Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya III ya Kipindi cha Kwaresima: Mambo msingi: Toba, Wongofu wa ndani na uaminifu kwa Mungu. Mspotubu mtaangamia. Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya III ya Kipindi cha Kwaresima: Mambo msingi: Toba, Wongofu wa ndani na uaminifu kwa Mungu. Mspotubu mtaangamia. 

Dominika ya III ya Kipindi Cha Kwaresima Mwaka C: Upatanisho!

Njia ya kwanza na kwa kweli ya msingi katika kuiishi toba hii ni maungano ya kisakramenti. Wakati mwingine mtu anashindwa kufanya mabadiliko ya ndani kwa sababu ndani ana moyo mzito, moyo uliobeba hatia, hofu na wasiwasi wa dhambi na hivyo kukosa utulivu. Maungano ya Kisakramenti hutuondolea mizigo hii moyoni na kuujalia moyo uwepesi wa kufanya maazimio mapya.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

UTANGULIZI: Ni dominika ya tatu ya Kwaresima. Katika masomo ya dominika hii tunaupokea mwaliko wa Yesu pamoja na msisitizo wake wa kutubu. Tunayasikia maneno makali ya Yesu anaposema na kurudia “lakini msipotubu, nanyi nyote mtaangamia vivyo hivyo.” Masomo kwa ufupi: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, tunaanza kuyafafanua masomo ya dominika hii kwa kuanzia na somo la Injili. Tunasoma kutoka Injili ya Luka (Lk 13:1-9) ambapo Yesu anapewa taarifa ya matukio mawili ya kusikitisha. Tukio la kwanza ni kuwa kuna watu walikwenda hekaluni kutoa dhabihu zao. Wakiwa hekaluni huko, Pilato, ambae alikuwa mtawala wa Uyahudi, anaamuru wauwawe na damu zao zichanganywe na damu za dhabihu za wanyama walizokuja kuzitoa hekaluni. Inawezekana watu hawa walikuwa ni wahalifu na hukumu ya Pilato inawafuata huko huko hekaluni na wanaangamizwa. Yesu anaposikia habari hiyo anawahoji wale waliokuwa wanamsikiliza “mnadhani watu hao walikuwa ni wadhambi kuliko wengine wote?” na kisha anawaalika “Msipotubu, nanyi mtaangamia vivyo hivyo.” Anaongeza na kutaja watu wengine waliopata ajali ya kuangukiwa na mnara ukawaua.

Vile vile akahoji “mnadhani hao ndio walikuwa wakosaji kuliko watu wote wa Yerusalemu?” Akaongeza tena “Msipotubu, nanyi mtaangamia vivyo hivyo.” Kuna msemo wa kiswahili usemao “ukiona mwenzako anayolewa, zako tia maji.” Usemi huu tunaweza kuutumia hapa ili kuelewa vizuri kile anachokisema Yesu na anachokusudia kufundisha. Ni kuwa matukio kama haya, habari kama hizi tunaposizikia au kuzishuhudia kuhusu wengine ni ujumbe tosha kwetu. Zisipite bila kutubadilisha kwa maana chochote chaweza kutokea kwa yoyote. Katika dini ya kiyahudi majanga kama ajali, ugonjwa na kadhalika yalihusishwa moja kwa moja na dhambi. Kumbe ndugu hao waliokuwa wanasikiliza habari hizi inawezekana walianza kujiuliza “hivi hao wamepatwa na majanga haya, wamefanya dhambi gani” Yesu anaonesha kuwa haipaswi kuhukumu wala kuhoji. Kitu cha kwanza ni kujiangalia mwenyewe na kurekebisha mahusiano yako na Mungu kwa sababu inawezekana wewe ukawa mdhambi zaidi kuliko hao wanaopaswa na majanga kama hayo.

Ni muda wa kujipatanisha na Mungu
Ni muda wa kujipatanisha na Mungu

Injili inatupatia pia mfano wa mtini: mti wa matunda ambao mwenye shamba alikwenda kutafuta matunda asiyaone. Mfano huu wa Yesu umetafsiriwa daima kama mwaliko wa imani inayozaa matunda. Imani isiyozaa matunda ni imani iliyokufa, ni kama mti usiozaa ambao mwenye nao ana haki ya kuukata. Mfano huu wa mtini unapowekwa pamoja na mafundisho hayo ya Yesu yaliyotangulia, yanatupatia ujumbe uliokamilika kuhusu maisha ya kikristo. Ni kuwa maisha ya kikristo hayapaswi kuwa tu ni vita ya kuikimbia dhambi, yaani kujitahidi kutokufanya dhambi kwa Mungu wala kutokuwakosea watu. Maisha ya kikristo ni pamoja na kutenda mema, yaani kutoa matunda ya kile tunachokiamini. Juhudi ya mkristo ya kuepuka dhambi na ya kujitahidi kujipatanisha na Mungu inapaswa kukamilishwa na juhudi ya kutenda mema. Kila mwanzo wa Misa tunapokiri dhambi zetu, tunakiri dhambi tulizozitenda kwa mawazo, kwa maneno na kwa matendo. Lakini hapo hapo tunakiri pia zile nafasi ambazo tulipaswa kutenda mema lakini hakututenda.

Sasa tukirudi katika somo la kwanza pamoja na somo la pili, masomo ya dominika hii ya III ya Kwaresima,  tunaona kuwa haya ni masomo yaliyo na ujumbe unaoshabihiana. Yanatupa picha kuhusu Mwenyezi Mungu kuwa ni yeye ni Mungu anayeokoa wale wanaomkimbilia na ni Mungu anayehukumu wale wanaojitenga naye. Somo la kwanza kutoka kitabu cha Kutoka (Kut 3:1-8a, 13-15), ndilo linalotupa picha ya Mungu anayeokoa. Ni kipindi ambacho waisraeli wako utumwani Misri. Mungu anamtokea Musa katika kijiti kinachowaka moto bila kuteketea na anamwambia anamwambia: “nimeyaona mateso ya watu wangu, nimesikia kilio chako nami nimeshuka ili niwaokoe.” Wokovu wa Mungu unaelezewa katika mambo hayo matatu: nimeona, nimesikia, nimeshuka niokoe. Matendo haya ya ukombozi hayakukoma na waisraeli wa wakati huo, ni matendo ambayo kwa njia ya Kristo, Mungu anayaendeleza kwa wote wanaomcha hadi leo. Huona mahangaiko yao, husikia kilio chao na hushuka kuja kuwaokoa kwa wakati wake na kwa namna inayoendana na mapenzi yake matukufu.

Kutoka katika sura hiyo ya Mungu anayeokoa, somo la pili, kutoka katika Waraka wa Mtume Paulo kwa Wakorintho (1Kor 10:1-6, 10-12) linakuja kututahadharisha dhidi ya kutokuutumia vibaya wema wa Mungu na asili yake ya kuokoa. Mtume Paulo anatuambia Mungu huhukumu pia. Katika barua hii kwa Wakorintho, Paulo anawaasa wakristo wa Korintho ambao baada ya ubatizo wao waliendelea kuabudu miungu wengine na waliendelea kuishi maadili yasiyoendana na imani waliyoikiri. Anawakumbusha dhambi ya uasi ambayo wana wa Israeli waliifanya kabla ya kuingia nchi ya ahadi, wakaadhibiwa na hakuna hata mmoja wa aliyeishiriki aliyeruhusiwa kuingia nchi ya ahadi. Mungu ni mwenye Huruma na Mungu ni mwenye Haki.

Kwaresima ni muda wa kujipatanisha na Mungu na jirani
Kwaresima ni muda wa kujipatanisha na Mungu na jirani

TAFAKARI: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, baada ya kusikiliza masomo ya dominika hii ya III ya Kwaresima na baada ya kupata ufafanuzi wake, ni wakati sasa wa kujiuliza na kutafakari: ninachota nini cha kunisaidia, cha kuniongoza na cha kuniimarisha katika imani yangu hasa katika kipindi hiki cha Kwaresima. Kwa hakika yapo mengi ambayo yametugusa na ambayo tunaweza kuyachukua. Katika nafasi hii, ninagusia moja ambalo ni toba. Hili tunalichota kutoka katika Injili, kutoka katika mwaliko ule ambao Yesu ameutoa: “Msipotubu, nanyi mtaangamia vivyo hivyo.” Toba. Maana ya kawaida kabisa ya neno toba ni kugeuza njia au kubadili njia. Mfano wake ni mtu anayesafiri na katikati ya safari anagundua amepotea njia, basi uamuzi wa kawaida kabisa ni wa kurudi mpaka pale atakapoipata njia ya kumfikisha aendako na hapo anachukua njia sahihi. Katika maisha ya kiroho, toba inabeba pia maana hiyo hiyo ya kubadili njia ya maisha. Lakini inakwenda mbali zaidi na kumaanisha kufanya mabadiliko katika maisha.

Mabadiliko haya yanaweza kuwa ya nje kama mtu anayeamua kubadili paa la nyumba au kupaka rangi kuta za nje, au yanaweza kuwa ni mabadiliko ya ndani, yaani mabadiliko yale yanayobadili muundo mzima au yanayogusa kiini cha maisha ya mtu. Mabadiliko haya ya pili ndiyo hasa ambayo Yesu amekuwa anayazungumzia. Na neno ambalo daima linatumika kumaanisha mabadiliko hayo ya ndani linaitwa metanoia. Kumbe, toba tunayoalikwa kutafakari leo na toba ambayo kipindi hiki cha Kwaresima kinatualika kuifanya ni ile inayogusa mabadiliko yetu ya ndani. Ni wakati muafaka kuomba neema ya Mungu itakayotusaidia kuangaza kile kinachoujaza undani wa maisha yetu na kutupa ujasiri wa kufanya mabadiliko mema. Njia ya kwanza na kwa kweli ya msingi katika kuiishi toba hii ni maungano ya kisakramenti. Hii ni njia ya kwanza kwa sababu ndiyo inayotufanya wapya. Wakati mwingine mtu anashindwa kufanya mabadiliko ya ndani kwa sababu ndani ana moyo mzito, moyo uliobeba hatia, hofu na wasiwasi wa dhambi na hivyo kukosa utulivu.

Maungano ya Kisakramenti hutuondolea mizigo hii moyoni na kuujalia moyo uwepesi wa kufanya maazimio mapya. Njia hii ya maungamo ndiyo msingi kwa sababu yenyewe huanzia pale pale palipo na mzizi wa tatizo. Katika maungamo, macho yetu tunayafumba yasiangalie watu wengine bali tujiangalie wenyewe. Na kwa kweli hapo ndipo ulipo msingi wa mabadiliko, pale ambapo mtu anaanza kujitathmini yeye kama yeye. Mwisho ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, ninakutakia tafakari njema ya dominika hii. Mwenyezi Mungu azidi kukubariki, kukuangaza na kukuimarisha katika kuifuata njia ya toba na akustahilishe kuifikia Pasaka ya Bwana na kuishiriki kwa moyo uliopatanishwa naye na kujazwa na amani yake.

Liturujia D 3 Kwaresima
18 March 2022, 15:17