Tafakari ya neno la Mungu Dominika IV ya Kipindi cha Kwaresima: Ujumbe ni furaha ya kumrudia Mungu kwa toba na wongofu wa ndani; furaha ya upatanisho na amani; maadhimisho ya Mafumbo ya Wokovu. Tafakari ya neno la Mungu Dominika IV ya Kipindi cha Kwaresima: Ujumbe ni furaha ya kumrudia Mungu kwa toba na wongofu wa ndani; furaha ya upatanisho na amani; maadhimisho ya Mafumbo ya Wokovu. 

Dominika ya IV ya Kwaresima Mwaka C: Furaha ya Toba, Upatanisho na Wokovu!

Kutoka kuitwa Injili ya mwana mpotevu, hadi kuitwa Injili ya waana wapotevu, somo hili limefahamika tena kama Injili ya Baba mwenye huruma. Na hapa anayeangaliwa ni baba wa waana wale wawili, baba ambaye haogopeshwi wala habadilishwi na makosa ya wanawe. Upendo wake kwa wanawe upo pale pale hata wanapokosa. Yeye hubaki nje akiwasubiri warudi na kuwapokea.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

UTANGULIZI: Dominika ya nne ya Kipindi cha Kwaresima. Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika tafakari ya masomo ya dominika hii ambayo pia huitwa "domenica Laetare" au “dominika ya furaha.” Tunafahamu kuwa katika kipindi cha Kwaresima matumizi ya ngoma, kinanda na nyimbo za furaha vinapunguzwa kwenye Liturujia. Dominika ya nne ya Kwaresima inatoa nafasi ya kusikia tena sauti hizi za furaha ili tu kutupa ujumbe kuwa Kwaresima sio kipindi cha huzuni, ni kipindi kinachotuandaa kuishiriki furaha ya kweli, furaha ya ukombozi wetu. Na masomo tunayoyasoma na kuyatafakari katika dominika hii, yote yanatuelekeza kuupokea ujumbe huo: furaha ya kumrudia Mungu, furaha ya kuishi katika amani na nafsi zetu, furaha ya kushi katika amani na Mungu. Masomo kwa ufupi: Tuyaangalie sasa masomo ya dominika hii kwa kuanza na somo la Injili (Lk 15:1-3, 11-32). Simulizi analolitoa Yesu katika injili ya dominika hii ni simulizi maarufu sana na lina utajiri wa mafundisho. Kutokana na utajiri wa mafundisho yake kumekuwa na namna nyingi za kuliangalia. Kwa wengi, somo hili linajulikana kama Injili la mwana mpotevu. Na mwana mpotevu huyu ni yule kijana mdogo aliyeomba urithi kwa baba yake akaodoka nyumbani, akaenda kutapanya mali zake, akaishi kwa taabu na mahangaiko nje ya nyumbani lakini baadaye akatubu moyoni na kuamua kurudi nyumbani.

Tunayasikia maneno yake ya toba akimwambia baba yake “baba, nimekosa mbele ya mbingu na mbele yako, sistahili tena kuwa mwanao, unifanye kama mmojawapo wa watumishi wako.” Katika nafasi nyingine, somo hili limejulikana pia kama Injili ya waana wapotevu kwa sababu inaonekana aliyepotea si yule mwana mdogo peke yake bali hata yule mwana mkubwa aliyebaki nyumbani. Mwana huyo mkubwa alibaki nyumbani lakini moyo wake haukuwa nyumbani. Alifanya kazi na baba yake kama mtu wa kibarua akitegemea kulipwa na si kushiriki upendo wa kinyumbani. Mdogo wake aliporudi, yeye alikataa kuingia ndani kushiriki furaha na upendo wa kifamilia. Hakuwa tayari hata kumtambua mdogo wake kwa jina, akamwita, akimwambia baba yake, “huyu mwana wako.” Huyu naye alipotea kwa sababu alijihesabia haki na alipotea kwa sababu alikataa kuingia ndani. Kutoka kuitwa Injili ya mwana mpotevu, hadi kuitwa Injili ya waana wapotevu, somo hili limefahamika tena kama Injili ya Baba mwenye huruma.  Na hapa anayeangaliwa ni baba wa waana wale wawili, baba ambaye haogopeshwi wala habadilishwi na makosa ya wanawe. Upendo wake kwa wanawe upo pale pale hata wanapokosa. Yeye hubaki nje akiwasubiri warudi. Na wanapozingatia moyoni makosa yao na kuomba toba, yeye yuko tayari kuwapokea na anawapokea bila masharti yoyote.

Furaha ya kushiriki mafumbo ya wokovu kama sehemu ya hija ya maisha.
Furaha ya kushiriki mafumbo ya wokovu kama sehemu ya hija ya maisha.

Tukirudi sasa katika somo la kwanza na la pili tunauona mwelekeo ambao liturujia ya leo inatupatia katika kulielewa na kulipokea fundisho la Kristo katika mfano huu anaotupatia. Somo la kwanza ambalo linatoka katika kitabu cha Yoshua (Yos 5:9, 10-12) linatupeleka katika tukio la waisraeli kuingia katika nchi yao ahadi na kula Pasaka kwa mara ya kwanza katika nchi yao hiyo ambayo Bwana alikuwa amewaahidia. Ni furaha ya kurudi nyumbani baada ya kipindi kirefu sana walichokitumia nje. Na hapa tunarudi tangu wana wa Yakobo walipoenda Misri kutafuta chakula, wakafanywa watumwa huko hadi Mungu alipowatoa kupitia mtumishi wake Musa na kuwaongoza jangwani kwa kipindi cha miaka 40. Ni tukio la furaha kubwa sana kwa sababu ndio tukio linaloonesha kukamilika ukombozi ambao Mungu alikuwa amewaahidia. Somo la pili, waraka wa pili wa mtume Paulo kwa Wakorintho (2Kor 5:17-21), linazungumzia upatanisho. Na upatanisho anaouzungumzia Paulo ni ule wa mtu kujipatanisha na Mungu. Upatanisho huu Paulo anauita kuingia katika maisha mapya: kuwa kiumbe kipya, kuyaacha ya kale na kuuvaa utu mpya.

TAFAKARI: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, baada ya kusikiliza masomo ya dominika hii ya IV ya Kwaresima na baada ya kupata ufafanuzi wake, tunapenda sasa kungalia tunachoweza kutoka nacho kama tafakari ya kutusaidia kuyaishi mafundisho yake. Tafakari hii tunaichota kutoka katika dhana ile ile inayotawala masomo haya: furaha ya kurudi nyumbani kama furaha ya kujipatanisha na nafsi zetu na furaha ya kujipatanisha na Mungu. Na hapa tunaona mifano miwili mikubwa ambayo Injili ya leo imeweka mbele yetu. Mfano wa kwanza ni wa yule kijana mdogo na wa pili ni wa baba yake. Yule kijana mdogo hakuwa anaishi maisha mazuri. Ni kijana anayewakilisha watu wanaoishi katika mahangaiko ya kutafuta utulivu katika maisha. Na katika kutafuta utulivu huo anakuwa anaongozwa na ndoto: “nikitoka hapa nitatulia, nikipata hiki nitatulia, nikifika huko nitatulia, nikiwa fulani nitatulia n.k.” Na ni kwa ndoto hizi aliomba urithi  wake mapema akiamini akiwa na mali atatulia, haikuwa hivyo. Akatoka nyumbani akiamini huko nje, mbali na labda kubanwa banwa na familia atatulia, haikuwa hivyo. Akatafuta kibarua akidhani kuwa labda ni kwa sababu hana kazi na akipata kazi atatulia, haikuwa hivyo. Yote hayo si kwamba hayana maana.

Injili ya Baba Mwenye Huruma.
Injili ya Baba Mwenye Huruma.

Kijana huyu aliruka au alipuuzia kipengele muhimu. Injili inatumia maneno “alipozingatia moyoni mwake” kuonesha ni wapi mambo yaliyopoanza kubadilika. Alipozingatia moyoni mwake akatambua alichokuwa anakifanya, akatambua muda aliokuwa anapoteza, rasilimali na hasa zaidi tunu alizokuwa nazo ambazo hakuzitambua awali kwa sababu tu alipendelea kuishi maisha ya juu juu yasiyo na undani, maisha ya vionjo bila misingi au kama tunavyoweza kusema “aliishi kwa kujidanganya mwenyewe.” Alipozingatia moyoni mwake ni pale alipoamua kuisikiliza sauti ya dhamiri yake ya ndani na kusema sasa basi. Siwezi kuendelea kuishi kwa kuukimbia ukweli kuhusu maisha yangu, siwezi kuendelea kuchukulia kwa juu juu kitu chenye thamani kubwa namna hii kama maisha. Akaamua kurudi nyumbani kwa maana huko ndiko alikouacha utulivu aliokuwa akiutafuta Mfano wa pili na wa msingi ni wa baba yake. Yeye amekuwa kichocheo kikubwa cha kuyatimiza matamanio ya mwanae kwa sababu amekuwa ni baba mwenye huruma. Amempokea bila kumuuliza chochote kwa sababu daima alikuwa akimsubiri. Ni wazi hapa Yesu anamzungumzia Baba yetu aliye mbinguni kwani ndiye pekee aliye na huruma kubwa kiasi hiki. Tena sio kwamba yeye ana huruma bali yeye ni huruma yenyewe. Ni yeye anayetuambia “mimi niko tayari kukupokea tena nyumbani nikupe kitulizo unachotafuta, sitakuuliza chochote, ninataka kuona tu utayari wako wa kutubu na kurudi.” Mfano huu unatualika kwa namna ya pekee zaidi kumrudia Mungu. Lakini tukiuangalia kwa undani zaidi unatualika kutambua kuwa hatuwezi kumrudia Mungu na kujipatanisha naye kabla hatujajipananisha na nafsi zetu. Hatuwezi kumrudia Mungu kama ile thamani Mungu aliyoiweka ndani yetu hatuioni na tunaipuuzia kwa namna moja au nyingine. Safari ya kumrudia Mungu ni safari ya kurudi katika nafsi zetu.

Liturujia D4 Kwaresima
24 March 2022, 16:26