Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya Matawi: Huu ni mwanzo wa maadhimisho ya Mafumbo ya Wokovu, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya Matawi: Huu ni mwanzo wa maadhimisho ya Mafumbo ya Wokovu, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. 

Dominika ya Matawi Mwaka C wa Kanisa: Mwanzo wa Juma Kuu

Yerusalemu ni mji Mtakatifu ambao umesheheni alama na ishara za Kipasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Yerusalemu ni kilele cha kazi nzima ya ukombozi iliyotekelezwa na Kristo Yesu. Dominika ya Matawi ni mwanzo wa maadhimisho ya Juma kuu. Kristo Yesu anaingia mjini Yerusalemu kwa unyenyekevu, kama Mfalme wa amani, haki na upendo.

Na Gaston George Mkude, - Roma.

Dominika ya Matawi Mwaka C: Yesu aliye chemchemi ya huruma misericordia anasulubiwa kati ya wahalifu wawili (Miseri). Amani na Salama! Mwinjili Luka kama zilivyo Injili pacha au zenye muono unaonafanana ndizo za Mathayo na Marko, na hata katika Injili ya nne, yaani ya Yohane, naye anatupa simulizi la mateso yake Bwana wetu Yesu Kristo. Zaidi sana ni katika Injili ya Luka tunaendelea kuonja Huruma na Upendo wake Yesu hata katika mateso yake na hasa pale juu msalabani. Hakika ni katika Injili ya Luka tunaweza kuona waziwazi juu ya dhana ya Mungu aliye upendo na mwenye huruma daima! Katika bustani ya Getsemani wakati wa kukamatwa kwake Yesu, tunaona Mtume Petro anachomoa upanga wake na kumkata sikio mtumishi wa kuhani mkuu. Kitendo ambacho Yesu anamkaripia Petro, na kinyume chake anamponya mtumishi yule, ni mwaliko wa kutolipa uovu kwa uovu na badala yake kusamehe na hata kuponya majeraha ya maadui zetu. Ni wito wa kusamehe daima hata kwa wale wanaotishia usalama wa maisha na uhai wetu, ndio huruma na msamaha wa Mungu kwetu daima. Akiwa katika nyumba ya kuhani mkuu, Petro anamkana Yesu mara tatu. Wainjili ndugu wote wanatuonesha jinsi Petro alivyojutia kitendo chake kwa kulia, ila ni Mwinjili Luka pekee anatuonesha kuwa Yesu aligeuka na kumwangalia Petro.

Kwa Kigiriki kitenzi kinachotumika siyo βλεπω (blepo) na badala yake anatumia neno εμβλεπω (emblepo). Neno blepo linamaanisha kuangalia ila hapa Mwinjili Luka anatumia emblepo likimaanisha sio tu kuangalia kwa juujuu au kwa nje nje ila kuangalia kwa ndani kabisa. Ndio kuangalia ndani na kuelewa undani wa mtu na hali yake halisi. Ni Mungu anayetuangalia ndani mwetu na kuona umaskini na uduni wetu, udogo na unyonge na udhaifu wetu kwani daima sisi mbele yake ni miseri, tunaohitaji huruma na rehema zake (Misericordia). Jicho la Yesu kwa kila mmoja wetu, sio la hukumu bali uangalia kwa jicho la huruma na upendo, ni kuangalia kwa kuelewa hali yetu ya ndani na mapungufu na mahangaiko yetu ya kibinadamu (Miseri). Ni Yesu pekee kwa jicho lake la Kimungu lenye huruma, ndilo pekee linaloweza kuangalia ndani mwetu na kuona unyonge na uduni wetu. Ni mwaliko kwetu tulio wafuasi wa Yesu kuangalia wengine kwa jicho la huruma na upendo na si kwa jicho na hukumu. Wakati wa mateso yake Yesu tunaona wanafunzi na wafuasi wake wanakosa kuwa waaminifu kwake; Yuda anamsaliti, Petro anamkana, karibu wote wanakimbia (Marko 14:50). Wakati Wainjili wengine wakionesha jinsi walivyokosa kuwa karibu na Bwana na Mwalimu wao, ni Mwinjili Luka pekee anatuonesha kuwa walisimama kwa mbali. (Luka 23:49). Na hata walipolala hatuoni akionesha kama Mwinjili Marko (14:37) Simoni umelala? Umeshindwa kukesha pamoja nami hata kwa saa moja?

Dominika ya Matawi ni mwanzo wa Juma kuu la mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu.
Dominika ya Matawi ni mwanzo wa Juma kuu la mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu.

Mwinjili Luka anatupa sababu ya kulala kwao kuwa walilala kwa sababu ya huzuni, ndio kusema anajaribu kuonesha jinsi jicho la Yesu lilivyowaona wanafunzi na wafuasi wake wakati wa majaribu yale magumu na makubwa kwao. (Luka 22:45) Mwinjili Luka ni kielelezo cha mchungaji wa Huruma ya Mungu, si kwamba anatetea dhambi, bali anaonesha jinsi Mungu anavyotuona na kuelewa udhaifu wa kibinadamu. Na ndio fundisho kubwa ndugu zangu tunaposoma na kutafakari mateso yake Bwana wetu Yesu Kristo kama yalivyoandikwa na Mwinjili Luka. Mfuasi wa Yesu ni kinyume na mantiki ya ulimwengu huu, ni mmoja anayesamehe na kuwapenda hata maadui zake. (Luka 6:27-36) Na ndio ujumbe ambao Petro Mtume anatuandikia katika Waraka wake (1Petro 2:23) hata katika mateso na madhulumu hatuna budi kujibu ubaya kwa ubaya. Ni mwaliko wa Mwinjili Luka kwa kila mfuasi wa Yesu Kristo kuishi maneno yale aliyoyatamka Yesu pale msalabani kabla ya kufa kwake, ni maneno ya msamaha: (Luka 23:34) Baba uwasamehe kwani hawajui watendalo.  Ni msamaha sio tu kwa wale maaskari wa Kirumi, au wale waliogawana mavazi yake bali hata kwa viongozi wa dini waliomshtaki. Hivyo msamaha ndio mwaliko kwa kila mfuasi wa Yesu. Tunakutana pia na shahidi yule wa kwanza Stefano akitamka maneno yale yale ya Yesu pale juu msalabani. (Matendo 7:60)

Maneno ya Yesu wakati wa kuwekwa kwa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu karibu sote tunayafahamu na kuyakumbuka kwa moyo kwani husemwa na kutamkwa katika kila adhimisho la Ekaristi Takatifu. Ila yafaa tukumbuke kuwa ni Mwinjili Luka pekee anaongeza maneno haya: FANYENI HIVI KWA KUNIKUMBUKA MIMI. (Luka 22:19) Kuumega mkate ni mwaliko kwetu kuishi fumbo hilo la kujitoa nasi kama alivyojitoa yeye kwa upendo kwa kuukomboa ulimwengu nasi kujitoa vile vile kwa ajili ya wengine katika maisha ya siku kwa siku. Adhimisho la Ekaristi ndio chemichemi na kilele cha maisha ya kila mwamini.  Fanyeni kwa kunikumbuka mimi, ni kutenda na kufanya kama alivyofanya yeye, ni kuwa wenye huruma na upendo kama yeye. Kuumega mkate hakuna maana kama hatupo tayari kuwa na jicho lenye huruma na upendo kama lake Yesu Kristo. Kushiriki Ibada ya Ekaristi Takatifu ni kutaka kushiriki fumbo zima la maisha yake Yesu Kristo, ni kuwa kielelezo hai wa Injili, kuwa mjumbe wa Habari Njema ya Wokovu ya Huruma na Upendo.

Saratani au ugonjwa mkubwa katika jumuiya zetu ni mapambano na vita ya kutaka kuwa na nafasi za kwanza, kuwa wa muhimu kuliko wengine, kuwa watawala wa wengine, kuwa na vyeo vya kutupatia sifa na ukuu na hata matajamara. Ni katika hali hiyo basi magomvi, majungu, migawanyiko inatokea kati yetu. Na ugonjwa huu si tu upo nyakati zetu bali hata nyakati za Yesu. Ni dalili kuwa bado hatujailewa vema Injili ya Yesu Kristo, mwaliko wa kuiga maisha yake ya kukubali kudharaulika na kuwa wa mwisho na kuwa mtumishi wa wote. Ni katika udogo na utumishi hapo tunakuwa kweli wafuasi wa Yesu Kristo. Ni katika karamu ya mwisho tunaona pia Mwinjili Luka anatuonesha fundisho la msingi la jinsi gani tuenende sisi rafiki na wafuasi wake Yesu Kristo. (Luka 22:24-27) Yesu anatumia fursa hiyo pia kuwafundisha rafiki zake kuwa katika jumuiya ya waamini mantiki inayopaswa kutawala ni ile yake Yesu aliye mtumishi na sio ya watawala wa ulimwengu huu. Ni kuwa mtumishi na mdogo, na sio kuwatawala wengine iwe kwa mawazo au kwa namna zangu, bali daima anabaki Yesu mwenyewe kama kielelezo katika maisha ya jumuiya ya Wakristo.

Dominika ya Matawi ina umuhimu sana katika maisha na utume wa Yesu.
Dominika ya Matawi ina umuhimu sana katika maisha na utume wa Yesu.

Agony”, ni neno la Kiingereza, nikiri nakosa neno muafaka kwa Kiswahili lakini mara nyingi tunaweza kusema ni neno tunalolitumia kuonesha hali ya mateso makali ya kimwili na kiroho aliyokuwa nayo Yesu kabla ya kifo chake pale juu msalabani. Neno hilo haswa lilitumika kuonesha hali ya mapambano na mashindano waliyokuwa nayo wale waliofanya mashindano ya mbio au riadha. Na ndio haswa linapaswa kueleweka katika muktadha wetu wa leo. Tangu mwanzoni mwa kazi yake tunaona Yesu yupo katika mapambano dhidi ya yule mwovu.  Hata baada ya kumjaribu kila aina ya jaribu shetani alimwacha Yesu kwa muda. (Luka 4:13) Hivyo hata katika mateso yake bado shetani aliendelea kumjaribu Yesu. Na ndio shetani akamwingia Yuda Iskariote. Yesu kama ambavyo walifanya wana riadha alipaswa kufanya maandalizi na ndio Mwinjili Luka anakazia juu ya SALA.  Ni katika wakati wa agonia yake pale bustanini anawaalika pia wanafunzi wake kukesha katika sala ili wasijeingia majaribuni.  Pale bustani alijitenga nao na kupiga magoti na kusali na hata akaingia katika agonia…lakini alisimama tena na kwenda kuwaalika wanafunzi wake kuamka na kusali. (Luka 22:39-46)

Ni mkazo katika sala na ndio Yesu anatualika nasi kusali daima kwani ni kwa njia ya sala pekee nasi tunaweza kumshinda yule mwovu, yaani shetani. Ni kwa njia ya sala tunajaliwa neema, yaani nguvu za rohoni kuweza kupokea na kuubeba msalaba katika maisha yetu. Ni katika muktadha huo wa kusali pale bustanini tunaona Mwinjili Luka anatuonesha juu ya uwepo wa malaika kutoka mbinguni. (Luka 22:43) Ni matunda ya sala. Uwepo wa malaika katika Biblia ni uwepo wa Mungu mwenyewe anayeingia katika hali zetu na kutujalia neema na nguvu zake za Kimungu. Ni kwa njia ya sala pekee tunaona Yesu anaingia katika majadiliano na Baba yake na hivyo kuweza kuelewa mpango wa Mungu Baba na kupokea kikombe kile cha mateso kwa ajili ya kuukomboa ulimwengu. Luka Mwinjili anatuonesha nasi kuwa ni kwa njia ya sala pekee nasi tunaweza kuvishinda vishawishi vya kutokubali mpango wa Mungu katika maisha yetu ya kila siku.  Ni katika agonia hiyo na sala, Mwinjili Luka aliyekuwa tabibu anagusia kuwa Yesu alitokwa jasho la damu. (Luka 22:44) Nini maana yake kwani tayari tunaona Mungu alituma malaika wake, ila hali hii ya ematoidrosi ilimaanisha ile hali aliyekuwa nayo kila mwanariadha au mwanamichezo wakati mashindano yalipokaribia sana. Ni kukosa utulivu wa ndani, ni mahangaiko ya ndani kabisa, ni mateso ya ndani kabisa yaliyosumbua sio tu mwili bali pia na roho na akili.

Mwinjili Luka anatuonesha kuwa Yesu alikutana na Herode, na ndio yule mwana wa Herode mkubwa aliyewaua watoto wa kiume chini ya miaka miwili wakati wa kuzaliwa kwake Yesu pale Betlehemu. Herode alisikia juu ya matendo na mafundisho yake Yesu wa Nazareti ila hakuwa amepata bahati ya kuonana naye kabla na hivyo anatumia fursa hii kumtaka Yesu afanye muujiza mbele yake na kumuhoji Yesu ila tunaona Yesu hajibu neno. Kwake Yesu ni mtenda miujiza tu na hivyo anataka kutumia fursa hii naye ajionee hiyo miujiza. Mwinjili Luka anatuonya nasi kwani mara nyingi tunasukumwa kwenda kwa Yesu ili atende tu miujiza katika maisha yetu, Yesu ni mtenda miujiza. Hakika tukimwendea na mtazamo huo hatutapata jibu kutoka kwake. Ukristo ni kuishi Habari Njema, ni maisha ya upendo na huruma kwa wengine na sio soko la miujiza. Yesu anatuonya kuwa tukiwaza na kufikiri namna hiyo basi tunakuwa ni watu tuliopotoka kwa kushindwa kumwelewa na kuelewa misheni yake ya kuutangaza na kuusimika Ufalme wa Mungu ulimwenguni. (Matayo 16:4) Mwinjili Luka pia anagusia juu ya wanawake walioambatana na Yesu hata wakati wa maisha yake ya utume wa kuhubiri ufalme wa Mungu. (Luka 8:1-3) Ni Mwinjili Luka pekee anagusia kuwa hata katika njia ile ya mateso Yesu anakutana na wanawake wanaomlilia na kupiga vifua vyao. (Luka 23:27-31) Wanawake hawa wanamlilia Yesu na pia wanawalilia wale waliomtesa Yesu bila kosa pale msalabani.

Mama Kanisa anakumbuka: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu.
Mama Kanisa anakumbuka: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu.

Pale Msalabani alisulibiwa pamoja na wengine wawili. Ni Mwinjili Luka anatuonesha kuwa mmoja wapo alimtukana Yesu ila mwingine alimkaripia na kumuita Yesu kwa jina ili amkumbuke anapoingia katika ufalme wake. Na ndio tunaona Yesu anamsamehe dhambi zake na kumhakikishia paradiso, yaani furaha ya milele mbinguni. Mwanzoni mwa Injili ya Luka tunaona Yesu anajifunua kwanza kwa wachungaji, watu wa mwisho, waliodharauliwa, watu najisi kadiri ya dini ya Kiyahudi. Wakati wa utume wake daima alikula na kuambatana na wadhambi, watoza ushuru na malaya na wadhambi. Hata pale juu msalabani hafi kati ya watakatifu wawili bali kati ya wahalifu wawili, ni kati ya wale aliowapenda daima katika maisha yake, yaani wadhambi. Ni mwaliko kuwa amekuja ili kuwavuta na kuwapeleka wadhambi kwa Mungu Baba, na ndio ukombozi yaani kututoa katika hali zetu za dhambi na kushiriki maisha pamoja naye na ndio maisha ya kuwa wana wa Mungu, kuwa rafiki wa Mungu, kushiriki utakatifu wa Mungu. Tunaalikwa kufa pale juu msalabani pamoja naye lakini tubaki na moyo wa toba wa kumuomba atukumbuke nasi katika ufalme wake, katika furaha ya milele mbinguni kama alivyofanya yule mmoja aliyesulubiwa pamoja na Yesu. Nawatakia tafakari njema ya Dominika ya Matawi na maadhimisho mema ya Juma Kuu, yaani Mateso, Kifo na Ufufuko wake Bwana wetu Yesu Kristo. Heri ya Pasaka na amani tele ya Kristo Mfufuka!

05 April 2022, 14:49