Dominika ya Pili ya Kwaresima: Utukufu wa Kristo Yesu na Kashfa ya Msalaba
Na Padre Gaston George Mkude, - Roma
Amani na Salama! Tunaongozwa na Injili ya Luka 9: 28b – 36: “Yapata siku nane baada ya kuyasema hayo, Yesu aliwachukua Petro, Yohane na Yakobo, akaenda nao mlimani kusali…”, ndivyo aya ile ya 28 ya sehemu ya Injili ya leo inavyoanza. Natumaini ni kwa sababu tu za mantiki wameondoa katika toleo la Kiswahili la Masomo ya Misa maneno yale ya mwanzo. “Yapata siku nane baada ya kuyasema hayo…” Ila kwa kweli ni maneno ya msingi sana ili kutuelekeza na kupata kuelewa kile alichokizungumzia Yesu kabla ya tukio la leo. Yesu siku nane kabla anazungumzia juu ya kukataliwa, kuteswa na kufa ila siku ya tatu atafufuka. Lilikuwa ni fundisho gumu sana kwa wanafunzi wake kwani walikuwa wanawaza bado kadiri ya mantiki ya ulimwengu huu. Hawaoni kwa nini hatima yake iwe kukataliwa, kuteswa na hata kufa juu msalabani. Na inakuwa ngumu zaidi pale anapotualika katika kumfuasa Yeye ni lazima kujikana nafsi na kubeba msalaba ili kumfuata. Ni Kerygma ya imani yetu, kwani ndio sherehe inayokuwa mbele yetu, yaani Pasaka ya Bwana. Ni fumbo linalotuonjesha huruma na upendo usio na mipaka wa Mungu mwenyewe kwetu sisi wanadamu. Ni kwa kutupenda sisi wanadamu anatufia pale juu msalabani, lakini anafufuka siku ile ya tatu kwani mauti hayana nguvu dhidi ya upendo, upendo unashinda nguvu za mauti na kifo. Ni mwaliko kwetu wa kutoa maisha yetu kwa upendo, ili kuwa kweli wafuasi wa Yesu Kristo.
Fundisho hilo lilikuwa gumu si tu kwa wale marafiki wa karibu wa Yesu bali hata kwetu nasi leo. Ni fundisho linalokwenda kinyume na mantiki ya ulimwengu huu, mantiki ya kujitafuta zaidi, kuwa wabinafsi zaidi, bali sisi wafuasi wa Yesu tunaalikwa kwenda kinyume na mantiki ya ulimwengu huu. Maisha ya Ukristo ni kukataa ile tunayoiita “Ego drama” na badala yake kuongozwa na “Theo drama”, ni kuukataa ubinafsi wetu na kukubali daima kuongozwa na mapenzi ya Mungu katika maisha yetu. Na ndio baada ya fundisho hilo gumu, leo ikiwa ni siku ya nane baadaye, yaani ndio Dominika, Yesu anawachukua baadhi tu ya wanafunzi wake na kwenda nao faragha kule mlimani ili asali. Hatuwezi kusema kwa hakika kwa nini aliwachukua baadhi tu yaani Petro, Yohane na Yakobo, labda walikuwa ni wale walioanza kuelewa zaidi juu ya mantiki na mpango wa Mungu kwa Mtumishi wake. Mwinjili Luka pekee anasisitiza lengo la kwenda mlimani ni ili kusali kama tutakavyoona katika tafakari yetu la leo. Akiwa anaelekea Yerusalemu anawafundisha wanafunzi wake juu ya hatima yake na pia kuwaingiza katika nafasi muhimu ya sala ili kujua mpango wa Mungu katika maisha yake na yetu pia.
Baadhi ya wahubiri wanatafsiri sehemu ya Injili ya leo kama maisha ya utukufu mbinguni, ili kuwaimarisha mitume na rafiki zake Yesu wa Nazareti atakayepitia majaribu magumu ya mateso na kifo pale juu msalabani. Hakika mantiki ya Yesu ni daima kuwaanda na uhalisia wa maisha ya ufuasi kwa wanafunzi wake na ndio maana Mama Kanisa anatenga kipindi cha Kwaresima kuwa mahususi kabisa kutuingiza katika tafakari ya fumbo la wokovu wetu na hasa mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Hivyo sehemu ya Injili ya leo ni vema kuingalia katika muunganiko huo, daima tumkazie macho Yesu Kristo anayejifunua kwetu katika kila nyakati za maisha yetu. Nawaalika kuwa makini sana tunapokutana na aina ya matukio kama hili la kugeuka sura Yesu pale juu mlimani. Mara nyingi wengi wanakimbilia kutafsiri na kuliona tukio kama hilo kama tukio la kihistoria, na hivyo mwishoni kupoteza utajiri mkubwa wa kitaalimungu unaobebwa nyuma yake. Tukio la kugeuka sura kwa Yesu linalopatikana katika Injili zote ndugu yaani, Marko, Mathayo na Luka ni moja ya masimulizi yanayopaswa kuangaliwa kwa jicho la imani na matumaini ili kupata ujumbe kusudiwa. Leo itoshe kuangalia kwa makini sehemu hii ya Injili kama ilivyoandikwa na Mwinjili Luka.
Awali ya yote ni Mwinjili Luka pekee anaonesha kinagaubaga sababu ya msingi ya Yesu kujitenga na kwenda mlimani pamoja na baadhi ya wanafunzi wake, ni kwa ajili ya KUSALI. Yesu alitenga mara nyingi muda wa kusali na ni katika sala kama mtu kweli aliweza kutambua misheni yake ya kuja ulimwenguni. Ni katika mojawapo ya nyakati zile za sala Yesu anang’amua kuwa mapenzi ya Baba yake kuja ulimwenguni ni ili kuukomboa ulimwengu kwa njia ya mateso na kifo pale juu msalabani. Mababa wa Kanisa la Kilatini walipenda kufundisha kuwa Yesu anajimwilisha ili sisi tuweze kupata wokovu, na wale wa Kanisa la Mashariki walipenda kufundisha kuwa anatwaa Mwili na kukaa kati yetu ili nasi tuweze kushiriki Umungu wake, zaidi sana leo Baba Mtakatifu Francisko anatukumbusha mara kadhaa kuwa alifanyika mwanadamu ili nasi tuweze kuwa wanadamu kweli, ndio kuwa wanadamu kadiri ya mapenzi na mpango wake Mwenyezi Mungu. Yesu Kristo anasimama kama kielelezo cha mmoja anayetaka kuishi kweli ubinadamu wake, ni kwa kupenda bila kujibakisha kama anavyotuonesha kwa njia ya maisha yake na pia katika Neno lake yaani Injili. Mwinjili Luka anaonesha jinsi makutano mwanzoni wanavyomfuata Yesu wa Nazareti kwa hamu na shauku kubwa, na taratibu tunaona wanaanza kuacha kumfuata kwa shauku na hamasa ya awali na hata wengine wanapanga jinsi ya kumwangamiza. Ni katika mazingira ya namna hii Yesu anaona haja ya kujitenga na kwenda mlimani ili apate wasaa wa kubaki na Baba yake katika sala.
Ni wakati akisali tunaona sura ya uso wake ikageuka, mavazi yake yakawa meupe, yakimeta-meta. Kung’aa kwa uso ni ishara ya mmoja anayeunganika na Mungu. Hata sura ya Musa iling’aa alipozungumza na Mungu pale mlimani. (Kutoka 34:29-35) Ni utukufu wa Mungu unaojidhihirisha kwetu, ni Mungu anayejifunua kwetu wanadamu, ni EPIFANIA! Ni mapenzi na mpango wa Mungu unaojifunua kwa njia ya Mwana wake wa pekee, na ndio hata nasi tunapokubali kutimiza mapenzi ya Mungu katika maisha yetu, hapo utukufu na ukuu wa Mungu unadhihirika na kujifunua kwa watu wake. Hakika kila kutaniko la kweli na Mungu daima linaacha alama katika maisha ya kila mmoja wetu. Tunapokutana na Mungu katika Neno lake na kumsikiliza kweli, hakika tunarudi nyumbani tukiwa na sura inayong’aa furaha, utulivu wa nafsi wenye faraja ndani yake, wenye nguvu ya kusonga mbele hata katikati ya magumu ya kila siku, wakarimu kwa wengine na hasa wahitaji. Na ndiko kung’aa sura kwetu kwani maisha yetu yanakuwa ni mwanga wenye matumaini kwa wengine. Maisha yetu yanaakisi mpango na mapenzi ya Mungu na maana ya sisi kuwa wanadamu kweli, watu kweli. Baba na Mwalimu wa Kanisa Ireneo anafundisha; “Gloria Dei homo vivens”, yaani, Utukufu wa Mungu ni katika mwanadamu kuwa na uzima tele. Mungu hasimami katika ushindani na viumbe vyake, bali daima uwepo na kuishi kwetu kunapaswa kuufunua ukuu na utukufu wake.
Mwinjili Luka pia katika sehemu ya Injili ya leo anatutajia watu wengine wawili, nao ni Musa na Eliya. Hao ndio ishara ya Sheria/Torati na Manabii wanaowakilisha Agano la Kale. Mara nyingi Agano la Kale tunapolisoma bila muunganiko na Yesu wa Agano Jipya linabaki kutoeleweka na hata linaakisi Sura ya Mungu isiyo sahihi. Hivyo vitabu vyote vya Agano la Kale ili kuvisoma kwa uelewa sahihi lazima kuvisoma kwa kumwangalia Yesu Kristo huku tukiongozwa na Roho Mtakatifu. Na hata tunapokutana na Nafsi ya Yesu Kristo ili aweze kueleweka kwetu hatuna budi kumwangalia kwa jicho la Agano la Kale na daima chini ya maongozi ya Roho wa Mungu. Na ndio tunaona simulizi la wanafunzi wa Emausi, Yesu Mfufuka anajaribu kuwarejesha katika Maandiko ya Agano la Kale jinsi lilivyomzungumzia yeye kuanzia Musa mpaka manabii. (Luka 24:27) Hata Wainjili Marko na Mathayo nao wanazungumzia juu ya Musa na Eliya ila ni Luka pekee anayegusia juu ya mdahalo au mazungumzo kati yao na Yesu: Walizungumza juu ya KUTOKA kwake ulimwenguni na kurudi kwa Baba yake. Neno KUTOKA hapa linatumika sawa na KUTOKA kwa wana wa Israeli walipotoka utumwani Misri kuelekea nchi ile ya ahadi ya maziwa na asali. Nuru katika sura ya Yesu imetoka katika Maandiko Matakatifu, Neno la Mungu hasa sehemu ile ya Agano la Kale. Hivyo Yesu anang’amua sasa kwa kuongozwa na Maandiko Matakatifu juu ya hatima yake ya kuteseka na hata kufa ili aukomboe ulimwengu. (Isaya 53) Yesu katika sala pale mlimani anapambanua mapenzi na mpango wa Mungu Baba kwake kama Mwana aliyejimwilisha, aliyekubali kuutwaa ubinadamu wetu, aliye Mungu kweli na mtu kweli.
Wanafunzi wale watatu, Petro, Yakobo na Yohane walibaki katika usingizi bila kuelewa chochote kinachojiri. Inaonekana kuwa walichoka pia kwa kuupanda mlimani na tukio linaonekana kutokea saa za jioni au usiku. Lakini pia macho yao yanalemewa na usingizi baada ya kupigwa na mwanga wa sura ya Yesu anayedhihirisha hatima yake, ni ugumu wa mioyo yao kuupokea mpango wa Mungu. Lakini moja la kujifunza hapa juu ya usingizi wa hawa wanafunzi wa Yesu zaidi ya uchovu na kuwa tukio la usiku. Hata pale katika bustani ya mizeituni wakati Yesu alibaki akikesha anasali wao pia walilemewa na usingizi, hivyo kila mara Yesu anapokuwa katika nyakati ngumu ya kupokea fumbo la mateso na kifo chake tunaona wanafunzi wake wa karibu wanalemewa na usingizi mzito. (Marko 14:32-42; Luka 22:45) Ni usingizi unaotulemea hata nasi tunaposhindwa kusali ili tuweze kutambua mapenzi na mpango wa Mungu katika maisha yetu. Kusali sio tu tendo la kuongea na Mungu, bali ni tendo la kuingia katika mahusiano ya ndani kabisa na Muumba wetu, ni kunyanyua mioyo yetu ili tuweze kuunganika nawe (Mt. Yohane wa Damasko), ili tuweze zaidi sana sio tu kumuomba au kumshukuru au kumsifu bali zaidi sana ni kumsikiliza, ni kujifunza mapenzi na mpango wake kwetu. Mwanafalsafa na Mteolojia wa Kidanishi Søren Kierkegaard anasema: “Sala ya kweli sio pale Mungu anapopaswa kuwa msikilizaji kwa kile tumuombacho; bali ni pale msaliji anapozidi kusali mpaka kufikia hatua ya kuwa msikilizaji: anasikiliza mapenzi ya Mungu.” Hivyo sala ya kweli ni kumsikiliza Mungu, ni katika kujifunza mapenzi na mpango wa Mungu katika maisha yetu.
Usingizi katika Maandiko Matakatifu pia ni lugha ya picha yenye kubeba ujumbe. Mtume Paolo anawaandikia Warumi anawakumbusha kuwa sasa ni wakati wa kuamka kutoka usingizini. (Warumi 13:11-12). Ni mwaliko wa kuamka kwa kuacha maisha ya kale na kuanza maisha mapya, ni mwaliko wa kubadili kichwa kama ambavyo nimejaribu kuelezea mara nyingi katika tafakari zetu za kila Dominika. Ni kuwa na mtazamo mpya juu ya mahusiano yetu na Mungu. Ni kuenenda kadiri ya mantiki ya Mungu na si ya ulimwengu huu. Hivyo kushindwa kubadili vichwa ni sawa na kubaki na kulemewa na usingizi, ni kutaka mambo yaende kadiri ya sisi na ndio ile tunayoiita “ego drama” na kinyume chake ni kukubali Mungu aongoze maisha yetu kwa njia ya kuruhusu na kuikubali “Theo drama”. Katika muktadha wetu usingizi unamaanisha ugumu kwa upande wa wanafunzi wake Yesu kuelewa na kuukubali ukweli kuwa Masiha hana budi kupitia mateso na kifo ili kuingia katika utukufu wa ufufuko. Tunaona wakati Yesu anatenda miujiza na makutano wanamfuata tunaona wanafunzi wake wanabaki macho ila kila anapoanza kuwaelezea juu ya Fumbo la mateso na kifo chake au kuwa wa mwisho na kuwa watumishi, kutoa uhai kwa ajili ya wengine tunaona wanafunzi wake wanalemewa na usingizi na ndio kubaki katika njozi za mantiki ya ulimwengu huu au “Ego drama”.
Na ndio hali inayotukuta hata nasi mara nyingi ya kujifungia katika mawazo na mipango yetu ya kibinadamu, kadiri ya mimi, nitakavyo na nionavyo mimi. Kanisa la Kisinodi sio mwaliko wa kujifunza kweli za imani bali zaidi sana linanitaka mimi na wewe kuanza kutambua na kujua jinsi ya kuishi kama Kanisa. Kanisa la Kisinodi ni lile linalokuwa tayari kutoka katika nchi ya tambarare, nchi ile ninayojisikia salama kadiri ya mantiki ya ulimwengu huu na kwenda juu mlimani kusali, kwenda juu ni kuanza kuishi mantiki ya mbinguni, ile ya Mungu mwenyewe ambayo kwa msaada wa Mungu Roho Mtakatifu tunaweza kuitambua kwa njia ya sala. Na ndio tunaona Kwaresma ni kipindi cha neema, ni Kairos, ni wasaa wa kwenda jangwani, ndio kuachana na malimwengu ili kwa njia ya sala tukwee mlimani na kukutana na Mungu. Juu ya vibanda vitatu tunaona ni ngumu sana kuelezea kwa hakika kama vile hata mnenaji mwenyewe Petro hakuelewa juu analolinena. Haidhuru tunakuwa na hakika anayejenga kibanda basi anahitaji kufanya makazi ya kudumu japo kwa muda fulani. Yesu kinyume chake daima yupo safarini, lazima akamilishe safari ile ya ukombozi na anawaalika wanafunzi wake kumfuata katika safari ile. Vibanda vitatu vinaonesha kiu na hamu ya Pietro ya kubaki pale mlimani ili kuendelea kuifurahia ile hali ya utukufu aliyokuwa nayo Yesu wakati akiwa katika sala.
Kanisa la Kisinodi ni lile linalotambua kuwa ni Kanisa hujaji, dunia sisi ni wasafiri kwani makao yetu na lengo la maisha ya kila mwamini ni kuufikia uzima wa milele, na ndio Ufalme wa Mungu tunaoalikwa kuujenga na kuusimika tangu tungali hapa duniani. Hata nasi kuna nyakati baada ya kukutana na Mungu katika sala tunaogopa kurudi katika safari ya maisha ya kila siku. Tunajawa na woga wa kurejea maisha ya kawaida ya kila siku. Matatizo na shida za kila siku zinatusababishia uoga wa kuyakabili. Tunajua kuwa hatuwezi kuishi maisha yetu yote kwa kubaki tu kanisani tunasali au katika nyumba za mafungo bali lazima kurejea katika maisha ya kawaida na kuwatumikia wengine kwa upendo na utumishi. Baada ya sala tunaalikwa daima kusafiri pamoja na Yesu kuelekea Yerusalemu ili tuyatoe maisha yetu kama zawadi isiyo na masharti kwa wengine. Wingu pia katika lugha ya Kibiblia ni ishara ya uwepo wa Mungu usioonekana. Tunakutana na ishara ya wingu hasa katika kitabu cha Kutoka, Musa anafunikwa na wingu pale mlima Sinai, na hata hema la mkutano lilifunikwa na wingu kwani ndani mwake kulikuwa na uwepo wa Mungu. (Kutoka 24:15-18; 40:34-35). Petro, Yakobo na Yohane wanaingizwa nao katika mpango wa Mungu ili waweze kuelewa mpango wa wokovu wa Mungu kupitia Mwana pekee wa Mungu Yesu Kristo. Nao wanaanza taratibu kuelewa kuwa hata nao walio wafuasi wa Yesu wanaalikwa kushiriki katika njia hiyo ya mateso na hata kifo.
Ikumbukwe Mwinjili Luka anaandika Injili yake kwa waamini wa jumuiya yake baada ya mateso, kifo na ufufuko wake Yesu Kristo, hivyo lugha ile ilieleweka vizuri kabisa kwa hadhira kusudiwa. Ni kutoka katika wingu sauti inasikika; ni tafsiri ya Mungu kwa kile kinachotarajiwa kama hatima ya Yesu Kristo. Sauti inaalika kumsikiliza huyu, hata kama anatualika kwenye safari iliyo ngumu, zinazokinzana wakati mwingine na mantiki ya ulimwengu huu. Hivyo Mwenyezi Mungu anapendezwa daima na yule anayemsikiliza Mwanae na kumfuata. Ni mwaliko kwetu sote wa kumsikiliza daima Yesu na ndio tunaalikwa kusikiliza Neno lake na kulielewa na kuliishi katika maisha yetu ya kawaida ya kila siku daima kwa msaada na maongozo ya Mungu Roho Mtakatifu. Kanisa la Kisinodi ni lile linalodumu katika kumsikiliza Mungu kwa msaada wa Mungu Roho Mtakatifu. Mwishoni tunaona Musa na Eliya wanapotea na anabaki Yesu peke yake. Ni lugha ya picha kuonesha kuwa Agano la Kale ni utambulisho wa huyu ambaye sasa tunaalikwa kumkazia macho yeye na kumsikiliza na kumfuata. Kumfuasa Yesu Kristo hakika sio jambo rahisi kwani daima tunaalikwa kuenenda katika njia yake na ndio ile ya kujikana sisi wenyewe na kuwa tayari kubeba msalaba ila nasi tuweze baada ya maisha ya hapa duniani kushiriki utukufu usio na mwisho mbinguni. Kufa kama mbegu ili kuweza kutoa matunda mengi. Kadiri ya mantiki ya ulimwengu wa leo ambapo mwanadamu anaangalia tu leo yake na kudiriki hata kutokuwa na matumaini katika maisha ya umilele hatuna budi kubadili vichwa vyetu ili kuupokea ukweli huu wa imani.
Tukio la kugeuka sura linajiri siku ya nane baada ya Yesu kuwafunulia wanafunzi wake kuwa inampasa kuteseka na kufa ila siku ya tatu atafufuka. (Luka 9:22-27) Siku ya nane ni siku baaada ya Sabato yaani Dominika, siku ya Bwana ambapo waamini Wakristo wanakusanyika kwa kusikiliza Neno na kuumega mkate. (Luka 24:13) Hivyo kila Dominika ni siku ya kupanda mlimani tunapokutana na utukufu wa Mungu katika adhimisho la Neno na Meza ya upendo wa Mungu, yaani Ekaristi Takatifu. Ni siku ya kukutana na sura tukufu ya Mungu kwa njia ya Neno lake na katika maumbo yale ya Mkate na Divai. Tunaona Mitume wale watatu baada ya kushuka kutoka mlimani Yesu anawaagiza kutoeleza kwa wengine maana bado walikuwa hawajaelewa katika ukamilifu juu ya mpango wa Mungu kwa mtumishi wake. Lakini kwetu leo hii ni kinyume chake tunaalikwa kuwashirikisha wengine utukufu ule wa Mungu tunaokutana nao kila Dominika katika Meza ya Neno na Ekaristi Takatifu. Ni baada ya mateso, kifo na Ufufuko tunaona sasa wanafunzi wa Yesu wanaelewa mpango wa Mungu katika njia ile ya ukombozi ya Yesu Kristo. Nawatakia tafakari na Dominika njema.