Dominika V ya Kwaresima: Mwanamke Mzinzi Uso Kwa Uso na Huruma ya Mungu
Na Padre Efrem Msigala, OSA, - Roma.
Karibu mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican katika tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya 5 ya Kipindi cha Kwaresima Mwaka C. Tukiongozwa na wazo hili "Yeye asiye na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza kumpiga jiwe." Katika tafakari hii tunaongozwa na Masomo: Isaya 43:16-21, Wafilipi 3:8-14, Yohane 8:1-11. Mpendwa msikilizaji: Masomo yanatukumbusha kwamba hatupaswi kujihesabia haki na kuona maisha ya wengine hayastahili, wakati Mungu anawaita kwa upole kwenye uongofu. Somo la kwanza laeleza jinsi Mungu mwenye rehema anavyosamehe dhambi za watu wake waliochaguliwa na kuwarudisha kutoka uhamisho wa Babeli, linatukumbusha kwamba sisi pia tumesamehewa, na tunaokolewa kutoka katika hali yetu ya dhambi. Katika somo la pili, Paulo anajionesha kuwa ni mwenye dhambi aliyesamehewa ambaye amebadilishwa kabisa na imani yake katika Kristo Yesu. Lakini bado anaendelea kupambana sababu anaona bado hajakamilika. Mtume Paulo anampenda Kristo sana anataka kushiriki katika mateso yake na hata katika kifo chake ili ashiriki pia Ufufuo wake. Yeye aliyekuwa mtesaji na muuaji wa wakristo, akatubu na akamwongokea Mungu. Injili ya Dominika ya tano ya Kipindi cha Kwaresima inaendelea kutoa somo kuhusu huruma na msamaha wa Mungu. dominika iliyopita tulisikia Mfano wa Mwana Mpotevu kutoka katika Injili ya Luka. Leo hatusikii mfano, bali taarifa kutoka Injili ya Yohane 8:1-11 ya kukutana kati ya Yesu, Waandishi na Mafarisayo, na Mwanamke waliyesema amekamatwa katika uzinzi, ingawa mwanaume aliyezini naye hawakumleta.
Mpendwa msikilizaji, Yesu anawaambia washtaki “yeye asiye na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza kumpiga jiwe”, Yesu anawataka washtaki kutathmini nafsi zao na kuchukua hatua. Hivyo, Yeye aliwapa haki washtaki na rehema kwa mwanamke mwenye dhambi. Hadithi hii ni ya kushangaza sana kwa sababu wanaume hao wanamwomba Yesu amhukumu mwanamke waliyesema amefumaniwa katika uzinzi bila kumleta mwanaume ili "kumjaribu" kuona hatua atakayochukua. Kadri ya sheria ya Musa, Mwanamke aliyekamatwa katika uzinzi alipaswa kuhukumiwa kwa kupigwa mawe. Jaribio lao lilikuwa: Ikiwa Yesu atamsamehe mwanamke huyo itasemwa kwamba amevunja amri za Musa; ikiwa atamhukumu, itasemwa kwamba haendani na ujumbe wake wa rehema kwa wakosefundiyo mtego na kitendawili alichowekewa Yesu. Lakini, Yesu alinyamaza kwa muda ili kuwaalika washtaki wajitafakari kabla hajauliza swali lililowafanya waanguke kwenye mtego wao. Mtakatifu Augustino anasema: "Yesu, katika jibu lake, hakukosa kuheshimu sheria wala hakuacha upole wake". Baada ya kutulia kwa muda alisema maneno haya: “Yeye asiye na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza kumpiga jiwe huyu mwanamke” akainama na kuandika chini. Hatujui aliandika nini. Injili inatuambia kwamba washtaki waliondoka mmoja mmoja bila kumpiga mawe yule mwanamke. Swali ni hili:
Kwa nini hawakumpiga mawe? Kwa nini waliondoka mmoja baada ya mwingine? Labda kila mmoja alijichunguza mwenyewe na kugundua kuwa yeye ni mwathirika wa dhambi kama hiyo au inayofanana na hiyo. Je, yawezekana kumrushia mshitakiwa mawe wakati mshitaki mwenyewe anapaswa kujipiga kwanza? "Je, na sisi hatuwapigi mawe wengine kupitia mitandao ya kijamii? Je, bado tunakumbuka kwamba mwenye dhambi anastahili upendo wa kindugu, marekebisho na rehema? Kwa nini tunapata furaha kwa mfano, kushiriki picha au video za wale walionaswa katika matendo ya dhambi kwenye mitandao ya kijamii? Na wakati mwingine hata kutengeneza tukio ili kumchafua mtu? Na pengine tunaofanya hivyo ni wadhambi zaidi. Je, Ikiwa Mungu angefichua kila mmoja wetu madhambi yake, nani angeweza kuinua kichwa chake? Tunakumbuka ile zaburi ambayo inasema “Bwana kama wewe ungehesabu maovu yetu nani angesimama...” (Zaburi 130,3). Hatufaidiki chochote kueneza au pia kutengeneza makosa ya wengine. Hatufaidiki chochote kwa kuwadharau wengine, na hatufaidiki chochote kwa kuwanyoshea wengine kidole. Sisi sote tuna hatia ni kama Mafarisayo waliomleta mwanamke, tunataka kuwapiga mawe baadhi ya watu au tayari tumewapiga mawe wengine. Leo Kristo Yesu anatuambia asiye na dhambi hiyo: kwa mawazo, maneno, matendo na kwa kutotimiza wajibu awe wa kwanza kutupa jiwe.
Basi mpendwa msikilizaji, kwa kadiri tunavyopaswa kulaani dhambi, tunapaswa pia kumpenda mwenye dhambi kama Kristo anavyofanya, tukimsaidia abadilike. Tunapotubu dhambi zetu tunapatanishwa na Mungu na kuunganishwa tena katika jumuiya ya waamini ambayo tulijitenga nayo kwa dhambi zetu. Dhambi inadhoofisha vifungo vyetu ndani ya jumuiya ya Kikristo, lakini toba na upatanisho huiponya na kuitia nguvu. Kristo alikuja kuponya majeraha ya dhambi zetu, tunapaswa pia kujitahidi kuponya kila mmoja wetu kwa mioyo yetu ya huruma. Kila mtu ni wa thamani kubwa kwa jamii na kwa familia ya Kikristo, hakuna mtu anayepaswa kuachwa, kulaumiwa, kutengwa au kupuuzwa. Tunapothaminiana, tunaonyesha rehema na upendo. Kanisa ni wakala wa uponyaji duniani. Sakramenti ya Kitubio huponya na kurejesha. Kuwa wakala wa uponyaji na si wa kuhukumu; hivyo ndivyo wito wetu wa Kikristo unavyohitaji. Usitende dhambi tena; ndivyo Mungu anavyotaka kutoka kwetu sio jambo lisilowezekana, mwenye dhambi anaweza kuwa mtakatifu. Kwa sababu watakatifu kimsingi ni wadhambi waliotubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu katika maisha yao na kuanza kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka.
Mtakatifu Paulo aliwahi kuwa mtesaji lakini neema ya Mungu ilimbadilisha. Yesu aliingilia kati na kuokoa maisha ya yule mwanamke maskini ambaye angepigwa mawe hadi kufa, na hivyo ndivyo alivyoingilia kati na kutuokoa kwa mwili wake msalabani. Huu ni wakati wa kutazama ndani na kuzipiga mawe hisia zetu za dhambi, kushutumu tabia zetu za dhambi na kuomba rehema ya Mungu. Yesu hakumhukumu yule mwanamke, kwa hiyo tusiwahukumu wengine kabla ya kujitafiti nafsi zetu wenyewe. Kumbuka maneno ya Yesu kwa yule mwanamke. “Wala mimi sikuhukumu; enenda zako, wala usitende dhambi tena” (Yn 8:11). Hakika Mungu anafanya jambo jipya katika maisha yetu kama tulivyosikia maneno hayo ya Yesu kwa yule mwanamke. Tuache maisha ya awali ya dhambi: kutoa mimba, biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya, kashfa, masengenyo, husuda, kiburi, dhuluma, ulevi, uasherati, ufisadi, wizi, uuaji n.k. na tumpe Mungu nafasi. Katika kipindi hiki cha Kwaresima Mungu atujaze zaidi neema ya toba ya kweli na rehema kwa wengine.