Dominika ya Kwanza ya Kwaresima Mwaka C: Majaribu ya Yesu Jangwani
Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.
Amani na Salama! Katika kila mzunguko wa mwaka wa Kanisa, somo la Injili la Dominika ya kwanza ya Kwaresima Mwaka C. Lk 4:1-13 linatualika kutafakari juu ya majaribu ya Yesu jangwani. Kwaresima ni kipindi cha neema (Kairos), ni kusafiri jangwani ila daima pamoja na Yesu Kristo mwenyewe na kamwe tusijaribu bila Yeye, hivyo tuongozwe nasi na Roho wake Mtakatifu katika safari hii ya siku arobaini jangwani. Kwa nini jangwani? Jangwani ni mahali pa ukame, ni mahali pa kuwa na machache na ya msingi tu katika maisha. Ni mahali pa upweke na ukimya, ni mahali za kuzama katika sala na tafakuri ya kina, ni kujitenga na malimwengu ili kubaki sisi wenyewe na Mungu wetu kwa njia ya sala. Ni mahalia ambapo tunaweza kuwa huru kwa kutokujishikamanisha na malimwengu. Leo dunia yetu ina uwoga wa maisha ya jangwani, maisha ya ukimya na tafakuri ya kina, yaani maisha ya sala zenye kina. Yesu anatuonesha leo umuhimu kwetu wa kwenda jangwani pamoja naye ingali tunaongozwa na Roho wa Mungu. Majaribu au vishawishi alivyopitia Yesu vimewekwa kwa namna ya kutusaidia nasi ili tuweze kutambua maisha yetu hapa duniani, ni safari yenye majaribu na vishawishi vingi kutoka kwa yule mwovu, na hivyo hatuna budi kuvishinda kwa kumsikiliza na kuitii daima sauti ya Mungu, anayetualika kufanana naye katika utakatifu. Yesu Kristo kwa kushinda majaribu yale anabaki kuwa kielelezo chetu, na hivyo hatuna budi kujifunza kwake kwa kumuomba neema na nguvu ya kimungu katika safari ya maisha yetu hapa duniani.
Kwa juu juu tunaposoma Injili ya leo tunaweza kuona majaribu ya Yesu jangwani hayaakisi moja kwa moja uhalisia wa maisha yetu ya siku kwa siku, kwa maana majaribu yake na yetu ya kila siku ni tofauti. Nani kati yetu angeweza kumsujudia shetani? Nani kati yetu anauwezo wa kubadili jiwe kuwa mkate au kujirusha kutoka juu kwa hakika ya kupokelewa na malaika? Hivyo tunaona majaribu ya Yesu ni tofauti kabisa na yale tunayokumbana nayo katika maisha yetu ya kila siku. Majaribu yetu ni magumu zaidi na yanayodumu sio tu mara moja au kwa siku kadhaa bali siku zote katika safari ya maisha ya kila mmoja wetu. Kwa kweli ugumu wa kupata maana ya sehemu ya Injili ya leo unatokana na kutokujua haswa aina ya uandishi iliyotumika na mwinjili Luka. Sehemu ya Injili ya leo sio simulizi la kihistoria hivyo kulielewa jinsi lilivyo na badala yake ni sehemu ya katekesi ambayo mwinjili aliiandika kwa lengo la kuwafundisha jumuiya ya waamini baada ya mateso, kifo na ufufuko wake Bwana wetu Yesu Kristo. Ni katekesi inayotuonesha kuwa hata Yesu Kristo aliyejitwalia ubinadamu wetu, naye alijaribiwa na si tu mara tatu bali siku zote za maisha yake hapa duniani, na hata akiwa pale juu msalabani bado alipitia majaribu na vishawishi sawa na mimi na wewe. Labda kuna maswali mengi wakati fulani lakini jibu rahisi ni kwamba, kama mtu kweli alipata kila aina ya jaribu na kishawishi ila tu hakuanguka dhambini kama tunavyosoma kutoka Waraka wa Waebrania. (Waebrania 4:15).
Kurahisisha ili kuelewa sehemu ya Injili ya leo si kwamba Yesu alipitia majaribu hayo matatu tu, bali kija jaribu linasimama kama mfano wa majaribu mengi aliyopitia katika maisha yake yote. Hivyo hayo majaribu matatu ni kuwakilisha kila aina ya jaribu na kishawishi alichopitia katika maisha yake ya hapa duniani alipojitwalia ubinadamu na kuwa mtu kweli na kukaa katikati yetu. Kabla ya kuendelea na tafakari yetu naona ni vema pia tukaangalia na Wainjili wengine wa zile Injili ndugu wanavyotuonesha tukio la kujaribiwa kwake Yesu. Tofauti na Mwinjili Mathayo ambaye anaweka majaribu baada ya Yesu kufunga kwa siku zile 40 (Mathayo 4:2); Mwinjili Luka yeye anatuonesha kuwa majaribu yaliendelea sambamba na mfungo wake kule jangwani. Kujaribiwa jangwani na kwa siku zile 40 tunaona kuwa Mwinjili Luka ana lengo pia ya kuunganisha tukio la Yesu na yale ya Wanawaisraeli walipokuwa safarini jangwani kwa miaka 40, wakati wanatoka nchi ya utumwa na kwenda nchi ile ya ahadi yenye maziwa na asali. (Kumbukumbu la Torati 8:2) Tofauti na Wanawaisraeli tunaona baada ya siku zile 40, Yesu anatoka akiwa mshindi kwani alishinda majaribu na kila aina ya kishawishi cha yule mwovu. Na ndio mwaliko kwetu wa kuwa jangwani kwa siku hizi 40 za Kwaresma, lakini hatunabudi tumalize tukiwa washindi pamoja na Kristo Mfufuka.
Namba 40 katika Biblia ni namba kamilifu, ikimaanisha muda mrefu, na kamwe tusione kuwa siku 40 zinahesabiwa kama tunavyoweza kuhesabu siku leo kwa sekunde, dakika, saa, majuma, miezi na miaka, la hasha bali ni sawa na kusema muda mrefu au muda wote wa maisha ya mwanadamu. Hivyo kujaribiwa siku 40 ni lugha ya picha inayosema kuwa siku zote alijaribiwa. Hivyo hata nasi majaribu si tu kwa siku hizi 40 za mfungo wa Kwaresma bali ni maisha yetu yote ya hapa duniani. Hata Wanawaisraeli kusafiri kwa miaka 40 ieleweke kwa maana hiyo hiyo kuwa walichukua au kutumia miaka mingi sana, kwani namba katika Biblia daima ni lugha ya picha. Jaribu la kwanza; “Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu liambie jiwe hili liwe mkate.” (aya 3-4) Simulizi la majaribu jangwani linafuata baada ya tukio la Yesu kubatizwa katika mto Yordani. Tunaona Yesu hakuanza kazi yake kwa kuwakaripia wadhambi ili wafanye toba na kuongoka na badala yake anajiona kuwa mmoja wao na hivyo kuomba kubatizwa Ubatizo ule wa toba wa Yohana Mbatizaji. Yesu anakuwa kama mdhambi, anachagua njia ya kujitanabaisha kama mdhambi ijapokuwa hakuwa na dhambi, anatembea nao katika safari yao, anakuwa mmoja sawa, anajishusha na kujinyenyekeza. Huo ndio Upendo wa Mungu!
Kuchagua kuwa sawa nasi haikuwa jambo rahisi, ila ndio ajabu ya upendo wa Mungu kwetu sisi wanadamu tulio wadhambi. Mungu katika wema wake anakuwa sawa na sisi isipokuwa hakuwa na dhambi. Na kwa kweli jaribu au kishawishi cha kwanza kabisa ni kumtaka Yesu aachane kuwa mmoja wetu na badala yake aishi tu umungu wake, aachane na ubinadamu wetu, kufanana na mwanadamu ila atende na aishi kimungu tu. Ukiwa ni Mwana wa Mungu liambie…Mwanadamu anayetembea katika mahangahiko ya njaa, kiu, maradhi, uchovu na kutindikiwa kwa kila namna na kila aina ya mapungufu. Ni Ibilisi anamtaka Yesu aache kujitanabaisha nasi tulio wenye njaa, na kiu, na maradhi na kila aina ya kutindikiwa maishani na badala yake aishi kama Mungu aliye Bwana na tajiri wa kila kitu, na badala yake atende muujiza na ndio kusema atende kwa ajili yake tu, Mungu si mbinafsi kama yule Ibilisi na ndio maana anajitanabaisha sawa na sisi! Ni jaribu linalotuonjesha wema na upendo wa Mungu kwetu wanadamu tulio dhaifu na duni.
Yesu aliiona hila yake yule mwovu na hivyo daima alitumia uwezo wake wa Kimungu katika kutenda miujiza sio kwa ajili yake bali daima alitenda na anaitenda kwa ajili yetu sisi wanadamu. Mungu sio mbinafsi! Mungu ni upendo wazi kwa kila mwanadamu. Na ndio upendo wake unakamilika pale juu msalabani. Ni katika kufanya ishara ya msalaba nasi tunaalikwa kuachana na ubinafsi wetu. Tukumbuke kila tunapofanya ishara ya msalaba, tunaanza kwa kuandika ishara hiyo kwenye paji la uso na kushuka kifuani hapo tunaandika herufi ya (I) yaani mimi, lakini tena tunamalizia kuandika ishara hiyo kwa kwa kuifuta hiyo (I) kwa (__). Ni ishara ya kujikana mwenyewe! Ni ishara ya kuukataa ubinafsi wetu, we need to cancel or delete ourselves for the other just like what Jesus did there on the cross. “Ronald Knox talked about the sign of the cross this way: the first two gestures form the letter “I” and the next two cross it out. That’s what the cross of Jesus meant and means.” Hata alipokuwa pale juu msalabani kama nilivyotangulia kusema pia alijaribiwa afanye muujiza kwa ajili yake mwenyewe, ili ashuke pale Msalabani. Lakini daima Yesu kama nilivyoeleza hapo juu kamwe hafanyi na wala hakutenda muujiza wowote kwa ajili yake, bali daima kwa ajili yetu wanadamu.
Huu ndio Upendo wa kimungu ambao nasi tunaalikwa kufanana nao na kuuishi katika safari hii ya Kwaresima na maishani. Ni kujisahau sisi wenyewe kwa ajili ya wengine, na ndio maana tunaalikwa kufanya matendo ya huruma. Nabaki na njaa na kiu na kutindikiwa, ili mwingine aliye muhitaji zaidi yangu aweze kuneemeka kwa kushirikishwa fumbo la upendo wa kimungu. Tukumbuke nasi kuwa kila mara Ibilisi anatushawishi kuwa wabinafsi, kuishi kwa ajili yetu tu na kujifungia katika ubinafsi, kuwaza na kufikiri kwa ajili yangu tu. Mfungo wa Kwaresma ni kutusaidia ili kuepuka ubinafsi wetu, najikatalia chakula au kinywaji au kitu fulani ili mwingine aneemeke. Kamwe haina maana kuacha kula huku tulichojinyima tunabaki nacho, huko ni kushinda na njaa tu. Nabaki na njaa au kiu au najikatalia kitu fulani ili mwingine apate chakula au kinywaji au msaada fulani kutoka kwangu. Hivyo jaribu hili la kwanza ni kutoa muhtasari wa jinsi na namna gani yatupasa tuenende mintarafu ulimwengu wa mali na vitu. Ni mwaliko wa kuishi maisha ya upendo na kutofungwa na kuanza kuabudu mali na vitu. Na ndio Yesu anatukumbusha kuwa mtu hataishi kwa mkate peke yake. (Kumbukumbu la Torati 8:3)
Jaribu la pili; “Akampandisha juu, akamwonesha milki zote za ulimwengu kwa dakika moja…Nitakupa wewe mali hii yote…Basi wewe ukisujudu mbele yangu yote yatakuwa yako”. (aya 5-8). Inaonekana kuwa imeongezwa chumvi mno hasa jinsi anavyojitapa Ibilisi! Tukiangalia vyema tunaona mantiki ya dunia hii inakinzana sana na heri zile za mlimani/tambarare (Mathayo 5-8; Luka 6:20-26) na badala yake inatawala ile ya yule mwovu. (Yohane 12:31; 14:30; 16:11). Wakati jaribu la kwanza ni angalisho na fundisho jinsi ya kuendana na mali na vitu vya ulimwengu huu bali hili la pili ni jinsi ya kuenenda katika mahusiano yetu na wengine. Uchaguzi ni kati ya kutawala au kutumikia. Kishawishi cha kutawala wengine kipo ndani mwetu kiasi kwamba hata aliye mnyonge bado anasaka aliyemnyonge zaidi yake ili awe chini yake. Tamaa na kiu ya kutawala wengine, kiu ya ukubwa na kuwa mabwana wakubwa ni kishawishi kikubwa katika maisha yetu ya siku kwa siku, hata katika maisha ndani ya Kanisa daima tunaona kishawishi cha kugombea madaraka na ukubwa. Kila mmoja kutaka kuwa wa maana na muhimu kuliko wengine.
Si jambo geni hata ndani ya Kanisa kusikia watu wakipambania madaraka na utawala, mimi ni wa maana zaidi kwani ni Paroko, au Askofu, au Askofu Mkuu au Kardinali au Baba Mtakatifu, au Mkuu wa Shirika, au Mwenyekiti wa Jumuiya au Parokia na mifano mingi kama hiyo. Uongozi ni karama na zawadi kutoka kwa Mungu kwa ajili ya jumuiya ili kuwezesha kila mmoja kuwa na furaha ya kweli. Ni kwa ajili ya utumishi na si kutumikiwa kama mantiki ya ulimwengu huu. Mmoja ni kiongozi anaalikwa kuongoza kwa manufaa mapana ya jumuiya na kamwe si kutawala wengine kwa ajili ya sifa na masilahi binafsi. Yesu angeweza kuwa kiongozi iwe wa kidini na hata kisiasa, lakini hakufanya hilo. Na ndio jaribu la Ibilisi la kutaka kumfanya Yesu awe mtawala kwa wengine. Yesu anachagua kuwa mtumishi wetu wa daima! Ni mwaliko kwetu daima hatuna budi kuwa watumishi wa wengine na kamwe tusiingiwe na roho na mantiki ya kidunia ya kutaka kutawala wengine. Kamwe tusiwe watawala na badala yake tuwe viongozi katika kutumikia wengine na hasa kuwaonesha mapenzi ya Mungu hapa duniani.
Jaribu la tatu hakika ni la hatari zaidi kwani sasa linagusa mahusiano yetu na Mungu. “Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, jitupe chini; kwa maana imeandikwa, atakuagizia malaika zake wakulinde…” (Aya 9-12) Unaona mara nyingi Ibilisi pia ananukuu Maandiko Matakatifu ili kuweza kumghiribu mwanadamu na hata anatumia nukuu za Maandiko kwa malengo yake maovu, hivyo hatuna budi kuwa makini. Lengo kuu la Ibilisi sio tu kutufanya tuanguke dhambini bali hasa kuvunja mahusiano yetu na Mungu. Kutuweka mbali na Mungu, mbali na upendo na huruma ya Mungu, ili tukose IMANI na MATUMAINI kwa Mungu wetu. Ni kutufanya tuwe na mashaka na Mungu. Ni kwa kuwa na mashaka basi kuingia katika kishawishi cha kumjaribu Mungu. Wakiwa jangwani Wanawaisraeli walipokuwa na njaa, kiu, uchovu wakaingia katika kishawishi hiki na kuanza kupiga kelele kuhoji kama kweli Mungu yupo pamoja nao au la. (Kutoka 17:7) Na hata kumtaka kama kweli Mungu yu pamoja nao basi afanye ishara au muujiza. Yesu kamwe hakuingia katika jaribu au kishawishi hicho kwa Mungu Baba yake na yetu. Hata katika nyakati ngumu hajawahi kuomba ishara au muujiza hata akiwa pale juu msalabani bado hakupoteza imani na matumaini yake kwa Mungu Baba. Ni mara ngapi wapendwa tunapitia magumu katika maisha na kuanza kuhoji kama Mungu yupo nasi au la?! Na hata wakati mwingine kuhoji uwepo wake, ndizo nyakati tunaanza hata kuwa na mashaka ya uwepo wake!
Kwaresima ni kipindi cha neema (Kairos), kwani tunaalikwa nasi kutafakari magumu na mateso mengi katika maisha ambayo tunapitia au tutapitia, ni tafakari ya kuona maana katika mateso na shida kwani Mungu daima yupo nasi hata kama anaruhusu kupitia magumu hayo kama alivyoruhusu kwa Mwanae wa pekee. Fumbo la mateso ulimwenguni! Mungu ni mwaminifu kwani anatujalia neema na nguvu za kimungu ili nasi tubaki waaminifu kwake hata kama tunapitia magumu ya maisha kama kutindikiwa, maradhi na magonjwa ya kila aina, au aina mbali mbali za mateso. Na ndio tunakumbushwa kusali daima kwani ni kwa msaada wa neema zake pekee nasi tunaweza kuyashinda magumu na majaribu katika maisha yetu. Mwinjili Luka anamalizia kwa kusema; “Basi alipomaliza kila jaribu, Ibilisi akamwacha kwa muda akaenda zake kwa muda” (aya 13). Hivyo tunaweza kuona kuwa Mwinjili Luka pamoja na kuonesha hayo majaribu matatu bado anakazia kuwa Yesu alipata kila aina ya jaribu. Hivyo haya majaribu matatu ni ufupisho wa majaribu yote kwani daima yanagusa maeneo matatu yaani, vitu, watu na Mungu. Mwinjili Luka anaonesha waziwazi kuwa Ibilisi alibaki kumjaribu hata pale juu msalabani, ndio kusema siku zote za maisha yake Ibilisi bado alibaki kumjaribu Yesu mintarafu vitu, watu na Mungu Baba yake. Nawatakieni nyote tafakari njema na mfungo mwema wa Kwaresma unazingatia kufanana zaidi na Mungu kwa Kufunga, Kusali na Kutenda matendo ya huruma:kiroho na kimwili.