Tafuta

Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC, katika Ujumbe wake wa Pasaka ya Bwana kwa Mwaka 2022 linapenda kujikita katika imani na matumaini yanayopyaishwa kwa: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu. Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC, katika Ujumbe wake wa Pasaka ya Bwana kwa Mwaka 2022 linapenda kujikita katika imani na matumaini yanayopyaishwa kwa: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu. 

Baraza La Makanisa Ulimwenguni: Ujumbe Wa Pasaka 2022: Imani Na Matumaini

Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC, katika Ujumbe wake wa Pasaka linapenda kujikita kattika Imani na Matumaini yanayopyaishwa kwa mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu! Watu wamekata na kujikatia tamaa kutokana na maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 ambao bado ni tishio kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu ni kilele cha ushuhuda na ukweli wa imani katika Kristo aliyeteswa, akafa na hatimaye kufufuka kutoka wafu kadiri ya Maandiko Matakatifu. Hii ni imani iliyotangazwa na kushuhudiwa kwanza kabisa na wanawake jasiri wa imani, Mitume wa Yesu na hatimaye waamini wa Kanisa la Mwanzo. Hii ni imani ambayo imethibitishwa kwa njia ya Agano Jipya, wakaitangaza na kuihubiri kwa ari na moyo mkuu kama sehemu muhimu sana ya Fumbo la Pasaka pamoja na Fumbo la Msalaba. Kristo Yesu amefufuka kutoka wafu. Kwa kifo chake alishinda mauti. Wafu amewapa uzima. Rej KKK 638. Ni ufunuo wa Uungu wa Kristo Yesu unaowapatia waamini maisha ya uzima mpya na hivyo kuhesabiwa haki pamoja na kufanywa wana wateule wa Mungu. Ufufuko wa Kristo ni msingi wa ufufuko wa miili na uzima wa milele ijayo! Ndiyo maana Pasaka ni Sherehe kubwa katika Kanisa. Hii ni Sherehe ya upendo, huruma na msamaha wa Baba wa milele unaofumbatwa katika Fumbo la Pasaka yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu. Ni katika muktadha huu, Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC, katika Ujumbe wake wa Pasaka ya Bwana kwa Mwaka 2022 linapenda kujikita katika Ujumbe wa Imani na Matumaini yanayopyaishwa kwa mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu! Watu wengi wamekata na kujikatia tamaa ya maisha kutokana na maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 ambao bado ni tishio kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni ugonjwa ambao umesababisha madhara makubwa katika medani mbalimbali za maisha.

Hofu na wasi wasi imetanda kutokana na UVIKO-19.
Hofu na wasi wasi imetanda kutokana na UVIKO-19.

Watu wamekata tamaa kutokana na vita inayoendelea kati ya Urussi na Ukraine sanjari na madhara makubwa yanayoendelea kusababishwa na mabadiliko ya tabianchi. Kuna ongezeko kubwa la wakimbizi na wahamiaji, wanaotafuta: hifadhi, usalama na maisha bora zaidi. Kuna ukatili, dhuluma na nyanyaso dhidi ya wanawake, watoto na wazee. Matukio yote haya linasema Baraza la Makanisa Ulimwengini, WCC ni dalili za utamaduni wa kifo, dhidi ya utu, heshima na haki msingi za binadamu. Hali hii inapelekea mateso, hali ya kukata tamaa na kupoteza matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Katika hali na mazingira kama haya, Mama Kanisa kama ilivyokuwa kwa wale wanawake jasiri mashuhuda wa Injili anasema tena “Msiogope.” Kristo Yesu aliyeteswa, akafa Msalabani amefufuka katika wafu. Rej. Mt 28: 5-7. Kristo Mfufuka anadhihirisha ushindi dhidi ya dhambi na kifo, chemchemi ya maisha mapya yanayosimikwa katika matumaini. Huu ni mwaliko kwa waamini kuimarisha: Imani, matumaini na mapendo kwa Kristo Yesu na Kanisa lake bila kujikatia wala kukata tamaa. Kaburi tupu na sauti za Malaika ni kielelezo cha mwanga angavu wa maisha, furaha, upendo na upya wa maisha. “Basi huu uharibikao utakapovaa kutokuharibika, na huu wa kufa utakapovaa kutokufa, hapo ndipo litakapokuwa lile neno lililoandikwa, Mauti imemezwa kwa kushinda. Ku wapi, Ewe mauti, kushinda kwako? U wapi, Ewe mauti, uchungu wako? Uchungu wa mauti ni dhambi, na nguvu za dhambi ni torati. Lakini Mungu na ashukuriwe atupaye kushinda kwa Bwana wetu Yesu Kristo.” IKor 15:54-55.

Hofu ya athari za vita kati ya Ukraine na Urussi imetanda sana
Hofu ya athari za vita kati ya Ukraine na Urussi imetanda sana

Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu ni chemchemi ya maisha na uzima wa milele; ni upyaisho wa mambo yote katika Kristo Yesu. Hii ni chemchemi ya uponyaji na maridhiano, ili kutibu na kuganga madonda ya chuki na uhasama. Ni furaha kwa wale waliovunjika na kupondeka moyo. Mwanga angavu kwa wale wanaotembea katika giza na uvuli wa mauti; uhuru kwa wale wanaosetwa na kudhulimiwa; umoja na upatanisho kwa wale waliofarakana. Kristo Yesu Mfufuka ni nguvu na mwanzo mpya, unaowaweka watu huru. Kristo Yesu amefufuka kweli kweli na maisha yanazidi sasa kusonga mbele. Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC linasikitika kusema kwamba, maadhimisho ya Pasaka ya Bwana kwa mwaka 2022 yamevurugwa na vita kati ya Urussi na Ukraine, changamoto na mwaliko wa kusikia tenda sauti ya Kristo Yesu ikisema, “Amani kwenu.” Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC linahitimisha ujumbe wa Pasaka kwa mwaka 2022 kwa kusema kwamba, amani ni zawadi inayopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu wa Mungu, kila mtu akijitahidi kuwajibika kuilinda, kuitetea na kuidumisha. Amani inapaswa kuwa ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utambulisho wa watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia. Hii ni changamoto kubwa kwa watu wa Mungu kumwilisha zawadi na Injili ya amani katika uhalisia wa maisha yao. “Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.” Flp 4: 7. Ni dhamana na wajibu wa watu wote wa Mungu kuhakikisha kwamba, amani ya Mungu inatawala katika akili na nyoyo zao kila siku ya maisha yao.

WCC Pasaka 2022
20 April 2022, 14:46