Tafuta

Dominika ya Matawi ni mwanzo wa maadhimisho ya ukombozi wa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu. Dominika ya Matawi ni mwanzo wa maadhimisho ya ukombozi wa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu.  

Dominika ya Matawi: Yesu Kristo Anaingia Yerusalemu Kwa Shangwe!

Dominika ya matawi imegawanyika katika sehemu mbili: sehemu ya kwanza Yesu kuingia Yerusalem kwa shangwe huku akishangiliwa na watoto wa Wayahudi waliobeba matawi ya mitende mikononi mwao. Sehemu ya pili ni simulizi la mateso na kifo cha Kristo Yesu, mwaliko kwa waamini kutubu na kumwongokea Mungu yatari kutembelea katika mwanga wa Kristo Mfufuka. Pasaka

Na Padre Efrem Msigala, OSA, - Roma.

Karibu mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican na msomaji wa Vatican news katika tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya Matawi. Dominika ya matawi imegawanyika katika sehemu mbili: sehemu ya kwanza Yesu kuingia Yerusalem kwa shangwe. Nasi huanza ibada yetu kwa kuingia kanisani kwa shangwe. Huanza na kubariki matawi ambayo waumini wanakuwa wameshika mikononi. Wakiwa nje ya kanisa, jirani au mbali na kufanya maandamano kwa shangwe kuelekea kanisani. Au kuanzia mlangoni mwa kanisa kadri ya mazingira. Waumini wakiwa wamekusanyika nje husomwa Injili na mwaka C inasomwa injili ya Luka 19: 28-40 na baada ya hapo maelezo mafupi. Inafuata kuingia kanisani wakiimba kwa shangwe na wakiwa na matawi mikononi huku wakiyatikisa, wakikumbuka Yesu kuingia Yerusalamu kwa shangwe, wakiimbia hosana hosana Mwana wa Daudi. Wanampokea Yesu kama Mfalme wa amani. Ndivyo walivyompokea Wayahudi alipoingia Yerusalem kwa shangwe.

Sehemu ya pili  si furaha tena bali uchungu, huzuni, masikitiko na mateso ya Kristo Yesu yaletayo wokovu. Injili inasimulia kwa urefu mateso ya Yesu. Mwaka C tunamsoma Mwinjili Luka 22:14-23,56; 23:1-49. Katika injili hiyo upo uwezekano kusoma somo fupi au kusoma yote. Ikisomwa Injili yote inaanza na simulizi la Karamu ya Mwisho na wanafunzi wake, baadaye mahangaiko ya wafuasi kujua nani mkubwa na nani anaweza kuwa kiongozi na baadaye Yesu kuwajibu kuwa uongozi ni huduma inayomwilishwa katika upendo. Baada ya hapo tunasikia utabiri wa Yesu kuwa Petro atamkana mara tatu. Baadaye Yesu yupo Getsmani katika sala na mahangaiko na baadaye anakamatwa na kupelekwa mbele ya Pilato na kusomewa mashitaka. Mashitaka wanayosema ni kuwa: “huyu mtu tumemkuta akipotosha watu wetu akikataza watu wasilipe kodi kwa Kaisari, na akisema kuwa yeye ni Masiha na mfalme”. (Lk.23:2)

Dominika ya Matawi: Yesu anaingia Yerusalemu kwa shangwe
Dominika ya Matawi: Yesu anaingia Yerusalemu kwa shangwe

Pilato baada ya kusikiliza mashitaka anaona Yesu hana hatia lakini anashindwa kutoa maamuzi, baadaye anampaleka kwa Herode. Herode ambaye alikuwa na hamu ya kumwona Yesu, anapomwona anamuuliza maswali lakini hajibu chochote, matokeo yake wakuu wa makuhani na waandishi wakamfanyia jeuri na dhihaka. Herode naye alishindwa kutoa maamuzi. Mwisho anaona hana hatia anamrudisha kwa Pilato. Naye Pilato anajaribu kupima uzito wa kosa anaona hana hatia na anaamua kumwachia lakini umati wa watu unasema hapana. Naye Pilato anabadili msimamo wake kwa lengo la kuwaridhisha watu. Kwa ajili ya kulinda cheo, kulinda maslahi binafsi, anakubaliana kuwa Yesu auawe ingawa anajua kuwa hana hatia. Hivyo anaidhinisha auawe. Yesu anapigwa mijeledi, anabeba Msalaba na hatimaye, alipofika Mlimani Kalvari akatundikwa juu ya Msalaba.

Kadri ya Mwinjili (Luka 23:39-43) anasema: Pale Msalabani kuna wanyang’anyi wawili waliotundikwa pamoja naye. Hawa nao wanatofautiana muono na mtazamo wao kwa Yesu. Mmoja akiwa pale Msalabani anamtukana Yesu na kumdhihaki akisema kwa dharau: “ikiwa wewe ni Mwana wa Mungu shuka msalabani na utuokoe na sisi”, kumbe mwingine anatambua kuwa Yesu hana hatia isipokuwa wao wamepata adhabu hiyo kutokana na matendo yao. Na anaona wanastahili kupata adhabu hiyo kutokana na matendo yao maovu. Anamwambia mwenzake kwanza awe na hofu ya Mungu. Akisema, wewe humwogopi hata Mungu? Ni mwaliko kwetu pia kuwa na hofu ya Mungu. Pia akasema kuwa Yesu hana hatia ila wao wanahatia kutokana na makosa yao. Baadaye akaomba msamaha kwa Yesu pale msalabani. Na Yesu akamwahidia mbingu dakika ya lala salama. Nasi ni vizuri kutambua kasoro zetu ili tutubu na kuomba msamaha. Yesu ametuwekea Sakramenti ya kitubio, chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake.

Mpendwa msikilizaji na msomaji wa Radio Vatican tunatafakari mambo ya fuatayo: Yesu aliingia Yerusalemu kwa shangwe akiwa amepanda mwanapunda na hakusindikizwa na polisi wala jeshi. Kupanda mwanapunda ni ishara ya: upole unyenyekevu na amani. Yesu hakupenda makuu. Ndiyo maana Paulo kwa Wafilipi anasema Yesu alijinyenyekesha akawa mtii hata mauti ya Msalaba (Wafilipi 2:8). Ufalme wa dunia ni kutukuzwa, kuheshimiwa, kuwa na magari ya fahari, kupigiwa mzinga na kadhalika. Nasi tujifunze unyenyekevu katika maisha. Tusipende makuu. Ufalme wa Yesu unalenga kutumikia na siyo kutumikiwa: “Na aliye mkubwa kwenu awe kama mdogo, na kiongozi awe kama mtumwa” (Lk 22:26). Hivyo viongozi wa ngazi mbalimbali kutambua kuwa jukumu lao ni kutoa huduma inayomwilishwa katika upendo.Katika bustani ya Gethsemane, askari walifika wakiwa na panga na marungu ili kumkamata Yesu. Inaonesha kuwa baadhi ya viongozi wa kidunia ni wa mabavu, vitisho, kuonea watu wasio na hatia, na wakati mwingine wengine wanainga madarakani kwa njia isiyo halali na kusababisha mauaji, mateso ya watu wao. Pia wapo viongozi wenye kulipa kisasi au kisirani n.k. Yesu alionyesha kinyume - ufalme wa amani na uponyaji - hata aliponya sikio la mtumishi wa kuhani mkuu, yule aliyekatwa sikio na Petro.

Yesu alipoletwa mbele ya Pontio Pilato na baraza lake, mashitaka mazito yalitolewa dhidi yake ambayo tumesikia hapo juu. Lakini kati ya mashtaka haya yote, Yesu aliinamisha kichwa chake kimya kimya. Ingawa mashtaka yote ni uzushi. Pilato pamoja na kuona kuwa Yesu hana hatia, lakini kwa ajili ya kulinda maslahi yake binafsi anakubaliana na umati kumhukumu Yesu kifo. Mimi na wewe mara ngapi tumebadili misimamo yetu sahihi na kwenda kwenye misimamo isiyofaa? Viongozi wangapi hushindwa kusimamia haki za watu wao wanaowaongoza sababu kufuata masilahi ya wachache, wapambe, marafiki na jamaa zao? Mtakatifu Petro aliyeahidi kuwa na Yesu mahali popote na kwa mazingira yote, na kuwa yupo tayari kufa kwa ajili yake, lakini aliposhtakiwa na watu watatu waliokuwa karibu wakisema ni mfuasi wa Yesu naye akamkana Yesu mara tatu. Mara ngapi tumeahidi kuishi imani yetu lakini katika mazingira fulani tumeshindwa kuisimamia? Mara ngapi tumemkana Yesu kwa dhambi zetu? Petro baadaye alikiri makosa yake aliomba msamaha na alilia kwa huzuni. Nasi tuombe msamaha tunapotambua makosa yetu.

Ufalme wa kidunia ni ule unaosimikwa katika uchu wa mali na madaraka; ni ufalme wa shutuma kila mtu anamshutmu mwingine, ni ufalme wa kuchafuliana sifa njema, kupigana na kuangamizana. Ufalme wa Yesu haushitaki, bali husamehe na kuwakaribisha wenye dhambi tena hasa wakitubu. Yesu anatoa nafasi ya toba.  Ndiyo maana pale msalabani kadri ya mwinjili Luka, Yesu alitoa msamaha kwa mwizi aliyetubu, akisema “amini na kwambia leo hii utakuwa nami mbinguni”(Lk 23:43) na kuwaombea watesi wake, akisema “Baba uwasamehe kwa maana hawajui walitendalo” (Lk 23.33). Kupitia haya yote, ufalme wa Yesu unaonyeshwa wazi - ufalme wake ni wa amani, wenye kusamehe, wa uponyaji; si wa kutaka kutawala kwa mabavu bali kutumikia; Mpendwa msikilizaji: Yesu anapoanza safari yake ya mwisho na yenye uchungu, anaingia kwenye malango ya Yerusalemu kama Mfalme - na anatualika tumfuate, kwa toba, unyenyekevu na wongofu wa ndani, tayari kutubu na kumwongokea, ili hatimaye, tuweze kuteseka na kufufuka pamoja naye. Tunainua na kutikisa matawi yetu ya mitende, tukifahamu kwamba Kristo aliteseka akafa lakini alifufuka siku ya tatu kama ilivyoandikwa. Alishinda mauti na dhambi. Juma Kuu tunalolianza lituletee baraka na neema tunazohitaji ili kumfuasa Mfalme wetu Yesu Kristo, Mfalme wa haki, amani, upendo na upatanisho. Nawatakia kila mmoja wenu Dominika njema ya matawi na baraka tele kwa Juma Kuu.

Matawi 2022
08 April 2022, 11:14