Tafakari ya neno la Mungu, Sherehe ya Huruma ya Mungu: Zawadi kuu: Amani ili kuondoa hofu, Roho Mtakatifu kuwaondolea watu dhambi na Madonda Matakatifu kuzama katika kiri ya imani. Tafakari ya neno la Mungu, Sherehe ya Huruma ya Mungu: Zawadi kuu: Amani ili kuondoa hofu, Roho Mtakatifu kuwaondolea watu dhambi na Madonda Matakatifu kuzama katika kiri ya imani. 

Sherehe Ya Huruma Ya Mungu: Amani, Huruma Na Kiri Ya Imani

Sherehe ya Huruma ya Mungu inawakirimia waamini zawadi ya amani ili kuwaondolea hofu na mashaka, tayari kutangaza na kushuhudia Fumbo la Pasaka yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu. Kristo Mfufuka anawajalia watu wake Roho Mtakatifu kwa maondoleo ya dhambi na Toma Mtume anapata fursa ya kugusa Madonda Matakatifu ya Kristo Mfufuka na kukiri imani yake!

Na Padre Efrem Msigala, OSA, - Roma.

Liturujia ya Neno la Mungu, Sherehe ya Huruma ya Mungu: Masomo: Matendo 5:12-16, Ufu 1, 9-11.12-13.17-19 , Injili: Yoh 20, 19-31. Kwa mara nyingine tena karibu mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican na msomaji wa Vatican News katika tafakari ya masomo ya Dominika ya Pili ya Pasaka, Dominika ya Huruma ya Mungu. Dominika hii ni siku ya nane katika Octava ya Pasaka, hivyo tunahitisha siku za Octava na kuendelea na kipindi cha Pasaka hadi Sherehe ya Pentekoste. Somo la Kwanza. "Kundi zima la waamini lilikuwa na umoja, roho moja na moyo mmoja". Huu ni umoja wa jumuiya na ushirika. "Hakuna mtu alidai kwa matumizi yake mwenyewe chochote alichokuwa nacho, kwani kila kitu walichokuwa nacho kilikuwa cha pamoja." Hakuna uchoyo wa mtu binafsi na ushindani ambao unaashiria jamii zetu leo. Kwa sababu hiyo, “hakuna hata mmoja wa washiriki wao aliyekuwa na uhitaji” kwa sababu wale waliokuwa na mali waliitoa kwa jumuiya. "Kisha iligawiwa kwa wanajumuiya ambao walikuwa na uhitaji Injili inasema: Wanafunzi wako ndani ya nyumba, na milango imefungwa kabisa, kwa sababu wanaogopa kwamba, wakiwa wafuasi wa karibu wa Yesu, wao pia watastahili kukamatwa na kuadhibiwa. Maneno ya uhakikisho waliyokuwa wamepewa hapo awali yamesahaulika ya kuwa Yesu atafufuka siku ya tatu.

Zawadi ya Kristo Mfufuka kwa Mitume: Amani, Roho Mtakatifu na Madonda Matakatifu.
Zawadi ya Kristo Mfufuka kwa Mitume: Amani, Roho Mtakatifu na Madonda Matakatifu.

Ghafla, wanamwona Yesu amesimama katikati yao, ingawa hawatambui kuwa ni yeye mara moja. Ukweli kwamba anaweza kuwepo licha ya milango iliyofungwa inaonyesha kwamba yeye si sawa na hapo awali, kwamba yuko kwa njia mpya. Anawasalimu "Amani iwe kwenu!" ni salamu yake. Ni salamu ya kawaida ya Kiyahudi ya "Shalom".  Lakini pia ni salamu inayoashiria kuwapa moyo, kuwaondoa hofu, woga, wasiwasi na mahangaiko waliyonayo. Anawaonyesha mikono na ubavu wake. Yeye sio mzimu usio na mwili bali ni Yesu yule yule aliyekufa Msalabani. Licha ya kuonesha hayo yote bado anarudia salamu yake “amani iwe kwenu” (Yn. 20:21)  anaendelea kuwapa utume wao. "Kama vile Baba alivyonituma mimi, nami nawatuma ninyi." Kisha akawapulizia. Pumzi ya uhai akisema: "Pokea Roho Mtakatifu." (Yn.20:22. Baada ya hapo ana wapa utume wao: “Kwa wale ambao mnawasamehe dhambi zao, wamesamehewa; kwa wale ambao mnawafungia dhambi zao, zimefungiwa.” (Yn.20:23) mwanzo wa Sakramenti ya kitubio. Yesu anawapa mitume uwezo wa kuondoa dhambi kwa jina lake. Huruma ya Mungu kwa Mwanadamu. Kazi inayoendelezwa na mapadre na maaskofu. Huo ndio utume wao wa kimsingi, ambao juhudi yao yote ni kurudisha mahusiano sahihi kati ya Mungu na watu wake na kati ya watu wenyewe. Lengo kupatanisha. Ndiyo maana Sakramenti ya Kitubio huitwa pia sakramenti ya upatanisho.

Lakini pia walipendana wao kwa wao katika jumuiya zao na wakawa ni wajenzi na mawakala wa amani, upatanisho na haki, ambayo inafungamana na Injili na Somo la Kwanza. Pamoja hayo kuna wengine walionesha hali ya kutoamini kile walichoambiwa na wengine juu ya ufufuko wa Yesu walisahau yale waliyoambiwa kabla alipokuwa pamoja nao kabla ya kifo akisema kuhusu kufa na kufufuka kwake. Mfano ni - Tomaso. Alipoambiwa kwamba wenzake “wamemwona Bwana”, alisema hataamini hadi aone kwa macho yake alama za majeraha na kuweka mkono wake kwenye jeraha lililokuwa ubavuni mwa Yesu. Tomaso anawakilisha wengi hata nyakati za sasa. Hayo aliyohitaji Tomaso,  wiki moja baadaye –kama  leo, wakiwa pamoja na milango yote imefungwa kwa ghafula Yesu alikuwa katikati yao. Baada ya salamu ya kawaida ya amani iwe kwenu alimwita Tomaso mbele na kumwambia aingize vidole vyake katika kovu za misumari na aone mikono yake.  Tomaso alijibu “Bwana wangu na Mungu wangu” Bwana akamwambia “wewe kwa kuwa umeniona umesadiki wa heri wasio ona wakasadiki” ( Yn.20:28).

Waamini wanahimizwa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upatanisho.
Waamini wanahimizwa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upatanisho.

Mambo tunayopata katika masomo ya Sherehe ya Huruma ya Mungu ambayo ni fundisho kwetu ni kama ifuatavyo: 1. Aliye Hai humshangaza kila mtu: Ikiwa kuna jambo ambalo wanafunzi hawakutarajia, ni kwamba Yesu Kristo, akifufuka kutoka kwa wafu, angerudi kwenye uzima na kuonekana kwao bila kupoteza utambulisho wake na Msulubiwa. Ndiyo maana Tomaso alihitaji uthibitisho. Anawashangaza wanawake waliokwenda kaburini na kulikuta tupu, anawashangaza wanafunzi wawili wakielekea Emau, anawashangaza wanafunzi waliokusanyika kwenye nyumba, kama tulivyosikia wakifiri mzimu. Kwa nini wanashangaa, ikiwa waliamini katika ufufuo wa wafu? Na walielezwa mara nyingi. Kwa nini wanashangaa ikiwa walikuwa wamemwona Lazaro, ndugu ya Martha na Mariamu, akifufuliwa na Yesu? Kwa nini wanashangaa, wakati Yesu alikuwa amewatabiria mara kadhaa wakati wa huduma yake ya hadharani? Inawashangaza kwa sababu kile ambacho macho yao yanatafakari ni kitu ambacho hakijasikika. Wao, kama Wayahudi wazuri, walioelimishwa na waandishi na Mafarisayo, waliamini katika ufufuo wa wafu, lakini... si kwa wakati, bali mwisho wa nyakati. Inawashangaza kwa sababu ufufuo wa kihistoria wa Yesu ni kisa cha pekee na ni tofauti kabisa na ule wa Lazaro, binti ya Yairo au ule wa mwana wa mjane wa Naini. Yesu yu hai, lakini maisha yake si sawa kabisa na yetu, ni maisha tofauti, mapya na bora zaidi. Inawashangaza kwa sababu ni jambo moja kusikiliza, kuelewa, na jambo jingine kabisa kupata uzoefu: wanafunzi hawasikii kwamba Yesu atafufuka kutoka kwa wafu siku ya tatu, wanamwona na kumsikia amefufuka, wanamwona kama mshindi wa kifo, anayeishi milele.

Baada ya ufufuko Kristo Yesu aliwazawadia yafuatayo:  1) Anawapa amani, amani yake. Walimhitaji, kwa sababu walikuwa wakitetemeka kwa hofu. Walimhitaji, ili kunyamazisha akili na mioyo yao wakati wa sasa na wa wakati ujao. 2) Anawapa utume:: Kama vile Baba alivyonituma mimi, nami nawatuma ninyi. Kwa miaka mitatu wamekuwa wakishiriki utume wa Yesu na njia ya kuutekeleza. Sasa Yesu anawazindua ili kuendeleza kazi yake katika Uyahudi, katika Samaria na hata miisho ya ulimwengu. 3) Anawapa Roho Mtakatifu, ili waweze kutekeleza utume wao kwa ujasiri na uhuru wa ndani. Bila kutenganishwa na utume wa Yesu Kristo,. Atafanya kazi yao ya kitume kuwa na matunda. 4) Anawapa uwezo wake wa kusamehe dhambi. Kwa kuwa ni Mungu pekee anayeweza kusamehe dhambi, watazisamehe tu katika jina la Yesu Kristo na kwa uwezo wa nguvu za Mungu. Msamaha huu ni jambo ambalo kila mtu anahisi hitaji lake, kwa sababu akiwa mkweli atajikuta ana hatia. 5) Anawapa upendo wake wa kujishusha, kama ilivyotokea kwa Tomaso, ili kuimarisha imani yake: "Nyosha kidole chako na uangalie mikono yangu; unyooshe mkono wako na uutie ubavu wangu. Wala usiwe asiyeamini, bali mwenye kuamini 6) Anawapa uwezo wa kulijenga Kanisa kwa njia ya mahubiri na maombi, kwa kufanya ishara na maajabu mengi, hasa uponyaji katika jina la Yesu.

Dominika Huruma
21 April 2022, 11:33