Dominika ya III ya Kwaresima Mwaka C: Toba Na Wongofu Wa Ndani
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, katika Dominika ya tatu ya Kipindi cha Kwaresima mwaka C wa Kanisa, siku ya kumi na tisa ya kujitakatifuza kama wimbo wa mwanzo kutoka kitabu cha Nabii Ezekieli unavyoimba; “Nitawanyunyizia maji safi, nanyi mtatakasika na uchafu wenu wote. Nami nitawapa ninyi moyo mpya, asema Bwana” (Ez. 36: 23-26). Ni utakaso wa kiroho tunaoupata kwa kufunga na kusali ndiyo maana katika sala ya Koleta Padre anasali kwa niaba ya Taifa la Mungu akisema; “Ee Mungu, wewe ndiwe asili ya rehema zote na mema yote. Umeonyesha kuwa dawa ya dhambi ni kufunga, kusali na kuwapa maskini. Utusikilize kwa wema sisi tunaokiri unyonge wetu, ili tunaponyenyekea moyoni, utuinue daima kwa huruma yako”. Masomo ya dominika yanatuelekeza kutubu dhambi ili tuokolewe. Toba ya kweli ni kumwelekea Mungu ambaye ndiye mwenye uwezo wa kutuokoa kama anavyotuasa mzaburi (Zab. 25: 15-16); “Macho yangu humwelekea Bwana daima, naye atanitoa miguu yangu katika wavu. Uniangalie na kunifadhili, maana, mimi ni mkiwa na mteswa”. Madhara ya kukaza shingo na kutokutubu ni kuangamia milele.
Katika somo la kwanza la Kitabu cha Kutoka (Kut 3:1-8, 13-15); Mungu anamwita na kumtuma Musa arudi Misri kuwakomboa watu wake Israeli akisema; “Nimeyaona mateso ya watu wangu walioko Misri, nimesikia kilio chao, nami nimeshuka ili niwaokoe, niwapandishe kutoka nchi ile niliyowaahidia baba zao”. Musa anaitwa akichunga kondoo wa mkwewe Yethro, kuhani wa Midiani. Kabla ya kuitwa, Musa alifanya safari kupitia jangwani mpaka mlima Horebu. Safari hii ni ishara ya safari aliyoifanya akikimbia kutoka Misri, safari atakayoifanya kurudi Misri na safari akakayoifanya tena akiwaongoza wana wa Israeli kutoka Misri mpaka mlima wa Bwana. Musa anaitwa akiwa mlimani baada ya kugeuka ili aone maajabu ya kijiti kiwakacho moto lakini hakiteketei. Mlima ni ishara ya uwepo wa Mungu na kijiti kilichowaka moto nacho hakiteketei ni ishara ya upendo na huruma ya Mungu isiyoisha milele. Musa anaomba kujua jina la Mungu. Mungu anamwambia; “Mimi Niko ambaye Niko”, Mungu ni yule yule Jana, Leo na hata milele. Mwaliko wa Mungu kwa Musa “kuvua viatu kwa sababu mahali aliposimama ni nchi takatifu,” ni alama ya toba na kusamehewa dhambi alizotenda akiwa Misri. Musa alipaswa kuacha chuki na hasira aliyokuwa nayo juu ya watu wa Misri.
Ni mwaliko wetu sote wa kuvua kwa nguvu rohoni mwetu yale yote yanavunja urafiki wetu na Mungu. Mungu anatualika tusafishe roho zetu, tutubu kweli, tufanye toba na upatanisho wa kweli. Somo hili linatufundisha kuwa Mungu wetu ni Mungu wa wanaoishi, sio Mungu wa wafu, ni Mungu anayewajali watu wake, hafurahii mateso bali anaona uchungu watu wake wanapoteseka. Mungu anayesikiliza kilio cha watu wake wanapomlilia na kuomba msaada kwani yeye amejaa huruma na neema, haoni hasira upesi, ni mwingi wa rehema na fadhili. Nasi tukimlilia Mungu katika taabu na mahangiko yetu atasikia kilio chetu na kutuokoa. Kama tunavyoimba katika wimbo wa katikati; Bwana amejaa huruma na neema. Akusamehe maovu yako yote, akuponya magonjwa yako yote, aukomboa uhai wako na kaburi, akutia taji ya fadhili na rehema (Zab. 103: 1-4, 6-8, 11).
Katika somo la pili la Waraka wake wa Kwanza kwa wakorinto (1Kor 10:1-6, 10-12); Mtume Paulo anatutahadharisha tusirudi katika dhambi baada ya kukombolewa kwa Damu Azizi ya Yesu na kuondolewa dhambi zetu kwa njia ya sakramenti ya ubatizo na kushibishwa kwa Ekaristi Takatifu chakula chetu cha kiroho kama Waisraeli waliookolewa toka utumwani Misri na wakalishwa kwa manna jangwani, tusije tukaangamia na kufa kama wengi wao walivyopotea na kufa jangwani sababu ya dhambi zao. Habari zao ziliandikwa ili sisi tuzifahamu tusije nasi kuingia katika shida na taabu kama wao. Hivyo tuchukue tahadhari ili tusirudi katika utumwa wa dhambi maana dhambi inaleta mateso, mahangaiko na mwisho wake ni kifo na kuangamia milele. “Kwa hiyo anayejidhania kuwa amesimama na aangalie asianguke” (1Kor. 10:12).
Katika Injili ilivyoandikwa na Luka (Lk 13:1-9); Yesu anatoa maonyo makali ya madhara ya kutokutubu na kuungama dhambi zetu - kuangamia milele. Maonyo na fundisho hili Yesu analitoa baada ya baadhi ya watu waliojiona kuwa ni wakamilifu wasio na dhambi kumpasha Yesu habari ya Wagalilaya ambao Pilato alichanganya damu yao na dhabihu zao walizokuwa wanamtolea Mungu Hekaluni na habari za watu kumi na wanne, walioangukiwa na mnara huko Siloamu wakafa. Watu hawa waliotoa taarifa hizi walijikinai na kujiona kuwa wao ni watakatifu, hawana dhambi kama Wagalilaya waliouawa na Pilato na kama wale walioangukiwa na mnara wakafa. Yesu anawaambia hakuna binadamu yeyote aliyemkamilifu. Sote mbele za Mungu tu wadhambi. Hivyo tusipotubu tutaangamia milele. Kufa au kuendelea kuishi, kuugua au kutokuugua, kupata majanga au mafanikio sio ishara ya utakatifu. Kuendelea kuishi ni mapango tu wa Mungu wa kumpa mwanadamu muda na nafasi ya kutubu makosa yake kama mwenye shamba anavyoupa mtini nafasi akiupalilia na kuutilia mbolea uzae matunda ili asife katika dhambi, akaangamia milele.
Katika mfano wa mtini usiozaa uliopandwa katika shamba la mizabibu ni wale watu wa taifa teule walioendea kuishi katika dhambi wakiukataa ujumbe wa Mungu wa kutubu dhambi zao kwa mahubiri ya Yohane mbatizaji na baadae kwa mahubiri ya Yesu kwa miaka mitatu; “Tazama, miaka mitatu hii naja nikitafuta matunda juu ya mtini huu, nisipate kitu; uukate, mbona hata nchi unaiharibu?” Mungu anatupa tena nafasi ya kujirudi na kuongoka; “Bwana, uache mwaka huu nao, hata niupalilie, niutilie samadi; nao ukizaa matunda baadaye, vema! La, usipozaa, ndipo uukate”. Ni mwaliko kwetu kujipatanisha na Mungu kwa kuziungama dhambi zetu katika Sakramenti ya Kitubio. Tukumbuke kuwa; “tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe wala kweli haimo ndani yetu. Lakini tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki, atatusamehe dhambi zetu na kutusafisha toka kwenye udhalimu wote. Kama tukisema hatukutenda dhambi, twamfanya Yeye kuwa mwongo na Neno Lake halimo ndani yetu” (1Yn. 1:8-10). Usipoziona na kuzitambua dhambi zako ujue kabisa umezizoea kiasi cha kutokuzitambua kama waswahili wasemavyo; “Mtu hawezi kunusa harufu yake mwenyewe”. Lakini pia yawezekana kuwa mizani yako ya kimaadili imekengeuka sababu ya kiburi kwa tujilinganisha na wengine wanaoteseka na majanga hivyo kujiona huna dhambi. Yesu anatuambia tusipotubu tutaangamia.
Dhambi inaua dhamiri, sauti ya Mungu inayotuwezesha kutambua mema na mabaya. Tunahitaji Kitubio ili kutunza dhamiri zetu ziwe hai. Ndiyo maana mzaburi anatuambia “Dhambi huongea na mtu mwovu ndani kabisa moyoni mwake; wala jambo la kumcha Mungu halimo kabisa kwake. Kwa vile anajiona kuwa maarufu hufikiri kuwa uovu wake hautagunduliwa na kulaaniwa. Kila asemacho ni uovu na uongo; ameacha kutumia hekima na kutenda mema. Alalapo huwaza kutenda maovu, wala haepukani na lolote lililo baya” (Zab.36:1-4). Kumbe, Kitubio kinatusaidia kurudisha urafiki wetu na Mungu. Dhambi ni kumkataa Mungu, na kumkataa Mungu ni kupoteza neema ya utakaso. Ni kitubio peke yake kinaweza kuturudishia Neema hii ya utakaso, yaani uwepo wa Mungu ndani yetu. Kitubio kinasaidia kurudisha urafiki wetu kwa wengine. Bila kitubio hatuwezi kupatana na wale tuliokoseana. Kwa sababu tunajiona wema, hatukubali makosa yetu. Tunaona kuwa sisi tunaonewa tu. Tunapokwenda kuungama, tumejikubali kuwa sisi tuna makossa, tuna dhambi na hii inatusaidia kuomba msamaha na kupatana na wale tuliokosana nao, kwani katika kitubio tunajazwa neema na baraka za Mungu na hivyo tunakuwa na nguvu ya kujipatanisha na wengine.
Tukumbuke kuwa Mungu anatusamehe dhambi zetu katika Sakramenti ya Kitubio kupitia makuhani aliowachagua na kuwaweka kuwa wapatanishi wetu naye. Katika maisha ya kawaida ili aliyekosa asamehewe anapaswa kukiri kosa na kuomba msamaha akisema; “nimekosa naomba unisamehe” na aliyekosa anahitaji kusikia; “nimekusamehe”, vivyo hivyo katika sakramenti ya kitubio tunahitaji kusikia - “Umesamehewa dhambi zako nenda na amani.” Maneno “nami kwa mamlaka niliyopewa na Kanisa nakuondolea dhambi zako” au “Nenda na amani dhambi zako zimeondolewa” yanatupatia uhakika wa kile tulichokipata na haya maneno hayawezi kutamkwa na yeyote yule isipokuwa na Padre anayefanya hivyo katika nafsi ya Kristo mwenyewe. Hivyo tunahitaji kuungama kwa Padre ili tupate hakikisho la msamaha wetu kwa kusikia maneno haya. Tunahitaji kuungama kwa Padre ili tupate ushauri wa kupambana na vishawishi baada ya kuungama. Tunapoungama kwa Padre licha ya malipizi tunayopewa ambayo ni ya muhimu sana, tunapata pia ushauri wa namna ya kupambana na vishawishi vilivyotuangusha dhambini visitushinde tena. Sakramenti hii iliweka na Yesu mwenyewe; “Wowote mtakaowaondolea dhambi wameondolewa; na wowote mtakaowafungia dhambi wamefungiwa” (Jn 20:23).
Tusisahau kuwa upatanisho wetu na Mungu unahitaji upatanisho wetu na ndugu zetu. Ili tusamehewe tunahitaji kusamehe ndiyo maana katika sala ya kuombea dhabihu Padre kwa niaba ya waamini anasali; “Ee Bwana utujalie kwa ajili ya sadaka hizi tujitahidi kuwasamehe jirani zetu, maadam tunakuomba utusamehe sisi dhambi zetu wenyewe”. Tukumbuke kuwa baada ya kifo hakuna tena nafasi ya kutubu, wakati uliokubalika ndiyo sasa, tufanye hima tujipatanishe na Mungu kabla ya kifo. Tuombe ituwie rahisi kuungama, tufanye toba ya kweli, tuvue kweli viatu ili tuweze kusimama mahali patakatifu na kusherekea vyema fumbo la wokovu wetu, yaani Pasaka ya Bwana.