Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya Pili ya Kipindi cha Kwaresima: Wazo kuu ni Ufunuo wa Kristo Yesu kuwa ni Mwana wa Mungu na umuhimu wa sala katika maisha ili kupambana na majaribu. Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya Pili ya Kipindi cha Kwaresima: Wazo kuu ni Ufunuo wa Kristo Yesu kuwa ni Mwana wa Mungu na umuhimu wa sala katika maisha ili kupambana na majaribu. 

Dominika ya Pili ya Kwaresima: Ufunuo wa Umungu wa Yesu na Umuhimu Wa Sala

Mawazo makuu yanayojitokeza katika Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya Pili ya Kipindi cha Kwaresima ni ufunuo wa Kristo Yesu kuwa ni Mwana mpendwa wa Mungu. Jambo la pili ni umuhimu wa maisha ya sala ili kuzungumza na Mwenyezi Mungu katika faragha, na hatimaye kupata nguvu ya kuweza kupambana na changamoto katika sera na mikakati ya uinjilishaji wa kina.

Na Padre Efrem Msigala, OSA, - Roma.

Katika Dominika hii ya Pili ya Kipindi cha Kwaresima Mwaka C wa Kanisa, wazo kuu tunalo pata katika masomo yetu hasa ni sala. Katika sala kuna kutenga muda wa kusali na kuacha mengine yote. Hivyo tuna kuwa mahali pa upweke na utulivu ili kuongea vema na Mungu. Masomo yanatupa mwono mpana wa sala na faida zake. Somo la Kwanza Mungu anaweka agano na Abramu, anamwahidia uzao mkubwa, akamtoa nje ahesabu nyota zote angani kama anaweza kuhesabu. Hiyo ni kudhihirisha jinsi uzao wake utakavyokuwa mkubwa. Ni jibu la ombi au sala ya Abramu ya kuomba apate uzao.  Zaburi inatupa mfano wa maombi au sala ya Mfalme Daudi katika uso wa hatari, ikisema: “Ee Bwana, uwepo wako nautafuta. Usinifiche uso wako…” Halafu Mtakatifu Paulo, katika Somo la Pili, anawahimiza Wafilipi kubaki imara katika imani kwa Yesu Kristo ambaye vitu vyote ni kwake. Anawakumbusha kwamba ingawa watu wengi wanakaza akili zao “katika mambo ya udongo… uraia wetu uko mbinguni.” Mawazo yetu ni kwa Mungu – pia tunahitaji sala. Hatimaye, katika Injili, Yesu anawaongoza wanafunzi wake watatu wa karibu kutoka katika pilika pilika za maisha, hadi kwenye kilele cha mlima, ambapo anakuwa katika upweke pamoja nao, na kuwapa somo la sala. Somo analifanya kwa vitendo. Katika mazingira ya utulivu na faragha, Yesu anasali ingawa wanafunzi wanalala, huko anageuka sura.

Tendo la kugeuka Sura linatukia kwenye mlima mbele ya wanafunzi wake watatu tu:Petro, Yakobo na Yohane. Hawa ni miongoni mwa wanafunzi wa kwanza ambao Yesu aliwaita. Ni Injili ya Luka pekee, ambayo mara nyingi humfafanua Yesu akiwa mlimani anasali, inayoonesha kwamba Yesu anasali huku sura yake ikibadilika na kuwa nyeupe na angavu. Luka anaonesha kwamba wanafunzi watatu walikuwa wamelala wakati Yesu anasali. Watakuwa wamelala tena Yesu anapoomba na kusali katika bustani ya Gethsemane kabla ya Mateso na kifo chake. Wanapoamka, Petro na wenzake wanamwona Yesu akigeuka sura na akiongea na Eliya na Musa wakiwa pamoja. Eliya na Musa, wote wawili watu mashuhuri katika historia ya Israeli, wanawakilisha Sheria na Manabii. Katika Injili za Mathayo ya sura 17 aya ya 3 na Marko sura ya 9 aya ya 4 kuna mazungumzo kati ya Yesu, Eliya, na Musa bila kutaja ni mazungumzo gani, kumbe, mwinjili Luka pekee anaeleza kwamba mazungumzo hayo yalihusu mambo ambayo Yesu alitimiza baadaye huko Yerusalemu. Walizungumzia juu ya kifo, na ufufuko wake Yesu.

Ufunuo wa Kristo Yesu Mwana wa Mungu aliye hai.
Ufunuo wa Kristo Yesu Mwana wa Mungu aliye hai.

Mpendwa msikilizaji mambo gani tunajifunza katika maisha yetu kutokana na masomo tuliyoyasikia? Hapa tunajifunza mambo kadhaa: Kwanza kabisa, sala ni mawasiliano yetu na Mungu. Tunazungumza na Mungu, naye anasikiliza. Mungu huzungumza nasi, nasi tunasikiliza. Tukiwa na mawasiliano haya tunakuwa karibu zaidi na Mungu, na tunahisi uwepo wake. Pili, Yesu aliwaalika mitume Petro, Yakobo na Yohane wapande pamoja naye mlimani. Alitaka wao binafsi wajionee uwepo wa Mungu katika sala na wawaimarishe wenzao baadaye. Ni Yesu ambaye anatualika kwenye sala. Tabia bora ya sala ni unyenyekevu na uwazi kwa Mungu. Sala kuu ni Misa Takatifu. Hivyo basi tunaonja namna hiyo ya unyenyekevu katika sala wakati wa Misa. Ni Yesu anayetualika. Kwenye Misa tunaanza na Ibada ya Toba, tunajinyenyekeza na kuomba msamaha kwa dhambi zetu. Hakuna nafasi ya majivuno bali ni unyenyekevu. Jambo la tatu, “Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu; msikilizeni Yeye.” Sauti ya Baba ni uthibitisho wa moja kwa moja wa Umungu wa Yesu: yeye ni Mwana wa Pekee wa Mungu. Kumwamini haimaanishi tu kukiri imani yetu, bali kufuata kila neno na amri yake: "Msikilizeni yeye", sauti ya Baba wa mbinguni ilisema.

Ikiwa tunaamini kweli kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu, tunapaswa kumfuata njia yote na bila kusita. Hili ndilo tatizo siku hizi. Watu wanajidai kuwa Wakristo. Lakini maisha yao hayapatani na mafundisho na mifano ya Yesu. Mbaya zaidi, badala ya kumfuata Yesu, wao hata wanatilia shaka mafundisho yake. Kila kitu wanaona si sawa. Pamoja na hayo mpendwa msikilizaji, Imani katika Yesu si suala la kukiri tu; inabidi ionekane na kuishi katika maisha yetu ya kila siku. Vinginevyo, tunatoa ushuhuda wa kupinga Injili. Hivi ndivyo Mtakatifu Paulo alifundisha waziwazi katika somo la pili akisema: “Kwa maana wengi hujifanya kuwa adui wa Msalaba wa Kristo”. Kipindi cha  Kwaresima ni mwito wa kugeuka sura yetu binafsi. Kinachotokea ni kwamba wengi wetu tumezama katika dhambi, na tumeacha kuhangaika kuinuka tena. Kipindi cha Kwaresima kinatupa neema tele za kuinuka tena, ili kutupilia mbali vazi chafu la dhambi, na kumfuata Yesu kwa azimio kubwa zaidi la kutotenda dhambi tena. Ni kipindi cha kupokea Sakramenti ya Upatanisho. Hatukukusudiwa kubaki wenye dhambi na wanyonge; tumekusudiwa kuishi maisha ya utukufu kama watoto wapendwa wa Mungu.

Umuhimu wa Sala katika maisha ya waamini
Umuhimu wa Sala katika maisha ya waamini

Mtakatifu Paulo anatukumbusha jambo hili katika somo la pili akisema: “Wenyeji wetu uko mbinguni. Yesu Kristo ataubadili mwili wetu wa hali ya chini ufanane na mwili wake wa utukufu kwa uweza unaomwezesha yeye pia kuvitiisha vitu vyote chini yake.” Basi, tusibaki katika dhambi, giza na fedheha; ni wakati wa kuishi kwa adabu kama watoto wa nuru, na wakati ndio sasa. Hebu tugeuzwe kweli - hebu tuoneshe mara moja na kwa wote sisi ni nani hasa: watoto wa Mungu na warithi wa mbinguni. Jambo la nne: Uzoefu wa Mitume pale mlimani uliwafanya wawe na furaha sana kwa kila walichoshuhudia na kuwasadikisha mara moja juu ya umungu wa Yesu. Ni Yesu ambaye alitaka wapate uzoefu huu, kwa lengo maalumu: Alikuwa akiwatayarisha kwa kashfa ya msalaba. Ilikuwa ni kuwapa mtazamo ufaao, maono na nguvu za kupitia mateso na kifo chake kinachokuja. Wakijua kwamba Yesu ni Mungu, wanafunzi watakuwa tayari kufanya lolote kwa ajili yake. Hii pia ni kweli kwetu. Mungu hutupa "uzoefu wetu wa mlima"  nyakati ambazo tuna furaha na mafanikio. Hizi ni nyakati ambazo tunasadiki kwamba Mungu yu hai kweli na anatupenda kwa njia ya pekee. Nyakati za shida na majaribu makali zinapokuja, tunafikiria "uzoefu wetu wa mlima", na inatupa ujasiri na msukumo wa kuendelea. Uzoefu huo ni katika sala zetu za kila siku.

Hivyo basi, sala inatupa fursa ya "kushusha" mizigo yetu, mawazo na hisia zetu. Katika sala Mungu husikiliza, na hakuna malipo kwa hilo. Sala hutusaidia kujenga utu wa kupendeza zaidi na wenye upendo. Kupitia sala, tunakuwa karibu na Mungu. Uhusiano wa namna hii na Mungu hutufanya tuwe na uhakika na amani. Hatufadhaiki, hatukasiriki na kuwashwa kwa urahisi. Utu wetu unakuwa wa kupendeza na tunajenga watu wengine. Sala inatupa maongozi ya Mungu, hekima na maarifa. Tunaposali, tunasikia ujumbe wa Mungu, tunapokea maongozi yake, hekima na maagizo. Ndiyo maana Yesu na mitume wake hawakukaa mlimani kwa muda mrefu. Ilibidi washuke chini na kuendelea kutimiza utume wao. Maisha ya Kikristo hayajumuishi sala pekee; pia inajumuisha kazi. Mtakatifu Augustino alisema: “Sali kana kwamba kila kitu kinamtegemea Mungu na fanya kazi kana kwamba kila kitu kinakutegemea wewe.” sala bila matendo mema haina uhai; kazi bila sala haina maana na haina matunda. Hivyo ni lazima tuhusianishe sala zetu na uwajibikaji katika maisha.

D2 Kwaresima
10 March 2022, 14:48