio wajibu wetu wa kitume wa kwenda kuwafanya wengine wajaliwe uzima na wawe nao tele na sio kuwajeruhi kwa namna yeyote ile, bali kuwavua na kuwaleta katika mwanga na maisha ya kweli, ni kwa kuwatoa katika hali hatarishi na ili wajaliwe salama ya kweli. Katika Biblia maji ya bahari ni ishara ya nguvu za yule mwovu zinazopelekea kifo.  Hivyo wanadamu wanaopaswa kuvuliwa ni wale wanaopaswa kuuhishwa, ni wale waliozama katika nguvu za yule mwovu na kupoteza uzima wa Kimungu ndani mwao, Mtakatifu Ambrosi alisema chombo cha uvuvi cha wahubiri Injili ni nyavu zinazomwokoa mwanadamu badala ya kumjeruhi na kumuua, bali zinamwokoa na kumtoa gizani na kumleta kwenye mwanga. Na utume huu si tu umekabidhiwa makasisi bali kila mbatizwa.

Ishara nyingine ni ile ya utume wa pekee wa Simon Petro anayeelekezwa leo kuusogeza mtumbwi na kuufikisha pale anapomwelekeza Yesu mwenyewe, ni yeye anayeamini katika Neno la Bwana kwa nafasi ya kwanza. Zote ni kuonesha nafasi ya pekee aliyonayo Simoni Petro kama kiongozi wa Kanisa na ndio wajibu na utume unaobaki mpaka leo kwa Baba Mtakatifu kama kiongozi wa Kanisa.  Ni yeye kusikiliza Neno na kuongoza mitume wengine kutenda kadiri ya Neno la Kristo na si kadiri ya akili au ujuzi au utaalamu wao bali kadiri ya Neno la Mungu. Na ndio tunaona mamlaka fundishi ya Kanisa. (Magisterium). Kanisa la Kisinodi linatutaka kurudi kutafakari tena nini maana ya kuwa Kanisa au Wanakanisa. Leo tunasikia kuwa ni kwa njia ya kulisikiliza Neno la Yesu kwa msaada wa Mungu Roho Mtakatifu, sisi sote kama Wabatizwa tunaweza kuwa mashahidi wa Injili hata katika nyakati na mazingira yetu. Kila Mbatizwa anatumwa kuwa mvuvi, ndio kuwasaidia wengine wanaokuwa mbali na Yesu, mbali na Injili ili nao waweze kupokea uzima na wawe nao tele. Nawatakia tafakari na Dominika njema.

02 February 2022, 18:06