Paraguay:Thamani ya katiba na mahitaji ya msaada kwa familia
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Kwa mujibu wa Askofu Miguel Ángel Cabello wa Jimbo la Concepción, nchini Paraguay ametoa ujumbe kwa njia ya video kupitia Mtandao wa Baraza la Maaskofu Paraguaye CE) ambapo amekumbusha jinsi ambavyo Katiba ya Nchi izingatie familia msingi wa Jamii. Amekumbusha hayo katika fursa ya Siku ya Kitaifa ya Familia ambayo inaadhimishwa kila mwaka katika Nchi hiyo mwishoni mwa mwezi Aprili, na kuwaalika wote kwamba wathamanishe Katiba yenye msingi juu ya muungano wa mwanaume na mwanamke katika kuheshimu misingi ya binadamu na Kikristo. Katika ujumbe wake Askofu Mhusika huyo wa Kichungaji wa Familia wa Baraza la Maaskofu, Paraguay ametoa ushauri kwa waamini, awali ya yote kuthamanisha zawadi ya maisha kwa kila hatua, kuanzia kutungwa kweke hadi kufikia kifo chake cha kawaida, na kusema kwamba Kanisa linakataa utoaji mimba, Eutanasia na kila aina ya majaribio ya kisayansi ambayo yanakwenda dhidhi ya hadhi ya kibinadamu.
Mamlaka ya Taifa iheshimu mamlaka ya wazazi kuchagulia watoto wao elimu bora
Baadaye Askofu huyo amewaalika wazazi kuwa wawajibikaji wa uzazi, katika kutunza na baadaye kuelimisha watoto wao, huku akiziomba mamlaka, ziheshimu mamlaka ya wazazi ambayo kwayo wazazi wana haki ya kuwachagulia watoto wao elimu bora na kwa maana hiyo alihimiza ushirikishwaji zaidi wa wazazi katika mchakato wa mabadiliko ya kielimu yanayoendelea nchini humo huku, akiwapati mapendekezo ya kufundisha watoto wao maadili mema kama vile mazungumzo, heshima, uelewano, mshikamano, msamaha, kwa kuwa ndiyo msingi wa maelewano ya familia.
Kanisa linakataa itikadi za kijinsia na upotoshaji wa ndoa
Akikataa itikadi ya kijinsia, inayotaka kupotosha ndoa, familia na kuharibu utambulisho wa asili wa mwanamume na mwanamke Askofu huyo, alibainisha Kanisa kutokubaliana na kuhalalisha utoaji mimba, ndoa ya ushoga na kupitishwa kwa watoto kwa upande wa watu wa aina moja, kwa heshima ya hadhi ya kuwa mwanadamu katika ujauzito na watoto walio katika mazingira magumu ambao hawawezi kujilinda. Kupitia Ujumbe huo kwa njia ya Video, Maaskofu wanaomba kuundwa kwa sheria na mipango ya sera za kisiasa na kwamba zitetee na kuhamasisha ustawi wa familia na kwamba zitoe msaada wa kila familia, hasa maskini zaidi, kupitia upatikanaji wa makazi yenye heshima, kazi, chakula, afya, elimu na usalama. Kwa kuhitimisha Askofu Cabello alialika familia uimarisha imani, matumaini na mapendo, kwa kufanya mazoea ya kusali kila siku, kutafakari Neno la Mungu na kushiriki katika sakramenti hasa Ekaristi. Na hatimaye, aliomba baraka na ulinzi wa Familia Takatifu ya Nazareti ili kusaidia ujenzi wa jamii yenye uadilifu, udugu, msaada na hadhi kwa wote.