Alhamisi Kuu: Ekaristi Takatifu, Daraja Takatifu na Upendo
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Neno la Mungu, siku ya Alhamisi Kuu, siku ya kwanza kati ya siku Kuu tatu za kuadhimisha Fumbo la Wokovu wetu, Pasaka - Mateso, Kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Hili ni adhimisho Kuu moja linalodumu kwa muda wa siku tatu - Alhamisi Kuu, Ijumaa Kuu na Jumamosi Takatifu na sio maadhimisho matatu yanayotofautiana. Siku ya Alhamisi Kuu, Kanisa linaadhimisha mambo makuu matatu, kuwekwa kwa; Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, Sakramenti ya Daraja Takatifu na Amri Kuu ya Upendo kama anavyosali Padre kwa niaba ya jamii ya waamini katika sala ya mwanzo: “Ee Mungu, tunaadhimisha Karamu takatifu ya Mwanao wa pekee. Yeye alilikabidhi Kanisa kwa siku zote sadaka mpya na karamu ya upendo wake. Tunakuomba utujalie, tujipatie wingi wa mapendo na uzima katika fumbo hili kubwa.” Fumbo Kuu la Pasaka tunaloliadhimisha linaanza rasmi na adhimisho hili la Karamu ya Mwisho, mlo aliokula Yesu na wanafunzi wake 12, kabla ya kukamatwa, kuteswa, kusulubiwa na kufa msalabani. Kumbe Alhamisi Kuu, ndiyo siku inapoanza Pasaka ya Kikristo (Mt 26: 26-29; Mk 14: 22-25; Lk 22: 15-20). Tukumbuke kuwa Alhamisi Kuu ni siku ya mapadre tuwaombee na kuwaenzi kwa kuwapongeza. Somo la kwanza la kitabu cha Kutoka (Kut 12:1-8, 11-14); linasimulia mwanzo, namna na masharti ya sikukuu ya Pasaka ya kwanza kwa Wayahudi walipokombolewa kutoka utumwani Misri, sherehe ambayo walipaswa kuiadhimisha kwa vizazi vyote (Kumb.12:14). Mlo wa sherehe hii ya Kipasaka ulifanyika kifamilia.
Masharti: walipaswa kuchagua mwana-kondoo au mwana-mbuzi mume wa mwaka mmoja, asiye na hila, walipaswa kumchinja jioni, siku ya kumi na nne ya mwezi, damu yake walipaswa kuitia katika miimo miwili na katika kizingiti cha juu, katika zile nyumba walizomla, walipaswa kuila nyama yake usiku ule ule, imeokwa motoni, pamoja na mkate usiotiwa chachu, na mboga zenye uchungu. Walipaswa kumla kwa haraka, wakiwa wamefungwa viuno vyao, wamevaa viatu miguuni, na fimbo mikononi, tayari kwa safari ndefu ya kuelekea nchi ya ahadi kwa mkono wa Mungu chini ya kiongozi wao Musa. Sherehe hii ya Pasaka, Wayahudi walipaswa kuisherehekea kila mwaka, kukumbuka mambo makuu aliyowafanyia Mungu. Pasaka hii ya Wayahudi ilikuwa ni dokezo la Pasaka yetu - wokovu ulioletwa na Kristo: Mwanakondoo wa Mungu, aliyejidhabihu msalabani, akajitoa kama chakula chetu cha kiroho katika karamu ya mwisho siku ya Alhamisi Kuu, katika juma la Pasaka ya Wayahudi ambapo Yesu na wanafunzi wake waliadhimisha sikukuu hiyo kwa mlo huu wa Kipasaka. Lakini mlo huu ni tofauti na ule waliokula wayahudi. Kristo ndiye Mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi za ulimwengu, hivyo hawakuwa na haja ya kuandaa na kuchinja mwanakondoo. Tendo lilelile la karamu siku ya Alhamisi Kuu na kifo cha msalabani Siku ya Ijumaa Kuu linaendelezwa na Kristo katika Sadaka ya Misa Takatifu iliyo karamu na sadaka ileile ya Kristo.
Somo la pili la Waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Wakorintho (1Kor 11:23-26); linatueleza kuwa Ekaristi Takatifu hutuunganisha wakristo wote kuwa ndugu. Pia kila tunapokula vema karamu hii tunashiriki na kutangaza kifo na ufufuko wake Kristo. Paulo anatuambia kuwa; “Bwana wetu Yesu Kristo, usiku ule aliotolewa alitwaa mkate, naye akiisha kushukuru akaumega, akasema; Huu ndio mwili wangu ulio kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu. Na vivi hivi baada ya kula akakitwaa kikombe, akisema; Kikombe hiki ni Agano Jipya katika damu yangu; fanyeni hivi kila mnywapo kwa ukumbusho wangu (1Kor.11:23-25). “Maana kila mlapo mkate huu na kukinywea kikombe hiki mwaitangaza mauti ya Bwana hata ajapo” (1Kor 11:26). Namna hii Yesu aliweka Ekaristi Takatifu, chakula chetu cha kiroho. Katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu Yesu yupo mzima, mwili wake na Damu yake, ubinadamu na Umungu wake katika maumbo ya mkate na divai. Amefanya hivyo ili akae nasi, tuongee naye, tumueleze hali zetu, shida zetu, matatizo yetu, furaha na huzuni zetu. Yupo nasi katika Neno lake, yupo nasi katika Ekaristi, yupo nasi katika Makasisi wake, yuko tayari kutusikiliza wakati wote. Ndiyo maana Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican unatufundisha kuwa; Kila Sadaka ya Ekaristi inapoadhimishwa, kazi ya ukombozi wetu inafanyika kwa ukamilifu wake (SC 2). Huu ndio utajiri tulionao katika Ekaristi Takatifu kwamba tunasamehewa dhambi zetu na kurudishiwa uhusiano na urafiki wetu na Mungu katika Sadaka ya Misa Takatifu. Ekaristi Takatifu, hutuunganisha na Kristo, hudhoofisha nguvu ya dhambi na ni amana ya uzima wa milele. Kwa hiyo, tuipende Ekaristi Takatifu, tushiriki maadhimisho ya Misa Takatifu na kupokea Ekaristi Takatifu kwa kustahili. Hii ndiyo amana aliyotuachia Yesu Kristo siku ya Alhamisi Kuu.
Injili kama ilivyoandikwa na Yohane (Yoh. 13:1-15) inamwonesha Yesu akiingia saa ya mateso na kifo chake kwa moyo mtulivu na kwa kutaka yeye mwenyewe. Alifanya hivi ili kuonyesha mapendo yake makuu kwa wanadamu wote. Kabla ya yote baada ya kula mlo wa mwisho, aliwaosha wanafunzi wake miguu, alama ya utumishi wake wa mapendo uliotimizwa kikamilifu msalabani. Kwa tendo hili la kuwaosha miguu wanafunzi wake, Yesu alituachia wosia, wosia wa kupendana; “Pendaneni kama mimi nilivyowapenda ninyi”. Yesu anatoa mfano ulio rahisi, lakini mgumu mno kuuelewa. Yeye aliye Bwana na mwalimu, mfalme, masiha, mwokozi, Mungu kweli katika nafsi ya pili, anajishusha, anajinyenyekeza, kwa upendo na utii mkubwa anawaosha wanafunzi wake miguu. Kisha anawaambia; “Kama mimi niliye mwalimu nimefanya hivi, ninyi nanyi fanyeni vivyo hivyo”. Tunapaswa kupendana kama Kristo alivyotupenda. Upendo ni utambulisho wetu, - “mkipendana ninyi kwa ninyi watu watawatambua kuwa mu-wafuasi wangu”. Kupendana ni kukaa ndani ya Kristo na kulishika neno lake; “Kaeni ndani yangu, nami nikae ndani yenu” (Yn.15:4), “mtu akinipenda atalishika neno langu, na Baba yangu atampenda nasi tutakuja kwake na kukaa naye” (Yn. 14:23).
Kwa tendo la kuwaosha Mitume miguu, Yesu aliwasimika kuwa makuhani/mapadre kwa ajili ya kutolea dhabihu na sadaka kwa Mungu katika maadhimisho ya Sadaka ya Misa Takatifu kama ilivyokuwa desturi katika Agano la Kale kwa makuhani kuoshwa miguu kabla ya kumtolea Mungu dhabihu - “Mwenyezi Mungu akamwambia Musa; “Utatengeneza birika la shaba la kutawadha lenye tako la shaba uliweke katikati ya hema la kukutania na madhabahu, na kutia maji ndani yake. Aroni na wanawe watatumia maji hayo kunawia mikono na miguu kabla ya kuingia kwenye hema la kukutania au kukaribia madhabahu ili kunitolea dhabihu mimi Mwenyezi Mungu…hii itakuwa kanuni kwao daima, tangu Aroni na uzao wake, vizazi hata vizazi” (Kut.30:17:21). Tujikumbushe thamani na umuhimu wa Padre katika maisha yetu. Padre ni mtu ambaye amejitoa maisha yake kwa ajili ya kuwahudumia watu. Padre ni mwanadamu aliyetwaliwa kati ya watu kwa mambo yamuhusuyo Mungu (Ebr. 5:1-4). Padre ni kuhani. Padre ni Kristo mwingine. Padre ni mwezeshaji na mtagulizi kwa mambo ya imani naye yuko na taifa la Mungu nyakati zote, kipindi cha kuzaliwa na kufa, wakati wa furaha na huzuni. Katika uchanga wetu, Padre yupo ili apate kutubatiza. Kwa uwezo aliopewa na kwa mikono yake, dhambi ya asili inaondolewa, na mbatizwa anafanywa kuwa mtoto mteule wa Mungu na wa Kanisa.
Katika uchipukizi na ujana wetu, Askofu hutupatia Sakramenti ya Kipaimara ambayo kwayo tunajazwa mapaji ya Roho Mtakatifu ili tuwe askari amini wa Kristo. Kila siku Padre hutupatia Ekaristi Takatifu kwa ajili ya ustawi wa roho zetu. Tunapokuwa wadhambi, tumezama katika dimbwi la utumwa wa shetani, sauti tulivu ya Padre yenye nguvu ya Mungu inatufariji ikituambia; “Nenda na amani umesamehewa dhambi zako.” Maneno haya humfukuza shetani na kutupatia utulivu na amani rohoni mwetu. Padre hubariki na kushuhudia makubaliano ya mume na mke wanapoahidi uaminifu katika sakramenti ya ndoa. Familia mpya, kiini msingi cha jumuia kanisa la nyumbani na shule ya awali, inapata baraka ya Mungu na kukua katika misingi ya imani kwa malezi elekezi ya Padre. Padre huunganisha jitihada zake na za wazazi katika kuelimisha watoto katika mambo ya imani na kuwaandaa kupokea Sakramenti. Padre hachoki, hata wakati wa magonjwa tayari yuko karibu nasi akitupatia Mpako Mtakatifu kwa kututuliza, kutuimarisha na kutuponya na udhaifu wa kimwili na kiroho. Tukifa tuna muunganiko na Kristo, kwenye mazishi yetu Padre yupo tayari kupumzisha miili yetu.
Na kila siku katika Misa Takatifu husali kwa ajili ya roho za marehemu walioko toharani. Palipo na huzuni Padre huleta furaha, pasipo na haki hutetea haki, kwa vijana huwatia moyo na kuwafundisha fadhila mbalimbali, utii, uaminifu, moyo wa uwajibikaji na heshima kwa watu na kwa Mungu. Huwakumbusha matajiri juu ya wajibu wao wa kuwasaidia wahitaji na waajiri kulipa ujira unaostahili. Huyu ndiye Padre. Hali ya kibinadamu ni hali ya unyonge, uchovu, kushawishika kukata tamaa. Ndivyo ilivyo pia kwa padre. Hivyo ni wajibu wa waamini kuwasaidia katika ubinadamu wao ili waweze kusimama imara katika kulihudumia taifa la Mungu. Tuwapende mapadre, tuwaombee mapadre, tuwafariji mapadre, tuwatie moyo mapadre ili wawe na nguvu ya kutuhudumia vizuri, pia tusali kuombea miito mitakatifu katika Kanisa ili tupate mapadre wema na waaminifu wanaojitahidi kumfuasa Kristo. Mwisho, Kanisa limeweka utaratibu wa kukesha na kuabudu Ekaristi Takatifu Siku ya Alhamisi Kuu baada ya Misa ili kukaa pamoja na Yesu, tukitafakari upendo wake kwetu sisi, upendo ambao alioudhihirisha katika kujitoa kwake Sadaka msalabani na sasa yupo Ekaristi Takatifu. Tutumie vema muda huo kumwabudu na kumshukuru Kristo kwa zawadi ya ukombozi na tumwombe neema ya kuweza kuwa waaminifu katika maisha yetu ya kiimani.