Dominika ya Matawi: Kristo Yesu Mfalme Wa Amani: Mateso & Kifo
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya Matawi. Dominika hii ina sura mbili - furaha na huzuni. Sura ya furaha tunaionja katika sehemu ya kwanza ya ibada ya Dominika hii, tunapokumbuka siku ile Yesu alipoingia Yerusalemu kwa shangwe akiwa amepanda mwanapunda kama ishara ya Mfalme wa amani na utakatifu wake ili apate kutimiza fumbo la Pasaka. Watu walimlaki kwa shangwe wakiwa na matawi ya mitende, huku wakiimba nyimbo za furaha wakisema: “Hosana, mwana wa Daudi; ndiye mbarikiwa, yeye ajaye kwa jina la Bwana, Mfalme wa Israeli: Hosana juu mbinguni (Mt. 21:9). Ilikuwa siku sita kabla ya Pasaka, wakati Bwana alipoingia mjini Yerusalemu, watoto walimlaki; nao walichukua matawi ya mitende mikononi, wakapaaza sauti wakisema: Hosana juu mbinguni: Mbarikiwa wewe uliyekuja na wingi wa rehema yako. Sisi nasi tunafanya maandamano ya kuingia kanisani kwa shangwe tukiwa na matawi mikononi yaliyobarikiwa kama ishara ya kuingia Yerusalemu mpya yaani mbinguni kama sala inayotumika kuyabariki matawi inavyosema: “Ee Mungu Mwenyezi wa milele, uyatakase matawi haya kwa baraka yako.
Nasi tunaomfuata Kristo Mfalme kwa shangwe, utujalie tufike Yerusalemu ya milele kwa jina lake. Kumbe tunapofanya haya maandamano sio kwamba tunaiga ama kurudia mambo ya kihistoria yaliyopita, bali ni ishara tu ya nje ya kumwungama Kristo aliyeteseka, akafa na kufufuka kwa ajili yetu sisi kuwa ni mfalme wetu. Baada ya matawi kubarikiwa kwa kunyunyiziwa maji ya baraka wakati huo watu wakiwa kimya wakitafakari inasomwa Injili inayosimulia kuingia kwa Yesu Yerusalemu kwa shangwe la Kimasiya. Katika mwaka huu C tunasoma Injili ya Luka 19:28-40. Baada ya kusikiliza hotuba fupi ndipo yanaanza maandamano kwa shangwe kuelekea kanisani na kuingia. Maandamano haya yanapaswa kupambwa kwa nyimbo za furaha na kumsifu Mungu kwa sauti kuu kwa matendo makuu aliyotundea, tukimshangilia Yesu “mbarikiwa Mfalme ajaye kwa jina la Bwana; amani duniani, na utukufu huko juu mbinguni” Katika maandamano haya mtumishi wa chetezo hutangulia mbele akiwa amechukua chetezo chenye kufuka moshi. Nyuma yake anafuata mtumishi mwenye kuchukua msalaba uliopambwa, kati ya watumishi wawili wenye kuchukua mishumaa iwakayo. Kisha anafuata Padre na watumishi wengine, na mwisho wanakuja waamini, wote wakiwa na matawi wakiimba kwa shangwe. Yesu anatuonya kuwa tusipoimba kwa shangwe na kushangilia kwa furaha au tukinyamaza “mawe yatapiga kelele”.
Sehemu ya pili ya ibada ya Dominika ya Matawi ni kukumbuka mateso ya Yesu Kristo yanayotuingiza katika Jumaa Kuu la kuadhimisha fumbo la ukombozi wetu, fumbo la pasaka yaani mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Hili ni adhimisho Kuu moja linalodumu kwa muda wa siku tatu mfululizo yaani Alhamisi Kuu, Ijumaa Kuu na Jumamosi Takatifu. Alhamisi Kuu, tutaadhimisha karamu ya mwisho yaani: Karamu ya mwisho mwisho aliyokula Yesu na wanafunzi wake muda mfupi kabla ya kukamatwa na kuanza kuteswa hadi kufa msalabani. Ni siku aliyoweka Sakramenti za Ekaristi Takatifu na Upadre na Amri ya mapendo. Ijumaa Kuu tutaadhimisha kifo cha Kristo msalabani na Jumamosi Kuu tutaomboleza kwa masikitiko makuu tukingojea ufufuko wa Yesu Kristo tunaoanza kuusherehekea kwa kesha la Pasaka ambapo kunakuwa na ibada ya Mwanga na kupigwa kwa mbiu ya kumshangilia Kristo mfufuka. Maadhimisho haya yanakuwa na maana kwa walioziishi vyema siku arobaini za Kwaresima, siku za mfungo mtakatifu, siku za kusali, kufunga, kutafakari neno la Mungu na kutenda matendo ya huruma na upendo ili kujipatanisha na Mungu.
Katika sehemu hii ya pili Kanisa linaweka mbele yetu mateso makali aliyoyapata Kristo na kutueleza mapato yake, ushindi dhidi ya dhambi na mauti, ushindi unaodhihirishwa na utukufu wa ufufuko wake kama anavyosali Padre kwa niaba ya jamii ya waamini katika sala ya mwanzo-koleta akisema; “Ee Mungu Mwenyezi wa milele, ulitaka Mwokozi wetu atwae mwili na kuteswa msalabani ili wanadamu wapate kufuata mfano wa unyenyekevu wake. Utujalie kwa wema wako tuweze kuwa na uvumilivu kama yeye, na kustahili kuishi mateso ya Yesu Kristo ambayo tunaweza kuyafahamu vizuri tu, tukiyatazama pamoja na ufufuko wake. Kwa hiyo liturjia ya adhimisho hili imejaa mwanga wa pasaka ikitudhihirishia kuwa Kristo si mshindwa bali ni mshindi. Katika somo la kwanza la Nabii Isaya (Isa. 50:4-7); tunatafakari utabiri wa Mtumishi wa Mungu aliye mwaminifu katika kazi yake, ambaye haogopi magumu wala mateso. Mtumishi huyu ndiye Yesu aliyevumilia mateso makali ili atukomboe kutoka utumwa wa dhambi na mauti. Kwa uaminifu wake, Mungu alimpa uwezo ili aweze kuwafundisha na kuwapa matumaini wanyofu, wanyonge, maskini na waliovunjika moyo. Kwa usikivu wake, Mungu alimwamsha asubuhi baada ya asubuhi, alizibua sikio lake apate kusikia Neno lake, alimpa nguvu na uvumilivu dhidi ya watesi wake. Mtumishi huyu, hakuficha uso wake asipate fedheha na kutemewa mate, hakukata tamaa bali aliwatolea watesi wake mgongo wake walipoamua kumchapa mijeledi, walipoamua kumng’oa ndevu mashavuni mwake, hakuficha uso wake. Kwa mateso haya sisi tumekombolewa.
Katika somo la pili la Waraka wa Mtume Paulo kwa Wafilipi (Flp. 2:6-11); tunaona na kuonja matunda ya utii, unyenyekevu na uvumilivu wa Yesu Kristo, mtumishi mwaminifu wa Mungu. Dhambi na mauti viliingia katika historia ya mwanadamu kwa kosa la kukosa utii kwa Mungu. Kwa utii wa Kristo, dhambi na mauti vimeangamizwa. Kwa kutotii kwa Adamu na Eva tulitengwa na Mungu, kwa kutii kwake Kristo tumeunganishwa na Mungu. Nasi tunaalikwa kutii. Tutii amri za Mungu na za Kanisa. Tutii mafundisho ya Kanisa, tuwatii na kuwasikiliza wazazi na viongozi wa Kanisa kwani; asiyesikia la mkuu huvunjika guu. Tukubali kutii kuwa sisi kwa asili tu binadamu, lakini tusiung’ang’anie kwa nguvu ubinadamu wetu bali tuuachilie, tujitwalie hali ya kimungu ili tukaishi milele yote mbinguni kwa Mungu Baba.
Injili ilivyoandikwa na Luka (Lk. 22:14; 23:56); inasimulia historia ya mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo. Kawaida siku ya Dominika ya Matawi na Ijumaa kuu injili inasomwa pasipo mishumaa wala chetezo na bila utangulizi wala ishara ya msalaba. Injili husomwa na shemasi baada ya kuomba na kupokea baraka ya Padre. na kama hakuna shemasi husomwa na Padre, lakini pia ili kuipanda liturujia hii injili huweza kusomwa na walei kwa kuimba, lakini sehemu ya Kristo lazima isomwe na Padre. Yesu anakamatwa akiwa bustanini Gethsemane akisali, naye bila ubishi anaanza safari ya ukombozi kuelekea Golgota kusulubiwa. Safari yenye mateso makali, anabebeshwa msalaba mzito, anafanyiwa dhihaka, anapigwa mijeledi, anavuliwa nguo, anatemewa mate, anatukanwa, anasulubishwa msalabani na hatimaye anakufa kwa sababu ya dhambi zetu na kuonekana kuwa mtu aliyelaaniwa na Mungu (Kum. 21:22-23). Ni mateso makali mno na kifo cha aibu mno. Lakini kwa kifo chake kilivyokuwa cha pekee, dunia ilitetemeka, jua lilififia, kukawa giza juu ya nchi, pazia la hekalu likapasuka mara mbili, walioshuhudia walisadiki uaguzi wa manabii na kusema hakika huyu alikuwa mwana wa Mungu. Naye alipochomwa ubavu kwa mkuki, vilitoka damu na maji, ndizo chemchemi za Sakramenti za Kanisa.
Katika simulizi la mateso ya Yesu, umati wa watu walipiga makelele wakisema: Asulubishwe! Asulubishwe! Nasi kwa mawazo, maneno na matendo yetu maovu na kwa dhambi zetu tunatoa mlio na makelele hayo hayo: Msulubishe! Msulubishe! Petro alijaribu kupambana na nguvu za giza kwa upanga. Kristo alipambana na kumshinda shetani si kwa mapanga na vitisho bali kwa uvumilivu wake, kwa unyenyekevu wake, kwa upole wake na kwa utii wake kwa Mungu Baba. Je, sisi hatuna fikra kama za Petro za kupambana na nguvu za shetani na Ibilisi kwa upanga wa giza, maseng’enyo, malumbano, mapigano, visasi na fitina? Je, hatusemi kila siku katika makundi ya watu; Msulubishe! Msulubishe! Mwondoshe! Mwondoshe! Tukumbuke kuwa hatupaswi kumpigania Kristo kwa upanga bali kwa ushuhuda wa maneno na matendo mema.
Mtume Petro alimkana Yesu mara tatu akisema mimi si mfuasi wa mtu huyu, akasisitiza mimi simjui mtu huyu. Sisi nasi tunafanya jambo hilo hilo kila tunapoionea aibu Injili, tunaporudi nyuma kiimani na kukosa matumaini kwa Kristo kwa sababu ya matatizo na magonjwa na hivyo kuamua kutafuta suluhu katika dhambi. Jogoo amekwisha wika mara ya tatu, tunaalikwa kujirudi, tujiweke chini ya msalaba, kwani hatuna tumaini lingine, japo kwao wanaopotea msalaba ni kikwazo na upuuzi, kwetu sisi ni nguvu ya Mungu, alama na bendera ya ushindi, kama tukiutazama kwa imani na moyo wa toba. Hata tunaposikia; Hatumjui mtu huyu! Mwondoshe! Mwondoshe! Msulubishe! Msulubishe! Tusikate tamaa au kukwazika na kurudi nyuma, bali tusonge mbele tukimtumainia Mungu huku tukimshuhudia Kristo, Mkombozi wa maisha yetu. Katika hili juma kuu tunalolianza, tuombe neema ya kuwa wasikivu na watii, tukisali pamoja na mtumishi wa Mungu kwa unyenyekevu tukisema; “Bwana Mungu amenizibua sikio langu, wala sikuwa mkaidi, huniamsha sikio langu lipate kusikia kama watu wafundishwao”. Tukubali kufundishwa na kuelekezwa. Tuwe watii. Tujipatanishe na Mungu ndipo tutakapokuwa na sababu ya kufurahia siku ya Pasaka na tunuie kutorudi nyuma tena mpaka tutakapomaliza safari ya maisha yetu hapa duniani, tukafurahi milele yote katika Pasaka ya Mbinguni.