Tafuta

2022.04.01 Uzinduzi wa Kituo cha Mafunzo na tafakari ya Sanda ya Torini “KWAUSO” jimbo la Bukoba Tanzania. 2022.04.01 Uzinduzi wa Kituo cha Mafunzo na tafakari ya Sanda ya Torini “KWAUSO” jimbo la Bukoba Tanzania. 

Ushuhuda wa Padre Stanislaus Mutajwaha kuhusu Sanda ya Torino!

Mimi nilifikiwa na wazo la Sanda kwa mara ya kwanza bila kutegemea mwezi Aprili mwaka 1985,ikiwa ni mwaka wangu wa 8 wa upadre,nilipokutana na taarifa juu yake katika gazeti moja linaloitwa National Geographic Magazine,Toleo la Juni mwaka 1980.Hisia zangu za kwanza baada kuisoma makala hii zilikuwa hasi na chanya kwa wakati mmoja.Ni Padre Mutajwaha wa Jimbo la Bukoba Tanzania katika utangulizi wa makala kuhusu Sanda ya Torino.

Na Padre Stanislaus Mutajwaha - Bukoba,Tanzania.

Wakati tunatembea pamoja katika mwondoko wa kisinodi kama tulivyoalikwa kufanya na Baba Mtakatifu Francis, tuweze kutenga kando muda wetu adimu kuitazama Alama ile Kuu ya upendo wa Bwana wetu Yesu Kristu inayojulikana kama Sanda ya Torino kwa kipindi kizima cha Kwaresima hadi siku ya Ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristu, tarehe 17 Aprili 2022 na kuendelea. Mimi ninaitwa Padre Stanislaus Mutajwaha, Padre wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Tanzania. Ninahudumia kama Mkurugenzi wa Shule ya Sekondari ya ‘KWAUSO’, Wilaya ya Bukoba vijijini, Shule ya bweni; Shule mchanganyiko ya wasichana kwa wavulana chini ya umiliki wa Jimbo Katoliki la Bukoba. Hii ni Shule iliyojengwa kama tunda au mrejesho wa tafakari ya dhati juu ya Sanda ya Torino hiyohiyo ili kumuenzi Yeye Yule tunayemkumbuka kila tunapoutazama Uso unaoonekana juu yake.  Mimi nilifikiwa na wazo la Sanda kwa mara ya kwanza bila kutegemea mwezi Aprili mwaka 1985, ikiwa ni mwaka wangu wa 8 wa upadre, nilipokutana na taarifa juu yake katika gazeti moja linaloitwa National Geographic Magazine, Toleo la Juni mwaka 1980.

Padre Mtajwaha akitoa akielezea juu ya Sanda ya Torino
Padre Mtajwaha akitoa akielezea juu ya Sanda ya Torino

Ni makala ya Vernon Miller wa Chuo cha Brooks, California, Marekani. Hisia zangu za kwanza baada kuisoma makala hii zilikuwa hasi na chanya kwa wakati mmoja. Makala hiyo ilinifanya nihisi mashaka makubwa na mvuto wa ajabu juu ya habari hii kwa wakati uleule. Kisa ni kwamba Makala hiyo ilizungumzia kitu halisi katika ulimwengu huu, tunachoweza kuona kwa macho yetu na kugusa kwa mikono yetu na bado kinafikirika na kuaminiwa na mamilioni ya watu kwamba kimemgusa Yesu Kristu kihistoria. Kwangu ilikuwa namna ya kitendawili kisichoepukika kikinitaka nichague kati ya haya mawili: Kukubali mvuto wake na matokeo yake au kuutupilia mbali mwaliko wa kukikumbatia kutokana na mashaka makubwa yaliyotawala kichwani mwangu. Wakati fulani, ndani kabisa moyoni na akilini mwangu nilijisikia kujisemea “Kama mwandishi wa makala hii alikusudia kumwaminisha yeyote juu ya jambo hili labda atawapata wengine lakini sio mimi”. Lakini kumbe labda kosa lilikuwa upande wangu maana mwandishi wa makala ile alikuwa anatoa taarifa tu juu ya kitu kilichopo kama kitu kilichopo duniani bila kuambatanisha ndoana wala mtego wa kumtaka msomaji yeyote akikumbatie au akikatae kama kitu kinachomnadi Yesu.

Kituo cha Sanda ya Torino huko KWAUSO Bukoba Tanzania
Kituo cha Sanda ya Torino huko KWAUSO Bukoba Tanzania

Kabla ya siku hiyo nilikuwa sijawahi kusikia wala kuona kimeandikwa chochote kuhusu Sanda ya Torino nikiwa mseminaristi au kabla ya kuingia seminari; nikiwa padre mpya au kwingineko. Lakini baada ya kuzingatia kwamba makala imeandikwa vizuri na imetoka katika gazeti lenye heshima niliamua kuisoma tena na hata kuirudia mara ya tatu baadaye jioni katika mazingira tulivu zaidi. Hata hivyo, siku hiyo mashaka hayakunitoka kichwani. Lakini pia shauku ya kutaka kujua zaidi mambo yakoje haikuzimika. Tangu hapo nimefuatilia na kujifunza kwa makini mambo yaliyogunduliwa kisayansi juu ya kitu hiki. Kadiri miaka inavyoongezeka juu ya mabega yangu, nimeendelea zaidi na zaidi kuvutiwa nacho. Matokeo yake nimeendelea kutambua na kukiri kwamba Sanda ya Torino si kitu kidogo kamwe wala kitu cha kupuuzwa kwa yeyote anayetafuta ukweli. Lakini pamoja na hayo yote, kuna jambo moja lisilopingika. Nalo ni hili. Yesu Kristu tunayemwamini aliishi kweli katika historia. Kwa hiyo hakuna lolote linaloharibika ikithibitika kwamba bado kipo kitu halisi katika mazingira yetu kinachoweza kuhusishwa na tukio fulani katika maisha yake na uwepo wake wa kihistoria nyakati zile. Ndugu msomaji kwa upande wangu leo hii imepita zaidi ya miaka 37 tangu nilipokutana na Sanda. Bado ninatafuta.  Katika kipindi hiki kirefu, licha ya dhoruba kali na magumu ya njiani, nimeweza kulipima suala hili la Sanda kiasi fulani nikitegemea kazi ya wataalamu wakubwa wenye zana za kisasa kabisa na uwezo wa kutosha kitaaluma wa kulichunguza kwa makini na utulivu. Nilichopata ni hiki kimoja: Kwa yeyote anayeitazama Sanda kwa dhati ni vigumu kushindwa kutambua kwamba kazi aliyoifanya Kristu kwa ajili yetu ni nzuri kupindukia na gharama iliyolipwa ili sisi tustahilishwe kuchuchumilia uzima wa milele ni kubwa, kubwa, kubwa.

Kuitazama Alama Kuu ya Upendo wa Kristo

Basi ndugu msomaji ninakukaribisha tuitazame Alama hii Kuu ya upendo wa Kristo Karibuni tukutane na kitu kizuri sana katika mazingira yetu katika ubora wake. Na kitu hicho ni Sanda ya Torino. Tusisite kukiendea kitu hiki tumejihami kwa uwezo wetu wa akili tuliyojaliwa na Mungu kama zana mojawapo tunayohitaji kuutafuta ukweli. Hata hivyo twende tukitambua pia kwamba Kristo, Mungu aliyefanyika mwili na kukaa kwetu kwa ajili yetu sisi ni Upendo na nafsi hai. Kwa hiyo twende tukikumbuka kwamba katika hali yake yeye kama upendo na nafsi hai Kristu hapatikani kwa nguvu au ukali wa sayansi wala usahihi wa mahesabu bali kwa uwazi na utayari wa kila mtu binafsi kumtambua katika kazi zake zenye utukufu. Twende tukijua kwamba utukufu huo sio lazima ujitokeze katika milipuko ya radi au matetemeko ya ardhi au matukio mengine ya kutisha. Mimi binafsi miaka yangu hii 37 ya kulitazama fumbo hili inaniambia kwamba licha ya ukimya na uhafifu wake Sanda ya Torino inaweza kuudhihirisha utukufu wa kazi zake Bwana kwa urembo na mng’aro tusioukuta katika viumbe vingi vinginevyo. Ndiyo sababu ninawaalikeni tujaribu kulifuatilia kwa pamoja fumbo hili la Sanda Takatifu, nikiamini kwamba hicho tutakachokutana nacho tutakipenda tu maana kinapendeza. Tena tuliendee fumbo hili bila makuu. Tujaribu kuliendea kwa unyenyekevu na kwa uwazi kama wanavyoenenda  watoto wadogo.

Je Huyu tunayemwona kwenye Sanda ni Yesu au mtu mwingine?

Alama ile Kuu inayojulikana kwa jina la Sanda ya Torino: Shuka la pekee  kabisa ulimwenguni: Shuka linalobeba simulizi la mojakwamoja la mateso na kifo cha Bwana wetu Yesu Kristu kwa ufasaha na urembo wa ajabu. Wengi wamelitazama kwa makini na busara Shuka hili na hatimaye wakaweza kulitambua kama zawadi yenye uwezo wa kuumwaga mbele ya macho yetu ujumbe kuhusu tendo la upendo usiopimika wa Mkombozi wetu Yesu Kristu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa ajili yetu. Karibuni tulitazame sisi pia. Karibuni tulijifunze sio tu kama fumbo la kisayansi bali zaidi sana kama mwaliko wa kutathmini upya maana ya uwepo wetu hapa duniani mbele ya kweli za mateso ya Bwana wetu zilizoandikwa ndani ya Shuka hili kama hati ya ushuhuda. Karibuni tulitafakari hasa katika kipindi hiki cha Kwaresima tukiwa tayari kuufaidi ujumbe wake wa kushangaza kama walivyowahi kufanya watu wengi wa nyakati mbalimbali akiwemo Mtakatifu Yohane Paulo II, Papa na mtakatifu wa nyakati zetu aliyetangazwa rasmi.

Kituo cha Sanda ya Torino huko KWAUSO Bukoba Tanzania
Kituo cha Sanda ya Torino huko KWAUSO Bukoba Tanzania

Ndugu Msikilizaji, tufungue mazungumzo yetu kwa kunukuu maneno ya John Jackson, mwanafizikia mmoja, askari katika kikosi cha Jeshi la Anga, Marekani, mtafiti mkubwa wa Sanda ya Torino aliyeongoza timu ya watafiti makini wanasayansi 40, chini ya mwavuli wa STURP (The Shroud of Turin Research Project, mwaka 1978): Mtaalamu huyu alisema: “Tunazo sababu za kusema kwamba picha ya Sanda haiwezi kuwepo. Hata hivyo picha hiyo ipo hata kama hatuelewi imetengenezwaje”. Kitaaluma swali la kwanza kabisa kuhusu Sanda ya Torino ni hili: Je, picha ya Sanda imetengenezwaje? Hili ni swali gumu kiasi kwamba sayansi haijaweza kutupatia jibu lake. Swali la pili ni hili: “Je, hii ndiyo Sanda yenyewe ya iliyohusika katika maziko ya Yesu wa Nazareti?” Hili pia ni swali gumu sana. Vernon Miller mwandishi wa makala “The Mystery of the Shroud”, National Geographic Magazene, June, 1980 ameandika hivi, “Wanasayansi na wanateolojia wanashikilia kauli moja kwamba (swali, kama huyu ndiye Yesu Kristu au la) ni jambo ambalo daima litabaki nje ya uwezo wa kuthibitisha”. Hata hivyo, kauli hiyo haimaanishi kwamba swali lenyewe haliuliziki tena wala kwamba majibu yake ya kuridhisha hayawezi kupatikana. Ukweli ni kwamba, swali hili linaulizwa mara nyingi kila siku.  Isitoshe, kwa upande wetu hatuwezi kuridhika kwa jibu jepesi litakaloonyesha kwamba kwetu haijalishi kama huyu ni Yesu au la. Sisi tunataka jibu lenye nguvu za kutuwajibisha, maana kama mhusika ni Yesu tutapenda kujua alipenda kutwambia nini kwa kututengenezea kitu hiki na kama sio yeye basi tunaweza hata kukitupilia mbali na kuhakikisha hakitusumbui.

Swali la kwanza: Je, Sanda inaonekanaje?

Jibu liko hivi: Sanda ya Torino ni shuka lenye urefu wa mita 4.36, kwa upana wa mita 1.10 na uzito wa kilogramu 2.450. Shuka hili linaitwa Sanda ya Torino kwa sababu tangu mwaka 1578 linahifadhiwa katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yohane Mbatizaji, Jimbo Kuu la Torino, mji mmoja katika nchi ya Italia, Kaskazini Magharibi. Kwenye Sanda, katika hali ya kukunjuliwa kwake, kunaonekana picha ya mtu mmoja, mwanaume, kifoni. Picha hii inazo sehemu mbili. Sehemu ya kwanza ya picha hii inamwonyesha mtu huyo upande wa mbele, kuanzia kichwani hata miguuni. Sehemu ya pili inaonyesha upande wa mgongo wake kuanzia kichwani/kisogoni hata miguuni. Hivyo, katika ujumla wake picha hii inamwonyesha Mtu mzima huyu vivyo hivyo alivyokuwa amezongwa katika shuka lililotumika kwa maziko yake. Hii ni picha nyororo sana inayofanana kama kivuli kisichoeleweka kinakoanzia wala kinakoishia. Kwa mtazamaji mgeni picha hii inaonekana kwa shida. (Pengine ndiyo sababu wapo watazamaji wageni wanaoiangalia Sanda mara ya kwanza na wakiulizwa wameona nini wataanza kueleza kwamba wanaona vitu kama meno ya wanyama au masikio au vitu vingine vya ajabu ambavyo kwa kweli havipo kabisa).

Sanda Takatifu
Sanda Takatifu

Mtazamaji akikaribia sana, picha inafifia kiasi cha kutoonekana. Hakuna mipaka ya brashi au alama zozote za uchoraji.  Vitu vyeusi vinavyojitokeza mara moja kwa jicho la mtazamaji vimejipanga mistari miwili sambamba ambapo picha, katika sehemu zake mbili imelala  katikati ya mistari hiyo. Picha ya mbele ni rahisi zaidi kutambulikana. Tukianzia  katikati mwa shuka hali limetundikwa kwa mapana yake tutaona kichwa cha Mtu mwenye Uso mrefu. Tukizidi kukazia jicho letu kuelekea kushoto, tutaweza kubaini uwepo wa kifua.  Kushoto zaidi inafuata mikono iliyokunjwa kuweza kukutanikia karibia kwenye kiwiko. Kushoto zaidi tena, yanaonekana mapaja, kisha eneo la magoti na hatimaye miguu. Hiyo ni sehemu ya kwanza ya picha. Ni picha ya mbele ya Mtu wa Sanda. Vivyo hivyo tena, tukianzia katikati kuelekea kulia, kinaonekana kichwa, kisogo, mabega, mapaja na miguu. Sehemu hii ya pili inaonyesha upande wa mgongo wa Mtu wa Sanda.

Padre Mtanjwaha akifafanua juu ya Sanda ya Torino kwa Maaskofu wa Tanzania
Padre Mtanjwaha akifafanua juu ya Sanda ya Torino kwa Maaskofu wa Tanzania

Swali la pili ni hili: Sanda inao mvuto tusiouhisi katika kitu kingine chochote kile ulimwenguni. Je, mvuto huo unatokana na nini? Jibu liko hivi: Sanda kama nguo, ni nguo; na ile picha iliyopo juu yake, hata kama sio picha ya kawaida ni picha. Kiini cha mvuto wa Sanda ni zaidi ya picha kama picha. Ni kweli picha hii, katika sehemu zake mbili zinazoonekana juu yake kama vivuli haikutokana na ufundi wo wote wa uchoraji unaofahamika hata leo. Lakini hilo halitoshi kuelezea sababu kubwa za mvuto wa Sanda kwa watafiti na wasiokuwa watafiti wa kisayansi. Kitu kinachowavuta watu wa tabaka zote katika utafiti huu ni ile fikra kwamba katika nguo hii na picha inayoonekana juu yake tunaweza tukawa tunakutana na alama iliyoachwa na Bwana wetu Yesu Kristu, Mkombozi wa ulimwengu. Sanda inagusa hisia na kupelekea majibu yanayokinzana. Leo hii mtu akisema mimi ninaipenda kucha ya kidole changu, hakuna atakayejisumbua kuyasikiliza tena maneno hayo. Lakini, akisema “Ninaipenda sana Sanda ya Torino” mvua ya mishale ya shutuma itamnyeshea palepale.  Kama ingekuwa inafahamika kwa uhakika wote kwamba Sanda hii haina uhusiano wowote na Yesu Kristu, mvuto wake ungeyeyuka mara moja. Lakini kumbe mambo hayako hivyo. Katika ukimya wake Sanda inazungumzia tukio lile kuu la kifo na ufufuko wa Mkombozi wa ulimwengu kwa staili ya namna yake. Na hapo ndio kunalala uzito wa mvuto wa Sanda ya Torino.

Askofu Kilaini akizindua Kituo cha Sanda huko KWAUSO Bukoba Tanzania
Askofu Kilaini akizindua Kituo cha Sanda huko KWAUSO Bukoba Tanzania

Neno “Mtu wa Sanda”:  Kwa desturi watafiti hupendelea kutumia neno “Mtu wa Sanda”  badala ya jina la Mhusika mwenyewe. Hii ni kwa sababu hawajapata jibu lililothibitika kisayansi kwamba mhusika ni nani. Katika mazungumzo yetu, sisi pia tutamwita vivyo hivyo kwa sababu ni vizuri kuziheshimu taratibu za  kisayansi. Mtazamo huo unasaidia kumjegea mazingira mtafiti/msikilizaji uhuru wa kuamua mwenyewe  bila kuingiliwa kuhusu swali hili zuri, “Je, kwangu mimi huyu anayeonekana kwenye Sanda ni nani na ujumbe wake kwangu ukoje?” Katika sura ifuatayo yatatolewa maelezo juu ya mazingira ya utafiti wetu unaounganisha fani mbalimbali za maarifa chini ya neno “Sindonolojia”.

01 April 2022, 14:53