Dominika ya IV ya Kwaresima: Wahudumu Wa Huruma ya Mungu!
Na Padre Efrem Msigala, OSA, - Roma.
Karibu mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican katika tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya nne ya Kipindi cha Kwaresima, Mwaka C wa Kanisa. Tunaongozwa na Sehemu ya Maandiko Matakatifu kutoka: Yoshua 5:9-12, 2Kor.5:17-21, Injili Lk.15:1-3,11-32. Masomo ya Dominika ya 4 ya Kwaresima ya Mwaka C yanatukumbusha kwamba Mungu anatungoja siku zote tumrudie ili tuweze kupokea uzima wa milele. Ujumbe wa: Upendo, Huruma na Msamaha wa Mungu. Leo ni Dominika ya nne ya Kwaresima dominika ya furaha. Dominika nyeupe. Maneno ya mwanzo wa Misa yanasema “Furahini, ee Yerusalemu, nanyi nyote mmpendao...” Masomo pia yanaonyesha furaha kwa nafasi mbalimbali. Nasi tunafurahia ile furaha ya maisha ya uzima wa milele inayopata chimbuko lake kutoka katika mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu.
Somo la kwanza linaeleza jinsi Waisraeli walivyosherehekea Pasaka kwenye uwanda wa Yeriko. Katika somo la pili Paulo anatuambia tupatanishwe na Mungu. Na katika injili, Yesu anasimulia mfano wa mwana mpotevu, na furaha kurudi kwake. Mpendwa msikilizaji: Waisraeli walisafiri kwa miaka arobaini jangwani wakikumbana na changamoto mbalimbali. Somo la kwanza kutoka katika Kitabu cha (Yoshua 5:9-12), hatimaye Waisraeli, walifika kwenye Nchi ya Ahadi, si tena chini ya uongozi wa Musa (aliyekufa tayari), bali chini ya uongozi wa Yoshua. Walisherehekea Pasaka yao ya kwanza katika Nchi ya Ahadi. Katika somo la pili, Waraka wa Pili wa Mtume Paulo kwa Wakorintho (5:17-21) inazungumza moja kwa moja kuhusu upatanisho ikisema: “Na hayo yote yatoka kwa Mungu, aliyetupatanisha sisi na nafsi yake kwa Kristo, akatupa huduma ya upatanisho, yaani, Mungu alikuwa akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake katika Kristo, asiwahesabie makosa yao, akiweka kwetu ujumbe wa upatanisho.” Kisha anatusihi akisema: “Twawasihi ninyi kwa ajili ya Kristo mpatanishwe na Mungu.”
Injili ya Luka inaelezea Mfano wa Mwana Mpotevu. Ni hadithi ya Yesu kuhusu mwana ambaye aliamua kuchukua njia inayoongoza kwenye anasa lakini mwishowe mahangaiko. Hata hivyo mahangaiko yalimpa fursa ya kujitafiti yuko katika hali gani na afanye nini. Alipotambua hali yake mbaya, alirudi kwenye fahamu zake na kuamua kurudi kwa baba yake, kuomba msamaha. Baba alimpokea kwa furaha na kufanya sherehe kwa kurudi kwake mzima. Baba anahuruma na upendo usio na mipaka. Baba aliwapenda sana wanawe. Baba alikuwa na hamu ya kumrudisha mikononi mwake, mtoto aliyetoka nyumbani kwenda alikojua yeye. Alipenda kumrudisha mahali pake panapofaa katika nyumba yake.
Mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican: Injili ya Luka sura ya 15 yote inaeleza mafundisho ya Yesu kuhusu utafutaji wa Mungu kwa wenye dhambi. Anatoa mifano mitatu ili kufafanua hili kama maelezo yake ya kwa nini alikuwa akishirikiana na watoza ushuru na wadhambi. Hayo anatoa baada ya kusikika manung’uniko ya mafarisayo na waandishi waliojiona wao ndiyo wenye haki zaidi kuliko watoza ushuru na wengine, waliojulikana kuwa wa dhambi. Mfano wa kwanza ni kuhusu Kondoo aliyepotea; wa pili ni kuhusu Sarafu Iliyopotea; na wa tatu ni kuhusu Mwana Mpotevu. Mifano hii yote lengo nikuelezea ukweli mmoja Mungu mwenye huruma na upendo. Katika injili tumesikia leo mfano ule watatu wa Mwana mpotevu. Aliyetaka uhuru, akaenda kuishi maisha yake mbali na familia yake. kumbe kijana mkubwa alishi pamoja na baba muda wote. Mwishowe Yesu anaonesha kuwa wote ni wadhambi. Mdogo alitambua kosa lake na kutubu, ndiyo watoza ushuru na wadhambi wengine waliosikiliza mafundisho ya Yesu na kujipatanisha naye. Mkubwa aliyebaki nyumbani muda wote lakini kumbe hakutambua upendo wa baba anakuwa na chuki, wivu, hasira, mwenye kuzira na kujiona yeye mwenye haki kuliko wengine. Yesu anamfananisha na mafarisayo na waandishi. Ni Wenye kujiona wenye haki na hawaoni sababu ya kutubu lakini wamebaki katika dhambi.
Mpendwa msikilizaji, maneno haya ya mwana mpotevu yatuguse katika maisha yetu kupokea sakramenti ya kitubio: “Nimemkosea Mungu. Nitaondoka na kwenda kwa Baba.” Nitumie nafasi hii kukumbusha mapadre wenzangu kuwa mtu anayekuja kwa ajili ya kuungama tayari ameguswa na neema ya Mungu. Ukweli tu kwamba ametambua dhambi yake na anaona haja ya kwenda kuungama. Kwa hiyo, makasisi tunapaswa kuwahudumia kwa ukarimu wenye kutubu. Inasikitisha sana mwenye nia ya kutubu anapohitaji huduma hiyo, padre anasema hana nafasi aende siku nyingine na wakati huo huyu mtu amefunga safari toka mbali na mhudumu anasema hivyo na hana jambo la pekee ambalo linamfanya asitoe huduma, bali ni kwa sababu ya uvivu na ubinafsi. Wakati mwingine maparokiani hatutoi fursa ya watu kupokea sakramenti ya kitubio. Natukitoa hiyo Sakramenti ni haraka haraka ingawa si wote wanafanya hivyo. Wakati mwingine watu wanahitaji mafundisho na ushauri wafanye nini kuepukana na dhambi, pia wanahitaji kusikilizwa nao pia wasikilize mafundisho toka kwa padre. Na wakati mwingine tunarahisisha sana kiasi kwamba tunawakwaza waamini. Wakati mwingine parokiani tumeweka ratiba siku za maungamo lakini hatuonekani. Leo tunakumbushwa na mfano wa mwanampotevu kuthamini na kujali kutoa hii Sakramenti ya kitubio na kuwa waangalifu.
Hata hivyo tuwaombee mapadre wetu waweze kutumia upadre wao kuwa uso wa huruma na upendo wa Mungu. Tuwaombee pia kwani pia wanakumbana na changamoto nyingi katika utume wao. Pamoja na hayo mpendwa msikilizaji, dhambi kimsingi ni ubinafsi. Hili liko wazi kabisa katika mtazamo wa mwana mpotevu. Hakumfikiria mtu mwingine yeyote. Alijifikiria tu nafsi yake. Kuchukua urithi wake wakati baba yake angali hai kwa lenyewe si jambo la kawaida nikutakia mabaya baba yake. Kwa maneno mengine urithi hutolewa kwa watoto baada ya baba kufariki. Hivyo mwanampotevu tungesema kwa kutaka urithi ni sawa na kumwombea baba yake kifo. Lakini baba yake hakumkatalia alimpa sehemu yake na akamwacha atumie uhuru wake. La muhimu ni kwamba alipata sehemu yake ya mali, yeye akaona aende atumie anavyotaka. Lakini hakutumia pesa ipasavyo. Alitapanya kila kitu kwa maisha ya anasa ya muda mfupi. Mwana mpotevu ni picha ya kila mmoja wetu tunapokuwa wabinafsi. Hatufikirii mtu mwingine yeyote. Hata hatufikirii juu ya Mungu. Tunachofuata ni kuridhika na tamaa zetu za ubinafsi. Matokeo yake tunajiumiza wenyewe. Ubinafsi hautufanyi tuwe na furaha, bali mahangaiko. Dhambi haitufanyi tuwe na furaha bali inatuangamiza tu, kama kutu inavyokula polepole chuma.
Mpendwa msikilizaji: katika mfano wa Yesu, mwana mpotevu - alipoteza kila kitu. Lakini angalau alipata ufahamu na kurudi kwa baba yake. Alikubali makosa yake kwa unyenyekevu, na hata alikuwa tayari kutendewa kama mfanyakazi na si kama mwanaye. Alijua kwamba alichofanya kilimfanya asistahili kupendwa na baba yake. Alikuwa na toba ya kweli na unyenyekevu ndani yake. Kumbe kwa upande mwingine, mwana mkubwa alikuwa mbaya zaidi. Ni kweli, hakutapanya pesa za baba yake, na hata hakutoka nyumbani. Lakini hakuwa na upendo wa dhati ndani yake. Alikuwa ndani ya nyumba ile lakini hakuhisi kabisa kuwa ni wa nyumba hiyo. Ndiyo sababu baba yake alilazimika kumkumbusha hivi: “Mwanangu, wewe uko pamoja nami siku zote; kila nilicho nacho ni chako.” Alikuwa na kiburi, tena asiyejali. Wakati akizungumza na baba yake, alimtaja mdogo wake kama yeye hamhusu akasema “huyo mwanao". Haoni kama ni mdogo wake na ndugu wa damu. Hakufanya juhudi yoyote kumtafuta mdogo wake. Na matokeo yake alichukizwa kuona amerudi na amekaribishwa kwa furaha na kufanyiwa sherehe. Yeye akazira hata kuingia ndani. Pengine nasi ni kama mwana mkubwa, ni wabinafsi tunashindwa kuwasaidia wengine kumrudia Mungu. Tunapokuwa na wivu pale tunapoona watu ambao walikuwa kama mwanampotevu wanarudi katika Kanisa. Na matokeo yake tunakosa furaha ya kweli kwa sababu hatuna upendo. Wakati huu wa Kipindi cha Kwaresima ulete mabadiliko ya kweli ndani yetu, tunaposhuhudia mfano wa mwana mpotevu.