Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Upendo unaomwilishwa katika huduma makini kwa watu wa Mungu kama ilivyokuwa kwa Kristo Siku ile ya Alhamisi Kuu. Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Upendo unaomwilishwa katika huduma makini kwa watu wa Mungu kama ilivyokuwa kwa Kristo Siku ile ya Alhamisi Kuu. 

Ekaristi Takatifu Ni Sakramenti Ya Upendo Katika Huduma Kwa Watu

Kati ya majina mengi yanayoitambulisha Sakramenti ya Ekaristi Takatifu ambayo Mama Kanisa anatualika leo kukumbuka siku ile ya kuwekwa kwake rasmi, jina la “kuumega mkate”, linabeba maana kubwa na nzuri kwetu mintarafu ujumbe wa Adhimisho la Ekaristi Takatifu na amri kuu ya Upendo tunayosisitiziwa kuyatafakari leo. Hii ni kumbukumbu endelevu ya upendo wa Yesu.

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma

Amani na Salama! Kati ya majina mengi yanayoitambulisha Sakramenti ya Ekaristi Takatifu ambayo Mama Kanisa anatualika leo kukumbuka siku ile ya kuwekwa kwake rasmi, jina la “kuumega mkate”, linabeba maana kubwa na nzuri kwetu mintarafu ujumbe wa Adhimisho la Ekaristi Takatifu na amri kuu ya Upendo tunayosisitiziwa kuyatafakari leo. Wanafunzi wa Emau walimtambua Kristo Mfufuka katika Kuumega mkate, (Luka 24:35) Wanafunzi wa jumuiya zile za kwanza walidumu katika kushika mafundisho ya Mitume na katika kuumega mkate. (Matendo 20:7). Ilikuwa pia katika tamaduni za Kiyahudi kila mara walipokutana kwa mlo, kwanza walibariki na pili kuumega mkate na ndipo mkubwa wa meza akaweza kuugawa kwa wote walioshiriki pale mezani. Tangu utoto wake Yesu alishuhudia na kukuzwa katika tamaduni hiyo. Mpaka sile ile iliyotangulia mateso yake, ndio naye alitwaa mkate, na kuubariki, na kuumega, na kuwapa wanafunzi wake, na hapo ndio anabadili maana ya mazoea yale, siyo tena mkate bali ni Mwili wake, sio tena divai bali ni Damu yake inayomwagika kwa ajili ya Wokovu wa ulimwengu mzima.

Sehemu ya Injili takatifu kama ilivyoandikwa na Mwinjili Yohane inatuacha tunabaki na mshangao, kwani hatuoneshi jinsi Yesu alivyoiweka rasmi Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, tofauti na masimulizi ya Injili Pacha zenye mwono unaofanana, yaani zile za Wainjili Marko, Matayo na Luka. Hotuba ya Yesu katika karamu ile ya mwisho anatenga sura tano yaani (Yohane 13-17), lakini bila kuonesha waziwazi jinsi Yesu alivyoiweka rasmi Ekaristi Takatifu, au Kuumega Mkate. Badala yake katika sura ya 6 tunaona Mwinjili Yohane anatumia sura nzima kutuelezea mafundisho juu ya Yesu kama mkate wa uzima, na pia karamu ya mwisho inachukua sehemu kidogo ya sura zile za (Yohane 13-17). Swali ni kwa nini Mwinjili hatumii muda na nafasi ya kutosha kutuelezae juu ya Sakramenti hii ya Ekaristi Takatifu ambayo leo Alhamisi Kuu tunasherekea siku ile ya kuwekwa kwake rasmi?  Hakika haikusahaulika na wala si lengo la Mwinjili Yohane kuiacha kwa bahati mbaya na badala yake kwa kuangalia tukio ambalo Mwinjili analielezea unaweza kupata maana na sababu za swali letu.

Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Upendo katika huduma
Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Upendo katika huduma

Badala ya simulizi la kuwekwa rasmi Ekaristi Takatifu, Mwinjili Yohane anatupa simulizi la Yesu kuwaosha miguu wanafunzi wake. Tukio hilo linaachwa na Wainjili ndugu, ila tunaona ni Mwinjili Yohane analipa kipaumbele na umuhimu mkubwa. Ni lengo la Mwinjili Yohane kwa jumuiya anayowaandikia kuwaonesha kuwa kuosha miguu na kusimikwa kwa Ekaristi Takatifu ni matendo yanayoshabihiana na yenye maana moja. Si rahisi kuelewa maana ya moja kati ya haya matendo mawili pasipo kulihusianisha na lingine. Kuosha miguu ni udhihirishaji wa kuumega mkate, ni tukio linaloonesha maana ya mfuasi wa Yesu Kristo kushiriki meza ile ya Mwili na Damu yake Kristo katika Ekaristi Takatifu. Ilikuwa karibu na Sikukuu ya Pasaka ya Wayahudi, ambapo walikumbuka Ukombozi wao kutoka utumwani Misri. Ni wakati huo huo pia Yesu anajiandaa kwa Pasaka yake, yaani kuukomboa ulimwengu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Ni kutoka kwake kutoka ulimwengu huu na kurudi kwa Baba yake, hivyo alipaswa kushiriki katika kina cha maji na giza la mateso na kifo ili kutupeleka sote katika uhuru wa kweli, yaani kuwa warithi pamoja na Mwana pekee.

Ni wakati wa ile saa yake, ambayo mara nyingi Mwinjili Yohane amekuwa akiizungumzia katika Injili yake. Katika harusi ya Kana (Yohane 2:4), alipogusia kuwa saa yake ilikuwa bado. Hata walipotaka kumkamata pale Yerusalemu walishindwa kwa kuwa saa yake ilikuwa bado. (Yohane 7:30; 8:20) Siku chache kabla ya mateso yake, Yesu anazungumzia juu ya kufika kwa saa yake. (Yohane 12:23,27). Saa yake ndio muda ule wa neema (Kairos) aliyoingojea kwa hamu na shauku kubwa, ni saa ile ya kuwapenda watu wake upeo, hivyo anajitoa yeye mwenyewe kama sadaka kwa ajili ya Wokovu wa ulimwengu. Saa yake ndio saa ya Wokovu, ndio saa ya upendo wake kwa ulimwengu mzima. Mwinjili Yohane anaonesha juu ya Uungu wa Yesu, ndiye yeye aliyetoka kwa Mungu na kwa Mungu anarejea. Ndiye yeye anayejishusha na kujinyenyekeza kiasi cha kufanyika mtumwa, Mwana pekee ambaye kwa kumuona Yeye ni sawa na kumuona Baba. (Yohane 14:9). Kwa desturi kabla ya kula milo ya Kipasaka, Wayahudi wachamungu walitawaza kwa maji safi. Kuanzia mkubwa wa meza mpaka kijana mdogo pale mezani walioshwa mikono na mtumishi na kama hayupo basi aliye mdogo kuliko wote aliweza kufanya utumishi huo wa kuwaosha mikono wakubwa.

Wakati wa karamu ile ya mwisho kikatokea kitu au jambo ambalo halikuweza kufikirika kati yao. Mbele ya Mitume wake, Yesu anasimama na kuvua mavazi yake na kujifunga kitambaa kiunoni mwake, na kuchukua chombo chenye maji, na kuanza kuwaosha miguu wanafunzi wake, na kuwakausha kwa mithiri ya taulo alilojifunga kiunoni mwake. Yote yanafanyika kukiwa na ukimya mkubwa. Wanafunzi wake walibaki kimya na hasa wakibaki na mshangao mkubwa, hivyo hawaamini wanayoyaona kwa macho yao. Yesu anafanya kama walivyokuwa wanapaswa kufanya watumwa au watumishi, na si tu anawaosha mikono bali anawaosha miguu, ni kujishusha na kukubali kuwa na hadhi hata chini zaidi ile ya mtumwa na kijakazi. Yesu aliye Mwana wa Mungu, aliye Mungu anajishusha na kuwa mtumwa kwa wanafunzi wake. Wanafunzi wake wanabaki na mshangao mkubwa. Walikuwa na Yesu kwa miaka mitatu, walimtambua kama Kristo, na walikuwa wanangoja kwa hamu ili atawale kama ambavyo walitegemea Masiha kuwa mtawala kama watawala wa ulimwengu huu.  (Zaburi 72:8-11). Ni katika karamu ile ya mwisho, tunaona mategemeo na matarajio yao yanafika ukomo na kufifishwa, ni Yesu anawafunulia kinagaubaga juu ya umasiha wake.

Ekaristi Takatifu ni kumbukumbu endelevu ya uwepo wa Kristo Yesu kati ya waja wake.
Ekaristi Takatifu ni kumbukumbu endelevu ya uwepo wa Kristo Yesu kati ya waja wake.

Ni katika kitendo cha kuwaosha miguu wanapata sasa kumtambua kuwa huyu ni mtumwa, ni mtumishi na si mtawala kwa mantiki ya ulimwengu huu. Huyu ndio Mungu kweli, Mungu anayekuwa mtumwa kwa mwanadamu, ni Mungu anayemtafuta na mwenye kiu ya kuwa na mahusiano mema na mwanadamu. Kinyume chake ni miungu tunayojiundia kichwani na hivyo kuwa mbali na sura halisi ya Mungu, wengi wetu tangu tukiwa watoto wadogo, labda kwa mafundisho au masimulizi tumejenga picha mbali mbali za Mungu, lakini ni katika kitendo cha kuosha miguu tunakutana na sura halisi ya Mungu. Mungu anayekuwa na kiu na mwanadamu, anayejishusha ili mwanadamu aweze kupata hadhi ya Kimungu. Ni Mungu anayetupenda upeo, ni Mungu anayekuwa wa kwanza kumsogelea na kuunda urafiki na mwanadamu! Sasa tunaweza kuelewa kwa nini Mwinjili Yohane anatoa nafasi na uzito mkubwa kwa tukio hili la kuoshwa miguu. Ni katika tukio hili kama nilivyotangulia kusema tunakutana na sura halisi ya Mungu, Mungu anayejifanya mtumwa wa mwanadamu na si mtawala wa mabavu, anayebaki katika viti vya enzi, anayengoja mwanadamu amuabudu na kumsujudu na kushindwa kufanya hivyo basi anajawa na hasira na hivyo kumwadhibu bila huruma, kwa kweli ni taswira potofu ya Mungu ambazo tunaalikwa kubadili vichwa vyetu.

Katika tafakuri za Dominika 3 zilizopita nimerudia kusisitiza kuwa hatuna budi kuwa na sura halisi ya Mungu na hasa siku hizi ambazo ulimwengu mzima umekumbwa na hofu kubwa ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 na vita huko nchini Ukrainia. Wapo hata wahubiri wanaothubutu kusema kuwa majanga haya ni adhabu ya Mungu kwa mwanadamu, kwa kweli kusema hivyo ni kukufuru. Mungu ni upendo tusioweza hata kuutafakuri kwa akili zetu za kibinadamu. Mungu ni huruma ya kweli kwa mwanadamu! Ni mwanadamu anayeharibu na kuyaangamiza maisha yake, kwa kukosa kuwa na mahusiano sahihi na mema na Mungu na wengine. Yesu anamfunua kwetu Mungu ambaye tunakiri ni tofauti kabisa na sura ya Mungu tuliyoijenga katika akili na mioyo yetu. Mungu anayepiga magoti mbele ya mwanadamu, kiumbe wake na kumuosha miguu, na kumtumikia. Huyu ndiye Mungu tunayealikwa kumwamini na kumfuata. Hii ndio sura halisi na sahihi ya Mungu inayofunuliwa kwetu na Yesu Kristo. Ni sura ya upendo na huruma ya Mungu kwa mwanadamu, na ndio tunayoiona na kuionja katika kila adhimisho la Ekaristi Takatifu! Ekaristi Takatifu ni adhimisho la upendo na huruma ya Mungu kwetu, ni Mungu anayekuja kwetu na kukaa kati yetu kwa njia ya Neno lake na pili katika meza ile ya karamu ya upendo wake.

Ni katika mazingira haya tunaalikwa hata nasi kutafakari nafasi za sifa ambazo mara nyingi tunapenda kujichukulia, kuitwa majina ya waheshimiwa, kuanza kuonekana na kuchukuliwa kuwa ni watu wa pekee na wa muhimu zaidi kuliko wengine, watu watusalimu kwa heshima na adabu na hata kutetemeka ikibidi, kubusiwa mikono au pete mikononi na mambo mengi ya namna hiyo. Kwa kweli ni kuwa kinyume na Injili ya Yesu Kristo, kinyume na sura halisi ya Mungu anayejifanya mtumwa na kumtumikia mwanadamu. Leo tunapoalikwa pia kuwaombea makuhani, tusali na kumwomba Mungu ili makuhani wetu waweze kutambua kuwa nao wamepakwa mafuta ili kuwa wadogo kama Kristo aliye mpakwa mafuta wa kwanza, tuwaombee wavae daima vazi la udogo na utumishi katika utume wao wa kuwatumikia watu wote bila ubaguzi wala upendeleo wowote ule. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika makuhani kutambua kuwa wamepakwa mafuta ili nao wakawapake wengine mafuta ya upendo na huruma ya Mungu, ili watu wote wapate Wokofu.

Na ndio tunaona Petro anapingana na kitendo hiki cha Yesu, kwa kweli si Mtume Petro tu bali wengi hata nyakati zetu wasiokubali sura halisi ya Mungu, Mungu anayejifanya mtumwa, mdogo na duni ili kumtumikia kiumbe wake, asiyejitafuatia nafasi za mbele na sifa na kusujudiwa bali kutemewa mate na kuburuzwa na kudharauliwa. Nawaalika tunaposoma masomo ya juma kuu, basi tuyasome kwa tafakuri. Kwetu makasisi ni nafasi pia ya kuutafakari wito wetu wa kuwa sio tu Kristo mwingine au “Alter Christus”, bali sisi tunaalikwa kuwa “Ipse Christus”, kuwa Kristo Mwenyewe. Kwa sakramenti ile ya daraja tunafanyika kuwa Kristo Mwenyewe na ndio maana wakati wa mageuzi hatutamki, twaeni huu ni Mwili wa Kristo bali tunatamka twaeni huu ni Mwili wangu, twaeni hii ni Damu yangu. Na ndio hatuna budi kila mara kukumbuka wito wetu ni kuwa Kristo mwenyewe anayejishusha na kuwaosha miguu wanafunzi wake. Siku ile ya upadrisho wetu, tulifanyika kuwa Kristo Mwenyewe, hatuna budi daima kuibeba sura halisi ya Yesu Kristo, kuwa watumishi na wadogo daima katika utume na utumishi wetu, kuwa watu wa upendo na huruma kwa watu wake Mungu! Tumepakwa mafuta matakatifu ili tukawapake wengine mafuta ya upendo na huruma ya Mungu.

Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya huduma na mshikamano
Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya huduma na mshikamano

Wewe hutaniosha kamwe miguu, huu ndio msimamo wa sote tunaobaki na sura isiyokuwa sahihi ya Mungu. Yesu hashangazwi na msimamo huo wa Petro ambao pia hata leo wengi wetu bado tunao. Ni kushindwa kufikiri pamoja na Mungu bali kwa kufuata mantiki ya ulimwengu huu. (Marko 8:33), tunaalikwa kuyawaza yaliyo ya Mungu na siyo ya wanadamu. Ni mwaliko wa kubadili vichwa vyetu ili tuongozwe na mantiki ile ya Yesu Kristo, ya udogo na utumishi kwa wengine. Yesu anamtahadharisha Petro kuwa kama hatakubali basi hatakuwa na shirika naye. Yesu anamwalika Petro kutozuia mpango wa Mungu wa kujifunua kwa watu wake. Ni tukio lenye katekesi kubwa ndani yake. Ni fundisho kwa vitendo, ni Mungu anayejifunua na kutuachia somo au fundisho sisi wafuasi wake. Ni Yesu anamwalika Petro na hata nasi leo kubadili vichwa vyetu, kukubali mantiki yake ya Kimungu. Kuokolewa ni kukubali mpango wa Mungu katika maisha yetu, kama tunavyosoma katika Waraka wa Mtume Paulo kwa (Wafilipi 2:5-8), ni kukubali kujishusha, kuwa ardhini na huo ndiyo unyenyekevu tunaoalikwa kuwa nao sisi wanafunzi wa Yesu. Safari ya Kwaresima tuliyoianza siku ile ya Jumatano ya Majivu inatualika kutambua wito wetu, kuwa wadogo na watumishi daima, kutambua uduni na unyonge wetu siku zote katika kumwelekea Mungu. Baada ya mazungumzo na Petro, tunaona Mwinjili Yohane anatueleza hata matendo madogo madogo aliyoyafanya Yesu katika tukio la karamu ya mwisho. Hivyo sasa anavaa tena mavazi yake na kuketi tena. Hivyo ndio kusema kila kitendo hata kama tunaweza kuona kwa nini anakitaja ni mwaliko kujua kuwa vyote vinabeba ujumbe.

Yesu alivua mavazi yake kwani kwa watumwa ili kuweza kutoa huduma kirahisi walipaswa kuvaa mavazi machache na yasiokuwa marefu. Na ndio Yesu anavua kabla ili kuwa sawa na watumwa na kufanya kile wanachofanya watumwa wanapotumikia mabwana wao. Na ndio Yesu anaonesha saa yake pale msalabani pia anabaki kuwa mtumwa kwa ajili ya Wokovu wa ulimwengu, saa ile anayovuliwa mavazi yake na kubaki na machache kabisa, ndio saa ya utumishi wa juu kabisa, ndio hasa pale juu Msalabani Ekaristi Takatifu inapopata maana na umuhimu wake. Na kwa kuvaa tena mavazi yake na kuketi tena ndio kusema sasa ni mtu huru.  Watumwa kwa upande mwingine walipaswa kuwa na mavazi ambayo yanakuwa rahisi kufanya utumishi wao na hata walipaswa kuwa wanasimama tayari kwa kufanya kadiri ya matakwa ya mabwana wao. Yesu baada ya kuwa mtumwa na hata kuteseka na kufa pale juu msalabani, anapomaliza kazi ile anarejea tena katika utukufu wake wa milele na Baba yake kumfanya aketi kuume kwake. Kuvaa tena mavazi yake, ni ishara ya Ufufuko wake, ni ishara ya ushindi wake, kwani alionekana ameshindwa saa ile ya mateso na kifo chake, lakini Bwana anamfufua siku ya tatu, ndio saa ya ushindi na utukufu wake wa kweli na wa milele.

Tulisema mwanzoni kuwa alijifunga kiunoni kitambaa mfano wa taulo ili kutumikia na baada ya kuwaosha hatusikii tena kama alikitoa kabla ya kuvaa vazi lake. Kwa kweli ndio kusema kitambaa kile cha kutumikia alibaki nacho. Ndio kusema hakuja duniani ili awe mtumishi na arudipo kwa Baba yake kurejea kuwa mtawala. Hapana anabaki daima na sura ile ile ya utumishi kwa mwanadamu! Ni fumbo la Upendo wa Mungu kwetu wanadamu! Anabaki daima mtumishi na hiyo ndio taswira na sura sahihi ya Mungu. Kitambaa kile mfano wa taulo alilojifunga nalo kiunoni ni ishara ya utumishi wake, ni nguo ambayo kila Mkristo anapaswa kuivaa daima. Kwani wakati wowote ule, mwingine anaweza kuwa na uhitaji nasi, akihitaji utumishi wetu, upendo wa kujitoa kwetu kwa ajili ya wengine wahitaji. Ni kwa kuvaa vazi hilo kiunoni nasi tunatambulika kama wanafunzi na wafuasi wake Yesu Kristo. Na ndio hapo tunaona baada ya kuwafundisha kwa matendo sasa anawaachia amri mpya ndio kupendana kama anavyotupenda yeye, ni kwa kupendana tu sisi tunatambulika kuwa ni wanafunzi wake Yesu. (Yohana 13:34-35) Ajabu Yesu hasemi tumpende Yeye au tumpende Mungu bali tupendane sisi kwa sisi. Ni kwa kupendana sisi kwa sisi hapo kweli tunaweza kusema tunampenda Mungu! Hivyo, kumpenda Mungu ni kumpenda jirani, ni kumtendea mema kwa kumuonjesha upendo na huruma ya Mungu, na kinyume chake hatuwezi kusema tunampenda Mungu wakati hatuwapendi wengine, hatuwatakii mema wengine, hatuna huruma na msamaha wala upendo kwa wengine.

Ekaristi Takatifu ni kielelezo cha maisha na utume wa Kanisa
Ekaristi Takatifu ni kielelezo cha maisha na utume wa Kanisa

Mfuasi na mwanafunzi wa kweli ni yule anayefuata nyao na mifano mema ya mwalimu wake. Ni kuenenda kadiri ya mafundisho iwe ya vitendo au nadharia ya mwalimu. (Wafilipi 2:5; Marko 10:45) Hivyo ili kuelewa vema juu ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, hatuna budi kuelewa maana ya fundisho la kuosha miguu kwa wanafunzi wake Yesu. Kushiriki Meza ya Ekaristi Takatifu, ni kukubali kwa hiari kamili kufuata mfano ule wa Yesu Kristo aliyejifunga kitambaa kile kiunoni ili apate kuwatumikia wengine kwa upendo. Hivyo kushiriki Mwili na Damu yake ni kukubali kuwa mwili mmoja naye. Ni kushiriki sadaka yake ya upendo kwa ajili ya wengine. Yesu anatuachia amri mpya katika Siku ya leo na ndio Amri ya Upendo inayomwilishwa katika huduma. Anatualika kupendana na kipimo cha upendo si mwingine bali ni yeye mwenyewe. Kupendana kama Yeye anavyotupenda sisi. (Yohane 13:34-35). Sisi tutajulikana kuwa ni wafuasi wake Yesu sio kwa ishara au kitu kingine chochote bali kwa kupendana sisi kwa sisi. Na ndio mwaliko wa Yesu wa kujifunza kutoka kwake, kwa kuenenda kama Yeye alivyotufundisha kwa kutumikiana kwa upendo, Ekaristi Takatifu ni kukubali nasi kupendana kama Yesu anavyotoa Mwili na Damu yake kwa ajili ya kila mmoja wetu bila ubaguzi, anatoa mwili na damu yake si kwa ajili ya wale wanaokuwa wema tu bali ni Sadaka ya upendo wa Kimungu kwa kila mwanadamu, kwani Mungu anatupenda upeo, upendo usio na masharti wala ubaguzi. Narudia Yesu hasemi tumpende Yeye bali tupendane sisi kwa sisi, kwani ni katika kupendana hapo kweli tunampenda Mungu.

Mtume Paulo katika Somo la Pili anatualika kabla ya kushiriki karamu ya Mwili na Damu yake Yesu kujihoji nafsini au dhamiri zetu kama kweli tunastahili na ndio kujihoji kama nasi tumejifunga kitambaa kile tayari kwa kutumikia kwa upendo aliye mhitaji, ndio dada na kaka zetu tunaokutana nao kila siku. Petro pale ziwani aligundua kuwa yu uchi na hivyo anakosa mastahili ya kuwa mbele ya Bwana na ndio mwaliko kwangu na kwako kila mara tunapoalikwa kushiriki na kuwa Mwili mmoja na roho mmoja pamoja na Kristo. Ni mwaliko wa kudumu tukiwa tumejifunga kitambaa kiunoni tayari kwa kuwaonjesha wengine upendo na huruma ya Mungu. Nawaalika kwa namna ya pekee leo Alhamisi Kuu kuwaombea watumishi wote wa Ekaristi Takatifu ili daima wavae vazi la utumishi na udogo na kamwe wasifuate mantiki ya ukubwa ya ulimwengu huu. Tusali pia ili Mwenyezi Mungu atujalie mapendo yake ya Kimungu kati yetu. Muwe na tafakari na Maadhimisho mema ya Pasaka, maadhimisho ya upendo na huruma ya Mungu kwa ulimwengu mzima.

13 April 2022, 07:46