Tafakari Neno la Mungu Dominika III ya Pasaka: Wakristo wanaitwa na kutumwa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Tafakari Neno la Mungu Dominika III ya Pasaka: Wakristo wanaitwa na kutumwa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. 

Dominika ya III Kipindi Cha Pasaka: Mashuhuda Wa Uinjilishaji Wa Kina

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu inawaonesha Mitume wa Yesu waliokata tamaa na kurejea tena katika hali ya maisha yao ya kwanza, katika uvuvi. Kristo Mfufuka anawatokea na kuwapatia tena utume wa kwenda kuinjilisha kwa watu wa Mataifa. Sharti kuu ni kuonesha upendo wa dhati kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Waendelee kumtumainia na kumtegemea Yesu katika utume.

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Sehemu ya Injili ya leo kama tunaisoma na kuelewa kama tukio la kihistoria hakika tunabaki na maswali mengi magumu bila majibu. Ni vema kuona lengo la mwandishi si kutupa ukweli wa kihistoria wa matukio na badala yake anatumia lugha ya picha kufikisha ujumbe muhimu hasa kwa jumuiya zile alizokuwa anawaandikia kama sehemu ya katekesi, yaani mafundisho ya Kitaalimungu. Mfano hata baada ya kuwatokea wanafunzi wake mara kadhaa kabla ya tukio la leo, tunaona bado wanashindwa kumtambua na hapo tunabaki na maswali juu ya mshangao wao hasa pale alipofanya muujiza wa uvuvi wakati alishatenda miujiza mingi hata kabla ya mateso, kifo na ufufuko wake. Na hata kuona leo Petro na mitume wengine hawaonekani wakiwa bado Yerusalemu, mahali ambapo Yesu alikamatwa, kuteswa, kusulubiwa na kufa pale juu msalabani, na badala yake Galilaya wakiwa wamerejea tena katika maisha yao ya uvuvi wa samaki kabla ya kuitwa kuwa wanafunzi wa Yesu wa Nazareti. Maswali haya yanatusaidia kutafakari vema Injili ya leo, na hasa kama tukiisoma kwa muunganiko na somo la kwanza kutoka Kitabu cha Matendo ya Mitume. Narudia si kila mara tunaposoma Injili tunakutana na kweli za Kihistoria bali mara zote kusudi ni ujumbe wa Kiteolojia unaopaswa kutufikia sisi tulio wafuasi wake Bwana wetu Yesu Kristo.

Mtume Petro mbele ya Baraza la Wazee wa Kiyahudi pale Yerusalemu bila uoga wala wasiwasi anasimama na kuonesha imani yake kwa Kristo Mfufuka. Ni kwa ujasiri huu Mtume Petro anakumbuka ahadi yake kwa Kristo Mfufuka kama alivyowatokea pale ziwa Galilaya na kumuuliza mara tatu kama kweli anampenda Kristo. Petro anatambua sasa maana ya utume na utumishi wake kama kiongozi wa Kanisa la Kristo. Dominika ya Pili,  Kristo Mfufuka anawatokea wanafunzi wake siku ile ya Pasaka, yaani siku ya kwanza ya Juma wakati Tomaso hakuwepo, na baada ya siku nane anawatokea wakiwa pamoja na Tomaso na huku milango ikiwa imefungwa. Mara zote mbili tunaona Kristo Mfufuka anawatokea wanafunzi wake siku ya kwanza ya Juma yaani Dominika na wakiwa bado Yerusalemu. Ila leo Kristo Mfufuka hawatokei siku ya Dominika na badala yake ni siku ya kazi au siku ya katikati ya juma ambapo tunaona mitume wakiwa wamerejea katika maisha yao ya kawaida ya awali kwa kurudia kazi yao ya uvuvi wa samaki na leo wakiwa katika mkoa wao wa Galilaya. Kristo Mfufuka aliwatokea kwa mara ya kwanza wanafunzi wake walipokuwa bado Yerusalemu, walipojifungia katika chumba cha karamu ya mwisho kwa hofu ya Wayahudi. Lakini pia Kristo Mfufuka anawaalika kwenda Galilaya na huko watamuona. Ni katika Galilaya ya mataifa, Yesu wa Nazareti alianza misheni yake ya kuutangaza na kuusimika ufalme wa Mungu.

Kashfa ya Msalaba iliwavunja Mitume nguvu wakaamua kurejea katika maisha yao ya awali.
Kashfa ya Msalaba iliwavunja Mitume nguvu wakaamua kurejea katika maisha yao ya awali.

Ni Galilaya aliwaita wanafunzi wale wa kwanza Simoni, Andrea na Yakobo na kuwaambia atawafanya kuwa wavuvi wa watu. Ni hapo tena anawaalika kuanza rasmi uvuvi ule sio tena wa samaki bali wa watu wote wa ulimwengu mzima. Ni Galilaya Yesu anataka utume wake uanze kwani ni kwa ajili ya watu wote, kwani Galilaya haukuwa mji wa Wayahudi peke yao bali hata na wapagani. Ndio kusema misheni ya Kristo Mfufuka sio tu kwa watu wa taifa au rangi au tamaduni fulani bali kwa ulimwengu mzima. Pamoja na nia ya Mwinjili Yohane kutuonesha kuwa Kristo Mfufuka daima anakuwa na wanafunzi wake siku ya Dominika, tunaona leo anatuonesha kuwa Mfufuka anatutokea hata katika shughuli na maisha yetu ya kila siku, itoshe tu kumsikiliza ili kazi na majukumu yetu yapate maana na baraka zake. Kila siku Kristo Mfufuka anatutokea ili aongoze maisha yetu. Maisha yetu yanapata maana kwa kukubali kuongozwa na mantiki ya Kristo Mfufuka. Mwinjili Yohane anatueleza kuwa wanafunzi wale walikuwa saba, namba saba haipo kwa ajali bali kwa makusudi mazima ya kupeleka ujumbe wa Kiteolojia. Namba 7 katika Biblia ni ishara ya ukamilifu, hivyo ndio kusema kwa uwepo wa wale wanafunzi saba wanawakilisha kila aina ya waamini wa Kanisa la Kristo. Ni jumuiya iliyokamilika, jumuishi ya watu wa kabila, rangi na mataifa yote ya ulimwengu mzima.

Bahari anayoizungumzia mwandishi kwa kweli ni ziwa Galilaya, ila kwa lengo moja tu, bahari katika Maandiko Matakatifu inawakilisha nguvu za giza zinazomkinza mwanadamu kufikia ukamilifu wake. Zinazomzuia kufikia furaha ya kweli. Na ndio maana Yesu anawaalika wamfuate ili awafanye kuwa wavuvi wa watu, ili wawaongoze watu katika uzima wa kweli, na ndio maisha ya urafiki na Mungu, maisha ya neema. (Marko 1:17) Na hata Mwinjili Mathayo anaufananisha ufalme wa Mungu sawa na nyavu au jarife iliyotupwa baharini na huko kuvua samaki wa kila aina. (Mathayo 13:47-48) Kuvua ni kumtoa mwanadamu katika hali duni, hali ya hatari ya kutawaliwa na nguvu za uovu na yule mwovu ili aweze kupata uhuru wa kweli. Wanavua usiku kucha, usiku ni ishara ya giza, na sio tu unakosekana mwanga na nuru bali hasa anakosekana Kristo aliye nuru ya kweli. Hivyo ni mwaliko hata nasi hatuwezi kupata matunda katika kumshuhudia Kristo Mfufuka bila ya kumshirikisha na kuongozwa naye, bila kusikiliza Neno lake na kutegemea akili zetu na ujuzi wetu. Hivyo kila mwanafunzi wa Yesu na hasa anayetaka kumshuhudia Kristo Mfufuka hana budi kuwa na Kristo katika kila hatua na hasa kumsikiliza Yeye kwa njia ya Neno lake. Kanisa la Kisinodi linatualika kuwa na ushirika, ndio muunganiko kwanza na Mungu mwenyewe anayetupa hadhi ya kuwa wana wake, ya kuunganika sisi kwa sisi kwa nafasi ya pili. Hivi ushirika wetu unatokana na kuunganika na kukubali kuongozwa na Yesu Kristo katika maisha yetu ya ufuasi.

Utume wetu wa Uinjilishaji utafanikiwa ikiwa sisi wenyewe tunakuwa mashahidi wa Habari Njema, yaani Injili ya mifano ya maisha yetu. Sisi hatuna budi kuwa Injili na hapo tunaweza kuwavuta wengi kwa Kristo Mfufuka. Baba Mtakatifu Paulo VI mara baada ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican alimuuliza rafiki yake wa Kiitalia aliyejulikana kama Giuseppe Prezzolini ambaye hakuwa mwamini. Papa alitaka kujua ni namna gani nzuri na bora za kuweza kuwafikia watu wasioamini au wapagani. Rafiki yake huyo akamjibu Papa na kumwambia hakuna njia yeyote iliyo njema na nzuri zaidi ya Wakristo kuwa wema. Na alizidi kumwambia Papa ulimwengu haujapungukiwa na kitu kingine chochote isipokuwa watu wema, na hakuna kitu kinachovuta wengine kama wema. Akazidi kusema ulimwengu haujapungukiwa watu wenye akili na utaalamu na ujuzi wa kila aina, lakini kuna uhaba na kuadimika kwa watu wema. Ni jukumu la Kanisa kuwafanya waamini kuwa watu wema, ndio kusema kuwa Habari Njema sisi wenyewe kwa nafasi ya kwanza iwe katika familia zetu, makazini, mitaani, kwenye jumuiya zetu mbali mbali na kadhalika na kadhalika. Hivyo njia bora ya kuwavuta wengine au kuwavua wengine kutoka katika uovu na yule mwovu ni sisi kuwa Injili, kuwa Habari Njema kwa maisha yetu na sio kwa maneno tupu bali kwa matendo.

Wakristo wanaitwa na kutumwa kumtangaza na kumshuhidia Kristo Yesu.
Wakristo wanaitwa na kutumwa kumtangaza na kumshuhidia Kristo Yesu.

Kristo Mfufuka hatuwezi kumuona na badala yake tunajisikia tupo wapweke na peke yetu kama tunakosa macho ya imani, kama tunakosa imani. Kristo Mfufuka anabaki na Kanisa lake siku zote mpaka ukamilifu wa ulimwengu, ila yatosha macho ya imani kumwona. (Yohane 14:18-19) Kristo Mfufuka hayupo tena katika mtumbwi bali yupo kando ya bahari, ndio ameketi kuume kwa Baba katika utukufu ila daima anatualika nasi kushiriki maisha hayo mapya ya kushiriki utukufu wa Mungu, yaani kushiriki utakatifu. Kristo Mfufuka anasafiri pamoja nasi sio tena kwa namna ile ya nyama kama alivyofanya miaka elfu mbili iliyopita bali daima ni kwa jicho la imani tunaweza kumwona katika maisha ya Kanisa, iwe katika Neno lake, Sakramenti ya Kanisa na hata katika sura ya kila mmoja tunayekutana naye. Ni mimi na wewe tunaalikwa sasa kumbeba Kristo Mfufuka kwa ushuhuda wa maisha yetu ya siku kwa siku. Kunapopambazuka na kuanza kuwa na nuru tena wanafunzi wanakutana na Kristo Mfufuka anayewaongoza na kuwalekeza nini cha kufanya na kwa namna ipi. Na ndio lengo la Mwinjili Yohane kutuonesha kuwa pamoja na kuwa Kristo Mfufuka ameketi katika utukufu mbinguni kuume kwa Baba ila bado anasafiri na Kanisa lake na kuliongoza. Tunahitaji kuwa na macho ya imani kukutana na kumuona Kristo Mfufuka.

Ni baada ya kumsikiliza Yesu anawaalika kurusha nyavu zao upande wa kulia, tunajua kwa hakika Yesu hakukulia karibu na ziwa akiwa mdogo au ujanani na hivyo si mzoefu wala mtaalamu wa kazi ya uvuvi, ila wanafunzi wale waliokuwa wabobezi katika kazi ile bado wanamsikiliza na ajabu hawamuulizi hata swali moja na badala yake wanatenda kadiri anavyowaagiza. Na matokeo yake ni upatikanaji wa samaki wale 153.  Namba 153 nayo ni lugha ya picha = (50 x 3) + 3, kwa Wayahudi namba 50 inamaanisha watu wote, na namba 3 ni ukamilifu na ndio pia inawakilisha Mungu mwenyewe, ni namna ya Kimungu. Hivyo ndio kusema ni ulimwengu mzima, ni watu wote bila ubaguzi wanaoalikwa kwenda kuwavua, kwenda kuwapatia uzima dhidi ya nguvu za yule mwovu, wokovu wa kweli ni kwa ulimwengu mzima kufanyika kuwa wana wa Mungu, kuwa watu wa Mungu, kufanyika rafiki wa Mungu. Na tunaona Petro anavuta wavu ule uliojaa samaki na bila kukatika anauvuta nchi kavu.  Na ndio misheni ya Kristo Mfufuka anapoinuliwa pale juu Msalabani kuwavuta watu wote kwake ili sote tupate uzima. (Yohane 12:32) Kwa damu yake ya thamani azizi na kuu ulimwengu wote unapata uzima wa kweli, unapata kukombolewa kwayo. Hakuna hata mmoja anayeachwa nje ya damu ile yenye thamani isiyo na kipimo wala kifani.

Na Kristo Mfufuka anawaalika kufanya nao karamu tena kwa kula samaki wale waliookwa na mkate, na ndio Mababa wa Kanisa wanatueleza hii ni ishara ya furaha ile ya milele baada ya kukamilisha kazi ya ukombozi ulimwenguni. Ekaristi Takatifu ni karamu sio tu ya ulimwengu huu bali ya milele yote, kwani ni sala kuu ya Upendo wa Yesu Kristo kwa Mungu Baba ambamo nasi tunaalikwa kushiriki pamoja na Mwana pekee wa Mungu. Ni karamu ya ufufuko, ni sherehe ya milele yote ambayo tutaendelea kuisherehekea daima na milele. Sehemu ya mwisho ya Injili ya leo tunaona utume maalumu au Ukulu wa Mtume Petro. Kama alivyomkana Yesu mara tatu anaulizwa kukiri upendo wake mara tatu na hapo anakabidhiwa jukumu la pekee na muhimu kama kiongozi wa Kanisa la ulimwenguni. Namba tatu hapa inajirudia tena, ni kama kamilifu lakini zaidi sana ni namba ya Kimungu, hivyo upendo kamili hauna budi kuwa ule wa Mungu mwenyewe, hivyo Petro anarudia mara tatu kuonesha anapaswa kuwa na upendo wa Kimungu, usiogawanyika wala kuwa na masharti. Petro anakabidhiwa utume huu kutuonesha daima Mungu anatuchagua sio kwa mastahili yetu bali ili neema, upendo na huruma yake ipate kuonekana kwetu. Ndio ni Petro aliyemkana mara tatu leo anakabidhiwa kuwa kiongozi wa Kanisa la Kristo. Jiwe la kwanza la kujikwaa ni hapo tunapoona Papa wa kwanza katika historia ya Kanisa ni Mtume Petro aliyemkana Yesu mara tatu kabla ya Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu.

Petro anaalikwa kulisha na kuchunga, na si kutawala maana yawezekana mwanzoni hata naye alishindwa kuelewa misheni ya Yesu kwake. Na ndio siku ile Yesu alipotaka kumuosha miguu alikataa kwa kuwa bado hakuwa ameelewa utume wake. Na hata nasi leo mara nyingi tunakosa kuelewa utume wetu kama Wabatizwa, kama watawa, kama mashemasi, kama makasisi, kama maaskofu. Yafaa tukumbuke misheni na utume wetu ni kutumikia, ni kuwa wadogo na sio mabwana wakubwa, au watu wa kuheshimiwa. Kuwa Mkristo maana yake ni kumbeba Yesu Kristo Mfufuka, ni kuongozwa na mantiki yake. Na ndio Kanisa la Kisinodi linatualika kuishi kama Kanisa, kuishi katika:Umoja, ushiriki na utume wa kila mmoja wetu. Kanisa ni familia ya wana wa Mungu, ni jumuiya ya Wabatizwa kimsingi na hivyo hakuna mmoja mwenye umuhimu zaidi ya mwingine, na kama kuna huduma na majukumu mbali mbali basi nia na madhumuni yake ni katika utumishi na si vingine.Haikuwa rahisi hata kwa Mtume Petro kuelewa mwaliko ule wa Kristo Mfufuka, kwani bado kama nasi mara nyingi tunaongozwa na mantiki ya ulimwengu huu. Ila ni katika somo la kwanza la leo tunaona Petro anafikia ukomavu na hata wakati wa kuteswa kwake na kudhulumiwa anabaki kuona hana budi kumsikiliza na kumtii Mungu na si mwanadamu. Petro kwa hiari yake anakubali sasa kuongozwa na mantiki ya Kimungu na si ile ya mwanadamu, hivyo kupelekwa na kufanya hata kule au vile asingependa yeye ila kuruhusu daima mpango wa Mungu katika maisha na utume wake.

Uinjilishaji ni jukumu la wakristo wote.
Uinjilishaji ni jukumu la wakristo wote.

Mwinjili Yohane pia anatoa fundisho hili kwa Kanisa lililokuwa linapitia madhulumu na mateso mengi, hata nyakati zetu leo bado tunapitia mateso mengi ila yafaa daima tukumbuke kuwa Kristo Mfufuka daima yupo nasi na itoshe kufungua macho yetu ya imani na kumsikiliza na kutenda kadiri yake kama hakika tunataka kupata matunda mengi. Kanisa la Kisinodi ni la Kimisionari, yaani utume wake ni Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Mtakatifu Paulo VI alisema Uinjilishaji ni neema na ni wito wa Kanisa, ndio kitambulisho cha Kanisa. Kanisa lipo ili Kuinjilisha, ili kushuhudia upendo na huruma ya Mungu kwa ulimwengu mzima. Na ndio kama tulivyotangulia kuona hapo juu kila mmoja wetu hana budi kusali na kuomba neema za Mungu ili kweli tuweze kuwa Habari Njema ya Wokovu kwa ulimwengu mzima, sio tu kwa maneno yetu bali zaidi sana kwa ushuhuda wa maisha yetu. Kanisa la Kisinodi ni ushirika yaani muunganiko na Mungu anayetufanya sisi sote kuwa wana wake, ni ushiriki kwani tunajaliwa neema za kuishi kwa kujaliana na kuthaminiana, kila mmoja ni jiwe hai kwa maisha ya Kanisa na tatu ni Kanisa la Kimisionari, lenye kuinjilisha, lenye kuwa Habari Njema kwa ulimwengu wetu wa leo.Nawatakia tafakari njema na Dominika njema.

29 April 2022, 07:39