Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika ya Kwanza ya Kipindi cha Kwaresima Vishawishi na Majaribu katika maisha ya mwanadamu. Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika ya Kwanza ya Kipindi cha Kwaresima Vishawishi na Majaribu katika maisha ya mwanadamu. 

Dominika ya Kwanza ya Kwaresima Mwaka C: Vishawishi Na Majaribu

Ni kipindi cha siku arobaini za kufunga, kusali, kulitafakari Neno la Mungu na kufanya matendo ya huruma. Ni kipindi cha kukuza fadhila mbalimbali: haki, kiasi, huruma na kujiimarisha zaidi kiimani na kujenga umoja na Mungu wetu katika kuwatumikia wengine ili kumwilisha utamaduni wa upendo. Ni kipindi cha kufa kuhusu dhambi na kuzaliwa upya katika maisha ya kiroho.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya kwanza ya kwaresima mwaka C wa kiliturujia katika Kanisa. Ni kipindi cha siku arobaini za kufunga, kusali, kulitafakari Neno la Mungu na kufanya matendo ya huruma. Ni kipindi cha kukuza fadhila mbalimbali: haki, kiasi, huruma na kujiimarisha zaidi kiimani na kujenga muunganiko na Mungu wetu mtakatifu katika kuwatumikia wengine ili kumwilisha ndani mwetu utamaduni wa upendo. Ni kipindi cha kufa kuhusu dhambi na kuzaliwa upya katika maisha ya kiroho. Kihistoria tangu zamani Kwaresima ni kipindi cha kuwaanda wakatukumeni kwa Sakramenti ya Ubatizo na kuwasaidia ili waache maisha ya kale ya kipagani, maisha ya dhambi, na kuanza maisha mapya ya kiroho na kuwarudisha waliobatizwa waliojitenga na jumuiya ya waamini kwa sababu ya dhambi. Kipindi hiki Kanisa linatualika kufanya toba na wongofu wa ndani “metanoia” mabadiliko na wongofu wa kina katika maisha ili kustahilishwa kuadhimisha Fumbo la Ukombozi wetu – mateso, kifo na ufufuko wa Yesu Kristo – siku ya Pasaka.

Somo la kwanza la Kitabu cha Kumbukumbu la Torati (Kumb. 26:4-10); ni maelekezo ya Musa kwa Waisraeli namna walivyopaswa kumtolea Mungu sadaka ya shukrani baada ya kuingia na kuikalia nchi ya ahadi ya Kaanani. Somo hili linatukumbusha mpango wa Mungu wa kumkomboa mwanadamu tangu kumwita na kumteua Ibrahimu kuwa baba wa mataifa yote mpaka walipotoka utumwani Misri na kuingia katika nchi ya Kaanani. Itakumbukwa kuwa Mungu alimpatia Ibrahimu ahadi mbili: ardhi ya Kaanani kuwa mali yake na uzao wake (Mwa 15:18-21) na mrithi wa uzao wake mwenyewe ndiye Isaka baba wa Essau na Yakobo (Mwa 17: 15). Yakobo alikuwa na watoto wa kiume 12, ndiyo makabila kumi na mawili ya Israeli. Kutokana na wivu, watoto wa Yakobo walimuuza ndugu yao Yosefu, mwana mpendwa wa baba yao, kwa wafanyabiashara waliokuwa wanaelekea Misri. Kwa mkono wa Mungu, Yosefu akawa kiongozi wa kukusanya chakula kama maandalizi ya kukabiliana na balaa la njaa lilodumu kwa miaka 7 kama ndoto ya Farao ilivyotafsiriwa na Yosefu. Wakati wa njaa kali ulipowadia, Yakobo na familia yake walifika Misri. Farao, kwa heshima ya Yosefu aliwapa ardhi ili wapate kuishi huko. Ni katika ardhi hii Yakobo alifariki katika uzee wake na kuzikwa huko.

Majaribu na vishawishi katika maisha ni mapambano endelevu
Majaribu na vishawishi katika maisha ni mapambano endelevu

Baada ya Farao asiyemjua Yosefu kuchukua madaraka na baada ya kifo cha Yosefu, Wamisri waliwageukia Waisraeli, wakawatesa na kuwageuza kuwa watumwa. Nao walipomlilia Mungu, aliwakomboa kwa mkono wa Musa na kuwaongoza kuelekea nchi ya Kaanani – nchi ya ahadi kwa kufanya miujiza mingi mbele ya Farao na watu wake na kuwapiga kwa mapigo saba, la mwisho likiwa ni kuwaua wazaliwa wa kwanza katika kila nyumba ya Mmisri, akiwamo mtoto wa kwanza wa Farao. Mungu aliwafungulia Waisraeli Bahari ya Shamu, njia kavu nao wakavuka, lakini majeshi ya Farao na magari yao akayateketeza kwa maji. Kwa sababu ya kukosa uaminifu kwa watu wa Israeli, iliwachukua miaka 40, wakitangatanga jangwani kabla ya kufika nchi ya ahadi – Kaanani. Baadae, kwa uwezo wa Mungu wakiongozwa na Joshua walipigana vita vingi na kuwashinda watu walioishi katika ardhi ya Kaanani, wakawafukuza na kuikalia ardhi yao. Hivi ndivyo Mungu alivyotimiza ahadi aliyomwapia Abrahamu: “Nitawapa uzao wako ardhi hii iwe yao” (Mwa 15:18).

Kabla ya kuingia katika nchi ya ahadi Mungu aliwapa maagizo matatu. Kila mzaliwa wa kwanza wa binadamu na wa wanyama ni mali Mungu (Kut 13:1, 11-14; 22:29; Hes 18:16) - watoto watatumikia hekaluni na wanyama watatolewe kama dhabihu hekaluni. Lakini mzaliwa wa kwanza wa punda atakombolewa kwa mwanakondoo na ambaye hakutaka kumkomboa alipaswa kumvunja shingo. Na pia mzaliwa wa kwanza wa wanadamu anaweza kukombolewa kwa kutoa sadaka ya mwanakondoo au njiwa 2 (Kut. 13:13). Mazao ya kwanza kutoka shambani ni mali ya Bwana (Kut 22:29-30). Ilikuwa ni katika ibada ya kutolea yale waliyoamriwa na Mungu, Waisraeli walirudia ahadi ya Imani kwa Mungu. Hili ndilo somo la kwanza katika dominika ya kwanza ya kwaresma, ambapo waisraeli walikiri upendo wa Mungu kwao na kumtolea dhabihu za shukrani. Somo hili linatukumbusha hali yetu ya utumwa na mateso yatokanayo na dhambi na kwamba ni Mungu tu ndiye awezaye kutukomboa kwa mkono wake kwa njia ya Yesu Kristo. Kristo ni njia, ukweli na uzima. Kwa ubatizo tulivuka bahari ya Shamu, tulivuka dimbwi la utumwa wa dhambi. Kristo kama Musa mpya anatuongoza salama kupita jangwa la dunia hii akitupeleka katika nchi ya ahadi - mbinguni. Kila mara hata sisi tunaasi njiani na kurudia maisha ya kale, utumwa wa dhambi. Kwaresma ni kipindi cha kujitafakari na kumrudia Mungu.

Somo la pili la waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi (Rum. 10:8-13); Linatueleza jinsi Mungu wakati wa Agano la Kale, alivyowafunulia watu mapenzi yake kwa njia ya torati. Lakini katika Agano Jipya, Mungu yu kati yetu katika Yesu Kristo aliyekufa na kufufuka. Hivyo amwaminiye Kristo ataokoka. Paulo anasisitiza kuwa kumkiri Yesu kwa kinywa ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni kuwa Mungu alimfufua katika wafu, ni njia sahihi ya kupata wokovu. “Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu. Kwa maana andiko lanena, Kila amwaminiye hatatahayarika”. Kumbe kipindi hiki cha Kwaresima tuweke matumaini yetu kwa Yesu Kristo, Bwana na mwokozi wa maisha yetu, tukijafanya toba ya kweli kwake aliyetukomboa kwa mateso, kifo na ufufuko wake. Injili katika Dominika ya kwanza ya Kwaresima daima inahusu majibu ya Yesu baada ya ubatizo wake na kujazwa Roho Mtakatifu (Lk. 4:1-13). Majaribu haya anayapata baada ya kufunga kwa muda wa siku arobaini usiku na mchana. Itakumbukwa kuwa namba 40 Kibiblia inamaanisha mda wa kutosha wa maandalizi ya tukio maalumu. Waisraeli walikaa jangwani miaka 40, Musa alikaa mlimani siku 40, gharika ilichukua siku 40 na waninawi walifunga siku 40.

Huko jangwani Yesu anafunga na kusali. Katika mazingira hayo ya upweke na kuona njaa, shetani anamjaribu kwa majaribu matatu. Jaribu la kwanza ni hitaji la kimwili – kufanya muujiza wa kubadili jiwe kuwa mkate. Jaribu la pili ni la tamaa ya mali na mamlaka – Ibilisi anaahidi kumpa Yesu enzi na fahari kama atamshujudia na kumuacha Mungu. Jaribu la tatu ni la kumjaribu Mungu, Ibilisi anamwambia Yesu aujaribu uaminifu wa Mungu kwa kujitupa chini ili amtumie Malaika wamuokoe. Shetani alitumia nukuu za Maandiko yanayothibitisha na kuidhinisha kila jaribu. Yesu pia ananukuu maandiko kumjibu shetani: “Mtu hataishi kwa mkate tu” (Kumb 8:3); “Usimjaribu Bwana Mungu wako” (Kumb 6:16); “Msujudie Bwana Mungu wako na umtumikie Yeye peke yake” (Kumb 6:13). Tujijengee utamaduni wa kulisoma, kulitafakari na kuliishi Neno la Mungu ndiyo silaha madhubuti ya kumuangamiza shetani nasi tutamshinda na kuingia kwa ushindi katika furaha ya milele.

Ni Kipindi cha Toba na Wongofu wa ndani
Ni Kipindi cha Toba na Wongofu wa ndani

Mama Kanisa anapotuwekea simulizi la majaribu ya Yesu mwanzoni mwa kipindi hiki cha Kwaresima ni kutuonyesha kuwa tunaingia katika mapambano dhidi ya mwovu, na mapambano haya yanaanzia ndani ya nafsi zetu, ndani kabisa mwa mioyo yetu. Tupambane na majaribu ya kutafuta mamlaka, kupenda vitu kuliko kumpenda Mungu. Tusitafute mamlaka, ufahari, na nguvu kwa kila namna hata kwa nguvu za giza na mauaji ya watu wasio na hatia. Injili inahitimisha majaribu ya Yesu ikisema; “Basi alipomaliza kila jaribu, ibilisi akamwacha, akaenda zake “kwa muda” (Lk 4:13). Hii inatuambia kuwa katika maisha yake yote, Yesu alijaribiwa na shetani muda wote. Hata sisi katika maisha yetu shetani daima ataendelea kutujaribu, anatuacha tu kwa mda. Tujitahidi kuvitambua vishawishi na tuwe tayari kukabiliana navyo.

Silaha za kupambana na vishawishi na majaribu katika maisha yetu ni kusali daima, yaani kutenga muda wa kuongea na Mungu, kushiriki Misa Takatifu na kupokea Sakramenti hasa Kitubio na Ekaristi, kufunga na kutenda matendo ya huruma. Yesu alikaa jangwani kwa siku 40 akifunga na kusali. Kutoka huko alijawa na nguvu ya kuvishinda vishawishi na majaribu. Ndivyo anavyosali Padre kwa niaba ya jamii ya waamini katika utangulizi wa Dominika hii ya kwanza ya Kwaresima akisema; Yeye alifunga chakula siku arobaini, akaonyesha ubora wa namna hiyo ya kufanya kitubio. Amewaepusha watu wote na hila za nyoka wa kale na kutufundisha kushinda chachu ya uovu. Nasi tunapoadhimisha fumbo la Pasaka kwa mioyo safi, utujalie hatimaye tuifikie Pasaka ya milele. Kumbe, sala, mafungo, Neno la Mungu na matendo ya huruma ni silaha nzito za kumwangamiza Ibilisi, Shetani. Basi tukeshe tukiomba na kufunga, ili tusije tukaingia katika majaribu (Lk 22:40) na tukiingia majaribu tuwe na nguvu ya kuyashinda.

Dominika 1 Kwaresima
03 March 2022, 07:53