Ukraine: Ulinzi mkali uliopo katika mji wa  Odessa. Ukraine: Ulinzi mkali uliopo katika mji wa Odessa. 

Askofu wa Odessa:watu ni waathirika kwa sehemu zote mbili!

Katika mahojiano Askofu Mkatoliki Stanislav Shyrokoradiuk (OFM)wa Odessa-Simferopol na Shirika la kipapa la Kanisa hitaji amebainisha jinsi ambavyo watu wa Urussi hawakuweza kupata habari kamili,kwa maana hiyo walio wengi wanakubaliana na serikali ya Urussi.Watu wa Ukraine ni waathirika wa vita na wa Urussi na waathirika wa propaganda.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Akizungumza na Shirika la Kipapa la Kanisa Hitaji, Askofu Mkatoliki Stanislav Shyrokoradiuk (OFM), wa Odessa-Simferopol, ameeleza sababu msingi za kuvamia Ukraine kwamba watu wa Urussi walikuwa wametaarifiwa vibaya kuhusiana na uvamizi huo. “Sisi Waukraine tu waathirika wa vita na watu wa Urussi ni wathirika wa propaganda”. Kwa mujibu wa Askofu Shyrokoradiuk amethibitishwa kwamba vita sio mgogoro kati ya watu wao wa sehemu zote mbili, lakini ni kutokana na kwamba watu ambao wanaishi Urusi, hawakuweza kupata habari kamili, kwa maana hiyo walio wengi wanakubaliana na serikali ya Urussi wanachowaeleza. “Hii inaongeza mafuta zaidi kwa uchokozi. Ninatumaini macho yao yaweze kufunguka, ili amani iweze kushinda” amesisitiza Askofu.

Kila eneo limewekwa vizingiti ndani ya mji huko Odessa
Kila eneo limewekwa vizingiti ndani ya mji huko Odessa

Askofu Shyrokoradiuk amesema kwamba nchi yake haina njia mbadala ya uhuru, uhuru na mwelekeo kuelekea Ulaya. “Hii ndiyo njia yetu tuliyoichagua. Tunataka kuendelea hivyo, hata kama kwetu sote ni njia ya kupitia msalaba”. Askofu huyo anasema kuwa mji wake wa Odessa kwa sasa uko kwenye kitovu cha vita. Kila siku kuna ving'ora vya mashambulizi ya anga na mashambulizi. Magofu mengi, machozi mengi, damu nyingi katika nchi yetu. Katika mwezi wa kwanza wa vita, mamia ya watoto waliuawa au kujeruhiwa vibaya. “Watoto walipoteza mikono au miguu wakati wa shambulio la bomu; ni mbaya isiyoelezeka! Hali halisi ni tete sana katika bandari nyingine mbili ya Kaskazini mashariki ya Kherson na Mykolaiv. Kherson imetwaliwa yote na warussi na pamoja na jeshi la Urussi kurudi nyuma kutoka mji wa Mykolaiv, kuna mashambulizi ya hanga kila siku ameeleza Askofu Shyrokoradiuk.

Kanisa la Kiorthodox huko Odessa
Kanisa la Kiorthodox huko Odessa

Katika usiku kati ya tarehe 28 na 29 Machi 2022 shambulio pia liliharibu jengo la parokia Katoliki, alisema askofu. “Hata hivyo watu wengi huko Mykolaiv wanataka kubaki, na hii ni wasiwasi wangu mkubwa. Makuhani wote katika maeneo yenye migogoro pia walibaki. Mapadre wanaendesha gari kutoka kijiji hadi kijiji wakiwapelekea watu mahitaji muhimu. Wana shughuli nyingi katika kazi zao, hata ikiwa ni hatari sana”. Kwa kuwa njia ya baharini imeingiliwa, Jimbo la Odessa-Simferopol limepanga magari yake ya mizigo, ambayo yatachukua chakula na dawa kutoka Lviv, mara nyingi katika hatari ya maisha. Lviv ndio sehemu kuu ya usambazaji wa bidhaa zinazowasili kutoka Poland na nchi za Magharibi. Msaada wa kibinadamu katika eneo la Odessa sasa umehakikishwa kwa kiasi kikubwa, amesema askofu: “Tunasaidia bila kujali dini au utaifa: watu kutoka mataifa 120 wanaishi Odessa.” Ushirikiano na madhehebu mengine ya Kikristo kusaidia idadi ya watu wanaoteseka unaendelea vizuri sana, hata na Makanisa ya Kiorthodox ya Kiukreni na Waprotestanti.

Mwanajeshi wa Ukraine akiwa mbele ya Jengo kwa ulinzi
Mwanajeshi wa Ukraine akiwa mbele ya Jengo kwa ulinzi

Askofu Shyrokoradiuk amebainisha kuwa Shirika la Kanisa Hitaji ni muhimu sana. Ni mfuko wa Kipapa ambapo si tu kuwa wa kwanza kutoa msaada lakini pia unajitahidi kufadhili magari ya ziada ili kuhakikisha vifaa kwa watu wa vijiji vya mbali.  Kwa upande wa Askofu Shyrokoradiuk.messisitiza kwamba “Tumeguswa sana na mshikamano huo”.

01 April 2022, 13:23