Dominika ya Kwanza ya Kwaresima Mwaka C: Imani na Majaribu ya Yesu
Na Padre William Bahitwa, - Vatican.
UTANGULIZI: Dominika ya kwanza ya Kipindi cha Kwaresima. Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, tangu Jumatano iliyopita: Jumatano ya Majivu, tumeingia katika kipindi cha Kwaresima. Tumeianza safari ya siku 40 za mfungo na mageuzi ya kiroho ili kujiandaa kwa maadhimisho ya Pasaka, yaan maadhimisho ya mafumbo makuu ya wokovu wetu. Masomo ya dominika tutakayokuwa tunayasoma katika kipindi hiki chote, yatakuwa yanatupatia sura mbili: sura ya kwanza itakuwa ni ile ya kuipitia historia ya ukombozi katika Agano la Kale. Tutayaona, kwa hatua mbalimbali, baadhi ya matuko makubwa ya historia hiyo ambayo Waisraeli waliyapitia na kuchota maana yake katika maisha yetu ya sasa. Sura ya pili itakuwa ni ile ya kupitia upya hatua mbalimbali za safari ambayo Bwana wetu Yesu Kristo aliifanya kuelekea Kalvari alipotoa sadaka ile kuu Msalabani.
MASOMO KWA UFUPI: Masomo ya dominika hii ya kwanza ya Kwaresima yanatupatia mambo mawili. La kwanza ni ungamo la imani katika Agano la Kale na la pili ni tukio la Yesu kujaribiwa na Ibilisi. Ndiyo kusema, tunaanza kuiangalia historia ya wokovu kupitia ungamo la imani walilolifanya wayahudi na tunaanza kuipitia safari ya Yesu kuelekea Kalvari tukianzia na lile pambano lake la kwanza na la waziwazi na Ibilisi. Pambano ambalo Yesu alikuja kulishinda moja kwa moja pale Msalabani. Ni katika somo la kwanza tunapoliona ungamo la imani la Wayahudi. Tunasoma katika kitabu cha Kumbukumbu la Torati (Kum 26:4-10) kuwa kabla myahudi hajatoa sadaka yake ya mavuno mbele ya Bwana alipaswa kuirudia historia waliyoipitia babu zake tangu kuitwa kwa Abrahamu hadi kipindi cha utumwa Misri na kutaja namna Mungu alivyowatoa utumwani na kuwaingiza katika nchi yao ya ahadi, nchi ambayo inawapatia mazao wanayomrudishia Mungu kwa shukrani. Ni ungamo ambalo mtu alikuwa anageuka nyuma na kuangalia alikotoka. Na huko alikiri kuwa ni mkono wa Mungu uliokuwa unamuongoza.
Katika mwelekeo huo huo wa ungamo la imani, somo la pili ambalo ni Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi (Rum 10:8-13), linaleta ungamo la imani la mkristo. Ni ungamo la Agano Jipya. Ungamo hili anavyotuonesha Mtume Paulo limejengwa juu ya Kristo: “ukimkiri Kristo kwa kinywa chako na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua siku ya tatu utaokoka.” Wakati ambapo ungamo la imani ya kiyahudi lilijijenga katika kuangalia nyuma walikotoka, ungamo la kikristo linaangalia mbele, tunakokwenda. Na huko tunakokwenda ni wapi, ni kuuelekea wokovu. Maungamo haya mawili ya imani hayapingani bali yanakamilishana katika kuijenga imani kamili. Katika somo la Injili tunaona tukio la Yesu kujaribiwa. Tunasoma katika Injili ya Luka (Lk 4:1-13) kuwa baada tu ya ubatizo, Yesu anaongozwa na Roho kwenda nyikani. Anakaa huko siku 40, hali kitu, akijaribiwa na Ibilisi. Utangulizi huu peke yake una maana kubwa sana katika historia ya ukombozi ambayo Waisraeli waliipitia katika Agano la Kale. Waisraeli walipotoka Misri, kabla ya kuingia katika nchi ya ahadi walipita nyikani (jangwani) na huko walikaa kwa muda wa miaka 40.
Miaka hiyo 40 haikuwa rahisi. Ilijaa kila aina ya majaribu. Kutoka katika Maandiko Matakatifu tunaweza kutaja majaribu makuu mawili ambayo waisraeli walishindwa kustahimili wakaanguka: pale walipotengeneza ndama wa dhahabu (Kutoka 32) na ule uasi wa Masa na Meriba (Kutoka 17: 1-7, Hesabu 20:1-13). Sasa Yesu anapokwenda Nyikani na anakaa huko siku 40 na yeye akijaribiwa na Ibilisi, maana yake ni kuwa kwa maisha yake anaipitia upya historia waliyoipitia Waisraeli. Anapita katika nyayo zile zile walizopita na kuwaonesha kile ambacho walipaswa kufanya na hawakufanya, yaani kuyashinda majaribu. Kwa namna ya pekee zaidi Yesu anapita mulemule walimokosea na kuanguka ili kwa kutokuanguka kwake aweze kurekebisha makosa yale ambayo wao waliyafanya na kuacha mfano kuwa inawezekana kuyashinda majaribu.
Majaribu anayokumbana nayo Yesu ni matatu. Jaribu la kugeuza jiwe kuwa mkate ili ashibishe njaa yake, jaribu la kumsujudia Ibilisi ili apewe enzi na fahari yote na jaribu la kujitupa chini ya mnara ili kupima nguvu za Mungu za kuokoa. Majaribu haya matatu yanaendana na mapokeo ya kibiblia ya kuonyesha dhambi katika utatu. Dhambi ya Adamu na Eva katika kitabu cha Mwanzo inaelezwa katika ngazi tatu: “Mwanamke alipoona kuwa ule mti wafaa kwa chakula, wapendeza kwa macho nao ni mti wa kutamanika kwa maarifa basi alitwaa katika matunda yake akala...” (Mwanzo 3:6). Barua ya kwanza ya Yohane kwa watu wote nayo inatumia ngazi tatu kuelezea ukamilifu wa dhambi: “tamaa ya mwili, tamaa ya macho na kiburi cha uzima hakitokani na Baba bali vyatokana na dunia” (1Yoh 2:16). Kumbe, vishawishi hivi vitatu ambavyo Yesu anavishinda huko nyikani ni kitovu cha vishawishi au makundi matatu yanayomaanisha vishawishi vyote ambavyo mwanadamu anaweza kukumbana navyo.
TAFAKARI: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, baada ya kuyasikiliza masomo ya dominika hii ya kwanza ya Kipindi cha Kwaresima na baada ya kusikiliza ufafanuzi wake, tunaweza kuchota nini cha kuondoka nacho: nini kutusaidia kukiishi vema kipindi hiki cha mfungo wa Kwaresima, kipindi cha mageuzi ya kiroho na kiimani? Ninawaalika tuyatafakari majaribu yetu katika mwanga wa majaribu ya Yesu. Kati ya maswali yanayotuhangaisha ni yale kuhusu majaribu katika maisha yetu: kwa nini vishawishi? Kwa nini majaribu? Kwanza yanatoka wapi? Kwa nini Mungu asiyazuie yote tuishi bila majaribu? Biblia yenyewe inatuambia “mtu ajaribiwapo, asiseme ‘ninajaribiwa na Mungu,’ maana Mungu hawezi kujaribiwa na maovu wala mwenyewe hamjaribu mtu. Lakini kila mmoja hujaribiwa na tamaa yake mwenyewe huku akivutwa na kudanganywa.” (Yakobo 1:13-14). Tukiyaangalia majaribu matatu ya leo ya Yesu tunauona waziwazi ukweli wa mafundisho haya ya Biblia.
Jaribio la kwanza la Yesu ageuze jiwe liwe mkate ale ashibishe njaa yake ni jaribio linalotukumba na sisi pale tunaposhawishika kuukataa uhalisia wa maisha yetu na kuamua kuishi katika ndoto za urahisi wa maisha, za kutafuta njia za mkato au kama tunavyoweza kusema kuishi kwa kukikimbia kivuli chetu wenyewe. Jiwe ni jiwe na litabaki kuwa jiwe na mkate ni mkate. Nje ya hapo ni udanganyifu wa Ibilisi. Katika jaribu la pili, Ibilisi anaendelea kuahidi hadi leo “nitakupa wewe enzi hii yote na fahari yote wewe ukisujudu mbele yangu...” kwa asili yake, Ibilisi hatoi vile vitu anavyoahidi. Hufanya kinyume. Huvichukua kutoka kwako. Anakuahidi ufahari lakini mwisho ni wewe unayempa fahari ya maisha yako, anakuahidi mali lakini mwisho ni wewe unayempa mali zako, anakuahidi uhuru na amani lakini mwisho ni wewe unayempa uhuru wako na amani yako na unaishia kuwa mtumwa, anakuahidi maisha lakini utaishia kumpa yeye maisha yako. Katika jaribu la tatu, Ibilisi huingiza mashaka katika maisha yetu. Hutujaza hofu na kuanza kuwa na wasiwasi wa mambo hata ambayo hayapo.
Sehemu anayoanzia daima ni katika imani. Mtu ambaye ameishika imani yake kwa muda mrefu, mtu ambaye amekuwa mcha Mungu na hajawahi kutetereka anaanza kuipa nafasi hofu na wasiwasi kuhusu manufaaa ya imani yake kwa Mungu na kama Mungu kweli ni wa msaada katika maisha yake ya sasa na yajayo. Mtakatifu Padre Pio alizoea kufundisha akisema: ndani ya Kristo hakuna nafasi ya kuwa ya kuwa na hofu na wasiwasi kuhusu maisha yetu kwa maana yale tuliyoyafanya huko nyuma yako mikononi mwa Huruma yake, yale ya sasa tunayaweka ndani ya Neema yake na yale yajayo tunayakabidhi katika Majaliwa yake. Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, tangu dhambi ya wazazi wetu wa kwanza Adamu na Eva, ubinadamu wetu umekuwa na maelekeo ya dhambi yaani umekuwa dhaifu mbele ya mapambano dhidi ya Ibilisi. Yesu anapoyashinda majaribu yake leo anatuonesha kuwa sisi wenyewe kwa nguvu zetu hatuwezi kustahimili mapambano haya. Anatualika kumbe tuishi tumeungana naye, yeye aliyeyashinda majaribu ili kwa muungano wetu naye tuweze na sisi kuyasinda majaribu yetu. Tena tuishi kipindi hiki cha majaribu kama safari tunayopenda kuifanya pamaoja na Yesu kuelekea Msalabani ili pamoja naye tuweze na sisi kuishinda vita yetu na vishawishi na majaribu yanayotusonga.