Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya V ya Kipindi cha Kwaresima: Kristo Yesu ni ufunuo wa huruma, upendo na msamaha wa Mungu kwa mwanadamu. Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya V ya Kipindi cha Kwaresima: Kristo Yesu ni ufunuo wa huruma, upendo na msamaha wa Mungu kwa mwanadamu. 

Dominika ya V ya Kwaresima: Nenda Usitende Dhambi Tena!

Katika kipindi hiki cha siku arobaini za Kwaresima, Mama Kanisa kwa njia ya Neno la Mungu anatuhimiza kwa kurudia tena na tena, mwaliko wa kufunga, kufanya toba, kusali, na kutenda matendo ya huruma. Huu ni muda muafaka wa kumwendea Kristo Yesu, kielelezo makini cha ufunuo wa huruma, upendo na msamaha wa Mungu kwa mwanadamu. Mwaliko na toba na wongofu wa dhati.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, katika Dominika ya tano ya kipindi cha Kwaresima mwaka C wa Kanisa. Kadiri ya utamaduni na mapokeo ya Kanisa, kuanzia Dominika hii misalaba inafunikwa, mpaka ijumaa kuu wakati wa kuadhimisha mateso ya Kristo na sanamu zinafunikwa, mpaka wakati wa maaadhimisho ya vijilia vya pasaka. Dominika hii huadhimishwa takaso la tatu la wakatukumeni watakaobatizwa usiku wa vijilia vya Pasaka. Katika kipindi hiki cha siku arobaini za Kwaresima, Mama Kanisa kwa njia ya Neno la Mungu anatuhimiza kwa kurudia tena na tena, mwaliko wa kufunga, kufanya toba, kusali, na kutenda matendo ya huruma. Siku ya Dominika ya 5 zinatimia 33 hivyo tunabakiwa na siku 7 tuingie Juma kuu linalofunguliwa na jumapili ya matawi. Ni mda mwafaka kujitafakari na kujiuliza: Je, ile dhambi ninayoipenda kuliko zote nimeiacha, tendo gani la huruma nimetenda tangu Kwaresima ianze, ni nini nilichojinyima kwa ajili ya wahitaji na nimesaidia wahitaji wangapi kwa siku hizi 33 tangu kwaresma ianze? Masomo ya dominika hii yanatuonesha upendo na huruma ya Mungu kwetu sisi wadhambi. Kila tunapokiri makosa yetu tunaambiwaò “Enenda zako; wala usitende dhambi tena” (Yn 8:11).

Katika somo la kwanza la kitabu cha Nabii Isaya (Isa 43:16-21); Mungu kwa upendo na huruma yake anaahidi kuwakomboa waisaraeli utumwani Babeli kama alivyowakomboa kutoka utumwani Misri. Utabiri huu unatizwa kwa mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Itakumbukwa kuwa Mungu alilichagua Taifa la Israeli kwa maandalizi ya kutuletea Mkombozi kwa kufanya nao Agano – makubaliano rasmi yaliyofanywa mlimani Sinai na kuwapa amri zake. Nabii Hosea anaueleza uhusiano uliokuwepo kati ya Mungu na Waisraeli kwa mfano wa uhusiano wa mume na mke – Bwana na Bibi Arusi. Waisraeli, kama bibi arusi wa Mungu, walikosa uaminifu kwa kumwasi Mungu. Matokeo ya uasi wao ni utumwa wa Babeli. Huko utumwani walitambua makosa yao wakayakri, wakamlilia Mungu na kuomba msamaha naye akawasamehe na kuwaahidi ukombozi mpya na kuwarudisha tena katika nchi yao. Mtume Paulo katika somo la pili la waraka wake kwa Wafilipi (Wafil. 3:8-14); anatufundisha kuwa, tukiwa na imani juu ya nguvu ya mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo, tutayaona mambo ya dunia hii si kitu ni ya kupita, hivyo tutafunua mioyo yetu kwa makuu ambayo mwenyezi Mungu anatutendea kwa njia ya Kristo na kuwa tayari kuacha dhambi na kukazana kutenda mema na kuukaza mwendo ili tulipate tuzo la uzima wa milele.

Toba na wongofu wa ndani ni kitovu cha furaha ya kweli katika maisha.
Toba na wongofu wa ndani ni kitovu cha furaha ya kweli katika maisha.

Injili ilivyoandikwa na Yohane (Yn 8:1-11); ni simulizi la tukio la kusisimua sana. Ni simulizi la mwanamke mzinzi mwenye aibu ya kufumaniwa, amejaa hofu ya kupigwa mawe mpaka afe. Dhambi ya uzinzi katika Agano la Kale ilichukuliwa kuwa ni dhambi mbaya sana. Ndiyo maana dhambi ya kuabudu miungu mingine ilifananishwa na dhambi ya uzinzi, kukosa uaminifu kwa Taifa la Israeli kwa Mungu wao na adhabu yake ilikuwa kuigwa mawe mpaka kufa  (Wal 20:10, Kumb 22:22-24). Lakini cha kusikitisha katika ulimwengu wa sasa uzinzi na uasherati unaonekana kuwa jambo la kawaida. Simulizi hizi lina mafundisho mazito mno. Kwanza linatuonyesha chuki ya Mafarisayo kwa Yesu kwa mafundisho yake, na hivyo wanafanya kila namna kwa mawazo, maneno na matendo yao ya hila ili wamwangamize, wateketeze uhai wake. Pili, linatufundisha kuwa mbele za Mungu hakuna binadamu asiye na dhambi na Mungu kwa upendo na huruma yake daima anatusamehe kila tukiri na kutubu makosa yetu, nasi hatuna mamlaka ya kuwahukumu wengine kwa adhabu ya kifo maana uhai wa mwanadamu ni mali ya Mungu. Uhai ni zawadi na tunu pekee ambayo Mungu ametupatia sisi wanadamu, hivyo ni jukumu letu kuupokea, kuutunza na kuulinda.

Thamani ya maisha yetu mbele za Mungu ni kubwa mno kwa kuwa tumeumbwa kwa sura na mfano wake. Thamani ya tunu hii, Kristo anaidhihirisha kwa kuwafanya mafarisayo na waandishi watambue kuwa hukumu ya kifo ni ukatili na uovu dhidi ya uhai hata kama sheria ya Musa iliruhusu uovu huo ikisema; “Na mtu aziniye na mke wa mtu mwingine, naam, yeye aziniye na mke wa jirani yake, mtu mume aziniye, na mwanamke aziniye, hakika watauawa”(Wal 20:10; Kumb 22:22). Walimu wa sheria na mafarisayo walizingatia kwa ushupavu sana sheria za Musa na manabii. Hivyo walijiona kuwa wao ni watu wenye maarifa, haki na waadilifu. Waliwachukia mno watu waliovunja sheria na watenda dhambi. Waliona kuwa Mungu hawezi kumsamehe mtu aliyetenda dhambi. Yesu alifundisha msamaha wa dhambi na kujihusianisha daima na wadhambi, hivyo akawa adui kwao. Kwa hiyo lengo lao hasa la kumleta mwanamke aliyefumaniwa ni kutafuta sababu ya kumshitaki Yesu ili auawe. Tukumbuke kuwa kipindi hiki wayahudi walikuwa chini ya ukoloni wa Warumi na hawakuruhusiwa kutekeleza adhabu ya kifo. Hivyo Yesu angesema watekeleze sheria ya Musa wampige kwa mawe huyu mwanamke mpaka kufa, yeye mwenyewe angekuwa na hatia ya kuuwa kadiri ya sheria ya serikali ya warumi, pili angepingana na mafundisho yake juu ya huruma, upendo na kutowahukumu wengine. Lakini pia angesema wasimuue angepingana na sheria ya Musa na yeyote aliyepingana na sheria ya Musa alistahili adhabu ya kifo. Yesu anatoa jibu la kuwashitaki wao akisema; “Yeye asiye na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza kumtupia jiwe” (Yn 8:7).

Injili inasema, kimya kimya, waliondoka mmoja mmoja, wakitanguliwa na wazee hata wa mwisho wao. Kisha Yesu anamwambia huyu mwanamke “Wala mimi sikuhukumu. Nenda zako; usitende dhambi tena” (Yn 8:11). Sababu ya kupelekwa huyu mwanamke peke yake kwa Yesu ina maana kubwa zaidi inayopita uelewa wa mafarisayo na waandishi. Mungu alimwambia Hosea; “Nenda tena ukampende mwanamke anayependwa na mume mwingine na ambaye ni mzinzi. Mpende kama Mimi ninavyompenda Israeli, ingawa yeye ameigeukia miungu mingine” (Ho.3:1). Tunapotenda dhambi tunakosa uaminifu kwa Mungu. Ubaya wa kukosa uaminifu kwa Mungu ni sawa na kuzini, hivyo Israeli alizini kwa kumwacha Mungu na kuitumikia miungu mingine. Na sisi kila tunapotenda dhambi tunakosa uaminifu kwa ahadi zetu za ubatizo tulizoziweka mbele za Mungu, maana yake tunazini. Ndiyo maana mwanamume hakuletwa katika tukio hili la kufumaniwa, ili kutuonyesha kuwa sisi sote tu wazinifu kwa dhambi zetu mbele za Mungu. Huyu mwanamke ni ishara tu ya Israeli aliyeasi na ni ishara kwetu sote tunaoishi katika dhambi. Hivyo kila tunapotenda dhambi tunakuwa sawa na huyu mwanamke na hivyo tunapswa kupigwa kwa mawe mpaka tufe. Lakini lengo la Mungu kutuumba si kutuangamiza bali kutushirikisha uzima wa milele. Thamani ya uhai wa mwanadamu ni kubwa mno na iko mikononi mwa Mungu peke yake. Ndiyo maana kwa upendo, Mungu aliamua kumtoa mwanae wa pekee ili atudhihirishie thamani ya tunu hii. Yesu mwenyewe alikubali kuutoa uhai wake, tena kwa hiari ili afe kwa ajili yetu sisi tuliostahili kufa. Alikubali kufa kwa hiari kifo cha Msalabani ili kwamba kusiwepo tena adhabu za vifo.

Kifo cha Yesu Kristo ni ishara na alama ya kukomesha hukumu za vifo. Lakini bado vifo na mauaji ya watu wasio na hatia yanaendelea. Katika ulimwengu wetu wa sasa dhamani ya mwanadamu ni ndogo kuliko vitu. Mwanadamu anatumiwa na vitu vinapendwa. Ni watoto wangapi wanauwa kwa utoaji mimba na hata wengine waliokwisha kuzaliwa wanatupwa, watu wangapi wanahukumiwa kunyongwa katika mahakama zetu, wangapi wanauwa kwa sababu za ushirikina na uchawi, na ni roho ngapi zinaangamizwa katika vita na ugaidi. Hii haimaanishi kuwa kifo cha Kristo msalabani hakikuwa na nguvu, bali ni kwasababu mioyo yetu imefungwa wala haijaguswa bado kwa kifo chake na hivyo hili fundisho bado hatujalielewa. Imani yetu juu ya nguvu ya mateso, kifo na ufufuko wake ni haba. Hatuamini. Lakini tukichunguza vyema dhamiri zetu, tutatambua kuwa ni kwa sababu tu wazinzi na tutaona hitaji la kuondoka mmoja mmoja kwenda kutubu. Tuepuke tabia ya kufurahia na kuyatangaza makosa ya watu wengine kwani yaweza kuwa sisi ni wakosaji zaidi kuliko wale tunaowatangaza vibaya na kuwachafulia majina yao.

Huruma ya Mungu itusaidie kupyaisha maisha, wito na utume wetu.
Huruma ya Mungu itusaidie kupyaisha maisha, wito na utume wetu.

Badala ya kuwahukumu wengine tuanze kujirudi na kutubu dhambi la sivyo sisi tutakuwa wanafiki kama Mafarisayo. Tunaalikwa kutowahukumu wengine na kutojihukumu wenyewe bali kufanya toba ya kweli. Wakati mwingine tukiangalia historia ya maisha yetu tunajiona sisi hatuna thamani yoyote. Kabla watu hawajatupiga kwa mawe, sisi wenyewe tunajipiga kwa mawe. Tunaona kabisa Mungu hawezi kutusamehe. Tuwe na ujasiri wa kusema kama Mtume Paulo; “Nayasahau ya zamani nikichuchumilia yaliyo mbele, nisiwe na haki yangu mwenyewe ipatikanayo kwa sheria bali ile ipatikanayo kutoka kwa Mungu kwa Imani”. Paulo alitambua kuwa akijiangalia alivyolitesa Kanisa kwa kuwaua wakristo asingeweza kuhubiri injili, lakini kwa imani anatambua kuwa “nguvu ya kufufuka kwa Kristo imemkomboa”. Tusikate tamaa. Tunaalikwa kuanza maisha mapya yasiyo na dhambi, maisha ya uadilifu. Tusifikiri kuwa kipindi cha Kwaresma ni kipindi cha kuacha kwa muda matendo maovu ambayo tutayaendeleza baada ya kumaliza kipindi hiki. Tubadilike kabisa toka ndani. Tumepewa onyo la kutoendelee kuishi katika dhambi wala mimi sikuhukumu, nenda zako usitende dhambi tena. Tuwaoneshe huruma wale wote waliokata tamaa kutokana na kuishi katika dimbwi la dhambi za kukatisha uhai wa wengine. Tuwatie moyo tusiwalaumu na kuwahukumu bali tuwasaidie waweze kutambua dhamani ya uhai na ya huruma ya Mungu na kufanya toba ya kweli ili mwisho wa yote tuweze kupata tuzo la uzima wa milele.

Huruma na Msamaha
31 March 2022, 16:33