Ijumaa Kuu: Fumbo La Msalaba Unaong'aa Utukufu wa Yesu Kristo
Na Padre Gaston George Mkude, Roma.
Amani na Salama! “Fulget crucis mysterium”, ni maneno ya lugha ya Kilatini ambayo naomba tuanze nayo katika tafakuri yetu ya leo. Maneno haya kwa tafsiri sisisi ni fumbo la kung’aa kwa Msalaba. Kwa kweli kwa tafsiri yake tunaona ni maneno yanayokinzana, iweje msalaba ung’ae?! Kuna utukufu gani katika mateso na Msalaba? Tunajua kifo cha Msalaba ni adhabu ya kifo cha aibu kwa wahalifu wakubwa katika enzi za utawala wa Kirumi katika dola lao. Tunapotafakari juu ya utukufu wa Fumbo la Msalaba siku ya leo, Mwinjili Yohane katika masimulizi ya mateso ya Yesu anatusaidia kupata maana ya matukio yaliyojiri kwa masaa yale matatu, ya mateso makali na kifo cha aibu pale juu Msalabani. Mwinjili Yohane anatusaidia kuelewa maana na sababu za mateso na kifo chake, kwani kwa kila aliyepata kuona mafundisho na matendo yake haoni sababu za kuhukumiwa kifo kile tena kwa njia ya mateso yenye ukatili usioelezeka. Ni Yesu aliyeponya wagonjwa, aliyewakumbatia watoto, aliyewapenda maskini na kujifanya mtumishi na haswa mtumwa na mtumishi wa wote. “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye”. (Yohane 3:16-17) Ndio, kwa kuwa Mungu ni upendo, wema na huruma isiyo na mipaka, ndio ile “Misericordia” ambayo kwao inataka kumuokoa mwanadamu.
Na hii ndiyo Habari Njema ya Ukristo! Hii ndiyo sura halisi ya Mungu ambayo Bwana wetu Yesu Kristo anaifunua kwetu. Lakini ukweli huu ndio ambao unakuwa kikwazo katika mioyo ya watu wengi si tu nyakati za Yesu bali hata kwetu leo. Ni ukweli unaokuwa kikwazo si tu kwa wale wasioamini bali hata kwa waaminio. Na ndiyo adhimisho letu la Ijumaa Kuu, si lingine bali juu ya Upendo na Huruma ya Mungu kwa watu wote. Yesu anayetundikwa pale juu Msalabani ni upendo na huruma ya Mungu ambayo imekuwa kikwazo na hivyo kushindwa kwetu kuamini, kuupenda na kuupokea katika maisha yetu. Ni leo tunaalikwa kuutafakari upendo huo wa Mungu tukiwa tumesimama chini ya msalaba wake Yesu. Kwa nini Yesu ateseke na afe pale juu msalabani? Ni kosa gani amefanya? Mwinjili Yohane katika Utangulizi wa Injili ile ya nne, anamtambulisha Yesu kama NURU iliyokuja ulimwenguni kuwaangaza watu wote lakini si wote wamechagua nuru, na badala yake wengine wamechagua kubaki gizani. (Yohane 1:4-5, 9 na 3:19). Miale ya nuru/mwanga ule umekuwa kero na makwazo baada ya kuangaza baadhi ya mioyo iliyo gizani, inasumbua na kuchosha macho yaliyozea kubaki gizani. Upande mwingine miale ya mwanga ule umekuwa msaada kwa mioyo minyofu iliyoupokea na hivyo kuweza kutembea katika nuru. Hivyo tangu mwanzoni mwa Injili ya Yohane tunakutana na makundi haya mawili.
Miale ya Nuru hii tunaona inagusa kwa namna 4 kwa makundi mawili yenye madaraka ya kidini na kisiasa. Ni hasa kwa sababu za kisiasa na za kidini tunaona Yesu anahukumiwa na hata kuonekana anapaswa afe tena kifo cha aibu pale juu msalabani. Muale wa kwanza ni juu ya sura halisi ya Mungu: Yesu alikutana na ukinzani mkubwa kwani viongozi wa dini kwa mapokeo daima walifundisha watu juu ya Mungu aliye hakimu mkali asiye na huruma na yeyote yule aendaye kinyume na amri na maagizo yake. Kinyume chake Mungu anayehubiriwa na Yesu ni Baba Mwema na si kingine bali Huruma yenyewe (Misericordia). (Matayo 5:45; 6:25-31 na 6:8 na kuendelea) Hivyo ni Mungu aliye Huruma hivi hakuna mdhambi yeyote aendaye kwake bila kupokea huruma na upendo wake wa Kimungu. Na ndio anamtuma Mwanawe ulimwenguni ili kila amwaminiye asipotee bali ajaliwe kuwa na uzima wa milele. (Yohane 3:16-17) Kwa Waandishi na Mafarisayo kwao Yesu ni sawa na mwendawazimu na mpotoshaji, kwao Mungu ni hakimu mkali asiye na huruma, na hivyo yupo mbali na wadhambi kama watoza ushuru na makahaba na wengine. (Yohane 8:48, 59 na Yohane 10:31, 39) Kwao Yesu ni mtu hatari na hivyo ni vema kumuondoa katika sura ya nchi kwani anahatarisha imani ile waliyorithi kutoka mababu zao, ndio mapokeo ya dini yao.
Ukristo ni zaidi ya dini, ni mahusiano ya upendo baina ya Mungu na mwanadamu, ni kuingia katika mahusiano na Nafsi tatu za Mungu Mmoja. Muale wa pili wa hiyo nuru unaangaza katika dini potofu. Kuna aina mbili za kuishi dini, aidha kuishi imani kwa namna ambayo inaleta amani katika nafsi ya mtu au ile dini iliyojaa amri na maagizo na masharti mengi, hivyo kukiuka moja ya amri na maagizo ni sawa na kuangamia milele. Hivyo kuishia kuwa ni mzigo mzito kwa mtu. (Mathayo 11:28-30) Ni dini inayokuwa mzigo mzito, kwani mahusiano na Mungu siyo yale yanayojengeka katika upendo bali katika amri na maagizo mengi ya kufuata. Ni vema tukatambua kuwa Ukristo si amri na maagizo yanayokuja kwanza bali ni mahusiano ya upendo na Mungu na jirani ndio hasa kiini cha imani yetu. Ukristo ni zaidi ya dini kama nilivyotangulia kusema hapo juu, ni mahusiano ya upendo! Yesu kinyume chake anatualika kuhusiana na Mungu kwa upendo na kwa si kingine chochote bali upendo. Siyo tena dini inayojikita katika amri bali katika roho na kweli, ni mahusiano ya upendo na Mungu aliye Baba yetu mwema na mwenye huruma. (Marko 7:7 na Yohane 2:13-22).
Ni mwanga huu unawasumbua kiasi cha Kaifa aliyekuwa kuhani mkuu kuwaalika wengine kuwa ni heri mtu huyu afe kwa ajili ya watu. (Yohane 11:50). Muale wa tatu ni ule unaoangaza juu ya mtu kweli ni yupi? Ni mtu wa aina gani anasimama kama mfano wa kweli katika jamii. Yesu anatupa kielelezo ambacho nacho kinaamsha hasira kali. Wakati wa Yesu, watu walioonekana waliishi maisha adilifu na ya mfano ndio wakuu wa Sinedrio, makuhani wa hekaluni, marabi na hivyo walivaa mavazi marefu na kupewa heshima wasalimiwapo na kuchukua nafasi za mbele katika masinagogi na katika sherehe. Hawa ni watu wa mfano. (Marko 12:38-39 na Yohane 5:44) Hata Yesu aliomba kutukuzwa na Baba yake lakini utukufu wake haupo katika kushangiliwa kama alivyoingia katika mji ule mtakatifu kama tulivyoadhimisha Dominika ya Matawi, bali katika saa yake pale Msalabani Kalvari Ni pale juu msalabani Yesu aliweza kuonesha ulimwengu nuru na mwanga wa Upendo wa Mungu kwa mwanadamu dhaifu na mdhambi. Tukiri sisi sote ni dhaifu na hivyo Ijumaa Kuu ni siku ya kuinuliwa kwetu ili nasi tuwezi kushiriki utukufu wa Mungu. Msalaba unaonekana kuwa ni kushindwa, fedheha, aibu na mateso bila sababu, bila mashiko, lakini leo tunapomwona Yesu pale juu msalaba, hapo tunauona upendo na ndio utukufu wa Mungu kwetu. Msalaba unapata maana na mashiko yake sio tena katika mantiki ya ulimwengu huu bali ile ya Mungu mwenyewe, yaani upendo wake kwa mwanadamu.
Kwa Yesu maisha yetu hayana budi kuwa kama mbegu inayokufa ardhini ili yatoe matunda kusudiwa, hatuna budi kufa kama mbegu inayosiwa ardhini, na anayeokoa maisha yake anayaangamiza ile yule anayeyaangamiza maisha yake anayaokoa. Ni mantiki ya Mungu na hivyo kinyume na mantiki yetu ya kiulimwengu. Kuwa mfuasi wa Yesu ni kukubali nasi kuishi na kuenenda katika njia ile ya Yesu mwenyewe. (Yohane 12:24-25). Hivyo Yesu anatualika kubadili vichwa vyetu kwa maana ya mitazamo yetu inapofika kuhusu maana ya maisha yetu, maana ya kuwa mtu kweli; Si yule anayeshinda bali anayepoteza, anayetawala bali anayetumikia, siye yule anayehesabu faida yake bali anayejitoa sadaka kwa ajili ya wengine. Si yule anayejilimbikizia na kuwa mbinafsi bali anayekuwa tayari kuwashirikisha wengine mema anayojaliwa katika maisha yake. Na ndio safari ya Kwaresima, safari ya mfungo na toba inapata maana yake kila mara tunapojifunza kuishi mantiki ya upendo wa Mungu katika maisha yetu. Adhimisho la Ijumaa Kuu sio juu ya mateso na kifo kwa vyenyewe bali juu ya upendo wa Mungu kwetu, na ndio nasi tunaalikwa kuingia katika mahusiano ya upendo na Mungu na wengine.
Na muale wa nne uliangaza jamii nzima. Sisi tunaishi katika ulimwengu wa ushindani. Na tangu tungali wadogo tunalelewa katika namna hiyo ya lazima kupambana ili kufanikiwa maishani. Ni lazima tuibuke washindi iwe shuleni mzazi anaalika watoto lazima wafaulu zaidi kuliko wengine. Kifupi maisha ni mapambano na hii ndio falsafa ya ulimwengu wetu wa leo. Ni mapambano katika kila nyanja ya maisha, iwe kwenye familia, mashuleni, kazini na pengine hata katika maisha yetu ya imani jumuiyani, maparokiani na katika jumuiya zile za makuhani na watawa. Ni mantiki na falsafa ya ulimwengu huu. Na ndipo siku moja Yesu akaketi na kumpakata mtoto mdogo na kuwaalika wanafunzi, kuwa anayempokea mtoto yule basi anampokea yeye na hivyo Baba aliyemtuma ulimwenguni. (Marko 9:36-37) Wakati wa Yesu watoto walikuwa ni ishara ya udhaifu kwani ni tegemezi kwa kila hali, ni muhitaji maana bado hajafika umri wa kujitegemea. Ni katika ulimwengu mpya wa Utawala wa Mungu tunaona wadogo ndio wanakuwa kielelezo cha maisha yetu. Ni wadogo ndio wanaoheshimika katika macho ya Mungu. Ni hawa wanaoonekana dhaifu na wadogo ndio wanapewa kipaumbele na ndio Kanisa leo linaalikwa daima kuwalinda watoto katika kila hali, na ndio linaalikwa daima kutenga kwa umakini na upendo mkubwa katika kuwalea na kuwakuza watoto hawa.
Maskini kwa namna ya pekee kabisa wanapaswa kuwa kipaumbele ya jumuiya zetu, iwe ndogo ndogo, kiparokia na majimboni mwetu. Katika mipango yetu ya Kichungaji lazima kuona kwa namna ya pekee tunawapa nafasi ya kwanza makundi ya wote wanaokuwa wanasahaulika na kutengwa katika jamii. Yesu anawakumbatia hawa wadogo na kuwabusu! Yesu angeweza kuepa kifo chake pale msalabani kwa kuzima miale ya mwanga wake. Angejikalia kimya kuepusha shari! Angekubaliana na fikra na mitazamo ya wengine tu! Labda hata nasi leo mara ngapi tunaepuka shari kwa kuacha kuangaza kwa maisha yetu uzuri wa Injili/ Habari Njema? Masimulizi ya Mateso ya Yesu kama yalivyoandikwa na kusimuliwa na Mwinjili Yohane tunaona tangu mwanzoni mwa kukamatwa kwake pale bustani ya Getsemani, tofauti na wainjili wengine wanaotuonesha kuwa Yesu alikuwa na huzuni kubwa kiasi cha kufa na hivyo kuwaalika wanafunzi wake kukesha naye katika sala, na badala yake Mwinjili Yohane anatuonesha kuwa Yesu alikuwa na utulivu na hata kuonekana kujua mwisho wa hatima yake. Hivyo Mwinjili Yohane anatuonesha sio maaskari wanaomkamata Yesu bali ni yeye mwenyewe anajikabidhi kwa watesi wake. Hivyo Yesu kwa ujasiri na utulivu anawaambia watesi wake kuwa, “Mimi ndimi” (Yohane 10:17-18) “Mimi ndimi”, katika Maandiko ni utambulisho wa Mungu, Mungu ambaye yupo, ndio uwepo wenyewe. Mwinjili Yohane anatualika kuelewa kukamatwa kwake Yesu kwa kuongozwa na (Zaburi ya 9:4 na ile ya 27:2).
Wakati Injili Pacha zinatuonesha baada ya kukamatwa kwa Yesu anapelekwa katika nyumba ya kuhani mkuu Kayafa. Na hapo wazee na waandishi wanajadiliana usiku kucha jinsi ya kutoa mashitaka yao mbele ya Ponsio Pilato. Yohane anatupa picha tofauti na hiyo. Yohane anatuonesha kuwa majadiliano yalifanyika mbele ya Anasi, mkwewe Kaifa. (Yohane 18:12-24) Anasi aliwahi kuwa kuhani mkuu na hata baada ya kumaliza muda wake alibaki kuwa ni mtu mwenye nguvu kimaamuzi, hivyo alikuwa ni mzee wa familia na mwenye ushawishi mkubwa katika mambo yahusuyo hekaluni. Ni yeye aliyehusika na uangalizi wa sadaka pale hekaluni, wabadili pesa, wauzaji wa wanyama. Kitendo cha Yesu kuwafukuza hekaluni wabadili pesa tunaona ni kuhatarisha uchumi wa familia ile. Hivyo Anasi anabaki kuwa ni ishara ya uongozi wa dini uliokuwa kinyume na Yesu Mgalilaya, mwana wa mselemala. Hivyo Mwinjili Yohane anamtumia Anasi kuwakilisha wale wote waliokuwa kinyume na Yesu mintarafu dini. Katika mahojiano Yesu anamjibu bila woga, kwa nini waniuliza mimi, waulize wale waliosikia mafundisho yangu. (Yohane 18:21) Mmoja wa watumishi wake anampiga kofi Yesu kwa kumjibu hivyo kuhani mkuu. Tunaona bado kuna utulivu mkuu kwa upande wa Yesu na anawaalika waoneshe kama amefanya ubaya wowote. (Yohane 18:23). Mtumishi huyu anatumika kama kibaraka kulinda masilahi ya bwana wake, ni kielelezo kwangu na kwa kwako ni mara ngapi hata bila kuwa na ufahamu wa jambo na hasa ukweli wake tunachukua upande kwa kulinda masilahi yetu na hasa kwa kutetea masilahi ya wakubwa wetu? Ni mara ngapi tunajitoa kupigania wakubwa wa ulimwengu huu kwa madai ya kutetea dini au uzalendo na kujikuta tukimpiga kofi Yesu, tutafakari!
Mwinjili Yohane anatusimulia kwa marefu zaidi ya Mwinjili Marko Yesu akiwa mbele ya Pilato. Mwinjili Yohane anatuonesha kwa msisitizo mkubwa kabisa jinsi Pilato, mtawala wa Kirumi alivyokuwa anaingia na kutoka ndani ya Praitorio. Ni kwa sababu za kidini Wayahudi hawapaswi kuingia katika nyumba ya mpagani kwani kufanya hivyo wangenajisika kwani walikuwa wanajiandaa kuila Pasaka. Mwinjili Yohane anatoa msisitizo hapa ili kukazia Ufalme wake Yesu. Tunakutana na wahusika mbali mbali zaidi ya muhusika mkuu Yesu, tunakutana na Pilato, Wayahudi, maaskari, Baraba. Na lengo la Mwinjili ni kuhusu Ufalme wa Yesu. Pilato anawakilisha ufalme wa ulimwengu huu kinyume na ule wa Yesu. Ni mfano wa yule anayeamini katika madaraka yake kiasi hata ya kumtoa mtu sadaka ikiwa sheria inataka hivyo, mmoja anayelinda sheria zisizo na haki. Wayahudi hawa ni wawakilishi wa wale wote wasiokuwa tayari kubadili vichwa vyao mintarafu sura halisi ya Mungu. Ni wale wanaoamini katika Mungu anayeshinda kwa kutumia nguvu na si kwa upendo, hivyo hawapo tayari kumpokea mfalme aliye mpole na mwema. Maaskari hawa ni wawakilishi wa wale wote wanaokumbwa kwa bahati mbaya na kwa ujinga wao katika makosa. Wapo mbali na nchi yao na familia zao na hata kudhalilishwa huku wakikubali kuuvua ubinadamu na kuuvaa unyama kwa ajili ya kulinda matakwa ya watawala. Ni wale wanaoamini katika nguvu za mabavu na si utashi na upendo kwa jirani. Baraba jina lake likiwa na maana ya mwanaharamu, mwana asiye na baba anayejulikana. Ni muhalifu, ni mwana wa yule muovu, ni mwakilishi wa wale wote wanaofanya ukatili mkubwa katika historia ya mwanadamu lakini kuna nyakati wanaonekana kuwa ni watu hodari na majasiri wa kuigwa.
Baada ya kuangalia wahusika mbali mbali sasa tuone pia muda wa matukio haya. Ilikuwa alfajiri (Yohane 18:28), ni mwanzo wa siku mpya, ndio jua linaanza kuangaza tena dunia baada ya kuisha kwa giza la usiku ule ambao Yuda Iskariote alitoka pale kwenye chumba cha karamu ya mwisho na kwenda kumuuza Yesu. Yuda anatoka na kwenda kwa wakuu wa Wayahudi usiku, wakati wa giza. Pia ni usiku maaskari wanafika kumkamata Yesu pale bustanini, ni usiku tunaona Petro anamkata sikio kijakazi wa kuhani mkuu, usiku pia Kayafa na Anasi wanafanya mashauri ya kumshitaki Yesu, na hata usiku tena Petro anamkana Yesu mara tatu. Hatimaye giza la usiku ule linaishia kwa kuanza kwa siku mpya. Mwanga na nuru ya mchana unaleta matumaini mapya. Ilikuwa mchana wa saa 6 (Yohane 19:14) Ni mchana wa jua kali ndipo Pilato atatangaza ukweli wa imani: Mwangalieni mfalme wenu (Ecce Rex vester) Katika sura hizi mbili yaani ya 18 na 19 Mwinjili Yohane anatumia neno mfalme kumuhusu Yesu mara 12. Mwinjili Yohane pia anatupa pia ishara ya ufalme wa Yesu nazo ndio taji la miiba, vazi la zambarau na pia kukiri kwa Pilato kuwa Yesu ni mfalme wa Wayahudi.
Yesu mwanzoni aliyehoji kofi la kijakazi wa Anasi, lakini tunaona hapingi wala hahoji ufalme wake unaotamkwa na Pilato. Anakiri kuwa yeye kweli ni mfalme ila ufalme wake sio kwa mantiki ya ulimwengu huu, kutawala kwa mabavu na kujichukulia nafasi ya heshima. Mtu kweli na mfalme kweli ni yule anayejitoa sadaka kwa ajili ya wengine. Ufalme wake ni wa haki, amani na upendo na si kingine! Kadiri ya mantiki ya ulimwengu huu, Yesu anaonekana kuwa ameshindwa na hasa katika wakati huu wa mashitaka na mateso na kifo chake. Yesu anapoteza sifa ya kuwa jembe, kuwa jiwe, kuwa mpambanaji wa kweli, kuwa mwanaume wa shoka asiyekubali kushindwa kirahisi. Ushindi na ufalme wake unaonekana kushindwa kwani ufalme wake sio kwa mantiki ya mapambano na mashindano, bali katika haki, amani na upendo! Yesu anabaki kimya hajibu neno wala hasemi kitu, hajitetei mwenyewe, anaonekana kushindwa na watesi wake. Yesu anabaki na kuonekana dhaifu kabisa. Yesu dhaifu mbele ya Pilato, mbele ya Wayahudi na maaskari! Mwinjili Yohane anatueleza kwa ufupi kabisa safari ya Yesu kuelekea Kalvario. Yesu anachukua msalaba wake na kupanda kwenye Kalvario. (Yohane 19:17) Hatusikii juu ya wanawake wanaomlilia wala Simoni wa Kirene anayemsaidia kuubeba msalaba. Wakati wa mateso yake Mwinjili Yohane kinyume na Wainjili ndugu anatupa tena baadhi ya kweli ambazo hatuzisikii kwa Wainjili wengine. (Yohane 19:18-37) Anwani iliyoandikwa juu ya msalaba wake kuonesha aina ya mashitaka yake. Anwani hii iliandikwa kwa lugha tatu yaani Kiebrania (Lugha ya Wayahudi), Kilatini (Lugha ya watawala wa Kirumi), Kigiriki (lugha iliyoongelewa katika sehemu kubwa ya dola la Kirumi). Bila kufahamu Pilato anafanya unabii unaobaki na kudumu siku zote kuwa hakika Yesu ni Mfalme wa Wayahudi na Mfalme wa Ulimwengu mzima sasa na hata milele.
Baada ya Yesu kusimikwa katika kiti chake cha ufalme yaani pale juu msalabani nini kinajiri? Mwinjili Yohane hatuambii juu ya matusi dhidi ya Yesu kutoka kwa wapita njia, makuhani wakuu, waandishi na wazee. Ni kwa sababu moja tu kuwa Yesu ni mfalme kweli hata kama ni ujinga kwa Wayunani na makwazo kwa Wayahudi. (1 Wakorintho 1:23) Ukweli unabaki daima iwe unapokelewa au unapingwa. Ni ukweli kwa wenyewe hivyo hautegemei mimi na wewe bali unasimama na kuangaza daima. Na ndio maneno niliyoanza nayo katika tafakuri yetu ya leo kuwa pale juu msalaba tunakutana na mwanga wa mfalme wa ulimwengu huu. Ni fumbo la upendo na huruma ya Mungu kwetu wanadamu, hivyo tunabaki na mshangao mkubwa tunapoutafakari wema na huruma ya Mungu kwetu wadhambi na dhaifu, anakubali kubeba dhambi na udhaifu wetu ili sisi tuweze kupata wokovu. Tunakiri “fulget crucis mysterium”, kung’aa kwa fumbo la msalaba! Yohane Mwinjili anatueleza kuwa joho lake waliligawa katika sehemu nne na ndio kusema ukombozi wake ni kwa ulimwengu mzima. Katika ulimwengu wa nyakati za Yesu joho pia linabeba nafsi ya mtu mwenye nalo, kazi zake, tabia yake na hata namna ya kuhusiana na wengine. Na ndio tunaona hata siku ya Ubatizo tunavalishwa vazi jipya, vazi jeupe likimaanisha cheo chetu kipya cha kufanyika wana wa Mungu.
Pale Msalabani Mwinjili Yohane anatuambia alikuwepo mama yake na Yesu. Uwepo wa Mama yake pale chini ya msalaba ni ukweli unaokuwa mgumu kuuelezea kiuhalisia kwa sababu nitakazojaribu kuzitaja hapa chini. Leo wanazuoni baadhi wa Maandiko Matakatifu wanajaribu kutuonesha kuwa Mwinjili Yohane anataja uwepo wa Mama Bikira Maria sio haswa kwa sababu za masimulizi ya Kihistoria bali zile za Kiteolojia kama tunavyoweza kuona hapa chini. Mwinjili Marko anaonesha kuwa kulikuwepo wanawake waliosimama kwa mbali na anawataja kwa majina na hataji uwepo wa Maria wala wa Yohane kama ambavyo wengi wanavyopenda kutafsiri kuwa mwanafunzi aliyependwa na Bwana alikuwa ni Yohane. Mwinjili Yohane hataji jina la mwanafunzi huyo, hivyo ni vema nasi tukajaribu kutafakari zaidi kuliko kuanza kumpa jina yule ambaye hatajwi kwa majina yake. Hata Yesu hamtaji Bikira Maria kama mama bali mwanamke, kama alivyotamka katika sherehe za harusi ya Kana. Na kwa kadiri ya tamaduni za Kiyahudi hakuna mtoto angeweza kumwita mama yake bimkubwa (kwa kweli kwa tafsiri sahihi ni mwanamke – Γυναι, ιδε ο νιος σου. Neno la Kigiriki “Gunai” linamaanisha mwanamke. Najua mara nyingi wahubiri wengi wanaelezea uwepo halisi wa Bikira Maria, mama wa Yesu na Yohane kama mfuasi aliyependwa na Bwana. Lakini yafaa sasa kutafakari ili tuweze kuona sababu za Kiteolojia anazokuwa nazo Mwinjili Yohane. Kwa Mwinjili Yohane, Mama ni lugha ya picha inayoashiria Israeli mwaminifu kwa Mungu. Katika Biblia Israeli ni bikira, mchumba na mama. Ni kutoka katika taifa hili sasa linazaliwa taifa jipya la Kimasiya, yaani Kanisa. Hivyo Yesu anaalika kwanza taifa la Israeli kama watangulizi wa kupokea ahadi za Mungu, kuingia na kushiriki katika Agano Jipya lake Yesu Kristo pale juu Msalabani.
Na pili anageukia kwa ile jumuiya mpya inayowakilishwa na yule mwanafunzi aliyependwa ili kumpokea mama Israeli ambapo kwayo imezaliwa, na ndio kuona misingi ya imani kuanzia Agano la Kale kutoka kwa wale waliopokea awali ahadi za Mungu. Kanisa au jumuiya mpya ya Kimasiha ndio mwanafunzi anayependwa na Bwana. Kila Mbatizwa ni mwanafunzi anayependwa na Bwana, na hivyo Kanisa ndio Israeli mpya, ndio mama mpya tunayealikwa kuingia katika mahusiano naye. Ni Mama Bikira Maria anayebaki kuwa kielelezo cha kila mfuasi wa kweli wa Yesu Kristo. Ni Mama Bikira Maria anayekuwa katekista wetu wa kwanza kabisa anayetufundisha nini maana ya kuwa wafuasi wa Yesu Kristo, anabaki kuwa Mama wa kila mmoja wetu kwa namna ya pekee kabisa. Ni Mama Bikira Maria anakuwa ndio kidole kila kinachotuonesha njia ya kweli katika kukua katika mahusiano ya kweli na Mungu na wengine. Kadiri ya Mwinjili Yohane tunaona kifo chake Yesu kinajiri kwa utulivu na ukimya mkubwa. Mwinjili Yohane haoneshi ishara za kutisha kama kulia kwa sauti pale juu msalabani, tetemeko la nchi, au giza juu ya sura ya nchi. Yesu pale juu Msalabani anakamilisha misheni yake ya kuja kutufunulia kikamilifu juu ya sura halisi ya Mungu yaani Mungu aliye upendo na huruma.
Ni pale juu Msalabani linafanyika Agano Jipya, Agano la upendo na huruma ya Mungu kwa ulimwengu mzima. Naona kiu, ni maneno anayotamka pale juu msalabani akionesha kiu na hamu na tamaa yake ya kuupa ulimwengu maji ya uzima kama alivyomwambia mwanamke msamaria pale kisimani. Msalaba ni ishara ya upendo na huruma ya Mungu kwetu, msalaba ni Agano la Upendo kati ya Mungu na ulimwengu mzima. Kiu yake inakamilika pale juu Msalabani, yaani kutukomboa kwa kutupatanisha na Mungu Baba. YAMETIMIA ni maneno anayotamka kumaanisha ukamilifu wa misheni yake, na ndio kukidhi kiu yake, maji ya uzima yenye kumaliza kiu ya mwanadamu, maji yaliyo chanzo cha uzima wa kweli, yanayowafikia wale wote wanaokuwa tayari kukaribia msalaba wa Yesu, huu mti wa msalaba ambao juu yake umetundikwa wokovu wetu. Msalaba unapata maana kubwa kwetu waamini kwa kuwa hatuoni tu mti bali tunauona upendo na huruma ya Mungu kwetu. Baada ya kifo cha Yesu yote yamekamilika na Yesu anaikabidhi roho yake mikononi mwa Baba yake. Ni katika maandalio ya Pasaka mwinjili Yohane anatuonesha kuwa amechinjwa, ametolewa sadaka, mwanakondoo wa Pasaka. Kwa kumwaga damu yake, Yesu anatukomboa kutoka katika utawala wa yule mwovu kwa kutuacha huru ili nasi tushiriki maisha mapya yaani kuishi kwa kuongozwa na Neno la Mungu.
Ni kwa sadaka yake tunaingia katika nyakati mpya, ndio mahusiano ya kweli na Mungu, yaani yale ya upendo usio na mipaka. Mwinjili Yohane pia anatuonesha kuwa askari mmoja anachoma ubavu wake kwa mkuki na humo inatoka damu na maji. Damu kwa Wayahudi ni ishara ya uzima, hivyo kumwagika mpaka tone la mwisho ni sawa na kutoa uhai wake. Ni kwa kutoka maji ishara ya kumiminwa kwa Roho yake. Ishara hizi za maji na damu daima zinatumika kuashiria uwepo wa Masakramenti katika Kanisa la Kristo na hasa sakramenti ile ya Upendo wake mkuu, yaani ya Mwili na Damu yake, ndiyo Ekaristi Takatifu. Ni humo tunakutana na Umungu na Ubinadamu wake, ishara iliyo kuu ya upendo wa Mungu kwa ulimwengu mzima. Mwili wake wanaupaka manukato ya gharama kubwa na yote ni kuashiria kuwa huyu kweli ni mfalme maana hawakutumia manukato ya kupaka maiti bali manukato yaliyotumika kupaka maharusi kama alivyofanya Maria dada wa Lazaro pale Betania, somo la Injili tulilolisikia Jumatatu ya Juma hili Kuu. Nawatakia Maadhimisho mema ya Fumbo la Pasaka yaani Mateso, Kifo na Ufufuko wake Bwana wetu Yesu Kristo.