Dominika ya V ya Kwaresima: Huruma + Udhaifu = Msamaha wa Mungu
Na Padre William Bahitwa, - Vatican.
UTANGULIZI: Dominika ya V ya Kipindi cha Kwaresima. Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika tafakari ya masomo ya dominika hii ambayo inatuandaa kuingia katika Juma Kuu la Mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Kama alama ya nje, kuazia dominika hii tunafunika misalaba na sanamu zote Makanisani. Kwa tendo hili, Kanisa linatualika kutambua kuwa hata sasa, tunapotenda dhambi tunaendelea kumsulubisha Kristo na hivyo hatuwezi kuwa na ujasiri wa kumtazama machoni isipokuwa tumeukubali ukosefu wetu na kutubu. Masomo kwa ufupi: Masomo ya dominika hii yanatualika kutambua kuwa sisi sote wanadamu ni wakosefu na hakuna aliye mkamilifu. Kwa makosa yetu Mungu hatukatii tamaa. Ni yeye anayeamsha daima ndani yetu tumaini la kuokolewa na hufanya hivyo kwa sababu yeye ni mwingi wa msamaha. Tukianza na somo la pili ambalo ni waraka wa mtume Paulo kwa Wafilipi, (Fil 3, 8-14) tunayasikia maneno ya Paulo “sio kwamba nimekwishafika au nimekwisha kuwa mkamilifu; la! Bali ninakaza mwwendo ili nipate kulishika lile ambalo kwa ajilil yake nimeshikwa na Kristo Yesu.” Kwa Paulo, Ukristo ni safari ya maisha kutoka hatua moja kwenda hatua bora zaidi katika mahusiano na Mungu. Safari hii ni endelevu na hawezi mtu kufika hatua akasema sasa amekwisha fika ukomo, amekwisha okoka au amekwisha kamilika. Wanatuambia watakatifu; katika safari ya imani hakuna kusimama, kuna kwenda mbele yaani kuzidi kukua kiimani au kurudi nyuma yaani kulegea na hata kupoteza imani. Mtume Paulo anatupa mfano wa kwenda mbele.
Tukirudi sasa katika somo la kwanza ambalo ni kutoka katika kitabu cha nabii Isaya (Is 43:16-21), tunaona ni Mungu mwenyewe anayeinua matumaini ya mwanadamu mkosefu. Waisraeli wako utumwani Babeli, utumwa waliongia kwa sababu ya kumwasi Mungu. Mungu hawaadhibu milele. Yeye ndiye anayekuwa wa kwanza kuwaahidia wokovu. Anawaambia “msiyakumbuke mambo ya kwanza wala msiyatafakari mambo yaliyopita.” Mambo hayo ni makosa yao ya uasi yaliyowapeleka utumwani. Hayo ni mambo ambayo Mungu anasema amekwisha samehe. Sasa ni yeye atakayewatengenezea njia jangwani ili warudi katika nchi yao. Mungu anayemtangaza nabii Isaya ni Mungu anayempa mwanadamu nafasi ya pili. Katika somo la Injili (Yn 8: 1-11) Waandishi na Mafarisayo wanamleta kwa Yesu mwanamke aliyefumaniwa katika uzinzi. Wanamweleza kuwa kadiri ya torati ya Musa inabidi mwanamke huyo apigwe kwa mawe hadi auwawe na kisha wanamuuliza “nawe wasemaje”. Waandishi na Mafarisayo wanamletea Yesu kesi ili ahukumu lakini mbele kidogo katika simulizi tunaona kumbe, ni wao walikuwa wanatafuta sababu ya kumhukumu.
Sheria ya Musa wanayoiongelea, wanainukuu kimakosa. Katika kitabu cha Mambo ya Walawi 20:20 na kitabu cha Kumbukumbu la Torati 22:22 sheria inasema katika tukio hilo wote wawili mwanaume na mwanamke inabidi waangamizwe kwa kupigwa kwa mawe. Wao walimleta mwanamke tu, hawakumleta na mwanaume. Kumbe sheria ya Musa pamoja na mwanamke waliyemleta ilikuwa ni namna tu ya kutimiza lengo lao. Yesu hakuwajibu neno bali aliinama akaandika chini kwa kidole chake. Hakupenda kuingia katika majibizano ya hoja kwa sababu tayari hoja zao zilikuwa na uovu. Kuandika chini ni kuugusa udongo uliomuumba mwanadamu, mwanadamu ameumbwa kwa udongo, na hivi Yesu alitaka watoke katika hoja zao za nadharia na wautazame undani wa ubinadamu wao na wa huyo mwanamke wanayetaka apigwe mawe. Anawataka wauangalie ubinadamu na uhai kwa ujumla kuwa si kama kitu cha kutolea maamuzi kutoka katika ufundi wa hoja ulio nje ya uhalisia. Na kutoka hapo, walipozidi kumhoji anawaambia “asiye na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza kumtupia jiwe”. Kisha anaimana tena na kuandika chini sheria hii mpya anayotaka sasa ndiyo iongoze maisha na mahusiano ya wote walio ndani ya Kristo. Alipokuwa anaandika, Mafarisayo na Waandishi wakaanza kuondoka mmoja mmoja na akabaki Yesu na yule mwanamke. Hakuna aliyemshitaki. Na Yesu anamwambia “wala mimi sikuhukumu, enenda zako; wala usitende dhambi tena”. Mungu mwenye huruma, upendo na msamaha!
TAFAKARI: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, baada ya kusikiliza masomo ya dominika hii ya V ya Kwaresima na baada ya kupata ufafanuzi wake, tunapenda sasa kungalia tunachoweza kutoka nacho kama tafakari ya kutusaidia kuyaishi mafundisho yake. Tunapenda kujikita katika Injili ili kutafakari fundisho kubwa kuhusu msamaha ambalo Kristo anatupatia. Mtakatifu Augustino, katika tafakari yake kuhusu Injili ya dominika ya tano ya Mwaka C wa Kanisa anasema, Mafarisayo na Waandishi walipompeleka yule mwanamke mzinzi kwa Yesu, bila kujua walijikuta waliukutanisha “udhaifu” na “huruma” – (misera et misericordia). Na hata baada ya mashitaka kwa Yesu baada ya mafarisayo na waandishi kuondoka mmoja mmoja kuanzia yule aliyekuwa mzee hadi yule wa mwisho wao, alipobaki Yesu na yule mwanamke vilibaki hivyo viwili – huruma na udhaifu. Huruma ya Mungu inapokutana na udhaifu wa mwanadamu; huruma ya Mungu inapokutana na mwanadamu anayekiri udhaifu wake, tunda ni msamaha.
Baba Mtakatifu Francisko aliyatumia pia maneno hayo katika ujumbe wake wa kuhitimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu kuonesha fumbo la upendo wa Mungu pale anapokutana na mdhambi. Alieleza kuwa msamaha ndio tendo linaloonesha moja kwa moja na kwa uwazi zaidi upendo wa Mungu kwa wanadamu. Ni kwa sababu hiyo tunapenda kuyaona Masomo ya dominika hii kuwa ni masomo yanatualika kuutafakari upendo unaojimwilisha katika msamaha. Msamaha ndio mahali ambapo nadharia ya upendo inachukua mwili, inapata mashiko; anayesema ninakusamehe anasema ninakupenda na anayesema anapenda awe tayari kusamehe. Injili inatuonesha kuwa msamaha huu una lengo la kuunda upya, una lengo la kuboresha ubinadamu na una lengo la kuimarisha mahusiano kati ya mtu na mtu na kati ya mtu na Mungu. Ni kwa jinsi hii Yesu anamwambia mwanamke “enenda zako wala usitende dhambi tena”. Kamwe msamaha si kivuli cha kufunika mambo wala hauombwi kuficha uwajibikaji bali ni hatua madhubuti ya kujikosoa na azimio la kujisahihisha. Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, kadiri tunavyozidi kuyasogelea maadhimisho ya mafumbo makuu ya wokovu wetu, tuvutwe kubadilishwa na fadhila za kimungu ambazo tunazitafakari tena na tena katika liturujia hizi. Tuvutwe kwa namna ya pekee leo kuwa sisi wenyewe watu wa msamaha.