Dominika ya III ya Kipindi cha Pasaka: Uinjilishaji Duniani Kote
Na Padre Efrem Msigala, OSA, - Roma.
Karibu mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican na msomaji wa Vatican News katika tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya tatu ya Pasaka ya Mwaka C wa Kanisa. Katika Injili ya Dominika ya Pili ya Pasaka, Yohane alituambia kwamba Yesu aliwatokea wanafunzi siku ya kwanza ya juma walipokuwa wamejifungia ndani kwa hofu. Leo, Yohane anatuambia kwamba Yesu anaonekana kwao baada ya kujaribu kuvua usiku kucha bila kufanikiwa. Hivyo anaonekana kwa mara ya tatu na kula pamoja nao. Somo la kwanza Matendo ya Mitume 5, 27-32.40-41: Baada ya Pentekoste wanafunzi walianza kutekeleza utume waliokuwa wamepokea, wakihubiri Habari Njema ya Yesu Kristo. Pamoja na kukatazwa waliendelea kuhubiri bila woga. Na walipopelekwa mbele ya baraza walisema hatuwezi kuacha kumtii Mungu sababu ya wanadamu. Na walipopigwa viboko wakizuiwa kutaja jina la Yesu waliendelea kufanya kazi hiyo kwa furaha. Somo la Pili: Ufu 5, 11-14: Yohane anaelezea maono ya sifa zenye kuimbwa juu ya Mwanakondoo kwa kila kiumbe mbinguni na duniani. Ni sehemu ya utume kwamba wanadamu sio tu kwamba wanamjua Kristo, lakini pia wanamwabudu kama Mungu na Bwana. Injili ya Mtakatifu Yohane Sura ya 21, 1-19 ambayo ni ya mwisho, inatuweka, kwa mara nyingine tena, karibu na Bahari ya Tiberia na inatuambia juu ya kutokea kwa mara ya tatu kwa Yesu mfufuka kwa Petro na wenzake.
Mtume Petro na marafiki zake, wakiwa wamekata tamaa, wanaondoka Yerusalemu na kurudi nyumbani, Kapernaumu, kwenye Bahari ya Tiberia, kwa kazi yao ya zamani waliyozoea kufanya kabla ya kuitwa kuwa Mitume. Wamerudi kwenye utaratibu wa kawaida. “Ninaenda kuvua samaki”, Petro anawaambia wenzake nao wanamfuata. Yote yalianzia Galilaya pale Yesu alipokuwa akitembea kando ya ziwa, aliwaona Simoni na Andrea na kuwaambia: “Njooni nifuate nami nitawafanya ninyi wavuvi wa watu.” Mara moja wakaziacha nyavu zao na kumfuata Mt.1:16-20. Na yote yanaishia Galilaya anaooneka kwa mara ya tatu baada ya ufufuko. Katika wito wa kwanza walimfuata Yesu wa Nazareti. Mtu ambaye alizungumza kwa uzuri, ambaye hakuhubiri tu katika sinagogi bali pia katika viwanja, ambaye aligusa watu wasioweza kuguswa, ambaye alifanya ishara za ajabu na ambaye aliwaahidi ufalme mpya na uhuru mpya. Katika mwito wa pili baada ya ufufuko na wa mwisho wanapaswa kumfuata Yesu Kristo, ambaye alikuwa amekufa lakini sasa yu hai na amefanywa kuwa Bwana na Mwokozi.
Yesu anajitokeza bila kujulikana kwao, anakuwa mgeni kwao, anawaamuru watupe nyavu upande wa kuume wa mashua, yaani upande wa mashariki, yaani kwa watu wasio Wayahudi ambao bado hakuna aliyeupeleka ujumbe huo mpaka pembezoni, kwa ulimwengu mzima. Upande wa kushoto, ukitazama Galilaya, kulikuwa na ulimwengu wa Wayahudi ambao tayari walikuwa wamepata nafasi yao. Idadi ya samaki 153 inawakilisha watu wa kila rangi, lugha na kabila hivyo ulimwengu mzima. Na baada ya kuvua samaki, Yesu anawapa kifungua kinywa kizuri. Wanapata kifungua kinywa pamoja naye. Baada ya kufungua kinywa tunasikia suali la Yesu kwa Petro. “Je, una nipenda kuliko hawa?” lisha kondoo wangu na mara tunza kondoo wangu nk. Swali hili ameuliza mara tatu na baada ya jibu anasisitiza lisha kondoo wangu na mara tunza kondoo wangu.
Mpendwa msikilizaji: Mambo kadhaa yanatugusa kwa namna ya pekee:jambo la kwanza Simoni Petro bado anaonyeshwa katika nafasi ya kiongozi: anapotangaza kwamba anaenda kuvua samaki, wanafunzi wengine wanafuata. Wanatumia usiku kucha wakivua lakini hawakufanikiwa. Yesu anawaita kutoka ufuoni, lakini kama vile Yesu alipomtokea kwa mara ya kwanza Mariamu Magdalena, wanafunzi hawamtambui mara moja. Jambo la pili ambalo ni la ajabu wanafuata maagizo ya mgeni wasiye mjua na wanafanikiwa kupata samaki wengi, tunaambiwa idadi yake ni 153. Ni wakati huu ambapo mmoja wa wanafunzi (“mwanafunzi ambaye Yesu alimpenda” ambaye ni Yohana) anatambua kwamba ni Yesu amewatokea. Aliposikia habari hizo, Simoni Petro aliongoza njia tena, akiruka kutoka kwenye mashua na kuogelea hadi ufuoni. Wanafunzi wengine wanafuata kwenye mashua, wakiwakokota samaki. Wanafunzi walipata samaki kwa idadi iliyotajwa hapo juu.
Jambo jingine la ajabu ni kwamba wanakuta Yesu ameandaa kitoweo yaani samaki na mkate juu ya moto wa makaa. Yesu anawaagiza wanafunzi walete samaki wao pia. Yesu ndiye mwenyeji wa mlo ulioandaliwa, aliwalisha wanafunzi mkate na samaki. Katika maelezo haya tunaona madokezo ya muujiza wa kuzidisha mikate na samaki katika Injili ya Yohane sura ya 6. Pia kuna madokezo ya Ekaristi, sisi pia tunalishwa na Yesu katika mkate na divai ambayo imekuwa Mwili na Damu yake. Pamoja na hayo mpendwa msikilizaji: Yesu alifanya pia mazungumzo na Petro akimuuliza swali moja mara tatu. Petro aliyemkana mara tatu na baadaye kuomba toba na akasamehewa. Baada ya ufufuko Yesu anataka Simoni Petro adhihirishe upendo wake kwake lakini pia akikabidhiwa majukumu: “Lisha wana-kondoo wangu . . . Chunga kondoo wangu. . . Lisha kondoo wangu.” Halafu anamwembia “ulipokuwa kijana ulizoea kuvaa mwenyewe na kwenda unakotaka, lakini utakapokuwa mzee kuna watu watakuvalisha na kukupeleka usikotaka wewe... kama kiongozi ataishi kadri ya miongozo yake.
Amri hizi zinaonesha kwamba Mtume Petro anapaswa kuwa kama Yesu, hata kutoa dhabihu kwa ajili ya kundi. Kama vile Yesu alivyomlisha Petro katika mlo pia nasi Yesu anatulisha katika Ekaristi. Nasi pia anatuuliza swali hilo kama tunampenda kuliko mengine yote. Je tunampenda Mungu kuliko mengine yote? Je, Mungu anapewa daima nafasi ya kwanza katika maisha yetu? Jambo jingine ni Utume wa Kanisa. Wainjili wote wanne kila mmoja anaonesha umhimu wa utume ambao Kanisa limekabidhiwa. Utume ambao Yesu ameliachia Kanisa ni kuendeleza ujumbe wake kwa ulimwengu wote. Yohane anatumia taswira ya Bahari kama sura ya ulimwengu. Kwa ufupi, utume wa Kanisa, katika bahari ya dunia, si mwingine ila ule wa kuwa wavuvi wa watu wote bila ubaguzi na kuwaongoza kwenye bandari salama ya imani na umilele. Kama walivyofanya Mitume waliendeleza kazi ya Bwana bila woga hata kama walipata upinzani lakini hawakurudi nyuma. Petro kama kiongozi alidhihirisha hilo katika somo la kwanza pale walipokuwa wakihubiri habari za Kristo mfufuka bila woga na kutorudi nyuma walipotishiwa.
Pamoja na hayo namna ya kutekeleza utume ni ibada, hasa mtazamo wa kumwabudu Yesu Kristo, Mwana-Kondoo aliyechinjwa. “Anastahili kuupokea uweza, na mali, na hekima, na nguvu, na heshima, na utukufu, na sifa” (Somo la pili). Ili utume wa mitume utimie kikamilifu, kuhubiri lazima kuelekeze kwenye ibada. Kujua kwamba Kristo alikufa na kufufuka kwa ajili yetu, bila kumwabudu kama Mungu wetu na Bwana, utume unakuwa haujakamilika. Tunaalikwa kumwabudu Yesu katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu. Kuwa na utulivu katika Misa zetu na hasa wakati wa mageuzo tukitambua kuwa Kristo anashuka kati yetu. Kila mmoja amwabudu kimya kimya.