Sherehe ya Pasaka ya Bwana ni kielelezo makini cha upendo unaomwilishwa katika imani na matumaini. Sherehe ya Pasaka ya Bwana ni kielelezo makini cha upendo unaomwilishwa katika imani na matumaini. 

Pasaka ya Bwana Ni Sherehe Ya Upendo Wenye Mvuto Wa Imani

Pasaka katika mwanga wa Sinodi. Kanisa linaalikwa kusafiri na kutembea kwa pamoja, sio kwa kuangalia majukumu na nafasi zetu tunazokuwa nazo, bali kwa kuongozwa na upendo, iwe katika familia, jumuiya zetu ndogo ndogo, vigango, parokia na hata majimbo yetu. Kanisa la kweli ni lile linalokuwa ni familia ya upendo, na ndilo linaloweza kuingia kaburini na kuona na kuamini.

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Mapema asubuhi, siku ile ya kwanza ya juma, ikiwa bado giza na ukimya mkuu, tunakutana na Maria Magdalena anakwenda kaburini alfajiri na mapema, siku ya kwanza ya juma. Baada ya kifo cha Yesu ile siku ya Ijumaa kuu, ni kama kila kitu kimefikia ukomo na mwisho wake, ni giza, ni ukimya, ni mashaka na ndio tunaona anajihimu mapema kungali giza bado na akiwa amejaa na uoga anaenda kaburini. Kifo kinaonekana kushinda katika hali na mazingira ya namna hiyo. Utawala wa mabavu, ubaguzi, rushwa, kukosa haki na mengi maovu yanaoneka kushinda. Ni kama ulimwengu ulisimama, hakukuwa na uhai wala matumaini tena baada ya kifo chake Yesu pale juu Msalabani. Upande mwingine mara baada ya Maria Magdalena kufika pale kaburini na kukuta kaburi li wazi tunaona kila kitu sasa kinabadilika na kuchukua sura nyingine. Maria Magdalena anakimbia kwa kasi na kwenda kwa Simoni Petro, na pia kwa yule mwanafunzi mwingine ambaye Yesu alimpenda. Nao pia wanatoka na kukimbia kwa pamoja kuelekea kaburini. Uhai au maisha yanaanza tena! Hata hivyo Maria Magdalena anafikiri kuwa wamemwiba Bwana kaburini, hivyo bado giza nene, bado safari ndefu. Mwinjili Yohane kwa mshangao hatuoni tena nini kilijiri kwa upande wa mwanamama Maria Magdalena na badala yake sasa anawaleta mbele yetu magwiji wawili, ndio mitume Petro na yule mwanafunzi mwingine mwenye jina la kivumishi kuwa mwanafunzi ambaye Yesu alimpenda.

Upendo unaomwilishwa katika imani ni chachu ya ushuhuda wa Kristo Mfufuka.
Upendo unaomwilishwa katika imani ni chachu ya ushuhuda wa Kristo Mfufuka.

 

Tunaona Mitume hawa wawili baada ya kupokea ujumbe kuwa kaburi li wazi kutoka kwa Maria Magdalena wanakimbia kwa kasi kuelekea kaburini. Yule mwanafunzi aliyendwa na Bwana anafika wa kwanza na anainama na kuchungulia na kuona vitambaa ila hakuingia. Na mwisho anafika Petro na hivyo anaingia wa kwanza kaburini na kuona vitambaa na yote ila pasipo kuuona mwili wa Yesu. Mtakatifu Yohane Krisostomo anasema labda Mitume nao walikuwa na mawazo haya yafuatayo: Kama mwili wake umechukuliwa kutoka kaburini basi kwa hakika waliouhamisha hawakupaswa kuuvua mwili sanda na leso, hivyo wangembeba kirahisi zaidi pamoja na sanda na leso alizozikwa nazo, hivyo hawakuwaza kuwa mwili wake umeibiwa kutoka kaburini. Mwanataalimungu Hans Urs Von Balthasar katika tukio hili anamtambulisha Simoni Petro kama “ecclesial office” na yule mwanafunzi mwingine kama “ecclesial love”, naomba ninukuu hapa maneno yake katika lugha ya Kiingereza: “Both disciples run there together yet not together, for, unburdened by the cares borne by the office, Love runs faster. Yet Love yields to Office when it comes to examining the tomb, and Peter thus becomes the first to view the cloth that had covered Jesus’ head and establish that no theft had occurred. That is enough to permit Love to enter, who sees and believes.” (Rej. Hans Urs Von Balthasar, Light of the Word, p. 71). Mitume wanaonekana kukimbia pamoja wote wawili lakini hawakuwa wamoja, kwani mmoja anazongwa na urasimu wa ofisi, hivyo ni upendo unaokimbia zaidi kuliko majukumu na urasimu utokanao na ofisi.

Hivyo ukweli wa ufufuko hatuwezi kuufikia kwa kuzingatia urasimu na mambo yanayotusonga katika ulimwengu huu bali kwa kuruhusu kuongozwa na upendo. Ni kwa njia ya kuruhusu upendo uingie katika kaburi lile hapo kwa hakika tunaweza kuona na kuamini. Sio tafsiri sisisi bali tunajaribu kupata maana ya nukuu hii ya Mwanataalimungu Urs Von Balthasar. Pasaka ni sherehe ya upendo! Hatuna namna nyingine yeyote inayoweza kutusaidia kuufikia na kukutana na Yesu Kristo Mfufuka isipokuwa njia ile ya upendo, yaani, “ecclesial love”. Kanisa la Kisinodi linaalikwa kusafiri na kutembea kwa pamoja, sio kwa kuangalia majukumu na nafasi zetu tunazokuwa nazo, bali kwa kuongozwa na upendo, iwe katika familia, jumuiya zetu ndogo ndogo, vigango, parokia na hata majimbo yetu. Kanisa la kweli ni lile linalokuwa ni familia ya upendo, na ndilo linaloweza kuingia kaburini na kuona na kuamini. Kila mmoja wetu katika Maadhimisho haya ya Kipasaka hatuna budi kuona ni kwa namna gani ninautanguliza upendo katika kukutana na Yesu Kristo Mfufuka, kwani bila upendo hatuwezi kuona na kuamini, na hivyo Pasaka inakosa maana na mashiko katika safari yetu ya imani. Hatuwezi kuifikia imani ya kweli nje ya upendo! Kila mmoja wetu aguswe na aone ni kwa namna gani tunaweza kuufikia ukweli huu wa Ufufuko kwa njia ya upendo!

Tunaona tofauti na Injili ya Luka hapa Mitume wanajikuta ni wao tu wenyewe bila Teofania au msaada wa mwanga kutoka mbinguni kama uwepo wa malaika. Wanabaki wanakutana na ishara za kawaida tu na mbaya zaidi ishara za umauti, ndio sanda na leso na jiwe na kaburi tupu. Ni ishara za Kisayansi, sio njia zinazoweza kutufikisha katika kerygma ya Imani, yaani ya ufufuko. Na ndio tunaona Petro hata baada ya kuingia anabaki bila kuelewa nini maana yake, kwa maneno mengi alikuwa bado katika giza nene. Yule mwanafunzi mwingine ambaye mwanateolojia von Balthasar anamtambulisha kama “ecclesial love”, baada ya kuingia na kuona anapiga hatua nyingine mbele anaamini. Hata mbele ya ishara zile za kifo, mwanafunzi aliyependwa na Bwana anafaulu kupiga hatua ya kufikia imani. Anaona ushindi dhidi ya umauti. Anakubali kuongozwa sio tena na mantiki na akili za kibinadamu bali na fadhila ile kuu ya upendo. Kwake mwanafunzi huyu anaonja upendo sio tu kabla ya mateso na kifo bali hata anapokuwa pale kaburini. Walikuwa bado hawajaelewa Maandiko, sentesi hii Mwinjili anaiweka hata baada ya yule mwanafunzi aliyependwa kuwa ameona na kuamini na kwa kweli sio kupinga alichoandika kabla, ila ni kuonesha jinsi gani jumuiya ya rafiki zake Yesu walikuwa bado na safari ya kufikia ukweli wa Pasaka ambao ni kwa maongozi ya Maandiko Matakatifu tunaweza kuufikia na si nje ya hapo. Ni ukweli wa kiimani hata kama ulitokea katika historia ya mwanadamu. 

Upendo ni chemchemi ya imani katika Fumbo la Ufufuko wa Bwana.
Upendo ni chemchemi ya imani katika Fumbo la Ufufuko wa Bwana.

 

Ni ukweli ambao hatupaswi kukutana nao mara moja tu katika maisha yetu bali kila siku na katika nyakati na mahali pote. Ni safari ya Imani ya maisha yetu yote. Kila siku hatuna budi kuwaonesha wengine kuwa sisi ni wafuasi wa Yesu Kristo Mfufuka, sio tu kwa maneno yetu bali zaidi sana kwa ushahidi wa maisha yetu. Hivyo mfuasi wa kweli wa Yesu daima anaongozwa na Neno la Mungu, ni kwa njia hiyo pekee nasi tunaweza kufikia imani na sio kama Tomaso aliyetaka ukweli wa ufufuko uwe sawa na ukweli wa Kisayansi, kwa kuuona kwa macho yake na kuushika kwa mikono yake. Wakarudi nyumbani kwao, ni baada ya kukutana na Yesu Mfufuka kila mmoja wetu anaalikwa kurejea nyumbani kwake na kutoa ushuhuda huo mkubwa. Ni mimi na wewe baada ya kukutana na Yesu Kristo Mfufuka, katika Neno lake na meza yake ya Ekaristi tunaalikwa kurudi na kushirikisha wengine furaha ya Upendo wa Mungu kwa watu wake. Ni vile inakuwa ni habari ya kukeleketa hivi hatuwezi kubaki nayo sisi tu wenyewe bila ya kuwashirikisha wengine. Ni habari inayotushika na kutukamata, inayotuacha na mshangao chanya hivyo hatuna budi kutoka kwa haraka na kushirikisha wengine na hayo ndio maisha ya ushahidi. Kwetu Kristo ni Habari kwani amefufuka kweli kweli, ameyashinda mauti na hayupo tena kaburini.

Siku hizi za mitandao ya simu na hasa internet, mara nyingi tunasukumwa kuwashirikisha wengine habari kadha wa kadha iwe njema na hata mbaya, na hata zile ambazo kwa kweli ni kinyume na imani yetu, hivyo hatuna budi kutambua sisi tunaalikwa kila siku ya maisha yetu kuguswa na ukweli huu wa imani, na kerygma hii ya Ufufuko, na hivyo kutoka na kuwashirikisha wengine upendo! Ukweli wa ufufuko si ukweli mwingine bali ni juu ya upendo na huruma ya Mungu kwa ulimwengu mzima, ni ukweli ambao kila mmoja wetu anaalikwa kuuishi katika maisha yetu ya siku kwa siku. Pasaka ni kutoka kaburini, ni kutoka katika utamaduni wa kifo na kuanza kuishi maisha ya mwanga, maisha ya kweli, maisha katika upendo wa kweli kwa Mungu na kwa wengine. Pasaka ni sherehe ya amani kwani tumepatanishwa na Mungu, hivyo amani haina budi kutawala katika maisha ya kila mmoja, katika familia zetu na jumuiya zetu mbali mbali. Kila mmoja wetu anaalikwa kutoka kwa furaha na kuwa mjumbe wa kweli za Pasaka. Pasaka hii tujaribu kuwa wajumbe au malaika wa upendo wa Mungu kwa wengine na hasa maskini na wahitaji ambao wanatuzunguka katika mitaa yetu, familia zetu, jumuiya zetu, vigango na hata parokia zetu. Tumle Mwanakondoo wa Pasaka, yaani Yesu Kristo Mfufuka pamoja nao, kuwashirikisha furaha ya Pasaka sio tu kwa maneno bali zaidi sana kwa matendo yetu, kwa kuwaalika na kushiriki nao, kwa kula na kunywa pamoja nao kama hatua ya kwanza na ya msingi kabisa ya imani yetu katika Kristo Mfufuka.

Waamini wawe mashuhuda wa upendo katika Kristo Mfufuka.
Waamini wawe mashuhuda wa upendo katika Kristo Mfufuka.

 

Kristo hayupo tena kaburini, katika ubinafsi, tamaa ya mali na madaraka, chuki, uchoyo, masengenyo, ulafi, kufarakanisha wengine na hata kuwahukumu wengine, ulafi, uongo, uzinzi, uasherati, tamaa mbaya, ushirikina, na mengi mabaya tunayoweza kuyaorodhesha katika maisha yetu. Kristo Mfufuka tutakutana naye katika upendo kwa Mungu na kwa wenzetu tunaokutana nao siku kwa siku. Kristo mfufuka tunakutana naye katika wadogo, wanyonge, wahitaji, maskini, wanaohitaji kuonja upendo na huruma kutoka kwetu. Pasaka hii ni mwaliko kwetu kutafakari ni kwa namna gani tumekuwa kweli wajumbe wa upendo na amani kwa wote wanaotuzunguka na kukutana nao siku kwa siku. Je, uwepo wangu ni furaha kwa wengine, Je, mimi ni Habari njema kwa wengine ninaokutana nao ? Je, wanapokutana nami wanakutana na Habari Njema ya Yesu Kristo Mfufuka anayeleta amani na furaha ya kweli ? Nawatakia tafakari na sherehe njema za Pasaka ya Bwana.

16 April 2022, 17:06