Tafuta

Habari ya uvuvi wa samaki yatufundisha kwamba Kanisa la Kristo daima litawapokea watu wa kila aina - wema kwa wabaya; lakini hali hiyo haiwezi kuvunja umoja wake. Habari ya uvuvi wa samaki yatufundisha kwamba Kanisa la Kristo daima litawapokea watu wa kila aina - wema kwa wabaya; lakini hali hiyo haiwezi kuvunja umoja wake. 

Dominika ya III ya Kipindi Cha Pasaka: Mashuhuda Jasiri Wa Imani Na Uinjilishaji

Masomo ya dominika hii yanasisitiza juu ya utii wetu kwa Mungu katika kuiishi na kuishuhudia imani yetu kwa Kristo Mfufuka bila kuogopa kwa maana ni Roho Mtakatifu ndiye anayefanya kazi ndani mwetu kama alivyowaongoza kwa ujasiri Mitume kumhubiri na kumshuhudia Kristo Mfufuka. Mkate na Samaki ni alama ya Fumbo la Ekaristi Takatifu na Jarife ni mchakato wa Uinjilishaji.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya 3 ya Kipindi cha Pasaka. Masomo ya dominika hii yanasisitiza juu ya utii wetu kwa Mungu katika kuiishi na kuishuhudia imani yetu kwa Kristo Mfufuka bila kuogopa kwa maana ni Roho Mtakatifu ndiye anayefanya kazi ndani mwetu kama alivyowaongoza kwa ujasiri mitume kumhubiri na kumshuhudia Kristo Mfufuka kama anavyosali Padre kwa niaba ya jamii ya waamini katika sala ya mwanzo; “Ee Mungu, watu wako na waone furaha sikuzote kwa ajili ya kutiwa nguvu mpya roho zao. Kwa vile sasa wanafunzi kwa kurudishiwa ile heshima ya kuwa wana wa Mungu, waitazamie ile siku ya kufufuka kwao, wakitumaini kupewa pongezi”. Ni katika kuumega mkate, Ekaristi Takatifu, mwili na damu ya Kristo, tunamtambua Yesu mfufuka. Somo la kwanza la Kitabu cha Matendo ya Mitume (Mdo. 5:27b-32,40b-41); latufundisha kwamba, kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, inatupasa kumhubiri Kristo Mfufuka bila hofu yoyote. Kwa njia hiyo tutafanana na Mitume, kama vile Petro, waliohiari kumtii Mungu kuliko binadamu. Ujasiri waliokuwa nao mitume baada ya ufufuko wa Kristo ulivyojidhihirisha katika somo la kwanza kutoka kitabu cha matendo ya mitume unashangaza na kutuacha na maswali. Iweje Mitume ambao walimkimbia Yesu alipokamatwa, walikamkana kwa kudai hawamjui, wakasimama mbali pale Karvari, tena baada ya kifo chake walionekana kukata tamaa na kujifichaficha, wakajifungia milango kwa hofu ya wayahudi leo hii wanaonekana imara na kumshuhudia kwa nguvu zao zote? 

Kristo Mfufuka ni nguvu thabiti kwa mashuhuda wa Fumbo la Pasaka.
Kristo Mfufuka ni nguvu thabiti kwa mashuhuda wa Fumbo la Pasaka.

Itakumbukwa kuwa alipowatokea kwa mara ya pili, Yesu mfufuka aliwavuvia na kuwajaza Roho Mtakatifu akiwaambia pokeeni Roho Mtakatifu wowote mtakaowaondolea dhambi watakuwa wameondolewa na mtakao wafungia wawatakuwa wamefungiwa na kisha akawaangiza na kuwatuma wakaihubiri habari njema. Kumbe, ni Roho Mtakatifu ndiye aliyewapa nguvu na ujasiri wa kutangaza habari za ufufuko wake na za mafundisho yake bila woga, wakianzia na Yerusalemu. Hawaogopi tena, hawana shaka wala wasiwasi wako vifua mbele wakisema; Mungu akiwa upande wetu ni nani wa kumwogopa? Mafundisho yao ya kijasiri yanawatia uoga wale walioshinikiza kuuawa kwa Yesu, kwa sababu watu wengi waliamini kufufuka kwake na kwamba anafanya kazi katika nafsi za mitume. Viongozi na wakuu wa wayahudi wanajaa mashaka na hofu nyingi kwamba watu wangeweza kulipiza kisasi kwa kosa lao la kumuuua Kristo tena bila kosa wala hatia yoyote. Hivyo wanatumia nguvu kuwanyamazisha bila mafanikio kama anavyosema Kuhani Mkuu akiwaonya Mitume: “Hatukuwaamuru ninyi kwa nguvu, msifundishe kwa jina la mtu huyu? Tazameni, mmeijaza Yerusalemu mafundisho yenu, na mnataka kuileta damu ya mtu yule juu yetu.”

Nguvu na ushawishi wa Yesu Kristo unatambulikana sasa zaidi baada ya kuwa amefufuka kutoka wafu. Hata hivyo viongozi wa dini ya Kiyahudi hawataki kukubaliana na ukweli huo na ndio maana bado wanawazuia mitume kuinjilisha. Msimamo wa Mitume unabaki ule ule; Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu. Mungu wa baba zetu alimfufua Yesu, ambaye ninyi mlimwua mkimtundika katika mti. Mtu huyo Mungu amemtukuza kwa mkono wake wa kuume, awe Mkuu na Mwokozi, awape Waisraeli toba na msamaha wa dhambi. Na sisi tu mashahidi wa mambo haya, pamoja na Roho Mtakatifu ambaye Mungu amewapa wote wamtiio. Hata walipopigwa na kuamuriwa kuacha kumtangaza Kristo, mitume walifurahi sana kwa kuwa waliaibishwa kwa ajili ya Kristo. Sisi leo furaha yetu iko wapi? Pamoja na vitisho vingi habari za Yesu Kristo mfufuka zilienea sehemu mbalimbali za Uyahudi na nje ya Uyahudi kama moto wa kiangazi kwa kauli mbiu ya mitume imetupasa kumtii Mungu kwanza kuliko mwanadamu.” Mitume sasa wanakumbuka mafundisho ya Kristo aliposema; “Chakula changu ni kuyafanya mapenzi ya Baba yangu”.  Huu ndio ulikuwa msimamo wa Yesu Kristo mwenyewe na hivyo katika utume wake. Msimamo huu ndio uliomfanya aonekana mchochezi, mvunja sheria, mwana mapinduzi. Je, sisi katika orodha ya vipaumbele vyetu Mungu ana nafasi ya ngapi? Kati ya mali, starehe, madaraka Mungu yuko sehemu ipi?

Somo la pili la kitabu cha Ufunuo wa Yohane (Ufu. 5:11-14); latueleza kuwa Yule Mwana Kondoo aliyejitolea kuwa sadaka kwa ajili yetu ndiye Yesu Kristo Mfufuka anastahili sifa na heshima ya pekee. Kwa kumhimidi yeye, viumbe vyote vya mbinguni na duniani vinashiriki utukufu wa huyo Mwana Kondoo na heri ya mbingu. Injili ilivyoandikwa na Yohane (Yn. 21:1-19); yatueleza mambo makuu matatu: Yesu mfufuka kujidhihirisha kwa mitume wakivua samaki; Yesu kuwaalika wanafunzi kufungua kinywa kwa kula samaki na mkate wa kuokwa ishara ya Ekaristi Takatifu na Yesu kumkabidhi Simoni Petro Kanisa lake kuwa mchungaji mkuu kwa ishara ya kondoo. Habari ya uvuvi wa samaki yatufundisha kwamba Kanisa la Kristo daima litawapokea watu wa kila aina - wema kwa wabaya; lakini hali hiyo haiwezi kuvunja umoja wake. Karamu ya samaki yaeleza juu ya Ekaristi Takatifu na heri mbinguni. Kule kumkabidhi Petro kondoo ni kwamba Yesu anamwachia Petro madaraka na mamlaka kamili juu ya Kanisa lake.

Mkate na Samaki ni Ishara ya Ekaristi Takatifu
Mkate na Samaki ni Ishara ya Ekaristi Takatifu

Tendo hili lilifanyika Yesu alipowatokea mara ya tatu wakivua samaki baada ya kufufuka kwake. Petro anakabidhiwa Kanisa baaada ya kuulizwa swali mara tatu, Simoni wa Yohane wanipenda. Baada ya Petro kujibu kwa mfadhaiko mara ya tatu Bwana wewe wajua kuwa na kupenda, Kristo akampa mamlaka ya kuliongoza kanisa lake alilolianzisha yeye mwenyewe kwa kumpa madaraka na mamlaka kamili juu ya Kanisa. Yesu anatimiza kile alichomwahidi Petro akimwambia: “wewe ndiwe Petro na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu” (Mt 16:18) baada ya Petro kukiri ukuu wa Yesu akisema; “Wewe ndiwe Kristo mwana wa Mungu aliye hai” (Mt 16:16) naye Yesu akamwombea akisema; “Nimekuombea wewe ili imani yako isitindike, nawe utakapoongoka, waimarishe ndugu zako” (Lk 22:32).  Mamlaka na madaraka haya anayapokea kila Baba Mtakatifu, Khalifa wa Mtakatifu Petro anapochaguliwa kadiri ya Mapokeo ya Kanisa.

Yesu anamuuliza Petro mara tatu; Simoni wa Yohane wanipenda; Namna hii ilikuwa ni utamaduni wa nyakati hizo ambapo madaraka yalitolewa kwa tamko mara tatu mbele ya mashahidi. Mamlaka haya anayopewa Petro juu ya kondoo wa Yesu yanadai upendo mkubwa kwa upande wa Petro. Ndiyo kusema, Petro ataweza kutekeleza madaraka yake kama mkuu wa Kanisa, ikiwa tu ataonesha mapendo makubwa kwa Bwana wake. Yesu anahitimisha madhehebu haya kwa kumwambia Petro nifuate (Mt 4:19, Yn 21:22). Hii ni safari ya maisha mpaka kuufikia uzima wa milele mbinguni. Injili pia inatuambia kuwa Yesu aliwaambia wanafunzi wake; “Njooni mfungue kinywa” (Yn 21:12), “Yesu akaenda akautwaa mkate, akawapa na samaki hivyi hivyo” akawapa wakala (Yn 21:13). Kisha Petro akapanda chomboni akalivuta jarife Pwani limejaa samaki wakubwa 153, na ijapokuwa ni wengi, jarife halikupasuka: Jarife kutokupasuka ni ishara ya Kanisa analokabidhiwa Petro naye sharti alivute kulifikisha Mbinguni. Jarife hili litakuwa na watu wengi kutoka pande zote za Dunia. Ndani ya Jarife – Kanisa kuna nafasi kwa kila mmoja wetu anayeishi duniani.

Licha ya kuwa kilikuwepo, kipo na kitaendelea kuwepo, kila kukicha kinamkuta ambaye mda wake umefika na kila mmoja wetu lazima kimpate mda wake ukifika, lakini bado kinabaki kuwa ni fumbo na kinatisha kuliko vitu vyote. Hiki si kingine bali ni kifo. Kifo kinatisha na kuogopesha, kila kikitokea kinaleta majonzi, huzuni, simanzi na masikitiko. Lakini maiti inatisha na kuogopesha zaidi ya kifo na ikitokea maiti imepiga chafya tunapatwa na mzungumkuti. Ikitokea maiti imezinduka au aliyezikwa akatokea panakuwa hapatoshi tunajawa na hofu na mashaka zaidi. Hivi ndivyo ilivyo katika maisha yetu ya kawaida. Kwa mitume wa Yesu, ni kinyume kabisa. Kila walipomwona Kristo mfufuka walijaa furaha wakawa na ujasiri wa kutangaza habari zake. Hii ni kwa sababu kwa kifo na ufufuko wake ameshinda dhambi na mauti, kifo hakimtawali tena.

Waamini wanaitwa na kutumwa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Mfufuka.
Waamini wanaitwa na kutumwa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Mfufuka.

Kumbe, tunaona kuwa imani kwa Yesu Mfufuka ni zawadi kutoka kwa Mungu na Mungu huwapatia wanyofu na wanyenyekevu wa moyo ambao wako tayari kuipokea. Kutokana na upendo wake kwa Yesu, Yohani alikuwa wa kwanza kumtambua Yesu mfufuka: “Basi yule mwanafunzi ambaye Yesu alimpenda akamwambia Petro “ndiye Bwana” (Yn 21:7). Waamini wote kwa Sakramenti ya Ubatizo, tumepewa jukumu la kumhubiri Kristo kwa maneno na matendo yetu. Tunapaswa kuwa jasiri na kusimama imara katika imani yetu na kuilinda, kuipigania wakati wote na ikiwezekana hata kwa gharama ya maisha yetu. Maelfu ya wafiadini wako mbinguni kwa kuwa waliifia imani yao kwa Kristo. Hawakuwa watu wa pekeee tofauti na sisi. Si kusema hawakupenda maisha ya hapa duniani. La! Ila imani yao na upendo mkubwa kwa Kristo ndio uliowafanya waone maisha ya duniani si kitu. Kwa Ubatizo na kwa Kipaimara tumepokea kutoka kwa Roho Mtakatifu paji la uimara. Tutumie paji hili kuilinda imani yetu ya Kwa kristo kwani anastahili yeye Mwana-Kondoo aliyechinjwa, kuupokea uweza na utajiri, hekima na nguvu, heshima na utukufu. Baraka na heshima, utukufu na uweza una yeye aketiye juu ya kiti cha enzi, hata milele na milele. Amina.

Dominika 3 Pasaka
28 April 2022, 17:55