Dominika ya Pili ya Kwaresima: Kashfa ya Msalaba na Uso wa Utukufu
Na Padre William Bahitwa, - Vatican.
Ni dominika ya pili ya Kipindi cha Kwaresima. Safari yetu ya siku 40 za mfungo na mageuzi ya kiroho inaingia katika juma la pili. Tafakari ya Neno la Mungu dominika hii inaongozwa na somo la Injili linalotupatia tukio la Yesu kugeuga sura. Yesu akiwa mlimani anasali pamoja na wanafunzi wake watatu Petro, Yohane na Yakobo, sura ya uso wake inageuka, mavazi yake yanakuwa meupe yakimetameta na sauti inasikika kutoka katika wingu: “huyu ni Mwanangu, mteule wangu, msikieni Yeye.” Masomo kwa ufupi: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News tukio la Yesu kugeuga sura linahusiana kwa ukaribu sana na Mateso, Kifo na Ufufuko wake. Ni tukio ambalo Yesu aliamua kuwaonesha wanafunzi wake hao watatu utukufu wake wa Kimungu kabla ya kuingia katika mateso yake. Mara nyingine tukio hili linaelezwa kuwa ni kama Yesu alikuwa anadokeza utukufu wa ufufuko wake kabla hata ya ufufuko wenyewe. Lengo la kufanya hivi ni nini? Lengo lilikuwa ni kuimarisha imani ya wanafunzi wake hao. Yesu anataka kuwaonesha kuwa haingii katika mateso yake kama mtu aliyeshindwa. Kukamatwa kwake na kufa Msalabani si kitu kinachomfikia kwa bahati mbaya. Sio kitu kinachokuja ghafla na kukatisha malengo ambayo bado alikuwa hajayatekeleza.
Wake sio mfano kama wa mpigania uhuru ambaye kwa bahati mbaya anajikuta mikononi mwa mamlaka inayomuweka kizuizini na kukatisha ndoto zake za kupigania uhuru. Yesu anaonesha kuwa anaingia katika mateso na kifo kwa sababu amechagua mwenyewe kutumia njia hiyo kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti na anaingia katika mateso hayo si kama mtu aliyeshindwa. Anaingia akiwa na uwezo na nguvu zake zote za kimungu na ni hizo ambazo anazidhihirisha kwao katika tukio lake la kugeuga sura mlimani. Tukirudi sasa kuliangalia somo lenyewe la Injili (Lk 9:28b-36) tunaona alama anazozitumia mwinjili Luka ili kufafanua fundisho hilo kubwa la imani. Tutaziangalia alama chache. Alama ya kwanza ni kuwa tukio hili linatokea mlimani Yesu alipokwenda kusali. Mahala palipoinuka humaanisha mahala palipo na ukaribu na Mungu. Mwinjili Luka anapenda kusisitiza kuwa kugeuka sura kwa Yesu ni kudhihirisha muunganiko wake na Mungu Baba. Muunganiko huu unachochewa pia na sala aliyokuwa akisali. Anageuka sura akiwa katika sala, akiwa katika mazungumzo na Mungu yaani akiwa katika muunganiko na Mungu Baba. Huu ni ufunuo anaoudhihirisha Yesu kwa wanafunzi wake. Kwa mara nyingine anawaonesha kuwa Yeye na Baba ni kitu kimoja.
Alama ya pili ni kutokea kwa Musa na Eliya. Hawa ni manabii wakubwa wa Agano la Kale ambao tunaweza kusema kuwa waliwakilisha pia unabii wote wa Agano la Kale. Wakati Injili nyingine zikitaja uwepo wa Musa na Eliya katika tukio la kugeuka sura Yesu, mwinjili Luka ndiye anayeeleza ni nini walikuwa wakiongea. Anasema walikuwa wakizungumza naye habari za kufa kwake. Ni hapa tunapopata msingi mwingine wa kiri yetu ya imani kuwa Yesu aliteswa, alikufa na alifufuka kadiri ya Maandiko. Musa na Eliya wanakuja kuthibitisha kuwa tangu enzi zao walikwisha andika habari za kifo cha Yesu. Kwamba ni Yeye ambaye kwa kifo chake ataleta ukombozi kwa ulimwengu. Kumbe Musa na Eliya wanakuja kama mashahidi wa unabii wa Maandiko kuhusu kile ambacho baada ya muda si mrefu kingemtokea Yesu.
Alama ya tatu na ya mwisho tunayopenda kuiangalia kwa leo ni lile ombi la Petro “Bwana mkubwa, ni vizuri sisi kuwepo hapa, na tufanye vibanda vitatu; kimoja chako wewe na kimoja cha Musa na kimoja cha Eliya.” Vibanda alivyoomba Petro viliweza kumaanisha tabernakulo ya wayahudi, yaani mahala walipoenda kukutana na Mungu na viliweza kumaanisha hema la kuishi, kama walivyokuwa wakiishi waisraeli huko jangwani katika safari yao kuelekea nchi ya ahadi. Katika namna zote mbili Petro aliomba waweke makazi huko. Huenda ni kwa kuvutiwa kwake na utukufu waliouona. Ombi hili halisikilizwi. Yesu inabidi ashuke toka mlimani aende kuyakabili mateso na kifo chake ili aurudie utukufu ule usio na mwisho baada ya ufufuko. Ni hapa tunaweza kusema “hakuna Pasaka bila Ijumaa Kuu”. Petro alipenda abaki katika utukufu huo bila kupitia njia ya msalaba. Yesu anamuonesha na kutuonesha sote kuwa utukufu huo aliowadokeza kwa kugeuka sura ni utukufu ambao njia yake ni njia ya Msalaba. Katika somo la Pili, kutoka Waraka wa Mtume Paulo kwa Wafilipi (Fil 3:17-4:1), Paulo anatafsiri kugeuka sura kwa Yesu kama utimilifu wa wokovu ambao sisi sote wakristo tunausubiri. Anasema “tunamtazamia Mwokozi, Bwana Yesu Kristo atakayeugeuza mwili wetu wa unyonge, upate kufanana na mwili wake wa utukufu.”
TAFAKARI: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, tunafahamu kuwa katika kipindi hiki cha Kwaresima tunafunga na kujinyima kama alama ya nje ya nje ya kuonesha kuomba toba. Mfungo unatusaidia pia kukua katika fadhila kwa kuimarisha utashi wetu wa ndani, kwa kukomesha vilema vyetu na kulegeza mioyo yetu ili iguswe na mahangaiko na tabu ambazo jirani yetu anazipitia. Injili ya dominika hii ya pili ya Kwaresima, Injili ya kugeuka sura kwa Yesu, kama tulivyoisoma na kuifafanua, inatupatia mantiki nyingine ya kwa nini tufunge; kwa nini tujitese na kujikatalia mambo mengi hasa katika kipindi hiki cha Kwaresima. Mantiki ya kwanza ni ule utukufu ambao tumeitiwa. Yesu anapogeuka sura na kuonesha utukufu wake wa kimungu, anaonesha pia utukufu ambao sisi sote wana wa Mungu tumeitiwa. Ni kama anatuambia “tazameni, huu ndio uso wa utukufu ambao kila mmoja wenu atavikwa na Mungu Baba. Huu ndio uso wa utukufu utakaokuwa wenu huko mbinguni.” Kisha Yeye mwenyewe anashuka kutoka mlimani na kwenda kuyakabili mateso yake na kifo chake Msalabani na siku ya tatu anafufuka na kuutwaa mwili wa utukufu. Ni namna hiyo anatuambia na sisi kuwa ili kuufikia uso huo wa utukufu tuwe tayari kama yeye kuyakabili maisha yetu.
Tuwe tayari kuyakabili mapambano yetu ya imani kwani ni kwa njia hiyo tunajitayarishia nafasi ya kuvikwa uso wa utukufu. Mfungo wetu wa Kwaresima na kujikatalia kwetu ni sehemu ya mazoezi ya kiroho yanayotuandaa katika kuyakabili mapambano ya maisha yetu na mapambano ya imani yetu. Sauti iliyotoka katika wingu wakati wa kugeuka sura Yesu ilituagiza tumsikie Yeye: ilisema “huyu ni mwanangu, mteule wangu, msikieni Yeye.” Ili kumsikia mtu anayeongea unahitajika ukimya. Watu wawili wanaoongea kwa wakati mmoja hawawezi kusikilizana. Inabidi mmoja anayamaze asikilize kwanza na pale mwingine atakaponyamaza basi na yeye anaweza kuongea akasikilizwa. Kumsikia Yesu anayeongea katika nafsi zetu kunahitaji ukimya wa ndani. Kuufikia ukimya huu sio kazi rahisi kwa sababu mtu anaweza kuwa amefumba mdomo, haongei, lakini ndani ya moyo wake kuna kelele na vurugu za kila aina. Mfungo na kujikatalia ni baadhi ya mazoezi ya kiroho yanayojenga utulivu wa ndani. Ni mazoezi ya kiroho yanayomsaidia mtu kujenga usikivu wa moyo na ni kwa namna hii mtu anaweza kuisikia sauti ya Kristo inayoongea daima ndani yetu kupitia dhamiri zetu njema. Mwisho ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, ninakutakia tafakari njema ya dominika hii. Kugeuka sura kwa Yesu kuchochee ndani yako kiu ya kutamani kuufikia utukufu ambao Kristo ametuahidia na kukuimarishe katika kuyaishi mazoezi ya kiroho ambayo kipindi hiki cha Kwaresima kinatupa nafasi ya kuyaishi.