Imeandikwa Wapendeni na Kuwaombea Adui Zenu: Msilipize Kisasi!
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya liturujia ya Neno la Mungu dominika ya 7 ya mwaka C wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya dominika hii yanatuhimiza kuishi kwa upendo, kupendana sisi kwa sisi na hata kuwapenda maadui zetu tuwasaidie kwa kuwaombea ili nao wawe watu wema na zaidi sana tuepuka kulipiza kisasi kwa wale waliotukosea. Somo la kwanza la kitabu cha kwanza cha Samweli (1Sam 26:2.7-9.12-13.22-23); linasimulia harakati za mfalme Sauli kumtafuta Daudi ili amuue. Sababu kuu hasa ni wivu wa Mfalme Sauli kwa sifa alizopewa Daudi kwa uhodari wake wa kuliongoza jeshi katika vita dhidi ya wafilisti na kushinda. Sauli alihofia kuwa sifa hizi zingemfanya Daudi kupewa ufalme na kuchukua nafasi yake. Wivu wa Sauli ulizaa chuki ndani yake na hivyo kutaka kumuua Daudi. Naye Daudi alipoambiwa anatafutwa auawe alikimbia machoni pa Sauli. Hivyo Sauli alichukua jeshi lake kwenda kumtafuta Daudi ili amwue. Kwa siku nzima walimtafuta bila mafanikio. Ilipofika usiku Sauli na jeshi lake walilala katika pango. Daudi aliwakuta wamelala fofofo, naye Abishai rafiki yake akamwambia, Mungu amemtia adui yako Sauli mikononi mwako, haya harakisha umuue. Daudi alikataa akisema; “Ni nani awezaye kuunyoosha mkono wake juu ya masihi wa Bwana, naye akawa hana hatia”? Daudi akaweka matumaini yake kwa Mungu akisema; “Naye Bwana atamlipa kila mtu haki yake, na uaminifu wake”. Daudi akamsamehe adui yake aliyemtafuta kumuua, akimuombea mema kwa Mungu kwa sababu ya upendo wake kwake ili ajirudi na kubadilika.
Baba Mtakatifu Yohane Paulo II katika Barua yake ya Huruma ya Mungu anasema; Pale upendo ulipo, huruma ipo; na huruma hii inajidhihirisha katika kujitahidi kurudisha uzuri na thamani ya maisha yaani kutoka hali mbaya aliyonayo mtu na kumrudishia matumaini na furaha katika maisha. Mtume Paulo katika somo la pili la Waraka wake wa kwanza kwa Wakorintho (1Kor 15:45-49); anatoa tofauti iliyopo kati ya mwili tulio nao sasa na ule utakaofufuliwa. Mwili wa sasa ni udongo, yaani dhaifu na mwili utakaofufuliwa na Yesu utakuwa na hali ya utukufu huko mbinguni. Hivyo tujitahidi kupambana na madhaifu kwani hakuna aliye mkamilifu, tukisaidiana sisi kwa sisi kwa upendo wa kidugu ili tuweze kuufikia utakatifu ndio wito wetu sote tunaoitiwa na Mungu Baba yetu aliyemtakatifu. Injili ilivyoandikwa na Luka (Lk 6:27-38); inahusu fundisho la amri kuu ya mapendo - kuwapenda maadui na kuwatendea mema wanaotuchukia, kuwabariki wanaotulaani, kuwaombea wanaotuonea, kumgeuzia shavu la pili anayekupiga moja, anayekunyang’anya joho, usimzuilie na kanzu, kumpa kila anayekuomba, na anayekunyang’anya vitu vyako, usitake akurudishie, kuwatendea watu tunayotaka watutendee na zaidi ya yote tuwe na huruma, kama Mungu Baba yetu. Tusiwahukumu wengine ili nasi tusijehukumiwa, tusilaumu, ili nasi tusilaumiwe, tuachilie ili nasi tuachiliwe. Tuwape watu vitu, nasi tutapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa na kusukwa-sukwa hata kumwagika, tutakachowapimia wengine ndicho tutakachopimiwa na sisi.
Fundisho hili kwa macho ya kibinadamu ni gumu kwani liko kinyume na mtazamo wetu mbele ya maadui zetu. Lakini kwa neema ya Mungu yote yawezekana kama kwa Daudi katika somo la kwanza, tukifungua mioyo yetu na kuacha upendo wa Mungu ufanye kazi ndani yetu kwa njia ya Roho Mtakatifu. Upendo huu si kingine isipokuwa kuiweka nafsi ndani ya nafsi nyingine na kuweza kuhisi anachohisi mwingine; iwe ni uchungu, furaha, au maumivu. Ni kukaa ndani ya mwingne: “Kaeni ndani yangu, nami nikae ndani yenu” (Yn.15:4). Ni kulishika na kuliishi neno la Mungu: “Mtu akinipenda atalishika neno langu, na Baba yangu atampenda nasi tutakuja kwake na kukaa naye” (Yn. 14:23). Kupenda ni kutotafuta faida binafsi bali ya wengine: “pasiwe na mtu anayetafuta faida yake mwenyewe tu bali faida ya mwenzake” (Fil. 2:4). Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto wa XVI katika barua yake ya Mungu ni Upendo “Deus caritas est” anasema; Upendo una hulka au tabia ya kuwafikiria wengine, hautafuti faida yake binafsi, bali faida ya mpendwa. Unapopenda unakuwa na majikatalio na uko tayari hata kujitoa sadaka kwa ajili ya umpendaye.
Huu ndio uzoefu wa wapendanao: kila mmoja anakandamiza matashi yake na kutekeleza ya mwenzake kwanza. Upendo wa aina hii ni zawadi/fadhila kutoka kwa Mungu ambao Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto wa XVI anauita “Moyo wa Mungu aliye asili ya upendo”. Upendo huu haununuliwi bali unajitoa wenyewe. “Mtu akijaribu kununua pendo, akajitolea mali yake yote, atakachopata ni dharau tupu” (Wim. 8:7). Mungu aliye upendo ametufunulia maana halisi ya upendo. Upendo ni kumwambia siri zako umpendaye – Mungu ametuambia katika maandiko matakatifu siri za umungu wake na matumaini makubwa kwa mwanadamu aliyeanguka na huu ndio ufunuo. Upendo ni kuteseka kwa ajili ya umpendaye – Mungu ameteseka kwa ajili yetu hata kufa Msalabani; “Hakuna upendo mkuu zaidi kuliko huu wa mtu atoaye uhai wake kwa ajili ya rafiki zake” (Yn.15:13). Upendo ni kuwa mmoja na umpendaye, sio tu katika umoja wa mwili bali umoja wa roho – Mungu ameweka Ekaristi Takatifu ili akae nasi katika maumbo ya mkate wa uzima. Upendo hutamani kuungana na umpendaye milele – Mungu ametuahidi heri ya milele mbinguni ambapo tutamwona kama alivyo - anasisitiza mtume Paulo - “Nasema ukweli mtupu; nimeungana na Kristo nami sisemi uongo” (Rum. 9:1).
Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto wa XVI katika Waraka wake wa “Caritas in veritate” anasema; “upendo ni msukumo usio wa kawaida, unaopelekea watu kuchagua kwa ushujaa kujishughulisha kwa ukarimu katika nyanja za haki na amani. Upendo wa kweli una nguvu kubwa: anayependa kikamilifu anajishikamanisha na matashi ya mpendwa wake. Mtakatifu Yohane Chrisostom, alisema; “Ni tabia ya mpenzi kutokuchoka kutenda kile kinachompendeza mpendwa wake.” Hakuna chenye kuamrisha zaidi kama upendo kwa kuwa “Pendo lina nguvu kama kifo”. Tena pendo lilivyo na nguvu, “maji mengi hayawezi kamwe kulizima, mafuriko hayawezi kulizamisha” (Wim. 8:6). Lenyewe kwenye shida liko imara, kadhalika kwenye furaha liko imara; kwake shida na raha ni mamoja. Mtume Paulo anauliza; “Nani awezaye kututenga na upendo wa Kristo...Je ni taabu, au dhiki, au mateso, au njaa, au ukosefu wa nguo, au hatari, au kifo?” (Rum. 8:35). “Hakuna kiwezacho kututenga na upendo wa Kristo – anajibu Paulo - wala kifo, wala uhai, wala malaika au nguvu nyingine za mbinguni, wala yanayotokea sasa, wala yatakayotokea baadaye; wala mamlaka; wala ulimwengu wa juu, wala wa chini kabisa. Hakuna kiumbe chochote kiwezacho kututenga na upendo wa Mungu katika Kristo Yesu Bwana wetu” (Rum. 8:38-39).
Mtume Paulo anapowaandikia Wakorintho Waraka wake wa kwanza anataja sifa za upendo; Upendo daima huvumilia, ni mpole, hauna wivu, haujidai, haujivuni, una adabu, tena hautafuti faida yake binafsi, haufurahii maovu, bali ukweli. (1Kor. 4-6). Hii ndiyo picha halisi ya upendo. Ni katika upendo Daudi hakunyanyua mkono wake kumuua Sauli aliyetaka kumuangamia nasi tuuishi upendo ambao kimsingi ni amri, ili tuingie mbinguni lazima tumpende Mungu na jirani hata kama ni adui vinginevyo hatuwezi kuiona mbingu.