Jubilei ya Miaka 50 ya WAWATA Tanzania kilele chake ni Mwezi Septemba 2022 kwenye Uwanja wa Taifa wa Mkapa, Jijini Dar Es Salaam. Jubilei ya Miaka 50 ya WAWATA Tanzania kilele chake ni Mwezi Septemba 2022 kwenye Uwanja wa Taifa wa Mkapa, Jijini Dar Es Salaam. 

WAWATA Tanzania Kuwasha Moto wa Injili Kwa Mkapa Septemba 2022

Katika kipindi hiki kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa WAWATA, hapo Mwezi Septemba 2022 kwa kuwasha moto wa Injili kwenye Uwanja wa Taifa wa Benjamin Mkapa, Jijini Dar es Salaam, wanaongozwa na kauli mbiu “Nuru Yetu Iangaze! Tuyatakatifuze Malimwengu. Miaka 50 ya WAWATA: Upendo, mshikamano na uadilifu wa uumbaji. Yaani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Taswira ya Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA ni kuona kila mwanamke mkatoliki wa Tanzania anaelewa nafasi na wajibu wake wa Kikristo kuanzia ngazi ya Familia, Jumuiya, Kanisa, Jamii na Taifa katika ujumla wake. Pia wanawake wanapata maendeleo fungamani ya kiuchumi ili kukidhi mahitaji msingi ya familia na hivyo kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa na Jamii na kufanya maisha ya hapa duniani kuwa chumvi na nuru katika Ulimwengu kama Mashuhuda wa Yesu Kristo na Kanisa lake. Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA, (The Catholic Women Of Tanzania Association) ni chombo kinachowaunganisha Wanawake Wakatoliki Tanzania kilichoanzishwa kunako mwaka 1972 kwa lengo la kujitakatifuza na kutakatifuza malimwengu. Jumuiya hii inaongozwa na kauli mbiu “tutumikie na kuwajibika”. Madhumuni makuu ya WAWATA ni pamoja na kuwaunganisha wanawake Wakatoliki nchini Tanzania katika juhudi zao zinazowahusu kama Wakristo, wanawake, na raia, wakiwa katika vikundi mbalimbali ambavyo hasa lengo lao ni kudumisha: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi!

Katika kipindi hiki kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA, hapo Mwezi Septemba 2022 kwa kuwasha moto wa Injili kwenye Uwanja wa Taifa wa Benjamin Mkapa, Jijini Dar es Salaam, wanaongozwa na kauli mbiu “Nuru Yetu Iangaze! Tuyatakatifuze Malimwengu. Miaka 50 ya WAWATA: Upendo, mshikamano na uadilifu wa uumbaji. Kauli mbiu hii inachota amana na utajiri wake kutoka katika Maandiko Matakatifu Lk. 1:39: Mapendo kwa jirani. Hivi karibuni wenyeviti wa WAWATA, Majimbo Katoliki Tanzania pamoja na wajumbe wa Kamati ya Jubilei ya Miaka 50 ya WAWATA walihudhuria Mkutano maalum kwa muda wa siku tatu. Huu mkutano ulikuwa ni sehemu ya vikao vya ndani na semina maalum kuhusu maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu inayonogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume” inayokazia pamoja na mambo mengine mambo makuu matatu yaani: Kukutana, Kusikiliza na Kung’amua. Maadhimisho ya Sinodi ni wakati wa Sala, Ibada na kumsikiliza kwa makini Roho Mtakatifu. Ni wakati wa kukutana na kutajirisha kutokana na karama, miito na utume katika ukweli, uwazi, uwepo na ujasiri!

Maandalizi ya Jubilei ya Miaka 50 ya WAWATA
Maandalizi ya Jubilei ya Miaka 50 ya WAWATA

Padre Florence Rutahiwa Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Uchungaji wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) ndiye aliyekuwa mwezeshaji mkuu. Alifafanua kuhusu: dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa; Aina mbalimbali za Sinodi na baadhi ya Majimbo nchini Tanzania ambayo tayari yamekwisha kuadhimisha Sinodi za Majimbo, Umuhimu wa Sinodi pamoja na ushiriki wa Wanawake Wakatoliki katika maadhimisho haya. WAWATA. Amegusia pia Maandalizi ya Maadhimisho ya Mkutano Mkuu wa 20 wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA. Tanzania ndiye mwenyeji wa Mkutano mkuu wa 20 wa AMECEA utakaofikia kilele chake mwezi Julai 2022. Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni mchakato unaowadai waamini kuinjilika ili waweze kuinjilisha kwa kuwa na mtazamo na mwelekeo mpya kuhusu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Maandalizi haya yanakwenda sanjari na sala maalum ya AMECEA, ili mkutano huu uweze kupata kibali cha baraka na amani inayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo.

Uzinduzi wa Jubilei ya Miaka 50 ya WAWATA Tanzania
Uzinduzi wa Jubilei ya Miaka 50 ya WAWATA Tanzania

Mama Evaline Malisa Ntenga Mwenyekiti wa Taifa wa Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania, WAWATA, amewahimiza WAWATA kujikita zaidi katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi kwa kutoa kipaumbele cha kwanza katika umoja, ushiriki na utume wa Kanisa. Wajitahidi kumjua, kumpenda na kumtumikia Mungu, ili kweli waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili kwa watu wa Mungu ndani na nje ya Tanzania. Anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwawezesha kufanikisha walau malengo ya uzinduzi wa Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya WAWATA katika ngazi ya Majimbo, Kanda na sasa wameanza kujielekeza kwenye Parokia na hatimaye, kwenye familia. Lengo ni kujikita katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili, kwa kuimarisha utume wa Wanawake Wakatoliki Tanzania, yaani WAWATA. Yaani sipati picha jinsi nyasi za Uwanja wa Taifa wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam zitakavyokuwa baada ya WAWATA kuwasha moto wa Injili! Yaani hadi raha!

WAWATA Tanzania
19 February 2022, 17:05