Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya Pili ya Kipindi cha Kwaresima: Kung'ara sura kwa Kristo Yesu: Utukufu na ukuu wake, ili kuwaimarisha wafuasi wake kukabiliana kikamilifu na Kashfa ya Msalaba. Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya Pili ya Kipindi cha Kwaresima: Kung'ara sura kwa Kristo Yesu: Utukufu na ukuu wake, ili kuwaimarisha wafuasi wake kukabiliana kikamilifu na Kashfa ya Msalaba. 

Dominika ya Pili ya Kwaresima: Kristo Yesu Mwana wa Mungu!

Kung’ara sura kwa Kristo Yesu ni alama ya: Ukuu, utakatifu, uzuri, furaha na chemchemi ya maisha mapya yanayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu. Hii ni siri ambayo walitakiwa kuizamisha katika sakafu ya mioyo yao mpaka baada ya mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu, tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu inayosimikwa katika Fumbo la Pasaka ya Kristo Yesu!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya pili ya kipindi cha Kwaresima mwaka C wa Kanisa, siku ya kumi na mbili ya kipindi cha majiundo ya kiroho. Masomo ya Dominika hii yanatuongoza kumtambua Yesu Kristo kuwa ni mwana wa Mungu kwa tukio la kugeuka sura mlimani Tabor. Somo la kwanza la kitabu cha Mwanzo (Mwa 15:5-12,17-18); linahusu Agano kati ya Mungu na Abrahamu baba wa imani. Alama na ishara ya agano hili ni moto uliopita juu ya nyama alizoziandaa Abrahamu. Moto huu ni alama wazi ya uwepo wa Mungu. Katika somo hili tunaiona imani ya Ibarahimu kwa Mungu jinsi alivyoweka matumaini yake yote kwake tangu siku alipoitwa na kuitika, hata katika majaribu alibaki mwaminifu kwa Mungu. Ili kulielewa vizuri somo hili ni vyema kujikumbusha habari za kuitwa na kuitika kwa Abrahamu tunazozisoma katika kitabu cha mwanzo sura ya 12. Mungu alimwita Abrahamu, akiwa na miaka 75, mtu tajiri wa mifugo mingi na mkuu wa ukoo. Abrahamu anaitwa kuacha nchi yake, mali na jamaa zake aende mpaka nchi asiyoifahamu. Abrahamu kwa Imani alitii sauti ya Mungu “akaenda kama Bwana alivyomwamuru” (Mwa 12:4). Abrahamu akafika Kaanani, nchi na ardhi aliyoahidiwa na Mungu kuwa mali yake yeye na uzao wake (Mwa 15:18), uzao utakaotoka katika viuno vyake (Mwa 15:4), licha ya uzee wake na utasa/ugumba wa mkewe Sarah.

Ili kumthibitishia Abrahamu ahadi hizi, Mungu alifunga Agano na kula kiapo kama ilivyokuwa desturi ya watu wa wakati huo. Walichinja mnyama/mmoja au zaidi na kumpasua katika vipande viwili na kuviweka kwa kutazamana. Katikati ya vipande hivi viwili waliacha njia ya kupita kwa wadau wa agano wakati wa kula kiapo, ishara kwamba, yeyote atakayefanya kinyume na kiapo hicho adhabu yake ni kifo. Hiki ndicho kinchosimuliwa katika somo la kwanza katika dominika ya pili ya Kwaresima mwaka C, ambapo Abrahamu aliwachinja wanyama - mwana ndama wa miaka 3, mbuzi mke wa miaka 3 na kondoo mume wa miaka 3, akawapasua katika vipande viwili viwili na kuvipanga kuelekeana kama ilivyokuwa desturi. “Ikawa, jua lilipokuchwa likawa giza, tazama, tanuru ya moshi na mwenge unaowaka ulipita kati ya vile vipande vya nyama. Siku ile Bwana akafanya agano na Abramu, akasema, Uzao wako nimewapa nchi hii, kutoka mto wa Misri mpaka huo mto mkubwa, mto Efrati”. Mungu kwa upendo na huruma yake anajishusha na kufanya Agano lake na Abrahamu, kuwa Baba wa imani ambaye kutoka kwake taifa teule la Israeli linazaliwa kwa maandalizi ya kumpokea Mwokozi wetu Yesu Kristo. Hivyo kutoka katika viuno vya Abrahamu, alizaliwa Isaka - Ahadi ya Mungu (Mw. 21:1-6). Kutoka viuno vya Isaka walizaliwa - Essau na Yakobo (Mw. 25:26-27). Na kutoka viuno vya Yakobo, walizaliwa watoto 12 wakiume ndiyo makabila 12 ya Israeli (Mw. 27:1-37:1). Hawa wote walikuwa ni wazao wa Abrahamu kadiri ya mwili. Kutoka kwa ukoo wa uzao wa Abrahamu amezaliwa Yesu Kristo (Mt. 1:1-17), na kutokana na Yesu Kristo taifa takatifu na la milele - Kanisa - limezaliwa. Sisi sote ndilo taifa jipya la Mungu na kwa sababu hiyo tuna haki ya kumwita Abrahamu kuwa Baba yetu wa Imani.

Kristo Yesu aliwaandaa Mitume Kukabiliana na Kashfa ya Msalaba.
Kristo Yesu aliwaandaa Mitume Kukabiliana na Kashfa ya Msalaba.

Mtume Paulo katika somo la pili la Waraka wake kwa Wafilipi (Filp 317-4:1); anawaonya Wafilipi wajihadhari na wale wanaotaka kuwashurutisha washike torati ya Wayahudi ili wawe wakristo, wafuate mfano wake aliyeweka tumaini lake kwa Mwokozi wetu Yesu Kristo; atakayeubadili mwili wetu wa unyonge, upate kufanana na mwili wake wa utukufu, kwa uweza ule ambao kwa huo aweza hata kuvitiisha vitu vyote viwe chini yake. Injili ilivyoandikwa na Luka (Lk 9:28-36); inatupa simulizi la kugeuka sura Bwana wetu Yesu Kristo mlimani Tabor. Injili Pacha zote zinasimulia tukio hili (Mathayo 17:1-9, Marko 9:2-11 na Luka Lk 9:28-36). Hii ni kuonyesha umuhimu wa tukio hili katika historia ya maisha ya Kristo. Katika kusimulia kuna mambo ya muhimu yanayojitokeza. Tukio limetokewa wakati Yesu ameenda kusali pamoja na wanafunzi wake watatu - Petro, Yohane na Yakobo - katika kusali kwake sura ya uso wake ikageuka, na mavazi yake yakawa meupe, yakimeta-meta. Katika tukio hili Musa na Elia walitokea wakiwa katika utukufu wakanena naye habari za kifo chake na baadae wanatoweka. Sauti ikatoka katika wingu ikisema “huyu ni mwanangu, mteule wangu, msikieni yeye.” Kwanini Yesu aliwachukua wanafunzi watatu tu na sio wote? Kwanini aligeuka sura mbele yao? Uwepo wa Musa na Eliya na baadae kutoweka maana yake ni nini?

Itakumbukwa kuwa tukio la Yesu kugeuka sura lilitokea baada ya Petro kukiri kuwa Yesu ni “Mwana wa Mungu na Masiha,” na baada ya utabiri wa Yesu kuwa imempasa mwana wa Adamu, kupata mateso mengi na kukataliwa na wakuu wa makuhani na wazee na waandishi na kuuawa (kifo cha msalaba). Utabiri huu ulikuwa kikwazo cha mitume kumfuata Yesu hata kukatokea majibizano kati ya Petro na Yesu. Petro alisema haiwezekani mambo haya kutokea na Yesu akamkemea na kumwambia; “Rudi nyuma yangu shetani wewe maana unawaza ya binadamu sio ya Mungu” (Mt. 16:22). Katika hali hii Mababa wa Kanisa wanatufundisha kuwa Yesu aliwachukua wanafunzi hawa watatu - Petro, Yohane na Yakobo akawawaimarishe kwa kuwaonesha utukufu atakaoupata baada ya mateso na kifo chake ili nao wakati wa majaribu wasitetereke bali wawaimarishe mitume wenzao wasipoteze imani, matumaini na mapendo kwa mwalimu wao. Imani kwa Petro, Papa wa kwanza ili aweze kushuhudia umungu wa Kristo bila mashaka kama anavyoshuhudia mwenyewe; “Hatukufuata hadithi zilizotungwa kwa werevu wa watu tulipowajulisha ninyi nguvu zake Bwana wetu Yesu Kristo, bali tuliona wenyewe ukuu wake (2Pt.1:16ff).

Matumaini kwa Yakobo Mtume wa kwanza kuteswa na kufa shahidi kwa ajili ya Kristo na Mapendo kwa Yohane aliyemkabidhiwa mama yetu Bikira Maria naye kukabidhiwa kwake. Idadi yao watatu ni ili kushuhudia kuwa tukio hilo ni la kweli ili na wengine waweze kuamini kwani kwa mila na desturi za wayahudi, ushahidi wowote wa jambo kubwa na zito ili uweze kukubalika ilibidi utolewe na wanaume wawili na kuendelea (ushahidi wa wanawake na watoto haukuwa halali). Kutokea kwa Musa na Eliya na kutoweka kwao ni ishara ya kuanza kutimia kwa yaliyoandikwa na kutabiriwa katika Agano la Kale. Musa akiwakilisha Torati/sheria, na Eliya akiwakilisha manabii. Torati na manabii kwa pamoja zinajenga msingi wa utabiri wa ujio wa masiha Yesu Kristo. Bila ufunuo huu wa torati na manabii katika Agano la Kale, Yesu angekuwa fumbo lisiloweza kufumbulika. Ndiyo maana baada ya ufufuko wake ili kuwafanya wanafunzi wa Emau waelewe maana ya: mateso, kifo na ufufuko wake aliwanulia maandiko kuanzia na Musa na manabii akiwaeleza mambo yaliyo mhusu yeye mwenyewe (Lk 24:27). Musa na Eliya kutoweka ni ishara kwamba wakati wa kuwasiliana na Mungu kwa njia yao umekwisha. Njia pekee ya kuwasiliana na Mungu ni mwanae wa pekee Bwana wetu Yesu Kristo.

Mashuhuda wa Fumbo la Pasaka: Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu.
Mashuhuda wa Fumbo la Pasaka: Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu.

Wingu jeupe kutokea juu ya mlima ni udhibitisho kuwa sauti iliyosema; “Huyu ni mwanangu mpendwa wangu msikieni yeye” ni sauti ya Mungu kwani katika Agano la Kale wingu lilimaanisha uwepo wa Mungu na mlima ni mahali patakatifu pa kukuta na Mungu. Maandiko matakatifu yanatuambia kuwa; “wema watang’aa kama jua katika ufalme wa Baba yao” (Mt 13:43), “Malaika alionekana kama umeme na vazi lake jeupe kama theluji” (Mt 28:43). Yesu kugeuka sura na kung’aa ni ishara wazi ya wema na utukufu wake aliouacha mbinguni akaja duniani. Kung’aa kwake kunatuonyesha jinsi atakavyokuwa baada mateso na kifo chake msalabani kwa ajili ya ukombozi wetu, utukufu atakaowashirikisha watakaomfuata kwa uaminifu hata ikibidi kuteseka na kutolea maisha yao kwa ajili yake. Utukufu huu ni wa mbinguni ambao Mitume walionja kwa kumwona Yesu akigeuka sura na kung’aa. Sisi tunauonja utukufu huu katika Sakramenti ya kitubio ambapo roho zetu zinang’arishwa na kwa Ekaristi Takatifu tunauonja utukufu wa mbinguni kama anavyosali Padre katika sala baada ya komunyo kwa niaba ya jamii ya waamini akisema; “Ee Bwana, baada ya kupokea mafumbo yako matakatifu, tunataka kukushukuru kwa maana ingawa tuko bado hapa duniani watushirikisha ya mbinguni”.

Basi tufanye hima tugeuze mienendo ya maisha yetu kutoka katika hali ya dhambi kuingia katika hali ya neema ili tuwe na uhusiano mwema Mungu pamoja na ndugu zetu. Tunaalikwa kutoka katika hali yetu ya zamani na kuwa watu wapya. Kuifikia hali hii ya ukamilifu si kazi rahisi maana ni njia ya mateso inayohitaji uvumilivu maana kuachana na dhambi ni sawa na kuogelea kinyume na mawimbi ya maji. Ili tuufikie utukufu wa kipasaka tunapaswa kuuonja uchungu wa Ijumaa na kuuvumilia. Ndivyo tunavyosali katika utangulizi wa dominika hii tukisema; Yeye aliwaambia mapema wafuasi wake kwamba atauawa; na pale katika mlima mtakatifu aliwaonyesha utukufu wake, akaonyesha kwamba kama ilivyoandikwa katika Torati na Manabii, atapata utukufu wa ufufuko kwa kuteswa. Tumwombe Mungu atujalie fadhila ya uvumilivu katika kupambana na yule mwovu ili nasi tuweze kung’aa kwa matendo yetu nayo yavutie watu wengine waweze kusema “ni vizuri sisi kuwepo hapa.”

D 2 Kwaresima 2022
09 March 2022, 14:15