Shindeni Chuki Na Uhasama Kwa Msamaha na Upendo wa Kimungu
Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.
Amani na Salama! Baada ya Injili ya Heri, leo Yesu anawageukia wanafunzi wake, na kuanza kuwahubiri juu ya upendo na msamaha bila masharti. Lk 6:27-38. Ni wito na mwaliko wa kushiriki maisha ya Kimungu, yaani upendo usio na mipaka wala masharti, ni upendo hata kwa adui na wanaotutesa na kutudhulumu. Ni mshangao mkubwa maana kwa mantiki ya kibinadamu hilo ni swala gumu na karibu tuseme haliwezekani! Tunaimba katika Zaburi ya wimbo wa katikati kuwa; “Bwana amejaa huruma na neema, akusamehe maovu yako yote, akuponya magonjwa yako yote, aukomboa uhai wako na kaburi, akutia taji ya fadhili na rehema”. Huo ndio wema na upendo wa Kimungu usiobagua mtu yeyote anayeukimbilia na kuutegemea. Haki ya Mungu ni kupenda bila masharti na bila kikomo, na ndio tunaona pia katika somo la kwanza Mfalme Daudi anamsamehe adui yake Mfalme Sauli. Abishayi anamshawishi Mfalme Daudi kutenda kadiri ya mantiki ya ulimwengu huu, yaani kulipa uovu kwa uovu, roho ya kisasi na kuangamiza anayekuwa adui au kinyume chetu. Hii ni mantiki ya kiulimwengu si tu nyakati za Abishayi bali hata nyakati zetu.
Na ndio mantiki ya uovu kuendelea kuzaa uovu, uhasama na chuki kuendelea kuzaa uhasama na chuki, kiasi kwamba hata leo tunasikia matukio mengi yenye kuukuza utamaduni wa kifo na umauti, utamaduni unaokinzana na kusudio la kuumbwa kwetu. Kama taifa leo tunashuhudia jinsi tunavyopitia katika wakati mgumu na wa majaribu kwa kusikia taarifa za watu kujiua, kuuana na kutendeana yaliyo maovu na mabaya. Mwanadamu anageuka kuwa mnyama mkali na wa kutisha kwake yeye mwenyewe na pili kwa mwanadamu mwingine. (Homo homini lupus est!) Mwanadamu anakataa kuishi kwa kuakisi ile sura na mfano wa Mungu ndani mwetu, yaani kukataa kuishi kadiri ya asili yetu, ndio asili ya kumpenda Mungu kwa nafasi ya kwanza na pia jirani. Mwanadamu anakataa kuishi katika ushirika na ujirani na Mungu aliye muumbaji wetu. Ni mwanadamu leo anayeishi sio tena katika urafiki na Mungu na wengine bali kinyume chake. Magomvi, ukatili, mauaji na kila aina ya uovu ni matunda ya kushindwa kuishi kweli za Injili. Ni mwanadamu anapoamua kujitenga na kuwa mbali na Mungu, hapo mwanadamu anaishi zile ole za Injili, yaani anayaangamiza maisha yake yeye mwenyewe.
Ole zile tulizozisikia katika somo la Injili ya Dominika ya VI ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa ni kilio cha huzuni na simanzi kubwa kwani Mungu kamwe hataki kumuona mwanadamu akiyaangamiza maisha yake, ni kilio cha msiba mkubwa kila mara tunapojiweka mbali na maisha ya heri, maisha kadiri ya mpango wa milele wa Mungu. Ni Mungu anayetuhurumia bila kikomo, ni Mungu anayelia ole ili kutukumbusha wajibu wetu wa kumkimbilia na kuishi kadiri ya mapenzi yake kwetu, kwani Yeye daima ni upendo na huruma kwa kila mmoja wetu. Ni matunda na matokeo ya yule mwovu na uovu. Uovu uzaa uovu! Dhambi uzaa kifo. Utamaduni wa kifo na umauti katika jamii zetu ni matunda ya dhambi, uovu na roho ya kisasi inayotawala jamii zetu, iwe katika familia, na hata jamii kwa ujumla. Uovu una hulka ya kutengeneza mnyororo wa uovu, hivyo hatuna budi kuukata mnyororo huo kwa kukubali kupokea kweli za Injili na kuanza kuongozwa nazo katika maisha ya kila mmoja wetu.
Kuutaka mnyororo huu hatuna budi kumruhusu Mungu mwenyewe, ambaye anatupenda daima na anakubali kuwa fidia kwa kujitoa Yeye mwenyewe afe pale juu Msalabani, bila Yeye kushiriki katika mauaji ya aina yeyote ile. Ni pale juu msalabani tunapatanishwa kwa nafasi ya kwanza na Mungu na pili na jirani, yaani na wengine wote. Ni kwa kumwangalia Yesu pale juu msalabani, hapo tunaweza kuchota tena upendo wa Kimungu na roho ile ya msamaha wa kweli. Msalaba ni darasa la Ukristo wetu, ni shule ya kila mfuasi wake Bwana wetu Yesu Kristo, ni msalabani tunajifunza kupenda na kusamehe, tunajifunza nini maana ya kuishi kama Wakristo. Ni msalabani tunang’amua kuwa dawa ya chuki na uovu ni upendo wa kujisadaka! Katika somo la Injili ya leo, tunaona Yesu anatualika kubadili vichwa vyetu (Metanoia), kwa maana ya kubadili mtazamo na mantiki ile ya ulimwengu na badala yake tunaalikwa kupenda na kusamehe kama afanyavyo Baba yetu wa mbinguni; Yeye anayetusamehe na kutupenda bila masharti, Yeye anayenyeshea mvua yake na kuwaangazia jua lake watu wote, wema na waovu.
Ni kwa kukubali kufanya mapinduzi ya kweli ya ndani, yaani kubadili vichwa vyetu, namna zetu za kuenenda isiwe kadiri ya mantiki ya ulimwengu huu bali kadiri ya Neno la Mungu, kadiri ya mapenzi na mpango wa milele wa Mungu, hapo ndipo tunaweza kusema tumefanya metanoia ya kweli. Metanoia ni neno lenye asili ya Kigiriki la muunganiko wa maneno mawili, meta na nous, meta likimaanisha juu ya, na nous likiwa na maana ya akili; Hivyo ni mwaliko wa kufikiri na kutenda juu ya akili zetu, ndio kwa kuongozwa sio tena na silka na hulka zetu za kibinadamu bali za Mungu mwenyewe. Anayefanya mapinduzi haya ya ndani na kweli, ni mmoja anayekubali kutenda yote kadiri ya Mungu na si kinyume chake. Ndiye mmoja anayejawa na hofu ya Mungu, hofu sio itokanayo na uoga bali ile itokanayo na upendo wa kweli kwa Mungu, kwani daima tunayo hakika kuwa sisi ni watu tunaopendwa na Mungu. Yesu anatupa maagizo au amri ya kupenda, kutenda mema, kubariki na kusali. Kadiri ya mantiki ya kibinadamu anayetukosea na kututendea mabaya, hana budi kulipia uovu au ubaya wake, na ndio haki kwa kuwa amefanya kosa basi anastahili kuadhibiwa. Yesu ni kinyume na mantiki hiyo. Yesu anatualika kubadili mtazamo wetu wa kuenenda dhidi ya yule anayetukosea.
Pale ambapo hulka na silka yetu ya kibinadamu inatuongoza kulipa uovu kwa uovu au ubaya kwa ubaya, badala yake mashauri ya Injili yanatualika kusamehe na kupenda hata adui zetu. Kuwa wafuasi wa Kristo ni kukubali kuongozwa sio tena na mantiki yetu bali ile ya Bwana na Mwalimu wetu, ndio ile ya mbinguni. Kugeuza shavu la pili haimaanishi kumruhusu kuendelea kufanya uovu bali ni mwaliko wa kutolipiza kisasi, yaani kulipa uovu kwa uovu. Ni sawa na mwaliko wa yule anayetuibia joho basi hata tunapomkuta bado anataabika kwa baridi, hatuna budi kumfunika na kanzu tulilobaki nalo, ni kupenda bila kujibakisha! Ni mapendo yasiyo na mipaka, ni upendo wa kujisahau sisi wenyewe kwa ajili ya mwingine aliyemuhitaji, ni upendo wa Kimungu. Na ndio tunaona kitenzi kinachotumika sio φιλειν (filein), bali kinatumika kitenzi cha αγαπειν(agapein). Filein ni ule upendo tunaoweza kuwa nao kama wazazi kwa watoto au marafiki, au ndugu na badala yake agapein ni upendo usio na masharti, na ndio upendo wa Kimungu ambao haubagui wala kuweka masharti kuwa nampenda huyu kwa kuwa ni mzazi au ndugu au rafiki yangu, ni upendo hata kwa adui na ndio mwaliko wa Injili ya leo.
Kwa hakika sio rahisi kupenda kama Mungu na ndio maana Yesu anatualika pia kusali na kuwaombea hao adui zetu. Ni kwa kusali nasi tunapata neema za Kimungu kuweza kushiriki upendo wake. Ni kwa njia ya sala nasi akili zetu si tu zinaongozwa na neema zake bali nasi tunaweza kufikiri na kutenda kama yeye. Hivyo kuishi amri na maagizo ya Kimungu hatuna budi daima kukumbuka umuhimu wa kusali. Sala kwa nafasi ya kwanza ni kuomba Mwenyezi Mungu atujalie neema za kung’amua mapenzi yake na pili tuweze kuyapokea na kuyaishi katika maisha yetu. Sala sio kumbadili Mungu au kutaka kutenda yale tunayotaka sisi, kwani mapenzi ya Mungu kwetu daima ni mema, hata kama tunapitia au tutapitia katika magumu na majaribu kiasi gani. Kamwe tusiwe na mashaka wala hofu kwani Mungu anatupenda daima na tena anatupenda bila masharti yeyote yale. Yesu Kristo leo anatupa pia ile kanuni ya dhahabu ya kumtendea mwingine kile ambacho nasi tungependa kutendewa nao au kutowatendea kile ambacho nasi tusingependa kutendewa nao. (Tobia 4:15) Ni kanuni si tunaikuta katika Maandiko Matakatifu iwe kwa Agano la Kale au Jipya bali hata katika dini nyingine na hata katika falsafa za Wapagani. Ni kutukumbusha wajibu wetu kwa jirani na kuwa watu wa kuwatendea wengine ambayo nasi tungetamani kutendewa nao. Huu upendo ambapo kipimo ni mimi, hivyo kama ambavyo kwa hulka na silka ya kibinadamu kila mmoja anategemewa kujipenda na kujitakia mema, basi hatuna budi kuwatendea na kuwatakia mema wengine.
Hapo juu tunaona ni wewe na mimi ndio kipimo cha upendo ila katika Injili ya leo kipimo cha upendo ni Mungu mwenyewe. Na ndio Yesu Kristo leo anatualika nasi kutafakari namna zetu za kupenda au kuwatendea wengine mema, maana mara nyingi tunatenda kadiri ya mantiki ya ulimwengu huu, yaani kuwapenda na kuwatendea mema wale tu wanaokuwa wema kwetu, ila leo tunaalikwa si tu wale wanaotutendea mema bali hata na adui zetu, au kuwakopesha hata wale wasiokuwa na uwezo wa kurejesha. Linatumika neno fadhili gani tunapata mara tatu, katika Maandiko Matakatifu neno la Kigiriki linalotumika ni χαρις(karis), lenye maana ya neema au upendeleo wa Kimungu. Hivyo, kupenda bila masharti, ndio kupenda bila kusubiri malipo kwa upande wetu, ni KUPENDA BURE na ndio KUPENDA BILA MASHARTI kwa maneno marahisi. Ni kupenda kwa namna ile ya Mungu mwenyewe, ndio ya kupenda sio kwa sababu sisi ni wema kwake, bali anatupenda hata pale tunapokuwa mbali naye kwa kujitanguliza sisi wenyewe, au kwa kukengeuka na kuenenda kadiri tutakavyo sisi.
Wapendeni maadui zenu, ni agizo linalowezekana tu ikiwa nasi tutakuwa na upendo usio na masharti, ndio kukubali kuunganika na Mungu mwenyewe, kushiriki maisha ya Kimungu, ndio hapo tunaweza nasi kupenda bure na kinyume chake utakuwa ni upendo kadiri ya mantiki ya ulimwengu huu. Kuwakopesha bila kusubiri kurudishiwa, na ndio upendo unaokuwa wazi kama vile Mwenyezi Mungu anavyotupenda sisi sote iwe tu wema au waovu. Na ndio thawabu ya wale wanaoruhusu kuongozwa na kuenenda kadiri ya upendo huo wa Kimungu ni katika kufanyika wana wa Mungu. Kuwa mwana kama tulivyowahi kuona mara nyingine ni ile hali ya kufanana, kuwa tukipenda kama Mungu anavyopenda basi nasi tunashiriki hali ya Kimungu ndani mwetu, na kwa kufanana naye, ni kuwa wana kweli wa Mungu. Ili tuweze kupenda kama Mungu anavyopenda hatua ya kwanza lazima kumruhusu Mungu mwenyewe, yaani neema yake ifanyekazi ndani yangu, kumruhusu Mungu aongoze akili na utashi wangu, awe taa ya njia zangu zote. Na mwishoni ni mwaliko wa kuwa na huruma kama Baba yetu wa mbinguni alivyo na huruma. Ni kuwa na umoja na Mungu katika namna zetu za kufikiri na kuenenda, Mungu ambaye anajua hata yaliyofichika ndani ya mioyo yetu, ila daima hatuhukumu bali anatualika kuongoka na kuishi maisha ya urafiki naye na jirani zetu.
Tusihukumu wala kulaani maana Mungu mwenyewe hatuhukumu wala kutulaani bali daima anatualika kushiriki maisha yake ya Kimungu, na ndio kuwa na uzima wa kweli na neema. Tunaalikwa kwa msaada wa neema za Mungu kusamehe na kuwapa wingine kwa kipimo kile cha kushindilia na ndio kuwapenda na kuwasamehe wengine bila mipaka wala masharti. Ni kwa kukubali kuongozwa na Roho wa Mungu, nasi tutaweza kweli kuishi mashauri ya Injili ya leo yaani kupenda na kusamehe. Tusali pia kwa ajili ya Taifa letu, Mwenyezi Mungu aguse mioyo ya kila mmoja wetu, ili sote kama Taifa tuweze kuenenda kwa kuisikiliza sauti ya Mungu ndani mwetu, ndio aamshe dhamiri hai na njema ndani ya kila mmoja wetu, ya kutambua na kuenzi thamani ya uhai iwe ya maisha ya mtu binafsi na ya wengine. Mwenyezi atujalie dhamiri hai na njema za kupenda na kusamehe kwa namna ile ile anayotupenda na kutusamehe kila mmoja wetu. Hatuna budi kukiri na kutambua matukio mengi ya kutisha na kufedhehesha ni matokeo ya kuwa mbali na Mungu, ni sisi tumechagua kuishi maisha ya ole, kwa kuyaangamiza maisha yetu, kwa kuenenda sio tena kadiri ya mapenzi na mpango wa milele wa Mungu kwetu, bali kadiri tutakavyo sisi. Tupige magoti kuliombea taifa letu, kusali pia kwa ajili ya dunia nzima ili daima wanadamu tukubali kuongozwa na Mungu aliye Muumbaji wetu. Nawatakia tafakuri na Dominika njema.