Liturujia ya Dominika ya IV ya Kipindi cha Kwaresima Kwa Mwaka C ni mwaliko wa kutafakari kuhusu: toba, wongofu wa ndani, huruma, msamaha na upendo wa Mungu kwa waja wake. Liturujia ya Dominika ya IV ya Kipindi cha Kwaresima Kwa Mwaka C ni mwaliko wa kutafakari kuhusu: toba, wongofu wa ndani, huruma, msamaha na upendo wa Mungu kwa waja wake. 

Dominika ya IV ya Kwaresima Mwaka C: Toba, Huruma na Upendo wa Mungu.

Masomo yanatuonesha huruma na upendo wa Mugu usio na kifani. Toba, wongofu wa ndani, huruma na upendo ni mambo makuu na mazito yanayohitajika ili kuendeleza mchakato wa: haki jamii, amani na maridhiano kati ya watu na kati ya mtu na nafsi yake ili kupata suluhu ya changamoto mbalimbali zinazomwandama mwanadamu katika hija ya maisha yake hapa duniani.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya liturujia ya Neno la Mungu, katika Dominika ya nne ya kipindi cha Kwaresima mwaka C wa Kanisa, siku ya ishirini na sita ya kujitakatifuza. Ni dominika ya furaha kama wimbo wa mwanzo unavyoimba Furahi, Ee Yerusalemu, mshangilieni ninyi nyote mmpendao; furahini, ninyi nyote mliao kwa ajili yake, mpate kunyonya, na kushibishwa kwa maziwa ya faraja zake” (Isa. 66:10-11). Tunaalikwa kufurahi kwasababu Pasaka i karibu. Litrujuia ya dominika hii inaruhusu altare kupambwa kwa maua, rangi ya mavazi ya Misa kuwa ya pinki badala ya zambarau pia ala za muziki zinaruhusiwa kupigwa. Katika Dominika hii huadhimishwa takaso la pili la wakatukumeni watakaobatizwa siku ya Pasaka. Masomo ya dominika ya Nne ya Kipindi cha Kwaresima yanatuonesha huruma na upendo wa Mugu usio na kifani. Toba, wongofu wa ndani, huruma na upendo ni mambo makuu na mazito yanayohitajika ili kuendeleza mchakato wa: haki jamii, amani na maridhiano kati ya watu na kati ya mtu na nafsi yake ili kupata suluhu ya matatizo na changamoto mbalimbali zinazomwandama mwanadamu katika hija ya maisha yake hapa duniani. Kuna haja kwa Mama Kanisa kujikita katika mchakato wa toba na wongofu wa ndani, ili kuongoa roho za watu, tayari kuambata huruma, haki jamii na amani ambayo kimsingi ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayomshirikisha mwanadamu.

Somo la kwanza kutoka kitabu cha Yoshua (Yos. 5:9a, 10-12); ni maagizo ya Mungu kwa wana wa Israeli namna ya kuadhimisha sikukuu ya Pasaka, wakikumbuka jinsi Mungu alivyowaokoa utumwani Misri na kuwafikisha katika nchi ya ahadi. Ni siku ya kukumbuka ile siku ambayo Mungu aliwaondolea aibu ya kuwa watumwa Misri, akawawezesha kupigana vita na kuichukua, kuimiliki na kuikalia nchi ya ahadi, wakaanza maisha mapya huko Kanaani maeneo ya Gilgali. Namna hii waliuonja wema wa Bwana kama mzaburi anavyotuambia katika wimbo wa katikati; “Onjeni mwone ya kuwa Bwana yu mwema ni mwaliko wa furaha” (Zab. 34:8). Hivyo wakala sikukuu ya Pasaka siku ya kumi na nne ya mwezi, jioni, katika nchi tambarare za Yeriko. Nao wakala katika mazao ya nchi siku ya pili ya kuiandaa hiyo sikukuu ya Pasaka kwa mikate isiyotiwa chachu, na bisi, siku hiyo hiyo. Ndipo ile manna ikakoma siku ya pili yake, baada ya wao kuyala hayo mazao ya nchi; na hao wana wa Israeli hawakuwa na manna tena; lakini wakala mazao ya nchi ya Kaanani kuanzia mwaka huo. Katika somo la pili la Waraka wake wa pili kwa Wakorintho (2 Kor. 5:17-21); mtume Paulo anatufundisha jinsi dhambi ilivyotutenganisha na Mungu, lakini Kristo alitupatanisha kwa kifo chake na upatanisho huo unaendelezwa na wajumbe waliotumwa na Kristo nasi tunapaswa kufanya jitihadi za kujipatanisha na Mungu kwa njia Kristo, yeye asiyejua dhambi lakini Mungu alimfanya kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika Yeye. Ni upendeleo wa hali ya juu sana tunaopewa na Mungu hivyo hatuna budi kuupokea kwa moyo wa shukrani na furaha.

Tunahitaji Kujipatanisha na: Mungu, Jirani na Mazingira Nyumba ya Wote
Tunahitaji Kujipatanisha na: Mungu, Jirani na Mazingira Nyumba ya Wote

Injili ilivyoandikwa na Luka sura ya 15 imebeba mifano mitatu ya Yesu inayoelezea Huruma ya Mungu - mfano wa kondoo aliyepotea (Lk 15:4-7), mfano wa sarafu – shilingi iliyopotea (Lk 15:8-10), mfano wa mwana mpotevu (Lk 15:11-32). Katika mfano wa mwana mpotevu na Baba mwenye huruma, Yesu anawafundisha Mafarisayo kuwa hata wakosefu wanaweza kuingia katika Ufalme wa Mungu kama wakitubu dhambi zao na wema wanaweza kuukosa ufalme wa Mungu kama watakengeuka kwa kiburi na kuwa kinyume na Mungu. Fundisho hili analitoa baada ya mafarisayo na waandishi kumnung¢unikia kwa kuwakaribisha watoza ushuru na wenye dhambi, akala na kunywa nao hata nao wakazidi kumkaribia ili wamsikilize wapate faraja na neno la furaha kutoka kwake. Simulizi hili linatuonyesha wazi huruma ya Mungu ilivyo kubwa kiasi kwamba tunapofanya toba ya kweli moyoni Mungu anatupokea mara moja, anatukumbatia, anatubusu sana, anatuvika mavazi mapya, anatufanyia sherehe kubwa, tunakuwa huru na kupewa hadhi ya kushiriki karamu ya Kristo, Ekaristi Takatifu ambayo ni kiini cha maisha yetu ya kikristo, nasi tunajaa furaha kubwa ndani mwetu, furaha isiyokifani na kuanza maisha mapya. Hii ndiyo furaha anayokuwa nayo mtu akifanya toba ya kweli na kuungama vyema dhambi zake, akizitaja waziwazi kwa ujasiri bila kuzimumunya wala kuficha chochote.

Ni furaha ya ajabu isiyoelezeka, furaha inayotuondolea mawazo ya kukata tamaa na inayotupa matumaini na nguvu ya kusonga mbele katika maisha yetu. Sakramenti hii ya ya kitubio inatuondolea aibu ya dhambi na kutuweka huru tukiwa wenye furaha. Waisraeli walipelekwa utumwani Misri kwa sababu ya dhambi na mwana mpotevu alipelekwa kwenye banda la nguruwe kwa sababu ya dhambi baada ya kula mali ya baba yake na makahaba. Nasi pia inawezekana dhambi imetupeleka utumwani au kwenye banda la nguruwe. Tunapaswa kutafakari na kuzingatia mioyoni mwetu na kujiuliza; “Misri yangu ni wapi?” na “banda langu la nguruwe ni lipi?” Je, ni kitu gani kimenipeleka huko? Je, ni dhambi ipi imenipeleka huko - ukahaba, uasherati, nyumba ndogo, ulevi, utoaji mimba, madawa ya kuzuia mimba, uchawi na ushirikina, uzembe, ubinafsi, masengàenyo, umbea, uongo, ulafi, kiburi, marafiki wabaya, madawa ya kulevya, wizi, ujambazi, rushwa, ukaidi, kutokufunga, kutokusali, kutokuwasaidia wahitaji au ni nini? Ni wakati wa kutafakari na kuzingatia moyoni na kuamua na kusema; inatosha, ninaondoka na kuachana na umisri au ubanda wa nguruwe. Usiogope rudi kwa Baba ukaungame na kumwambia nimekosa nihurumie. Mama Kanisa anatufundisha kuwa dhambi inaondolewa kwa njia ya sakaramenti ya ungamo la Dhambi. Sakramenti hii inaitwa pia Sakramenti ya toba, Sakramenti ya kitubio, Sakramenti ya maungamo, Sakramenti ya msamaha, Sakramenti ya Upatanisho. Kuungama ni ile hali ya mdhambi aliyetayari kutubu kwa kujishutumu mwenyewe kutokana na dhambi alizozitenda mbele ya mhudumu halali wa Kanisa ili kujipatanisha na Mungu.

Sakramenti ya Upatanisho ni kielelezo cha huruma, msamaha na upendo wa Mungu
Sakramenti ya Upatanisho ni kielelezo cha huruma, msamaha na upendo wa Mungu

Mwenyezi Mungu tuliyemkosea ndiye anayeanzisha upatanisho nasi. Anafanya hili kwa njia ya mwanae wa pekee Bwana Yesu Kristo. Mwaliko tunaoupewa wa kufurahi kwa sababu Pasaka i karibu, unatudai tuondoke, tuende kwa Baba, tukaungame, tukamwambie tumekosa. Hiki ndicho alichokifanya mwana mpotevu lakini ni baada ya kutafakari na kuzingatia moyoni mwake ndipo akaondoka, akaenda na kumwambia Baba, nimekosa, nihurumie, nasi tunapaswa kufanya vivyo hivo. Lakini kuondoka na kwenda si rahisi. Inahitaji ujasiri na neema ya Mungu, kila mmoja katika hali yake anahitaji ujasiri na kusema sasa imetosha, nitaondoka na nitakwenda. Kamwe tusikubali ukubwa wa dhambi utukatishe tamaa ya kupata msamaha, kwani jinsi dhambi ilivyo kubwa ndivyo nguvu ya huruma ya Mungu ilivyo kuu zaidi. Bwana ni mwema na mwenye huruma, hapendi wadhambi wapotee na si mwepesi wa hasira ni mwingi wa huruma (Zab. 130). Tunapaswa kumrudia Mungu kwa kusema kama Mfalme Daudi; Unihurumie, Ee Mungu, kulingana na pendo lako kuu, kwa wingi wa huruma yako kuu uniondolee dhambi zangu” (Zab. 51). Lakini tujue wazi kuna wapo watakaochukiza na maamuzi yetu kama mafarisayo na waandishi walivyomnungàunikia Yesu au kama kaka wa mwana mpotevu.

Na wale tuliozoea kuishi nao Misri na katika banda la nguruwe watachukizwa na pengine watatusema vibaya. Tusiogope kwani furaha tutakayoipata ni kubwa na ya maana zaidi kuliko kuendelea kubaki misri na kuishi ndani ya banda la nguruwe, yaani kubaki katika dhambi kwani madhara yake ni mabaya zaidi. Tukumbuke kuwa dhambi ikiingia moyoni hamuachi mtu salama mpaka atakapoamua kutubu na kuungama. Madhara ya dhambi ni makubwa mno. Kila dhambi inaadhiri akili, inadhoofisha utashi. Dhambi inaua dhamiri na kupoteza dira ya mdhambi. Dhambi inampumbaza mtu, inampa mtu mawazo na kumwambia nafasi hii ya dhambi ni ya leo tu, usiogope, hakuna shida. Kila unapotenda dhambi unapunguza uwezo wa dhamiri kugonga/kuuma/kukusuta. Hisia zinavurugika na hivyo kupoteza mizani ya maadili. Mdhambi anakuwa na chuki kwa Mungu kimoyomoyo pia anapoteza imani ya uwepo wa Mungu. Dhambi inadhuru afya kwani humfanya mtu kuwa na hasira na chuki ndani mwake hivyo yaweza kusababisha magonjwa mengine kama vile vidonda vya tumbo au ugonjwa wa moyo (BP) kwani dhambi iko moyoni ndani kabisa. Magonjwa haya ni matokeo ya hasira, chuki na uchu wa kulipiza kisasi vinavyopambani ndani moyoni. Hata magonjwa ya akili yanaweza kuchangiwa na dhambi hasa dhambi za mauaji.

Mwanzo wa maisha mapya katika mwanga wa Kristo Yesu
Mwanzo wa maisha mapya katika mwanga wa Kristo Yesu

Dhambi inaharibu lengo la jumuia/jamii ya wakristo wote katika safari ya kumfikia Mungu (Mt. 5:48) pia inaharibu mwili wa fumbo wa Kristo (1Wakor. 12:26). Dhambi inafanya roho ya mkosaji kukosa amani na zaidi sana Neema ya Utakaso. Mtu akikosa dhamani ya Mungu lengo na dhamani ya maisha yake inapotea na hivyo anaanza kuwayawaya na kuhangaika haoni cha maana na hivyo linalobaki kwake ni dhamiri iliyojaa mawazo maovu tu kwani upendo, amani, furaha, msamaha kwake ni mwiko. Kumbe ni vyema sasa tufanye maamuzi ya mwana mpotevu, tuamue kujinasua na dhambi. Tuweke nia ya kujikosoa kwa unyofu, kutojihusisha na dhambi na kutubu kweli.  Tuseme kwa dhati, imetosha, nitaondoka, nitakwenda kwa Baba na kumwambia nimekosa.  Dhambi hii naiacha!  Uamuzi wa kwanza ni juu ya tamaa yako na uamuzi wa pili ni kuijongea sakramenti ya kitubio. Kitubio kinatuzoeza kunyenyekea na kujikubali kuwa tu wanyonge mbele ya Mungu na kinatustahilisha kupokea Ekaristi, chakula cha kiroho kinachoimarisha imani na fadhila nyingine. Tuepukane na Komunyo za mashaka na kufuru kwani huko ni kuila hukumu yetu wenyewe. Tunapaswa kujibidisha siku zote na kusogelea mara nyingi Sakramenti hii, tukijua wazi kuwa kutofanya hivyo ni kukaribisha maanguko.

Kuungama mara nyingi kunatupa fadhila ya unyenyekevu - kujijua na kujikubali kuwa tu dhaifu (1Yn. 1:8-9). Tusikate tamaa tunapoungama mara nyingi.  Njia ya msalaba ni ndefu na yenye maanguko mengi: Kila dhambi ni mpya tuanze upya kwa kuungama dhambi zetu tukisema kwa ujasiri bila kuogopa; “Mimi ni mwenye dhambi” (Lk. 5:8). “Ole wangu kwa sababu, mimi ni mtu mwenye midomo michafu, nami nakaa kati ya watu wenye midomo michafu” (Isa. 6:5), kama Mtume Petro tusiogope kusema; “Ondoka kwangu ee Bwana kwa kuwa mimi ni mdhambi”, naye Yesu atakuambia; “Usiogope tokea sasa utakuwa unavua watu” (Lk. 5:10). Tumwombe Mungu atujalie neema tuguswe na huruma yake. Tuchukie dhambi na kuamua kuondoka na kurudi kwa Baba. Yeye ni mwenye huruma atatupokea na kutuandalia karamu ya Pasaka.

Dominika 4 Kwaresima 2022
23 March 2022, 15:37