Dominika ya IV ya Kwaresima Mwaka C: Injili ya Baba Mwenye Huruma
Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.
Amani na Salama. Tunaongozwa na Injili ya Luka 15: 1-3, 11-32. Simulizi la leo, la “Mwana Mpotevu”, kama wengi wanavyopenda kuliita ni moja kati ya masimulizi yajulikanayo na wengi, na mara nyingi linatumika katika Ibada za kitubio, ili kutualika kufanya toba na kumrudia Mwenyezi Mungu. Kama nilivyotangulia kusema linajulikana kama simulizi la “Mwana Mpotevu”, yafaa tuseme kutoka mwanzo jina hilo linapotosha ujumbe kusudiwa na hasa muhusika mkuu wa simulizi lenyewe. Katika simulizi tunasikia wahusika watatu, mwana mdogo, mwana mkubwa na baba mwenye huruma, nawaalika leo tutafakari kwa pamoja na hivyo kuiona waziwazi nafasi ya mhusika mkuu ambaye ni baba, na ndio kusema simulizi hili ni vema kuliona ni juu ya “Mungu mwenye Huruma, Baba mwenye Huruma, Baba mwenye Upendo”. Na hasa katika simulizi hili Yesu anatualika kuwa na taswira au sura halisi ya Mungu, kuwa ni mwenye huruma na upendo kamili kwetu. Ni kwa kuangalia simulizi zima tunaweza kupata sababu kwa nini Yesu hamalizii simulizi hili mara baada ya kurejea nyumbani yule mwana mdogo na kupokelewa na baba yake na kufanyiwa sherehe kubwa, na hivyo sehemu ya mwisho ya simulizi la leo inayomuhusu mwana mkubwa ingeonekana kutokuwa na maana. Simulizi letu linakosa hitimisho, kwani hatusikii zaidi juu ya mwana mkubwa kama alikubali ombi la baba yake na kujumuika kwenye furaha ya kurejea kwa ndugu yake au la.
Yafaa tangu mwanzo kukumbuka kuwa simulizi la leo Yesu hakuwa anawahubiria wadhambi, bali kwa mafarisayo na waandishi waliolalamika baada ya kumuona Yesu akila na kunywa pamoja na wadhambi na watoza ushuru. Na si wadhambi au watoza ushuru waliotubu au kubadili maisha yao, bali ni wale walioonekana kukomaa bado katika uovu wao. Na ndio lalamiko la mafarisayo na waandishi, kwani wangekuwa ni wadhambi waliofanya toba basi malalamiko yao yangekosa mashiko. Ni Mafarisayo na Waandishi ambao bado wana taswira au sura ya Mungu isiyokuwa sahihi. Hivyo Yesu anatumia fursa ya simulizi la leo ili waweze kubadili vichwa vyao, kubadili mtazamo wao na kumwangalia Mungu Baba kuwa daima ni Mwenye Huruma na Upendo usio na masharti, hivyo anatupenda wote wema kwa waovu bila ubaguzi, huu ndio Upendo wa Mungu! Unashangaza na kutafakarisha kwa hakika! (Sura ya 14:1) inayotangulia sehemu ya Injili ya leo, tunaona Yesu anaalikwa katika nyumba ya mfarisayo, na leo tunaona anaitika pia mwaliko wa kwenda na kula na kunywa pamoja na wadhambi na watoza ushuru. Ni katika muktadha huu tunaona mafarisayo na waandishi waliojiehesabia haki na kujiona ni watu wa dini wanakwazika kumuona Yesu akila na kukaa pamoja na wale walioonekana ni wadhambi na hivyo mbali na Mungu. Ni katika mazingira haya tunaona Yesu anatumia fursa hii kuwapa simulizi la Huruma ya Mungu, simulizi la Upendo wa Mungu bila masharti.
Ni sehemu ya mwisho ya simulizi hili tunaona msingi wa simulizi pale anaporejea kutoka shambani kijana mkubwa, ambaye kwa hakika anawakilisha mafarisayo, waandishi na hata wengi wetu katika jumuiya ya waamini. Dini yetu ya Kikristo ni mwaliko wa kubadili vichwa, kubadili mtazamo, na ndio tunaweza kusema ni dini inayotutaka tutoke kwenye mazoea ya dini na kuivaa imani, kuingia kwenye mahusiano ya kweli na Mungu, wengine na viumbe vyote. Mwana mdogo anaomba sehemu ya urithi inayomwangukia na kwenda mbali na nyumbani kwa Baba yake. Kuomba sehemu ya urithi ni ishara wazi kuwa kwake hataki tena mahusiano ya baba na mwana, ni kumchukulia baba yake sawa na mmoja asiyeishi tena. Ni katika tamaduni na mila nyingi hata zile za ulimwengu wa Yesu kuwa mtoto anaweza kuchukua urithi wa mzazi mara baada ya kifo cha mzazi na si kabla. Hivyo ndio kusema kwake baba yake haishi tena, hataki tena mahusiano naye. Ni kujiona hataki tena kuishi chini ya uongozi wa baba yake na hivyo kwenda mbali ili aishi maisha ya uhuru na kupata furaha. Ni kama mwanadamu yule wa mwanzo aliyekataa kuishi kama kiumbe kwa kuwa na mipaka yake, hivyo mwana mdogo anaakisi uhalisia wa kila mmoja wetu mbele ya Mungu Baba yetu.
Mwana mdogo anamuona baba yake ni kikwazo kwa uhuru wake, kwani alikuwa na picha au mahusiano yake na baba yake ni kama ya bwana na mtumwa, ni mahusiano yasiyo na afya, hivyo ana kila sababu ya kuwa huru kwa kwenda mbali na baba yake. Kwake baba yake ni bwana mkubwa, ni mtawala, ni dikteta anayetoa amri na maagizo hivyo yeye anabaki kama mtumwa tu. Lakini pia anaona ili apate furaha na uhuru basi hana budi kuwa mbali na huyu baba anayekuwa kama bwanamkubwa na mtawala. Hivyo mahusiano yake na baba hayakuwa kama baba na mwana, bali kama bwana mkubwa na mtumwa wake. Mara nyingi tunaishia kudhani kuwa ni mwana mdogo tu aliyekosa kujua sura au taswira halisi ya baba, bali hata mwana mkubwa aliyeonekana mtii na kubaki nyumbani kwa baba. Tutaona jinsi pia mwana mkubwa anavyofikiri, alivyojaa majivuno na kujihesabia haki kwa kuwa alibaki kuwa mtii na mshika maagizo yote ya baba yake, na hivyo kwake baba yake hapaswi kumsamehe ndugu yake, na hata haoni tena kuwa aliyerudi ni ndugu yake mdogo, bali kwake ni mwana wa baba na hivyo hataki kujihusianisha naye. Labda hata na sisi mara nyingi tusingependa kujihusianisha na wale wanaoneekana hawafai au wadhambi au wakosaji katika maisha yetu ya kila siku. Mwana mkubwa kama mdogo walikosa kuwa na mahusiano sahihi na baba yao, na ndio hali inayokuwepo ndani mwetu kila mara tunapokusa kuuonja upendo na huruma ya Mungu kwetu, kwa kumtii Mungu hatuwi watumwa au kudogoshwa naye bali ni kuingia katika mahusiano ya ndani zaidi naye.
Mwana mdogo anaishia katika nchi ya mbali. Si tu mbali kijiografia bali mbali na mila na tamaduni na zaidi kiimani. Anaenda nchi ya kipagani, nchi waliofuga nguruwe kwani wana wa Israeli wasingeweza kufuga nguruwe kwani ni haramu kwao. Hivyo simulizi kusema aliishia nchi ya mbali na kumaliza mali zake zote na mwisho kuomba kazi ya kulisha nguruwe, ni ishara tosha kuwa alikuwa mbali pia kidini na kiimani. Ni kujitenga si tu na familia yake, bali na watu wake, na taifa lake, ni kutokuwa na shirika tena na watu wake. Ni kuishi mbali si tu na jamaa zake bali zaidi sana na Mungu na ndio kuishi katika nchi ya kipagani. Kuishi nchi ya Kipagani ni sawa na kuukana utaifa wake, kuwa si mmoja tena kati ya wana wa Israeli. Kuwa mbali na nyumba ya baba ni kukosa furaha na amani. Ni kusaka furaha na amani mahali pasipo sahihi. Ni kudhani tutapata furaha ya kweli kwa kukosa shirika na baba na watu wetu, kwa kujitenga na imani na dini yetu. Kila mmoja wetu anahitaji mahusiano sahihi na Mungu na wengine. Na ndio maana ya kuwa wafuasi wa Kristo, ni kukubali kufanyika wana wa Mungu kwa njia ya Mwana pekee, yaani Bwana wetu Yesu Kristo.
Tunaposoma kwa makini sehemu ya Injili ya leo, tunajiuliza kama mwana yule mdogo alifanya toba ya kweli. Anasukumwa na njaa na mahangaiko ya kuwa mbali na nyumba ya baba yake, na kukumbuka baba yake anawafanyakazi wengi wanaokula na kusaza na yeye anakosa mkate, anakosa chakula hivyo anaona arudi nyumbani ili naye apate mahitaji yake, na hivyo ili kuweza kupata mkate hana budi kuomba msamaha, hivyo sababu ya kurudi kwake ni tabu na mateso aliyoyapata akiwa mbali na nyumbani. (Luka 15:17-19) Labda ingekuwa tofauti kama angefikiri moyoni mwake, ona ni kwa nini nimefika hapa, kwa nini nimevunja mahusiano yangu na baba yangu? Nimeharibu maisha yangu, hivyo kabla ya kufa nirudi nyumbani kwa baba yangu na kuomba msamaha na kumkumbatia tena baba na ndugu yangu. Niterejea nyumbani na kwa vile sistahili basi sitapokea hata kikombe cha chai kwa kuwa mimi ni mkosaji. Kinyume chake yeye anasukumwa zaidi na hali yake ya uhitaji na njaa, na hivyo anarudi nyumbani ili apate kula na kunywa kama ilivyokuwa awali kabla ya kuondoka kwake. Hata tunaona tafakuri yake kabla ya kurejea ni jinsi ya kumshawishi baba yake ili aweze kukidhi mahitaji yake.
Baada ya kutakafari mara moja anaondoka na kurejea, na hata kurudia mbele ya baba yake yale yote aliyokuwa anayawaza kutamka kabla ya kurejea. Hivyo hapo mara moja anaingia muhusika wa pili ambaye kwa hakika ndio muhusika mkuu wa simulizi hili, ambaye ni baba yake. Katika tukio la kurejea nyumbani mwana mdogo, tunaona baba anafanya mambo makuu matano: Ni mambo ambayo wasikilizaji wa mfano wa Yesu na labda hata nasi mara nyingi tunaona hakupaswa kutendewa yule mwana mdogo kwani alipaswa kuwajibishwa kwa makosa na madhambi yake, kwa ukaidi wake wa kwenda mbali na kutapanya mali za baba yake, lakini Injili ya leo inatuonesha upendo na huruma ya ajabu ya Mungu kwa kila mmoja wetu anayetubu. Hebu tuone Habari Njema ya huruma na upendo wa Mungu! Anamwona akiwa mbali. Inawezekanaje kumuona akiwa mbali na katika hali yake mbaya baada ya kumaliza mali zake zote? Kwa hakika unapokutana mtu mliyeachana miaka mingi na akawa kwa kutumia lugha ya mtaani, baada ya kupigika sana kwa hakika hata sura na umbo linabadilika, hivyo si rahisi tena kumtambua. Ni wazi na kweli kabisa baada ya kupoteana kwa miaka mingi ila kwa wale watu tunaowapenda kweli daima wanabaki katika mioyo yetu, ndio kusema tunawaona hata wakiwa mbali kwani wanabaki katika mioyo na vichwa vyetu kila mara au kila siku. Ni watu tunaowakumbuka na kuwaona iwe mchana au usiku, kwani wapo mioyoni mwetu. Ni upendo tu unaoweza kutuunganisha hata na wale wanaokuwa mbali na hivyo kuweza kuwaona na hasa hali zao duni na mbaya.
Na ndio anamwonea huruma! Hii hali aliyekuwa nayo baba kwa Kigiriki inajulikana kama “splagknizomai” likimaanisha hasa ile hali anayokuwa mama kwa mwana wake wa kumzaa. Ni upendo au uchungu anaokuwa nao mama kwa mwana wake aliyembeba katika tumbo lake la uzazi. Mara nyingi utasikia akina mama wakisema tumbo la uzazi lilinicheza katika mazingira haswa anapoona kuna baya linamkuta mwana wake. Labda ni vema kumuuliza mwanamama jinsi anayotabika anapoona mwana wake katika hali ngumu! Katika Agano Jipya neno hili linatumika mara 12 likionesha upendo wa Mungu kwetu. Ni upendo wa ajabu usijali hali ya mwana. Mama anampenda mwana wake hata akiwa ni mtenda maovu, machoni kwake anabaki na thamani ile ile ya kuwa ni mwana wake. Anamkimbilia: Ni kitendo kinachosukumwa na upendo kwa mwana wake. Simulizi linaonesha wazi huyu baba alikuwa na umri mkubwa ila hakujali uzee au utu uzima wake na hivyo hakujali hatari ya kudondoka kwani alimpenda mwana hivi hakujali hatari yeyote. Na ndio upendo wa Mungu kwetu, daima anatukimbilia kututoa katika hali mbaya ya kuwa mbali naye. Ni Mungu anayetuona tungali mbali na ni Yeye anayekuwa wa kwanza kutujia na kutukumbatia. Akamlaki: Kwa kweli ni zaidi ya kumbatio, kitendo hiki tunakutana nacho pia kwa wazee wa Kanisa la Efeso walipomuaga Paulo, wakijua hawatamuona tena, hivyo walimuaga kwa kumbatio hilo la pekee huku wakibubujikwa na machozi ya uchungu yaliyojaa upendo wao kwa Mtume Paulo. Mungu daima anatulaki na kutukumbatia kila mara tunapokuwa tayari kuanza naye mahusiano ya Baba na mwana.
Alimbusubusu: Si tu busu la kumkaribisha mgeni, bali ni busu la upendo wa ndani kabisa, ni busu la msamaha, ni busu endelevu kwani halina kikomo. Hivyo baba hakuruhusu mwana wake apige magoti na kuomba msamaha bali alimkumbatia na kumbusu kwa upendo. Ni Upendo wa aina gani huu! Na ndio tunaona mwana mdogo anaanza kurudia tena yale maneno aliyoyatakafari kabla ya kuanza safari ya kurejea na tunaona kabla ya kumaliza maneno yake mara moja baba yake anaanza kutoa maagizo kwa watumwa wake: Vazi refu na zuri: Kwa kawaida ni mwana ndiye aliyevaa vazi refu kwani watumwa daima walipaswa kuvaa makanzu mafupi kwa kutumikia kirahisi. Wateule kule mbinguni nao wanavaa mavazi haya marefu mbele ya Mwanakondoo. (Ufunuo 7:9). Pete kidoleni: Sio pete ya ndoa au uchumba bali ile ya muhuri. Ni pete ya mamlaka na umiliki, hivyo ni mwana kweli na ana mamlaka kwa wafanyakzi wa baba yake na hata mali zake. Na viatu miguuni: Ni ishara ya mtu aliye huru. Watumwa hawakuvaa viatu walitembea pekupeku. Nyumbani kwa baba hakuna watumwa bali wana walio huru. (Yohana 15:15) Mungu wetu sio mtawala wa kuogofya, bali daima ni Baba yetu anayepaswa kupendwa kwani yeye daima anatupenda hata tukiwa mbali naye, hata tukiwa katika hali ya dhambi na kupotea, anatualika kurejea kwake na daima anatupokea na kutupa tena na tena nafasi ya kuwa wana na warithi pamoja na Mwana pekee, Bwana wetu Yesu Kristo.
Kurejea kwake nyumbani kwa baba kunahitimishwa na sherehe kubwa. Kwa Wayahudi Mungu anafanya sherehe kwa wale wadhambi wanaofanya toba ya kweli, hivyo sehemu hii ya mwisho ya simulizi letu inabaki kuwa ni kikwazo kwao. Sura ya Mungu inayohubiriwa na Yesu katika sehemu ya Injili ya leo ni tofauti na ile waliyokuwa nayo mafarisayo na labda hata wengi wetu leo; Ni Mungu anayefanya sherehe hata kwa wale wasiostahili, anawakaribisha shereheni hata wale ambao bado hawajafanya toba ya kweli, anawakumbatia na kuwabusu bila kuwauliza lolote au kuwaadhibu kwa makosa na madhambi yao. Ni hii tofauti ya Yesu na Mafarisayo na waandishi na hata baadhi yetu. Kama Yesu angekuwa anawakaribisha na kufika kwa wadhambi waliofanya toba, basi kwa hakika mafarisayo kama nilivyotangulia kusema wasingekwazika. Ila alifika na kula na kunywa na watu waliokuwa bado kufanya toba, kwani watoza ushuru waliendelea na kazi yao na hata wadhambi waliendelea na hali yao. Ndio kusema anafunua sura ya Mungu iliyo sahihi, Mungu anayetupenda wote bila ubaguzi, bila masharti, bila mastahili kwa kuwa ni wema bali hata tunapokuwa wadhambi. Ni Mungu anayeangazia jua lake kwa wema na waovu, anayetujalia mvua yake bila ubaguzi. (Mathayo 5:44-48) Huruma na upendo wa Mungu kwetu sio matunda ya mastahili yetu bali daima ni upendeleo wa Mungu kwa kila mmoja wetu.
Ni katika muktadha huu tunabaki na maswali na hasa kama Mungu anatupenda sote kwa nini nifanye toba, kwa nini kubadili maisha yangu? Kujibu swali hili hapo tunakutana na muhusika wa tatu wa simulizi la leo, yaaani mwana mkubwa. Anarejea pia nyumbani mwana mkubwa akiwa amechoka na kazi za siku nzima, na labda kutumika pale nyumbani kwa miaka mingi akiwa peke yake. Anawasili na kupigwa na butwaa kukuta sherehe kubwa nyumbani kwao. Sherehe ambayo si tu hakualikwa bali pia kutaarifiwa kabla. Hivyo anamuita mmoja wa watumwa na kuhoji juu ya sherehe ile. Hata baada ya kuelezewa na mtumwa yule bado alibaki bila kuamini na zaidi alipatwa na uchungu na kukasirika. Hivyo baba anatoka nje na kumsihi ili naye ashiriki furaha ya kurejea kwa ndugu yake. Baba anamsihi sana ila yeye anaanza kujihesabia haki kwa kuorodhesha mastahili yake: Hajawahi kuvunja au kwenda kinyume na maagizo ya baba yake, alimtumikia baba yake kiaminifu. Kwa kweli mwana mkubwa anaonesha kikamilifu mtazamo wa mafarisayo na hata baadhi yetu tunaokuwa nao kwa wadhambi. Tunaweza kurejea sala ya mfarisayo aliyefika hekaluni kusali na kuanza kumshukuru Mungu kwani yeye ni tofauti na wengine walio wadhambi, wazinifu na hata alifunga mara mbili kwa wiki. (Luka 18:11-12) Hata kama maneno anayosema kidogo yanakosa upendo kwa ndugu yake lakini ni kweli kabisa. Labda hata nasi tunaweza kuungana naye na kusema ana haki ya kumhoji baba yake.
Ni kama mwana mkubwa ndivyo mafarisayo na waandishi walivyokuwa wanawaza na kufikiri na hata nasi mara nyingi tunawaza na kufikiri kama mwana mkubwa. Ni mantiki yetu ya kibinadamu inatusukuma kuona kuwa mkosaji hana budi kuadhibiwa, hivyo kuwajibika kwa makosa au madhambi yake. Mara nyingi tunabeba uhusika wa wana wote wawili, lakini yafaa tutambue na kuchagua leo; Je, tunataka kufanana na mwana mdogo anayekuwa mdhambi na mkosaji na anayetambua hali yake ya ndani kuwa alikuwa “misera” na hivyo alihitaji huruma na msamaha wa baba yake “misericordia”, au tunataka kubaki kama mwana mkubwa anayejihesabia haki na kujiona sio mdhambi na mkosefu lakini ndani mwake anabeba ubaya na kukosa upendo na huruma kwa mdogo wake? Baba kwani daima ni “misericordia”, yaani huruma na rehema yenyewe, kamwe hatulazimishi kubaki kwenye mahusiano mema naye, kwani angalifanya hilo angepoteza sifa yake ya kuwa wema wenyewe, ya kuwa upendo wenyewe, kwani Mungu ametuumba sio kwa kulazimika bali kutokana na upendo wake, na hivyo akatukirimia kufanana naye, ndio kutupatia sura na mfanano wake, yaani akili ya kutambua mema na mabaya na utashi wa kuamua kuchagua mema na kuepa yaliyo maovu na mabaya.
Hivyo, hata mwana mkubwa pamoja na kubaki nyumbani kwa baba yake bado hakuwa ametambua sura halisi ya baba yake, kuwa baba yake hakuhitaji watumwa nyumbani mwake bali wana tena walio huru. Na ndio tunaona mwana mdogo anatamka neno baba mara tano, na kwa mshangao wetu mwana mkubwa neno baba halitamki hata mara moja. Kwake baba bado ni mtawala au bwana mkubwa na hivyo mahusiano yake na baba ni katika kutii maagizo na amri zake, hivyo anakosa kuwa na sura sahihi ya baba. Na kwa kukosa mahusiano sahihi na baba pia anakosa mahusiano sahihi na ndugu yake na hivyo hataki kumtambua kama ndugu yake bali ni mwana wa baba. Na baba tunaona mara moja anamsahihisha kwa kusema ni ndugu yako amerejea aliyekuwa amekufa. Mwana huyu mkubwa, ndio kila mmoja wetu ambao tunaweza kujiona tunabaki nyumbani kwa Baba, lakini mioyo yetu ipo mbali naye kwani tunakosa kuwa na mfanano na Baba, ndio kukosa huruma na rehema. Tunaweza kuwa ni watu tunaoshiriki Ibada kila siku, kusali kila siku, kusoma na kusikiliza Neno lake na kulitafakari kila siku lakini ndani mwetu bado tunabeba roho ile isiyofanana na ya Mungu Baba yetu aliye huruma yenyewe, yaani, “misericordia”. Kufanya toba ni kukiri kuwa sisi ni wana wa Mungu, na hivyo hatuna budi kuingia katika mahusiano mema kwanza na Mungu, na pili na ndugu zetu, yaani wengine wote wanaotuzunguka.
Simulizi la sehemu ya Injili ya leo linamalizika bila kuwa na mkia au hitimisho, kwani bado tunabaki na maswali kama je, mwana mkubwa alikubali kuingia karamuni na nini kilitokea baada ya kumuona ndugu yake mdogo amerejea nyumbani, je alijawa na furaha ya bashasha au chuki kwa ndugu yake hata baada ya baba yao kumsihi na kuomba abadili roho na moyo wake au kubadili kichwa chake? Je, aliweza kumkumbata kwa busu ndugu yake mdogo aliyepatikana tena akiwa hai, yaani, kumsamehe na kumuonjesha upendo wa kindugu? Injili haisemi kitu, kwani inatualika sisi wasikilizaji wa Neno leo tuingie ndani mwetu na kujiuliza juu ya mfanano wetu wa ndani kama tunafanana kweli na sura halisi ya Mungu au la. Wapendwa sehemu ya Injili ya Dominika ya leo ni juu ya Huruma na Upendo wa Mungu usio na masharti, Mwenyezi Mungu siku zote za maisha yetu anatualika kurudi kwake na hata tunapobaki mbali naye yeye daima anatupenda. Kwaresma ni kipindi cha kufanya toba, kurejesha mahusiano mema na Mungu na wenzetu, ni kipindi cha neema, kwani tunaalikwa kufanana na Mungu, na pili kuwa na sura halisi ya Mungu. Nawatakia tafakari na Dominika njema sanjari na matayarisho mema ya maadhimisho ya Fumbo Kristo (PASAKA).