Tafuta

Kristo Yesu Mfufuka ni Mshindi dhidi ya Dhambi na mauti, mwaliko kwa waamini kumtangaza na kumshuhudia katika uhalisia wa maisha yao. Kristo Yesu Mfufuka ni Mshindi dhidi ya Dhambi na mauti, mwaliko kwa waamini kumtangaza na kumshuhudia katika uhalisia wa maisha yao. 

Pasaka ya Bwana: Yesu Mfufuka Ni Mshindi Wa Dhambi Na Mauti

Siku ya kwanza ya juma Maria Magdalena alipokwenda kaburini akakuta kaburi li wazi. Huu ni ushuhuda wa kwanza wa ufufuko kuwa Yesu hayumo tena kaburini, ni mzima, kwa chenyewe kinaweza kisitoshe kushuhudia ufufuko. Ni kitendo lakini kinachotazamwa pamoja na utabiri wa manabii pamoja na neno lile ambalo Yesu mwenyewe alikuwa akiwaambia wanafunzi wake.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

UTANGULIZI: “Kristo amefufuka, Aleluya, Aleluya.” Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, karibu katika kipindi hiki cha Tafakari ya Neno la Mungu. Leo tunatafakari masomo ya dominika ya Pasaka, sherehe ya furaha kubwa ya kufufuka kwake Bwana wetu Yesu Kristo. Na kwa kweli ni sherehe ya furaha kubwa kwa sababu Pasaka ndiyo sherehe kubwa kuliko sherehe zote za Kanisa na kimsingi ndio chimbuko la sherehe na maadhimisho yote ya Kiliturujia. MASOMO KWA UFUPI: Tuingie sasa katika ufafanuzi wa masomo ya Misa. Somo la Injili (Yoh 20:1-9) ndilo linalotupatia simulizi la ile siku ya ufufuko,  siku ya kwanza ya juma Maria Magdalena alipokwenda kaburini akakuta kaburi li wazi. Huu ndio unakuwa ushuhuda wa kwanza wa ufufuko kuwa Yesu hayumo tena kaburini, ni mzima. Kitendo hiki cha kukuta kaburi wazi, kwa chenyewe kinaweza kisitoshe kushuhudia ufufuko. Ni kitendo lakini kinachotazamwa pamoja na utabiri wa manabii pamoja na neno lile ambalo Yesu mwenyewe alikuwa akiwaambia wanafunzi wake. Yesu mwenyewe atathibisha ufufuko wake kwa ushuhuda wa pili baada ya huu wa kaburi wazi pale atakapoanza kuwatokea wafuasi wake.

Kristo Yesu alifufuka Siku ya kwanza ya Juma, mwanzo mpya wa maisha.
Kristo Yesu alifufuka Siku ya kwanza ya Juma, mwanzo mpya wa maisha.

Tukibaki katika somo hili bila kwenda mbele zaidi ya yale tunayoyasikia leo tunaelewa nini kuhusu ufufuko wa Yesu? Yapo mambo mengi ambayo Mwinjili Yohane anayaeleza kuhusu ufufuko wa Yesu katika somo hili. Tuyaagalie matatu tu kwa ufupi. La kwanza ni siku yenyewe ya ufufuko. Yesu anafufuka siku ya kwanza ya juma. Kwa wayahudi, kilele cha wiki kilikuwa ni siku ya sabato, kwetu ni jumamosi. Baada ya sabato wiki ilianza kwa siku ya kwanza. Kufufuka kwa Yesu siku ya kwanza ni kuashiria kuanza kwa nyakati mpya. Nyakati zinazotangaza kukombolewa kwa ulimwengu na watu wote kufanyika wana wa nuru. Ndiyo maana tangu ufufuko wa Yesu siku hiyo ya kwanza ya juma, ambayo kwetu ni jumapili, imekuwa ni siku ya kuadhimisha ukombozi wetu na kumtukuza Kristo mfufuka.

Jambo la pili ni hiyo alama ya kaburi wazi ambayo tumekwishaigusia hapo mwanzo kuwa ni alama inayodhihirisha ufufuko. Mwinjili Yohane anaeleza kuwa wale wanafunzi walipoingia mle ndani ya kaburi waliangalia namna vitambaa na sanda vilivyolala na ile leso iliyokuwa kichwani imezongwazongwa mahali pa peke yake. Hii maana yake ni nini? Vitambaa na sanda vilikuwa vimetupwa tupwa au vilikuwaje? Kwa msaada wa Biblia ya kiyunani inayohifadhi lugha asili aliyotumia mwinjili Yohane, tafsiri ya maneno haya haimaanishi kwamba mle ndani walikuta vurugu na vitu haviko katika utaratibu. Ni kuwa vitambaa na sanda vilikuwa vimelazwa vizuri pale ulipokuwa umelazwa mwili wa Yesu na ile leso iliyokuwa kichwani pake ilikuwa imeviringishwa pembeni katika nafasi ya kichwa kwa utaratibu uleule kama ilivyokuwa awali. Yohane anashuhudia kuwa kwa ufufuko, Kristo aliingia katika mwili wa utukufu bila kuvuruga mpangilio wa vitambaa na sanda zilizokuwa zimemfunika. Na kwa hali hii haiwezekani kuwa kwamba mwili wake uliibwa kwa sababu isingewezekana kuuchukua mwili wa Yesu bila kuvuruga namna ambavyo vitambaa, sanda na leso vilikuwa vimeufunga mwili huo.

Jambo la tatu na la mwisho ni kuhusu mashuhuda ambao Yohane anawatumia katika Injili hii. Wa kwanza ni Maria Magdalena, wa pili ni mwanafunzi asiyetajwa kwa jina ila anaelezewa kuwa ni yule ambaye Yesu alimpenda na wa tatu ni Petro. Wahusika hawa wanatuonesha kuwa ufufuko, japokuwa ni tendo la kihistoria, ni tendo pia linaloenda zaidi ya historia na kuwagusa watu wa nyakati zote. Maria Magdalena ambaye ndiye shuhuda wa kwanza wa ufufuko na yule mfuasi ambaye Yesu alimpenda wanakuwa ni kielelezo cha watu wa nyakati zote ambao kwa upendo mkubwa wanamtafuta Yesu. Watu walio na kiu Yesu aingie katika mioyo yao. Wanaomtafuta hivi humpata kwa sababu Yesu mfufuka hakai kaburini bali hukaa katika mioyo yao wamtafutao. Shuhuda wa tatu ni Petro. Huyu ndiye anayeachiwa nafasi ya kwanza ya kuingia kaburini. Petro kwa nafasi yake ya kiongozi ni kielelezo cha Kanisa ambalo ndilo linapewa mamlaka na wajibu wa kuhifadhi na kushuhudia fumbo la ufufuko wa Kristo kwa nyakati zote.

Kristo Mfufuka ni Mwanga wa Mataifa.
Kristo Mfufuka ni Mwanga wa Mataifa.

Baada ya kuliangalia somo la Injili, tutupie macho sasa katika masomo mawili yaliyosalia. Somo la kwanza ambalo linatoka Kitabu cha Matendo ya Mitume (Mdo. 10: 34a, 37-43) linatuonesha sasa namna Mitume na Kanisa lilivyolichukulia fumbo zima Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo katika uzito wake. Fundisho msingi walilolitoa mitume, ile Habari Njema waliyoitangaza popote pale walipoenda ilikuwa ni habari ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo. Ni hapo ndipo Kanisa lilipotoa msingi wa uinjilishaje wake wote. Ndiyo hayo maneno anayotangaza Petro akisema “Kristo yule ambaye wayahudi walimkataa, wakamsulubisha, sasa amefufuka.” Somo la pili, kutoka Waraka wa Mtume Paulo kwa Wakolosai (Kol 3, 1-4 ) linaweka sasa uwiano kati ya fumbo la Pasaka na maisha ya kawaida ya muumini. Paulo anaonesha kuwa yule anayekiri imani kwa Kristo mfufuka na kubatizwa ni mtu anayeanza maisha mapya ya ufufuko hivyo mtindo wake wa maisha ni lazima uwe unamwelekea Kristo na wala usiwe na maelekeo ya kiulimwengu. Maana yake ni kwamba kanuni zinazoongoza maisha ya mkristo zinapaswa kuwa ni kile alichofundisha na kukiishi Kristo mwenyewe. Na huko ndiko kumvaa Kristo.

TAFAKARI: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, katika sherehe ya Pasaka tunaimba pamoja na mzaburi “Hii ndiyo siku aliyoifanya Bwana, tuifurahie na kuishangilia” (Zab 118:24). Pasaka ni furaha, Pasaka ni amani, Pasaka ni neema kwa sababu wokovu ulimwengu uliokuwa unausubiri umetimia. Kristo Mfufuka na awe mwanga wa kuyaangazia maisha yetu ili tusitembee tena katika giza la dhambi bali katika uangavu wa nuru yake.

Pasaka Ufufuko
16 April 2022, 15:57