Tafuta

Ijumaa Kuu: Kristo Yesu, Wokovu wa binadamu ametundikwa juu ya Msalaba! Njooni, tumwabudu, tumtukuze na kumheshimu. Ijumaa Kuu: Kristo Yesu, Wokovu wa binadamu ametundikwa juu ya Msalaba! Njooni, tumwabudu, tumtukuze na kumheshimu. 

Ijumaa Kuu: Wokovu wa Mwanadamu Umetundikwa Msalabani, Yesu Kristo!

Msalaba ni alama kuu ya Ukristo na hii ni kwa sababu unawakumbusha walimwengu juu ya upendo wa Kristo aliouonesha kwa wanadamu kwa njia ya mateso na kifo chake. “Na sisi tunamtangaza Kristo aliyesulubiwa,” (1Kor 1:23). Paulo anasema “ujumbe wa kifo cha Kristo Msalabani ni upuuzi kwa wale wanaopotea; lakini kwa wale wanaookolewa ni nguvu ya Mungu."

Na Padre Efrem Msigala, OSA, - Roma.

Karibu mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican na msomaji wa Vatican News katika Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu Ijumaa Kuu. Ijumaa kuu kanisa linaadhimisha mateso na kifo cha Bwana wetu Yesu Kristo. Ni siku ya maombolezo,  huzuni lakini na matumaini ya ufufuko. Ni siku ambayo Kanisa haliadhimishi Ibada ya Misa Takatifu. Ibada ya Ijumaa Kuu imegawanyika sehemu tatu: Liturujia ya Neno, Kuabudu Msalaba na Komunyo Takatifu. Katika tafakari hii tutatafakari zaidi juu ya thamani ya Msalaba wa Kristo, msalaba wa wokovu, msalaba wa uzima uliotundikwa pale mlimani Kalvari. Msalaba ni alama kuu ya Ukristo na hii ni kwa sababu unawakumbusha walimwengu juu ya upendo wa Kristo aliouonesha kwa wanadamu kwa njia ya mateso na kifo chake. “Na sisi tunamtangaza Kristo aliyesulubiwa,” asema Mtakatifu Paulo (1Kor 1:23). Zaidi ya hayo, Mtume anasema, “ujumbe wa kifo cha Kristo Msalabani ni upuuzi kwa wale wanaopotea; lakini kwa wale wanaookolewa ni nguvu ya Mungu” (1Wakorintho 1:18). Paulo alielekeza ujumbe huu kwa Wayahudi ambao wanaona msalaba kama mzigo kwa wahalifu na kama adhabu kwa wenye dhambi (Kumb 21: 20-23). Kwa hiyo, Wayahudi wanafikiri ni jambo lisilofaa kumwamini mtu aliyesulubiwa. Kwa sababu mtii wa msalaba ulitumika kuadhibu wakosefu kutokana na matendo yao mabaya.

Msalaba wa Kristo Yesu ni chemchemi ya wokovu wa mwanadamu
Msalaba wa Kristo Yesu ni chemchemi ya wokovu wa mwanadamu

Wagiriki, kwa upande mwingine, wanafikra sawa na wanafalsafa mashuhuri wa wakati huo, waliona msalaba kuwa ishara ya upumbavu. Pamoja na maarifa yao yote hawakuweza kuelewa jinsi Mungu anavyotumia “mambo ya kipumbavu” kudhihirisha ukuu wake. Mtakatifu Paulo kwa Wagalatia anasema “Sisi lakini inatupasa kuona fahari juu ya msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo” Ijumaa Kuu tunapata fursa ya kuabudu Msalaba wa Yesu Kristo. Msalaba ambao tumepatia wokovu. Tukiongozwa na maneno haya ambayo hurudiwa kwa kuimba mara tatu: “Huu ndiyo mti wa msalaba, ambao wokovu wa dunia umetundikwa juu yake”:  hayo husemwa na Padre au Shemasi na baadaye wote huitikia wakisema: “Njooni njooni tuabudu” maneno haya ya mwaliko yatufikirishe kutambua uthamani wa msalaba wa Kristo, Msalaba unaoponya, msalaba wa ukombozi. Lakini tuutazame kwa jicho la imani. Msalaba una ujumbe kwa waamini wote leo kwani unatoa maana kwa majaribu na matatizo ya ulimwengu na kuwa ishara ya upendo pamoja na ushindi. Majaribu ni njia isiyoepukika ya kupata wokovu na ushindi. Katika maisha yetu kama wanadamu majaribu hatuwezi kukwepa.

Yesu alisisitiza jambo hili waziwazi kwa wafuasi wake anaposema: “Mtu yeyote akitaka kunifuata, ajikane mwenyewe, aubebe msalaba wake, anifuate” (Mt 16:24). Msalaba wa Yesu ni ushahidi wa wazi wa upendo wake, ambao aliutoa uhai wake kwa ajili yetu, na anatupa changamoto kufanya vivyo hivyo kwa ndugu zetu akisema “pendaneni ninyi kwa ninyi hakuna upendo mkubwa kama huu wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake” (Yohane 15:12-13; 1 Yoh. 3:16). Yesu, aliyekufa kwa ajili ya dhambi zetu, aliyepigiliwa misumari msalabani. Alipigiliwa misumari mikono na miguu. Wsanateologia wa karne za kati walihusisha misumari na dhambi zetu na walisema wengine misumiri mitatu wengine wakasema minne. Basi leo sisi misumari hiyo tuone ni matendo yetu binadamu, tuone ni dhambi tunazofanya.  Msumari wa kwanza ni msumari wa busu la unafiki na usaliti. Ndivyo alivyofanya Yuda Iskariote, Yesu anamuuliza "Yuda, Je, unamtoa Mwana wa Adamu kwa kumbusu?" (Lk.22:48. Yuda, mwandani kabisa wa Yesu, tena mtunza mfuko. Akiwa na tamaa zake za kujinufaisha na mambo yake binafsi. Anaamua kumsaliti mwalimu wake anamuuza apate fedha. Alimfanya mwalimu kuwa kitega uchumi, kwa manufaa yake binafsi. Lakini pia anatumia busu kama ishara ya kujulisha maadui wajue ni yule mhusika wa kumkamata. Hivyo busu na vipande 30 vya fedha alizopewa tungeweza kusema ni bei ya msumari wa kwanza wa kumsulubisha  Yesu. Jinsi busu la usaliti linawaka! Jinsi pesa za usaliti, za ubinafsi, za biashara chafu, zinavyotesa! Msumari huo wa kwanza ulitoboa mkono wa kushoto wa Yesu.

Je, ni mara ngapi tumemsaliti Kristo Yesu?
Je, ni mara ngapi tumemsaliti Kristo Yesu?

Katika tukio hili la Yesu, nasi tujitazame tunafananaje na Yuda? Wewe na mimi tumemsaliti Bwana kwa busu mara ngapi? Na pia tumemuuza mara ngapi kwa ahadi zetu hewa, tunapokuwa tumeahidi kuchangia kitu fulani kwa ustawi wa Kanisa na baadaye hatutekelezi? Yuda, baada ya kumsaliti kwa busu lake na kuona mwalimu wake amekatwa na kuteswa alikata tamaa, hakuona dhamana ya maisha tena, hakuona sababu ya kutubu wala kuomba ushauri, badala yake akaamua kujinyonga. Mara ngapi nasi wakati mwingine tunakata tamaa na kupoteza imani na matumaini ya maisha na kutohitaji hata ushauri na wala kupokea sakramenti ya kitubio na tunatoa maamuzi yasiyofaa? Tusiwe kama Yuda aliyekata tamaa na kujinyonga bali kama Petro  licha ya kasoro zake lakini hakukata tamaa bali zilimpa fursa kujitafiti na kuomba msaamaha baada ya kumkana  Bwana mara tatu. Alipotambua kosa lake alilia kwa uchungu juu ya dhambi yake na kutubu. Msumari wa pili ni msumari wa vurugu, wa ukatili, wa kupiga makofi wa kutemewa mate. Yesu alipopigwa makofi na yule mlinzi (Yn 18:22) Kwa msumari wa usaliti wa rafiki huongezwa msumari wa kupigwa makofi, wa vurugu, za askari. Lakini pia Pilato na watu wake walimtendea vibaya, wakampiga, wakamtemea mate, miiba kichwa na kuweka maonyesho machafu na ya kikatili na fedhuli. Pilato akisema tazameni mfalme wenu. Yesu ni mtu yeyote tu, anayeteseka kwa jeuri ya nguvu inayoweka msumari kwenye mkono wake wa kulia. Lakini sisi pia tunaishi katika jamii yenye jeuri, katili na kandamizi.

Tukiangalia katika mitaa yetu, vijiji vyetu, parokia zetu, majimbo yetu na katika familia zetu, kuna watu wanatendewa ukatili wa kila aina.  Pengine nasi tunashiriki kwa namna fulani kuwatendea ukatili wengine. Tumuombe Mungu radhi kwa msumari huo wa ukatili kwa wengine. Msumari uliopigilia mkono wake Yesu wa kulia. Msumari mwingine ni ule wa ugeugeu katika maisha kama mtu binafsi au kama jamii. Katika simulizi la mateso ya Yesu tumesikia watu mbalimbali kwa nafasi tofauti zinazoonesha ugeugeu. Tukianza na Yuda Iskariote anamgeuka mwalimu wake anamweka kitega uchumi,  Petro ambaye aliahidi kufa kwa ajili ya Kristo lakini akamkana mara tatu, Pilato anabadili msimamo wake wa kusimamia haki na kulinda uhai kama kiongozi kwa watu anaowaongoza. Lakini kwa sababu ya maslahi binafsi hata kama anajua kuwa Yesu hana hatia anakubali auawe na kumwachia Baraba ambaye ni mhalifu, huyu anaachwa huru. Kwa upande mwingine maaskari, na  umati wa Wayahudi ambao Dominika ya Matawi walimpokea Kristo kwa shangwe wakiimba hosana hosana mwana wa Daudi tena wakitambua kuwa mfalme. Hawa hawa walioimba hosana hosana na kutambua kuwa mfalme leo wanasema si mfalme wao ila yeye alikuwa akisema hivyo, wanamkataa, pia wakisistiza msulubishe, msulubishe. Wewe na mimi mara ngapi tumeshiriki kushawishi wengine wasulubiwe? Mara ngapi tumekuwa vigeugeu katika imani yetu, mara ngapi tumevutwa na wahubiri wa wanaoahidi wokovu bila msalaba? Mara ngapi watu wamedanganyika kwa suala la mafuta yenye upako, maji yenye upako, chumvi ya upako, utajiri wa haraka haraka? Mara ngapi watu  wamedanganyika na miujiza fake? Watu hawa wanakuwa wakatoliki lakini pia mguu mwingine upande mwingine. Huo ni ugeugeu wa maisha. Ni msumari mwingine wa kumpigilia miguu Yesu.

Msalaba wa Kristo Yesu ni alama ya matumaini na ushindi
Msalaba wa Kristo Yesu ni alama ya matumaini na ushindi

Pamoja na hayo mpendwa msikilizaji: Ijumaa kuu hii ya 2022 tunaadhimisha tukiwa katika changamoto mbalimbali. Tupo katika mahangaiko ya uviko 19, vita vinavyoendelea Ukraine na Urusi na pia sehemu nyingine na kusababisha ulimwengu mzima kuathirika. Kwani wengi wamepoteza maisha yao, wamekuwa wakimbizi, uharibifu mkubwa wa nyumba, miji na misingi ya kibinadamu kutikiswa. Tunaona bei ya vitu kupanda juu hivyo kusababisha watu wengi wanyonge wasio na hatia kuhangaika. Tuombe amani duniani kote, Kristo aliyekufa msalabani akashinda mauti atujalie nasi tuweze kuyashinda haya mapito tunayopita sasa. Ijumaa kuu ni siku ya kusimama na kufikiria juu ya maana ya mateso na kifo cha Yesu Kristo. Pia ni wakati wa kutafakari jinsi majeraha yake yanavyoleta uponyaji kwa wengi na jinsi kifo chake kinampa kila mtu tiketi ya wokovu. Msalaba una nafasi ya heshima katika Ukristo kama vile umwilisho na ufufuo ni marejeo muhimu katika uchumi wa wokovu wa Kikristo. Tumaini la ufufuo hutoa maana kwa mateso na kifo, ambavyo huadhimishwa siku ya Ijumaa Kuu. Wataalamu wanasema: Msalaba kisha unakuwa ishara ya tumaini, lakini pia hakuna taji bila msalaba; hakuna msalaba bila taji; Hakuna mapato bila maangaiko. Basi tukumbuke maneno ya Mt. Paulo kwa Wagalatia (6:14 lakini nisijisifu kamwe ila Msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambao kwa huo ulimwengu umesulubishwa kwangu, na mimi kwa ulimwengu.

Mateso ya Kristo
14 April 2022, 17:09