Tafuta

Sherehe ya ufufuko wa Yesu Kristo ni chimbuko la maadhimisho yote katika mwaka wa Liturujia wa Kanisa. Sherehe ya ufufuko wa Yesu Kristo ni chimbuko la maadhimisho yote katika mwaka wa Liturujia wa Kanisa. 

Pasaka ya Bwana: Kristo Yesu Jua La Haki Mwanzo Wa Maisha Mapya

Sherehe ya ufufuko wa Yesu Kristo ni chimbuko la maadhimisho yote katika mwaka wa Liturujia. Tunaalikwa na Mama Kanisa kufurahi na kushangilia ushindi dhidi ya shetani, dhambi na mauti kama anavyoimba mzaburi; “Hii ndiyo siku hii, aliyoifanya Bwana, tuishangilie na tuimbe aleluya” (Zab 118:24). Mungu amewafungulia mlango wa milele kwa njia ya Kristo Yesu aliyeshinda mauti.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya Pasaka, Sherehe ya ufufuko wa Yesu Kristo, siku ya tatu baada ya kifo chake kama wimbo wa mwanzo unavyoimba; “Nimefufuka na ningali pamoja nawe; umeniwekea mkono wako, maarifa hayo ni ya ajabu, alaluya” (Zab. 139:18, 5-6). Bwana amefufuka kweli kweli, aleluya. Utukufu na ukuu una Yeye hata milele na milele (Lk. 24:34; Ufu. 1:6). Sherehe ya ufufuko wa Yesu Kristo ni chimbuko la maadhimisho yote katika mwaka wa Liturujia. Tunaalikwa na Mama Kanisa kufurahi na kushangilia ushindi dhidi ya shetani, dhambi na mauti kama anavyoimba mzaburi; “Hii ndiyo siku hii, aliyoifanya Bwana, tuishangilie na tuimbe aleluya” (Zab 118:24). Ndiyo maana katika sala ya mwanzo Padre kwa niaba ya waamini anasali; “Ee Mungu, umetufungulia mlango wa milele kwa njia ya Mwanao wa pekee aliyeshinda mauti. Tunakuomba utujalie sisi tunaodhimisha kufufuka kwake Bwana wetu, tufufuke katika nuru yako kwa kufanywa wapya na Roho wako”. Somo la kwanza la kitabu cha Matendo ya Mitume (Mdo. 10:34; 37-43); ni hotuba ya Mtume Petro kwa wapagani/wakatekumeni waliokuwa wakijiandaa kupokea ubatizo. Hotuba hii ni ufupisho wa mafundisho yote ya Kikristo. Petro anagawanya mafundisho yake katika sehemu kuu nne akitaja matukio makuu katika maisha ya Yesu Kristo ya kwamba: Yesu alikuwa Mtu kweli kama sisi isipokuwa tu hakuwa na dhambi.

Yesu alienda huku na huko akifundisha habari za Ufalme wa Mungu, akiponya wagonjwa na kutenda mema mengine. Yesu ni mjumbe wa Mungu ambaye watu wake hawakumkubalika, hivyo walimtesa, wakamtundika msalabani, wakamuua. Lakini Mungu alimfufua siku ya tatu ili kuthibitisha na kuthihirisha utabiri wa Manabii juu yake. Mitume na wafuasi wa Kristo ndio mashahidi wake wa kweli kwa kuwa waliishi naye, walikula na kunywa naye, waliyasikia mafundisho yake na aliwatuma wakafundishe kile walichojifunza, walichoona kwa miujiza aliyoifanya kwa kuwaponya na kuwafufua watu. Kwa Sakramenti ya Ubatizo sisi nasi tumefunuliwa kwa njia ya Roho Mtakatifu maisha, mateso, kifo na ufufuko wa Yesu. Hivyo tunapaswa kuwa kweli mashahidi wake. Ikiwa katika Ubatizo maisha yetu yalibadilika kwa kuuvua utu wa kale, utu wa dhambi – tukauvaa utu mpya wa Kristo mfufuka basi tunapaswa kumshuhudia Kristo kwa maneno na matendo yetu na kuyakemea maovu yote yanayojitokeza katika maisha yetu kwa ujasiri bila hofu wala woga wowote. Katika dominika ya ufufuko wa Bwana Misa ya mchana, Mama Kanisa ameweka masomo mawili ya kuchagua kwa somo la pili. Linaweza kusomwa somo la waraka wa Mtume Paulo kwa Wakolosai (Kol. 3:1-4) au somo la Waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Wakorintho (1 Kor. 5:6-8).

Liturujia ya Pasaka ni kiini cha liturujia zote za Mama Kanisa.
Liturujia ya Pasaka ni kiini cha liturujia zote za Mama Kanisa.

Somo la Waraka wa Mtume Paulo kwa Wakolosai (Kol. 3:1-4); linatufundisha kuwa; Katika Ubatizo tulikufa na kufufuka na Kristo; tukaahidi kumfuata daima katika maisha ya taabu na raha, hivyo yatupasa kuishi kadiri ya ahadi hiyo tukiacha mabaya na kutenda mema. “Basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu, Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu...Kwa maana mlikufa, na uhai wenu umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu. Kristo atakapofunuliwa, aliye uhai wetu, ndipo na ninyi mtafunuliwa pamoja naye katika utukufu.” Somo la Waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa wakorinto (1 Kor. 5:6-8); linatufundisha kuwa; Kabla ya kula mwana kondoo wa Pasaka Waisraeli walitoa chachu yote ya zamani nyumbani mwao – kujipatanisha wao kwa wao, na kujipatanisha wao na Mungu. Tendo hili ni alama ya kuacha maisha mabaya ya zamani na kuanza maisha mapya, maisha mema, maisha ya baada ya kifo na ufufuko wa Bwana. “Kujisifu kwenu si kuzuri. Hamjui kwamba chachu kidogo hulichachusha donge zima? Basi, jisafisheni, mkatoe ile chachu ya kale, mpate kuwa donge jipya, kama vile mlivyo hamkutiwa chachu. Kwa maana Pasaka wetu amekwisha kutolewa kuwa sadaka, yaani, Kristo; basi na tuifanye karamu, si kwa chachu ya kale, wala kwa chachu ya uovu na ubaya, bali kwa yasiyochachika, ndio weupe wa moyo na kweli”.

Injili kama ilivyoandikwa na Yohane (Yn. 20:1-9); inaweka wazi ukweli mkuu wa imani yetu kwamba Kristo amefufuka kweli. Ushahidi ni wazi: Kaburi liko tupu, vitambaa alivyolalia, na baadaye akajionyesha kwa wafuasi wake. Kumbe ufufuko wake ni utimilifu wa ukombozi wetu. Ilikuwa asubuhi na mapema siku ya kwanza ya Juma, Maria Magdalena alipofika kaburini.” Maneno haya ya ufunguzi wa Injii yanaashiria ushindi wa Kristo dhidi ya kifo na mauti. Kulikuwa na ukimya mkubwa duniani na utulivu wa hali ya juu, kungali bado giza lakini Maria Magdalena hakuona shida kwenda kaburini ili aweze kuupaka mwili wa Yesu manukato kama ilivyokuwa desturi ya kuzika kwao ili kukamilisha ibada za maziko. Naye alipofika aliona kaburi li wazi. Kisha kuona vile alirudi mapema kuwapa habari Petro na mitume. Ushuhuda wa wanawake nyakati hizo haukudhaminiwa. Lakini, Petro na Yohane wanatoka mbio kuelekea Kaburini. Yule mwanafunzi mwingine alienda kwa mbio zaidi kuelekea kaburini, alipofika hakuingia kaburini, Petro naye akafika akaingia, akaona sanda na leso vimetawanywa. Kisha yule mwanafunzi mwingine aliingia kaburini, akaona na kuamini.

Yesu alifufuka siku ya kwanza ya juma - kwa Wayahudi ni siku ya Jumatatu. Wakristo walianza kuiita “Siku ya Bwana” – Dominika (Mdo 20:7, Ufu 1:10). Siku hii ikawa muhimu sana na kuchukua nafasi ya sabato ya Kiyahudi. Ilikuwa siku hii ya kwanza ya juma Mungu alipoumba mwanga: Mungu akasema; “Iwe Nuru” ikawa Nuru. Mungu akaona ya kuwa Nuru ni njema, Mungu akatenga Nuru na Giza, Mungu akaiita Nuru Mchana na giza Usiku, ikawa asubuhi ikawa jioni, siku moja (Mwa 1:3-5). Kristo ni mwanga mpya na jua la haki. Katika siku hii ya kwanza ya Juma, maisha yanaanza upya. Mungu anaanzisha historia mpya ya maisha ya mwanadamu. Yesu Kristo amefufuka. Kifo hakitutawali tena. Kwa sasa tunao mwanga wa Pasaka. Kwa mwanga huu giza haliwezi kututawala tena. Sisi ambao wakati wa vijilia tuliingia kanisani katika hali ya giza kisha mwanga utokanao na mwanga wa Pasaka ulituzukia hatuna sababu ya kuogopa. Uzima unatawala dhidi ya mauti, wema unatawala dhidi ya uovu. Wanawake katika familia za Kiyahudi ambao walihesabiwa kati ya watumwa au vitu alivyomiliki mwanaume, mwanamke ambaye hakuaminika, hakuruhusiwa kutoa maoni yake mbele ya wanaume, hakuruhusiwa kutoa ushahidi ndiye ambaye Mungu anamfanya kuwa shahidi wa kwanza wa ufufuko na ukombozi wa mwanadamu.

Waamini wanaitwa na kutumwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu
Waamini wanaitwa na kutumwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu

Mwanamke anashirikishwa katika kazi ya ufufuko na kwenda kuwa mashuhuda wa ufufuko kwa Mitume. Hawa ndiyo waliokuwa watangazaji wa habari njema. Wakiisha kuwatangazia Mitume habari hii njema, ndipo Petro na mitume nao wakapata ujasiri wa kutoka kwenda kaburini kushuhudia habari hizi. Ufufuko wa Yesu unaleta uhai mpya, mwanga mpya na uumbaji mpya katika maisha ya kiroho tuliyopata kwa njia ya ubatizo. Kristo mfufuka ndiye mwanga mpya wa maisha yetu ya kiroho. Ufufuko wa Yesu unatuwezesha kuelewa maana ya mateso na kifo chake. Mateso na kifo cha Kristo ulikuwa mpango wa Mungu wa kutukomboa sisi kutoka utumwa wa shetani na dhambi na kutufanya kuwa watoto wake. Hii inatusaidia nasi kuyapokea mateso, kifo na magumu ya maisha tukiamini kwamba ikiwa Mungu ameruhusu yatupate ni kwa sababu jambo jema litatiririka katika hayo. Maisha yetu ni kama mbegu, ili iote lazima kwanza ioze – “Punje ya ngano isipoanguka katika nchi ikafa, hubaki hali hiyo hiyo, bali ikifa huzaa mazao mengi”. Kwa hiyo kifo chetu kinapata maana kwa ufufuko wa Yesu. Akifufuka kutoka wafu, Bwana Yesu ameondoa giza la kifo na dhambi na kutuongoza kwa Baba yake na Baba yetu. Kwa kuwa Kristo alifufuka kutoka wafu, maisha mapya, maisha katika Roho yanapatikana kwa wote walio tayari kuyapokea. Yeyote anayekufa kuhusu dhambi na kumkataa shetani anapokea hali mpya ya maisha ya kiroho, ni sawa na kuumbwa upya.

Tunapomwamini Kristo, maisha halisi ya Kristo yanakuwa maisha yetu pia. Upendo wake unatuleta katika imani kwa Mungu na upendo kwa Jirani zetu. Upendo kwa Jirani ni kama cheche inayoamsha imani kwa Bwana Yesu ndani ya mioyo yetu. Upendo kwa jirani ni hitaji msingi kama tunataka imani yetu kwa Mungu ikue na kuzaa matunda nasi tutaimba kwa furaha; “Mkono wa Bwana umeniinua, sitakufa bali nitaishi, na kutangaza aliyonitendea Bwana” (Zab 118:16-17). Tumsifu Yesu Kristo Mfufuka. Amina.

Pasaka Jua La haki
16 April 2022, 12:45