Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya 6 ya Mwaka C wa Kanisa. Kristo Yesu anatangaza Heri za Mlimani na Ole za Mlimani; Mafundisho Makuu ya Kristo Yesu Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya 6 ya Mwaka C wa Kanisa. Kristo Yesu anatangaza Heri za Mlimani na Ole za Mlimani; Mafundisho Makuu ya Kristo Yesu 

Neno la Mungu Dominika VI: Heri na Laana Katika Maisha

Tunaalikwa tutafakari juu ya njia mbili katika Maisha yetu – “Njia ya baraka au heri” – kujiachia mikononi mwa Mungu na “njia ya Laana” – kuyakumbatia malimwengu na kumuweka Mungu pembeni. Hizi ni njia mbili pingamizi za kuyaangalia maisha ambazo lazima kila mmoja achague kwa hiari yake - kuweka tumaini lake kwa Mungu au kuyakumbatia na kuyafumbata malimwengu.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu dominika ya 6 ya mwaka C wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya dominika hii yanatualika tutafakari juu ya njia mbili katika Maisha yetu – “Njia ya baraka au heri” – kujiachia mikononi mwa Mungu na “njia ya Laana” – kuyakumbatia malimwengu na kumuweka Mungu pembeni. Hizi ni njia mbili pingamizi za kuyaangalia maisha ambazo lazima kila mmoja achague kwa hiari yake - kuweka tumaini lake kwa Mungu au kuyakumbatia na kuyafumbata malimwengu. Lakini tutambue kuwa njia iliyo sahihi ni kutokuyafumbata malimwengu kwa sababu hatutadumu kuishi hapa duniani lazima tutayaacha na kwenda kwenye Maisha yajayo mbinguni. Katika somo la kwanza la Nabii Yeremia (Yer 17:5-8); tunaalikwa kuweka tumaini letu kwa Mungu na sio kwa malimwengu. Kadiri ya Yeremia mtu yeyote anayeweka matumaini yake kwa mwanadamu, anamlaani na mtu yeyote anayeweka matumaini yake kwa Bwana anambariki. Maneno “kumtumainia mwanadamu” ni kuweka matumaini katika malimwengu: nafsi zetu, fedha, mali, watu wenye mamlaka na uwezo. Kuafanya hivyo ni kutokumuhitaji Mungu. Kujiona kuwa unajitosheleza katika yote. Ni kujiona mwenyewe kuwa kamungu na hivyo kujiabudu na kutaka kuabudiwa na wengine.

Wekeni matumaini yenu kwa Mungu na wala msijiamini wenyewe!
Wekeni matumaini yenu kwa Mungu na wala msijiamini wenyewe!

Nabii Yeremiah anawalinganisha watu hawa na kichaka kilichoota jangwani; hakitoi matunda, na wala majani yake hayana kivuli na kwamba miiba yake ni mikali na kuwaumiza wote wanaogusa. Hawa ndio wale ambaye Yesu anawatamkia “Ole” katika Injili. Kinyume chake watu ambao “huweka matumaini yao kwa Bwana” ni wale wanaoelewa madhaifu na mapungufu yao, na wanaelewa kwamba Mwenyezi Mungu ndio kimbilio na nguvu yao wakati wote. Wanaelewa adha ipatikanayo kutokana na kugandamizwa na wenye nguvu na watu waovu, ila pia wana hakika kwamba Mungu anawapenda na kutokana na huruma yake hakika atawaokoa katika taabu yeyote itakayowajia njiani. Watu hawa, kwa Yeremia, ni kama mti uliopandwa kando ya maji, uenezao mizizi yake karibu na mto, jani lake litakuwa daima bichi, hautaacha kuza matunda. Na kwa sababu watu hawa wanaelewa maana ya mateso, wanayapokea kwa moyo mkuu, wanawaonea huruma wale wanaoteseka, na daima wako tayari kuwasaidia. Mbele za Mungu watu hawa wanazaa matunda mengi na yaliyo bora, matunda yaliyotoka katika mizizi ya upendo wa kidugu. Ni watu kama hawa Yesu anawatakia “Heri” katika maisha. Kwamba ijapokuwa sasa wanaonekana kuwa maskini, wanaolia, wanaoteseka, na kadhalika, hawa wana heri kwani tegemeo lao ni Bwana ambaye hatawatupa.

Katika somo la pili la Waraka wake wa kwanza kwa Wakorintho (1Kor 15:12, 16-20); Mtume Paulo anatuambia kuwa; uhakika wa ufufuko na wokovu wetu ni katika Yesu Kristo mfufuka, aliyeshinda dhambi na mauti na hivyo shetani hana tena mamlaka juu yetu kwa kuwa Kristo limbuko lao waliolala amefufuka katika wafu. Katika Injili ya Luka (Lk 6:17, 20-26); Yesu anatangaza heri; wana heri wale wanaoishi maisha ya fadhila; wanaojinyima na kuona njaa, wanaotoka machozi, wanaochukiwa, wanaotengwa na kushutumiwa, kwa ajili ya Mwana wa Adamu, kwa ajili ya imani yao wanapaswa kufurahi na kurukaruka, kwa kuwa thawabu yao ni kubwa mbinguni. Tuzo lao ni kukaa raha msitarehe mbinguni. Lakini, ole wao waliolikinai, waliolishiba wanaolidharau na kulicheka neno la Mungu huku wakiwasifu manabii wa uongo kwa kuwa wataomboleza na kulia. Heri ninyi mlio maskini, kwa sababu ufalme wa Mungu ni wenu. Nini maana ya kibiblia ya kuwa maskini? Katika lugha ya kawaida maskini ni mtu asiyekuwa na pato la kutosha; ni mtu fukara, mtu asiye na mali.

Heri Maskini wa roho maana Ufalme wa Mungu ni wao
Heri Maskini wa roho maana Ufalme wa Mungu ni wao

Katika lugha ya Biblia, Kuwa umaskini maana yake ni kumtegemea mungu. Maskini ni mtu yule ambaye anajiona kuwa kwa nguvu zake mwenyewe hawezi kufanya lolote. Katika mahitaji, katika shida, katika huzuni, katika furaha yeye daima anamwendea Mungu kumshukuru anapofanikiwa na kuomba msaada anaposhindwa, huyu ni mtu maskini. Hivyo umaskini anaousifia Yesu ni ile hali ya mtu kujitambua kuwa yeye ni kiumbe dhaifu na anabaki katika kumtumainia Mungu katika kila kitu; ni mtu ambaye moyo wake haushikamani na malimwengu na wala hafumbatani nayo, ni mtu ambaye moyo wake ameufungua, ameuweka wazi mbele ya mpango wa Mungu wa ukombozi. Ni wazi umaskini wa kutokuwa na mali au chochote kinachomsaidia mtu kuendesha maisha yake, ni kitu kibaya. Umaskini si jambo zuri na si jambo la kujivunia. Ni umaskini ambao lazima tuupige vita. Ndio maana Waisraeli waliona umaskini ni pato la dhambi: ziwe ni dhambi za mtu husika, dhambi za viongozi, au dhambi za jamii nzima. Umaskini wa kutokuwa na fedha au mali sio kigezo cha mmoja kuingia mbinguni. Maana unaweza ukawa maskini na bado ukawa na moyo mgumu katika kuitegemeza jamii yako au kanisa lako hata kwa mawazo mazuri ndiyo maana mtakatifu Teresa wa Kalkuta anasema hakuna maskini asiye na chochote cha kumpa Mungu.

Katika mwendo wa kawaida wa maisha yetu tuna vipimo tulivyojiwekea ambavyo pengine vinatusaidia kupanga mambo, vitu na hata watu. Kwa mfano mtu akiwa na mali nyingi tunamwona kama ni mtu aliyependelewa na Mungu. Au tunapoona tunaandamwa na umaskini na maradhi tunaona kuwa tumelaaniwa na Mungu. Umaskini au utajiri wa vitu mbele ya Mungu si lolote; jambo la msingi ni hili: katika hali yako ya umaskini, au katika hali yako ya utajiri, Mungu ana nafasi gani katika maisha yako. Je, lengo kubwa la maisha yetu tumeliweka katika mali, fedha, starehe, biashara, kazi, siasa au katika vitu vya nyakati zetu simu za kila aina, compyuta, magari, nyumba na mengine mengi kiasi cha kuona ni kwa uwezo wetu tunavyo vyote hivo na kwa hiyo Mungu hana tena nafasi. Vyote hivyo na yote tufanyayo hapa duniani viwe kwetu kama daraja la kutupeleka kwenye ufalme wa Mungu. Kwa walimwengu, Yesu anaposema “heri walio waskini”, wao wanasema ole wao na pale anaposema Yesu ole wao matajiri wao wanasema heri yao matajiri. Tuishi maisha ya kusaidiana huku tukimtumainia Mungu.

Heri ni kujiaminisha kwa Mungu! Ole ni kuyakumbatia malimwengu.
Heri ni kujiaminisha kwa Mungu! Ole ni kuyakumbatia malimwengu.

Maskini anapata mastahili mbele ya Mungu kwa kumtumainia Mungu. Na tajiri naye anapata mastahili mbele ya Mungu kwa kumtumainia Mungu lakini zaidi ya yote ni katika kuwasaidia maskini kwa mali alizojaliwa na Mungu ili kwa hekima na busara awagawie. Sote ni lazima tubaki katika kumtumainia Mungu. Matumaini kwa Mungu yanahusisha uvumilivu. Tunapoona na kushawishika kwamba Mungu hajanipa kile ninachomwomba, pengine tunaona kumtumainia Yeye inakuwa ni vigumu. Tuepuke kufikiri kuwa Mungu ametuacha. Hatuna budi kuvumilia. Matumaini kwa Mungu yanahitaji uimara/ustahimilivu. Tunapopatwa na magumu tusikate tamaa. Mungu anatupatia kile ambacho kinatufaa sisi kwa wakati. Tukiamini katika ahadi zake, tumkabidhi Mungu mipango yetu ya kila siku kwa kuwa ili tupate ulinzi wake hatuna budi kuwa na Mungu katika mambo yote tufanyayo. Basi tuzidi kumtumainia Mungu katika mambo yote. Tujikabidhi katika ulinzi wake ili siku ya kiyama, siku tutakapotakiwa kutolea hesabu ya maisha yetu, Kristo atuambie heri ninyi mliobarikiwa na Baba yangu ingieni katika ufalme wake. Hivyo, tusali kwa imani ili Mungu atujalie neema na nguvu za kumtumainia Yeye katika maisha yetu. Tumsifu Yesu Kristo.

Dominika 6 Mwaka C
09 February 2022, 15:52