Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya V ya Kipindi cha Kwaresima: Mwanamke Mdhambi mbele ya Huruma ya Mungu Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya V ya Kipindi cha Kwaresima: Mwanamke Mdhambi mbele ya Huruma ya Mungu 

Dominika ya V Kipindi Kwaresima: Mdhambi Na Huruma Ya Mungu

Mwanamke alikuwa mzinzi na, kadiri ya Torati, alihukumiwa afe kwa kupigwa mawe. Na Yesu, ambaye kwa mahubiri yake na kwa kujitoa kabisa sadaka, hadi Msalabani, alirejesha sheria ya Musa kwenye asili yake ambayo kiini chake ni upendo wa Mungu, ambaye anajua kusoma moyoni mwa kila mtu, na kugundua hamu iliyofichama ndani kabisa, ambayo lazima itangulie juu ya yote.

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na salama ! Kwaresima ni kipindi cha toba, ni wakati wa neema wa kupokea huruma na upendo wa Mungu anayekubali kuteseka, kufa, na siku ya tatu kufufuka, ili sisi tulio wadhambi tuweze kufanyika warithi pamoja naye, na ndio kuwa wana huru na Mwana pekee wa Mungu. Ni kipindi cha neema, ni wakati muafaka na uliokubalika, ni fursa ya kiroho yaani KAIROS. Na ndio Injili ya leo inatuonesha haswa kuwa Kwaresma ni kairos kwetu, kwani tunapofanya toba hakika tunapokea huruma na upendo wa Mungu. Kwaresma ni kipindi cha kutafakari upendo na huruma ya Mungu kwetu, mateso na msalaba wake Bwana wetu Yesu Kristo vinapata maana yake katika upendo na huruma ya Mungu kwetu wanadamu. Yesu Kristo amekuja kuhubiri na kuufunua upendo, na ufalme wa Mungu kwetu, na ndio sababu ya yeye kufanyika mwili na kukaa kati yetu. Ni kwa sababu ya upendo wa Mungu kwetu, yeye anakataliwa, kuteseka na kufa pale juu msalabani. Ni upendo wa Kimungu unaoshinda dhambi, unaoshinda mauti, unaomshinda yule muovu na uovu. Ni upendo wa Mungu uliotundikwa pale juu msalabani ili kutufanya sisi kuwa wana huru wa Mungu. Na ndio tunaona leo mwanamke aliyekutwa katika uzinzi, anayekuwa kinyume na upendo na uaminifu wa maisha ya ndoa, analetwa mbele ya Yesu aliye ishara kamili ya upendo, huruma na uaminifu wa Mungu.

 

Ni simulizi linalotuacha mdomo wazi na hata kwa wengine kukwazika kwani Yesu hamuhukumu huyu mwanamke, na badala yake anamuonjesha huruma na upendo wa Mungu. Mwanamke huyu ni muwakilishi wa kila mmoja wetu kwani ni mara nyingi tunakosa upendo na uaminifu kwa Mungu na kwa jirani. Maudhui na mtindo wa uandishi wa sehemu ya Injili ya leo, unaakisi zaidi mtindo na maudhui ya Injili ya Luka kuliko ya Yohane. Na ndio baadhi ya wanazuoni wa Maandiko Matakatifu wanaona sehemu ya Injili ya leo, sehemu yake stahiki ni katika sura ya 21 ya Injili ya Luka. Hivyo kwa kuisoma unaweza kuona wazi kuwa ni tofauti katika mtiririko wake wa kimantiki na ile hotuba ndefu aliyoitoa Yesu wakati wa sikukuu ya vibanda katika sura ya 8 ya Mwinjili Yohane.  Mtindo na hata lugha ya sehemu ya Injili ya leo unakaribiana zaidi na ule wa Mwinjili Luka, Injili ya Huruma na Upendo na Msamaha wa Mungu kwa wadhambi. Didascalia Apostolorum (Maandiko ya Mafundisho ya Mitume) inaweka wazi kuwa simulizi hili linaweka wazi Huruma na Upendo wa Yesu kwa wadhambi na wakosefu, na pia jinsi alivyokuwa kinyume na wale wanaojihesabia haki kwa kuhukumu wengine na ndio maana inaitimishwa kwa maneno ya Yesu; “Wala mimi sikuhukumu. Enenda zako; wala usitende dhambi tena”.  (Yohane 8:15) Ni Injili ya Injili, kwa maana ya Habari Njema kweli kwetu tulio wadhambi na wakosefu, kila tunapokutana na Yesu hapo tunakutana na upendo na huruma ya Mungu kwetu na kamwe sio hukumu.

Kristo Yesu Ni Ufunuo wa Huruma na Upendo wa Mungu
Kristo Yesu Ni Ufunuo wa Huruma na Upendo wa Mungu

Mwanzoni mwa simulizi anayeonekana kuwa ni muhusika mkuu ni huyu mwanamke aliyekutwa katika uzinzi, hivyo analetwa mbele ya Yesu kama mdhambi, mkosefu, na mbaya zaidi ni mwanamke, ikumbukwe katika ulimwengu wa Wayahudi ni mwanamke tu ndiye anayeonekana mkosaji katika dhambi ya uzinzi na hivyo ilipaswa apigwe mawe hadi kufa na kamwe si mwanaume. Na kwa adhabu hiyo ya kifo ilionesha juu ya uzito na ukubwa wa dhambi ya uzinzi. Ni jamii yenye kutawaliwa na mfumo dume, hivyo kila baya linamwangukia mwanamke. Ni jamii inayoakisi pia jamii zetu nyingi za Kiafrika hata leo mintarafu nafasi ya mwanamke. Na ndio maana hatusikii mwanaume aliyekutwa naye katika uzinzi isipokuwa huyu mwanamke anayeletwa mbele ya Yesu hekaluni. Yesu anawekwa njia panda, katika mtego kati ya makundi mawili, kundi la kwanza ni lile la mafarisayo na waandishi, kwao hakuna msamaha kwa mwanamke anayekutwa katika uzinzi. Mafarisayo na waandishi hawa ndio wale wanaojiona kuwa wanashika maadili na ni watu wa dini kweli kweli, hivyo mbele ya jamii walionekana kuwa ni watu safi wasio na mawaa yeyote. Ni mtego kwani kama kweli Yesu ni mtu wa haki na mtu wa Mungu kweli basi hana budi kuwa na mtazamo kama wao.

Kwa kumsamehe mwanamke huyu basi Yesu angekuwa kinyume na sheria ya Kiyahudi ambayo haikuwa na msamaha kwa dhambi ya aina ile ya uzinzi. Lakini pia kumuhukumu kifo, atakuwa ameingilia mamlaka ya dola ya Kirumi ambayo yenyewe tu ndiye ingeweza kutoa hukumu ya namna hiyo katika dola lake lote la Kirumi. Hivyo chaguzi zote mbili zingetosha kumweka Yesu matatani kwa kunasa katika mtego. Injili ya leo kwa ufupi, ni wadhambi wanamuhukumu mdhambi mbele ya Yesu. Katika mazingira hayo tunaona Yesu anabaki kimya na mtulivu na hata anainama anaandika kwa kidole chake, kwa hakika ni juu ya jiwe la hekalu maana tukio lilijiri hekaluni. Kuna tafsiri imeenea tangu enzi za Mt. Yerome, kuwa Yesu wakati anaandika chini kwa kidole chake hapo alikuwa anaandika madhambi ya wale washtaki, kwa kweli hapana si sahihi hata kidogo maana kama nilivyotangulia kusema hapo juu kuwa tukio hili lilijiri katika mazingira ya hekaluni. Hivyo si rahisi kusema kuwa aliandika pale juu ya sakafu ya jiwe kwa kidole na watu kuweza kuona madhambi yao. Tafsiri hiyo si sahihi hata kidogo, na hivyo tuiepuke kuisambaza.

Wapo wengine wanaosema pia kuwa Yesu alibaki kimya na kuanza kuandika ardhini, ili kupata fursa ya kufikiri na kuwapa jibu linalokuwa sahihi, na hata pia kuwapa muda wa kutuliza jazba na hasira zao dhidi ya huyu mwanamke aliyekutwa katika uzinzi. Niseme bado hatuwezi kusema kwa hakika kwa nini anainama na kuandika chini kwa kidole chake. Na hata wengine wanahusianisha na (Yeremia 17:13) “Ee Mwenyezi Mungu tumaini la Israeli, wote wanaokukataa wataaibishwa; wanaokuacha wewe watatoweka, kama majina yaliyoandikwa vumbini…” Kwa kweli kama nilivyotangulia kusema bado hatuwezi kusema kwa hakika maana ya kitendo kile cha Yesu kuandika sakafuni. Lakini pia Yesu angeliweza kabisa kuwapa jibu kirahisi na hivyo kuepa mtego wa hila wa hawa waliomleta mwanamke mbele yake. Kwa vile ilikuwa ni hekaluni, Yesu angeweza kuwaambia wampeleke kwa baraza la mahakimu wa dini ya Kiyahudi yaani Sanhedrini, ambalo ilikuwa ni umbali mdogo wa chini ya mita 100 kutoka hekaluni. Kufanya hivyo ni kuwapa ushindi wale waliomuhukumu na hivyo kuendelea na mtazamo wao wa kuhukumu wengine na wao kujihesabia haki daima.  Yesu ananyanyua kichwa chake na kuwauliza, asiye na dhambi awe wa kwanza kumtupia jiwe huyu mwanamke.  Na baada ya hapo akainama tena na kuendelea kuandika juu ya jiwe la hekalu.

Neno la Mungu: Huruma, Upendo na Uaminifu
Neno la Mungu: Huruma, Upendo na Uaminifu

Ni mwaliko wa kila mmoja wao kuingia katika chumba chake cha ndani, yaani dhamiri, kwani ndio sauti ya Mungu ndani mwetu na kujihoji kwa dhati kabisa. Ni mwaliko wa kujiangalia nafsi na hasa dhamiri zetu kila mara tunapokuwa na kishawishi cha kuhukumu wengine. Ni hapo tunaona kila aliyekuwa anamuhukumu huyu mwanamke alipata fursa ya kujiona ndani kabisa katika nafsi na dhamiri zao. Na hapa tunasikia waliondoka wote, si tu wale waliomleta huyu mwanamke bali hata makutano waliokuwa wanamsikiliza Yesu nao kwa hakika walikuwa na mtazamo kama ule wa mafarisayo na waandishi. Waliondoka kuanzia wazee yaani presbiteri, na hivyo kubaki tu wawili yaani Yesu na yule mwanamke. Ni hapo sasa tunaona wahusika wakuu wa simulizi la Injili ya leo wanabaki wawili tu. Ni mwanamke mdhambi na Yesu hakimu mwenye huruma. Na ndio Mtakatifu Augustino anaelezea Injili ya leo kuwa; “RELICTI SUNT DUO: MISERA ET MISERICORDIA”. Ni maneno ya lugha ya Kilatini yakiwa na maana ya, “walibaki wao wawili: mdhambi na huruma”, naomba nikiri sio tafsiri sahihi sana kwani haiakisi hasa hali ya huyu mwanamke aliyekutwa katika uzinzi, kwa kweli neno “MISERA”, linataka kuonesha hali yake ya ndani mbele ya washitaki wake, jinsi alivyoonekana mbele ya jamii, jinsi hata yeye mwenyewe alivyojiona na hivyo kupoteza thamani na utu wake.

Ni maskini na mkosaji wa kila hali mbele ya jamii na Mungu. Hapa tunaona wanabaki wawili tu, ni huyu aliyekosa thamani, mdhambi, asiyekuwa na mastahili na upande mwingine yupo yeye mwenye Upendo na Huruma yote, asili ya msamaha na utu wetu wa kibinadamu. Yesu ndio huruma yenyewe, ndio rehema yenyewe, ndiye anayeifunua sura halisi ya Mungu kama tulivyoona katika ujumbe wa Injili ya Dominika iliyopita. Na ndio kipindi cha Kwaresma tunaalikwa kila mara kubaki mbele ya Huruma ya Mungu, Upendo wa Mungu, Msamaha na Rehema ya Mungu! Kwaresma ni nafasi ya kubaki wawili tu, mimi na wewe tulio wadhambi mbele ya Huruma yenyewe, yaani Mungu mwenyewe! Ni kipindi cha kufanya toba ya kweli, ya kujikubali unyonge na uduni wetu kwani kila mmoja wetu ni “misera”, anayekutana na Yesu aliye “Misericordia”. Yesu anaendelea kubaki pale chini wakati mwanamke aliyekamatwa katika uzinzi akiwa amesimama pale katikati. Yesu anabaki pale chini sehemu au nafasi ya mtumwa na sio juu katika kiti cha hukumu akimwangalia mdhambi au mkosefu. Ananyanyua kichwa chake na kumtazama kwa uso wa huruma na upendo na kumsamehe madhambi yake. Ona WEMA NA HURUMA ya Mungu kwetu wadhambi na wakosefu!

Na ndio tunaposoma Maandiko Matakatifu tunaona ni Mwenyezi Mungu mwenye kiu ya mwanadamu na si kinyume chake, ni Mungu anamtafuta mwanadamu ili amrejeshee ile hadhi yake ya awali, ya kuwa na mahusiano naye sahihi, yaani ya Baba aliye huruma yenyewe na sisi tulio wadhambi na wakosefu. Yesu anamwambia mwanamke aliyekutwa katika uzinzi kuwa hata nami sikuhukumu, hivyo kutenda mema na kufanya maovu ni sawa sawa tu mbele yake? Ni swali la haki kabisa baada ya kusikiliza sehemu ya Injili ya leo. Hakika dhambi ni mbaya kwani inatuondolea urafiki na mahusiano yetu na Mungu na jirani na hivyo kutuweka mbali na Mungu na jirani. Na Yesu hakumwambia mwanamke huyu kuwa ulilofanya ni jambo la kishujaa na linalostahili pongezi la kumsaliti mume wake, na hivyo endelea hivyo hivyo, ila badala yake tunaona Yesu anamsamehe dhambi yake na kumwalika aende na asitende dhambi tena. Na ndio huruma ya Mungu kwetu kila mara tunapomwendea kujipatanisha naye, anatualika baada ya kutusamehe dhambi zetu kubadili maisha yetu kwa kumfuata na kukaa naye daima. Metanoia ya kweli ni kuacha kichwa cha kale na kuvaa kichwa kipya, na huo ndio wongofu tunaoitiwa katika safari ya maisha ya ufuasi. Toba ya kweli ni kukubali kubadili njia zetu, ni kuanza maisha mapya yenye kuakisi mahusiano ya upendo kwa Mungu na kwa jirani.

Huruma na Upendo wa Mungu Vyadumu milele
Huruma na Upendo wa Mungu Vyadumu milele

Na ndio Mtume Paulo katika somo la pili baada ya kuonja wema na msamaha wa Yesu anaona mambo mengine yote kuwa ni takataka, na hata Isaya anawaalika wana wa Israeli kuangalia mbele na kamwe wasiangalie nyuma, yaani kuangalia madhambi yao kwani daima sote tunaalikwa kuangalia Huruma na Upendo wa Mungu unaotualika kwake. Na ndio Kwaresma inabaki kuwa ni Kairos, ni wakati wa neema, ni fursa adimu na adhimu kwangu na kwako tulio wadhambi kupokea huruma ya Mungu. Mwenyezi Mungu anataka kufanya yote mapya, yote yachipuke upya katika maisha yetu. Mungu aliye huruma yenyewe, kamwe hatuiti kwa majina yatokanayo na madhambi na makosa yetu, bali kwa majina yetu halisi tena kwa upendo, kwani yeye hasimami kama hakimu mkali kama wengi tunavyopenda kumuona bali kama huruma na rehema kwa kila mmoja wetu. Kamwe tusiingie kwenye kishawishi cha kuwaona na kuwatambua wengine kwa majina ya dhambi au makosa wanayofanya bali tuwatambue kwa majina halisi waliyoitwa na Mungu siku ile ya Ubatizo wao. Kamwe tusiwatambue watu kama wazinzi, malaya, wezi, mafisadi, vibaka, walevi, walafi, waongo, wambeya, wadaku, wapiga majungu na kadhalika na kadhalika, kwani kufanya hivyo ni kuwakuhukumu, ni kuwapiga mawe na hilo kwa kweli sio hulka ya maisha ya Mkristo, badala yake sisi tuwe wenye huruma kama Baba yetu wa mbinguni alivyo na huruma. Walibaki wao wawili: Mdhambi na Huruma! “relicti sunt duo:misera et misericordia” Nawatakia tafakari na Dominika njema pamoja na maandalizi mema ya maadhimisho ya fumbo Kristo la Juma Kuu!

30 March 2022, 16:38