Ufufuko Wa Kristo Yesu Kutoka Kwa Wafu Ni Ushuhuda Wa Imani
Na Padre Gaston George Mkude, Roma.
Ijumaa Kuu baadhi ya wanawake waliomfuata Yesu katika safari yake ile ya mateso kwa kusimama kwa mbali (Luka 23:49) na kushuhudia hatima pale juu msalabani; Jumamosi walipumzika kwani ni siku ya amri, hivyo walirejea mjini na kuandaa mafuta na manukato ili siku ya kwanza ya juma waweze kurudi kaburini na kuupaka mwili wake mafuta. (Luka 23:55-56). Ilikuwa ni desturi kuwa baada ya maziko wanawake walirudi kaburini; kwao waliamini kuwa kwa siku nne za mwanzo baada ya kifo, ile pumzi ya uhai ilikuwa ikizunguka karibu na mwili na hivyo ingeweza kurejea tena na kuupatia tena uhai. Kama ilivyotokea wakati wa manabii Eliya na Eliseo na hata Yesu aliwarejeshea uhai baadhi ya watu mfano mwana wa mjane wa Naini, mwana wa Yairo na rafiki yake Lazaro. Lakini hawa wote hata baada ya kurejeshewa uhai, mwisho wao wote ni umauti, hivyo hawakuwa na uzima usio na kifo. Ufufuko maana yake si kurejea katika uzima wa awali, yaani kuvaa tena mwili unaokufa, bali kuwa na maisha mapya na tofauti na ya awali. Ni maisha yasiyojua tena umauti. Labda kwa haraka haraka tunaweza kujiuliza kama wanawake walitegemea kukuta mwili wa Yesu ukiwa umerejea na uhai wa awali baada ya mateso na kifo cha kikatili kiasi kile kilichotokea mbele ya macho yao, kwa hakika hapana. Je, walitegemea ufufuko? Ni kweli Yesu aliwafundisha mara kadhaa juu ya ufufuko wake, ila tunaposoma Maandiko tunakuwa na hakika kuwa hakuna hata mmoja hata wale mitume wake waliolielewa fundisho hilo. Kwa kweli wazo la ufufuko halikuwepo kwa wale wanawake na hata kwa mitume wake Yesu.
Karne mbili kabla ya Kristo tunaona kati ya Wayahudi kutoka kitabu cha Nabii Danieli (12:2), tayari kuna wazo kuwa wataamka wale wote waliolala katika vumbi la ardhi. Lakini pia kufufuliwa kwao kulifikirika na kutegemewa kutajiri ile siku ya mwisho wa ulimwengu huu. Hivyo wanawake wanafika kaburini alfajiri mapema na kwa mshangao mkubwa mbele yao ni KABURI TUPU, kukuta jiwe limeondolewa kaburini, kwao wanabaki si tu na butwaa bali na uoga mkubwa. Hawaelewi maana ya jambo hilo, na hivyo wanawaza labda mwili wake umeibwa kutoka ndani kaburini. (Yohane 20:2). Mwinjili Luka anatualika kutafakari kwa msaada wa maneno anayotumia, anatumia neno kukuta mara mbili; Kwanza wanakuta jiwe limeondolewa na hawakuti mwili wa Yesu ndani yake. Kristo Mfufuka hawezi kukutwa kama tunavyoweza kukuta vitu vya ulimwengu huu na badala yake tunakutana naye kwa imani tu. Kristo mfufuka hana tena mwili unaoweza kufanyiwa tathmini kwa njia za Kisayansi katika maabara, na badala yake ni kwa njia ya kiroho na kiimani tunaweza kuufikia ukweli huo. Sio ukweli tunaoweza kuukuta kwa akili zetu kama walivyoweza kukuta jiwe pembeni, kaburi tupu na vitambaa na sanda. Hizi ni kweli zinazokuwa ndani ya uwezo wa njia zile za Kisayansi lakini ukweli wa ufufuko unapita kweli zote tunazoweza kuzithibitisha Kisayansi na akili zetu za kibinadamu.
Mashaka na hofu yao kama inavyoelezwa na Mwinjili Luka ni απορειν – aporein, ni neno la Kigiriki linalomaanisha mshangao wenye mashaka makubwa na ndio hata katika Kiingereza leo kuna neno euphoria ile hali mtu anakuwa nayo ya msisimko mkubwa wa kihisia ndani mwake na kujiona kama yupo ulimwengu mwingine. Katika Maandiko daima tunaona kuna safari ndefu kabla ya kuamini, kabla ya kujaliwa neema ile ya imani. Imani ni kukutana na Kristo Mfufuka! Wanawake wale wanajikutaka katika mashaka makubwa, na bila kujua wafanye nini katika hali hiyo. Wanaendelea kubaki katika mashaka yao kwani tunaona hata mitume hawakuwa tayari kupokea ushahidi wao. Ni katika nyakati za namna hiyo tunaona wanahitaji mwanga kutoka juu ili kuwaangazia juu ya ukweli wa tukio lile, na ndio wanatokewa na malaika wawili (Luka 24:23). Mwinjili Marko anazungumzia juu ya kijana, Mwinjili Matayo anazungumzia juu ya malaika wa Bwana akashuka kutoka mbinguni na Yohane Mwinjili anazungumzia juu ya malaika wawili. Malaika anawaalika KUKUMBUKA MANENO YAKE kabla ya kifo chake. Malaika ni msaada kutoka juu, ni uwepo wa Mungu mwenyewe, yaani kwa kutujalia neema zake, hata nasi tunaweza kuifikia imani kwa Kristo Mfufuka.
Kila Mwinjili anatumia lugha yake lakini ujumbe kusudiwa ni ule ule. Hapa Wainjili shabaha yao ni kutufikishia ukweli wa imani na sio masimulizi tu ya Kihistoria ingawa Ufufuko wa Bwana wetu Yesu ni ukweli pia wa Kihistoria. Ni Mungu mwenyewe katika hali ya mashaka makubwa kiasi kile anawapelekea mwanga ili wapate kung’amua juu ya tukio hilo, ili waweze kulitafsiri vema tukio hilo. Hata baada ya kutokewa na malaika, wanawake wale bado wanajawa na hofu, ila sasa ni hofu ya Mungu na hivyo kuinama vichwa vyao chini kama ambavyo tunajua katika Maandiko kila mwanadamu anapokutana na Mungu, hana budi kuupokea ufunuo wake kwa unyenyekevu mkubwa. Kwa nini mnamtafuta aliye hai kati ya wafu? Ni swali kutoka kwa malaika. Hayupo hapa amefufuka! Ni tangazo la imani kutoka pia kwa malaika. Ufufuko kama tulivyoona hapo juu si sawa na kurejeshewa tena uhai wa zamani, wa mwili unaokufa tena, na hivyo kuweza kuthibitishwa kwa njia za Kisayansi na kitabibu, bali ni kuwa na maisha ya umilele tofauti na haya ya ulimwengu huu. Hivyo, ufufuko sio jambo linalokuwa ndani ya uwezo wa Kisayansi, wala kugundulika na kufikiwa kwa akili zetu za kibinadamu, ni ukweli tunaoweza kuufikia kwa neema za Mungu pekee, ni ukweli wa imani, ni kerygma! Kristo amefufuka kwa kuwa Mungu Baba amemjalia maisha mapya, hivyo wanawake hawakupaswa kumtafuta Yesu kati ya wafu. Yeye yu hai na kwa kifo chake amewatoa wote katika utawala wa yule mwovu na kutukaribisha katika maisha mapya ya uhai wa milele na ndio urafiki na Mungu iwe tunaishi hapa duniani na hata baada ya maisha ya hapa duniani.
Hivyo baada ya siku ile Pasaka tunakuwa na hakika kuwa hatuwezi kuwatafuta wafu wetu makaburini kwani huko inabaki miili yao inayoharibika bali roho zao zipo mikononi mwa Kristo Mfufuka. Miili yao hakika itafufuliwa siku ile ya mwisho na kufanana na Mwili wa Kristo Mfufuka, kwani haitovaa tena kuharibika bali kutokuharibika. Mwaliko wa malaika kwa wanawake na hata kwetu ni kujua wapi tunaweza kukutana na Yesu Kristo Mfufuka na kumuona, ni katika Neno lake na katika Masakramenti yake. Ni katika Neno lake nasi tunaangaziwa na hata kumuona Yesu na sio kwa kurudi makaburini kama walivyofanya wanawake wale. Bila kuongozwa na Neno kamwe hata nasi leo tulio wafuasi na marafiki wa Yesu hatuwezi kuufikia ukweli juu ya ufufuko wake. Ufufuko kama nilivyotangulia kusema sio swala la Kisayansi hivyo kuingia maabara na kulithibitisha bali ni kwa njia ya Neno lake tunakuwa na imani hiyo. Kwenda maabara ili kukutana na ukweli wa Kristo Mfufuka ni kupotea njia, ni sawa na kurudi na kumtafuta makaburini. Mwinjili Luka anatuonesha nafasi muhimu ya wanawake katika ufuasi, kwani daima pamoja na mitume pia walifuatana na Yesu. (Luka 8:1-3) Ila katika siku ya Pasaka tunaona wanawake hawa wanafikia kilele cha utume wao. Ni wao wanakuwa wa kwanza kupokea ufunuo juu ya ufufuko kutoka mbinguni, wanakuwa wa kwanza kukumbuka Maandiko na hata kuwapelekea mitume na wafuasi wengine Habari Njema ya Ufufuko.
Kadiri ya tamaduni za Wayahudi, ushahidi wa mwanamke si kitu cha kutiliwa maanani, hivyo mara nyingi ulipuuzwa na ndio maana hata wasingeliweza kuitwa mahakamani ili kutoa ushahidi. Hivyo ni mwaliko kwa Mungu katika sikukuu za Pasaka kubadili vichwa na mitazamo yetu ya kijamii inayomuondolea mwanamke na mwanadamu mwingine yeyote yule hadhi yake. Kama asemavyo Mtume Paulo kuwa Mungu anachagua mambo yaliyodharauliwa katika ulimwengu huu ili kuwaadabisha wenye hekima. (1Wakorintho 1:27-28.) Mitume hata baada ya kupokea taarifa za ufufuko kutoka kwa wanawake tunaona nao pia hawaamini ujumbe huo na hata wanafadhaika. Hata kwa wale walioamini juu ya ufufuko bado walitarajia iwe ile siku ya parousia, ile siku ya hukumu ya mwisho na si kabla. Hata Paulo mtume alipokuwa mbele ya washitaki wake alipogusia juu ya ufufuko, tunaona Festo alimkaripia na kumuona kama amerukwa na akili. (Matendo 26:24) “Paulo, una wazimu, kusoma kwako kwingi kumekugeuza akili”. Ufufuko kama ulivyo msalaba wa Yesu Kristo ni makwazo na ujinga. Mtume Petro hakuamini na hivyo naye anaanza safari kama ile ya wanawake ya kwenda kaburini na pale anakuta vitambaa kaburini bila mwili wa Yesu. Ni vitambaa ndio kwani hivi kwa macho yetu ya kibinadamu tunaweza kuviona na hata kuthibitisha Kisayansi kama leo hii inavyozungumziwa ile sanda ya Torino (Sindone), lakini sio rahisi kwa ukweli kuhusu ufufuko.
Lakini kwake Petro ilikuwa ni hatua muhimu katika safari yake ya imani. Hatua nyingine muhimu kwake ni pale atakapotokewa na Yesu mfufuka na kumkumbusha maneno yote aliyosema kabla. (Luka 24: 44-47) Hivyo imani ni safari, ni kutoka katika mitazamo yetu na kweli zile za Kisayansi na kwa unyenyekevu kupokea kweli kutoka juu kwa msaada wa neema za Mungu mwenyewe ndani mwetu. Na ndio Mwinjili Luka anatuonesha ugumu wa kuamini kwa upande wa mitume hata baada ya wanawake kupokea ufunuo kutoka mbinguni. Hata hivyo safari yao ya imani ni ndefu na ngumu kama inavyokuwa mara nyingi hata kwetu leo. Yote katika yote tunaona Mwinjili Luka pale mwanzoni wakati wa masimulizi ya kuzaliwa kwake Yesu anatuonesha watu wa kwanza kupokea ujumbe walikuwa ni wachungaji, ni watu wa daraja la chini na najisi kadiri ya dini na mtazamo wa Kiyahudi, na hata leo pia wanawake ndio wanakuwa wa kwanza kupokea kutoka mbingu juu ya ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo, ndio kusema Mungu anatualika kubadili vichwa vyetu, mitazamo yetu na hasa kufuata mantiki mpya ya Mungu na si ya ulimwengu huu. Pasaka ni sherehe ya imani kuu, ni sherehe ya ushindi ya upendo wa Mungu kwa ulimwengu mzima. Ni upendo wa Mungu unaoshinda mateso yote na hata mauti; mateso na hata kifo hakina tena kauli ya mwisho kwani sisi sote tunatazama maisha kwa matumaini na furaha baada ya kukutana na Yesu Kristo Mfufuka! Nawatakia maadhimisho mema ya Fumbo la Ufufuko wake Bwana wetu Yesu Kristo!