Sherehe Ya Huruma Ya Mungu: Yesu Ni Ufunuo Wa Huruma ya Mungu
Na Padre William Bahitwa, - Vatican.
UTANGULIZI: Dominika inayofuata baada ya Sherehe ya Pasaka ni Dominika ambayo Kanisa huadhimisha Sherehe ya Huruma ya Mungu. Fumbo la huruma ya Mungu ni fumbo linalotambulisha namna Mungu anavyohusiana na mwanadamu anayesongwa na vikwazo vingi vya udhaifu wake. Bwana wetu Yesu Kristo tunayeendelea kusherehekea na kuadhimisha ufufuko wake ndiye uso wa huruma ya Baba na ndiye ambaye kwa Fumbo lake la Pasaka, yaani Mateso, Kifo na Ufufuko wake ameidhihirisha huruma kuu ya Mungu kwa kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti na kumwingiza katika nuru ya waana wa Mungu. Masomo kwa ufupi: Masomo ya Misa tunayokwenda kutatafakari, yanabeba taswira mbili zinazoadhimishwa katika dominika hii. Taswira ya kwanza ni ile ya fumbo la Pasaka, kuzidi kulifafanua kwetu fumbo hili na taswira ya pili ni ile ya fumbo la Huruma ya Mungu. Masomo yanafafanua fumbo la Pasaka kwa kutoa ushuhuda wa ufufuko wa Kristo. Na ushuhuda unaotolewa na masomo yote ya dominika hii ni kwamba Kristo kujidhihirisha, au kujionesha kwa kuwatokea wanafunzi wake. Somo la kwanza (Mdo. 5: 12-16) linaonesha ishara na miujiza mbalimbali ya uponyaji ambayo Mitume waliifanya. Somo pia linashuhudia kuongezeka kwa waamini wapya, wake kwa waume. Ni kwa namna hii somo hili linatoa ushuhuda kuwa ni Kristo mfufuka anayefanya kazi ndani ya Kanisa lake. Ni yeye anayewawezesha Mitume kufanya ishara na miujiza ya uponyaji na ni yeye anayewaangaza watu kwa nuru yake wamfungulie milango ya mioyo yao na wampokee kwa imani.
Katika somo la pili kutoka Kitabu cha Ufunuo wa Yohane (Ufu 1,9-11a, 12-13, 17-19), linaelezea mwanzo wa maono ya Yohane. Katika maono hayo, Yohane anashuhudia kuwa alitokewa na Kristo mfufuka. Anasema katika maono hayo Yesu mwenyewe alimwambia “Usiogope, mimi ni wa kwanza na wa mwisho, na aliye hai: nami nilikuwa nimekufa na tazama ni hai hata milele na milele.” Ni ushuhuda mwingine kuwa Yesu mfufuka amejidhihirisha mwenyewe kuwa amefufuka kwa kumtokea Yohane. Katika mwendelezo huu huu wa Yesu mfufuka kujidhihirisha, Injili (Yn 20:17-34) nayo inatupatia ushuhuda mwingine. Jioni ya siku ile ile ya ufufuko, siku ya kwanza ya Juma, Yesu anawatokea wanafunzi wake wakiwa wamejifungia ndani kwa hofu ya wayahudi. Anasimama mbele yao na kuwaambia “Amani iwe kwenu”. Baada ya siku nane anarudia tena kuwatokea ili kuimarisha imani ya Tomaso ambaye hakuwepo Yesu alipowatokea mara ya kwanza na hivi akasema “nisipomwona sisadiki”. Na hapa, pamoja na kuwa Yesu anawatokea wanafunzi mara ya pili ili kuimarisha imani ya Tomaso, tunaona lakini msisitizo ambao mwinjili Yohane anauweka katika jambo hili.
Yesu anawatokea mara mbili kuendelea kudhihirisha kuwa kweli ni yeye, aliyekuwa amekufa na sasa yu hai. Taswira ya pili ambayo pia inadokezwa katika masomo ya leo ni ile ya Huruma ya Mungu. Hii tunaiona katika somo la Injili ambapo Yesu anaweka sakramenti ya kitubio ambayo ni sakramenti ya Huruma. Sakramenti hii Yesu anaiweka anapowatokea mitume na kuwapa uwezo wa kuondolea na kufungia dhambi. Anasema “wowote mtakaowaondolea dhambi wameondolewa na wowote mtakaowafungia dhambi wamefungiwa.” Mungu kumpa mwanadamu uwezo kuondolea dhambi kwa jina lake ni ishara kubwa sana ya huruma yake hasa ukizingatia kuwa mojawapo ya sababu za Yesu kuambiwa amekufuru ni pale aliposema kuwa anao uwezo wa kusamehe dhambi. Tendo hili ambalo kimsingi ni la kimungu, Mungu mwenyewe amelishusha na kulikabidhi Kanisa kama kushuka Yeye mwenyewe kati ya wanadamu na kuwa Huruma iliyojimwilisha kati yao.
TAFAKARI: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, Fumbo la Pasaka yaani Mateso, Kifo na ufufuko wa Kristo ni fumbo linalodhihirisha Huruma ya Mungu kwa maana ni katikati ya Fumbo la Pasaka, pale Msalabani, ndipo palipotoka chemchemi ya Huruma kuu ya Mungu kwa mwanadamu. Na kimsingi, ni katika siku ambapo Kanisa linaadhimisha kifo cha Kristo Msalabani, siku ya Ijumaa Kuu ilipo mizizi ya Huruma ya Mungu na ni siku ambapo novena ya Sherehe ya Huruma ya Mungu huanza. Ni Kristo mwenyewe aliyeagiza kuadhimishwa hivi kwa sherehe hi ya Huruma ya Mungu pale alipomtokea Mtakatifu Faustina na kumwambia; “Dominika inayofuatia dominika ya Pasaka ninataka iadhimishwe Sherehe ya Huruma ya Mungu.” Na akaongeza “Mwanangu, utangazie ulimwengu wote juu ya Huruma yangu isiyo na kikomo. Katika siku hiyo nitafungulia milango yote ya Huruma yangu na roho itakayopokea Maungamo na Ekaristi Takatifu siku hiyo itapata maondoleo ya dhambi pamoja na adhabu zake zote.”
Baba Mtakatifu Francisko anafundisha kuwa “huruma ndilo jina lingine la Mungu”. Hii ni kweli kwa sababu historia nzima ya wokovu wa mwanadamu, ni historia inayomfunua Mungu kuwa ni Bwana aliyejaa Huruma na neema (Rej Zab 103:8). Tunaweza kusema pia kuwa kama jinsi ambavyo mitume walikuwa wamejifungia ndani kwa hofu, ndivyo pia mwanadamu katika mwendo wa maisha amejikuta amejifungia ndani yeye mwenyewe kwa sababu ya udhaifu wake wa kibinadamu na kupoteza kabisa tumaini la kuinuka na kuanza upya safari ya kuishi kitakatifu. Sherehe ya Huruma ya Mungu inamkumbusha mwanadamu aliyejikatia tamaa katika udhaifu wake, mahangaiko ya Yesu kama alivyojifunua kwa Mtakatifu Faustina, “kwa nini watu wangu wanapotea wakati huruma yangu ipo”? Ni sherehe inayotualika basi kutambua kuwa huruma ya Mungu ni kubwa kuliko udhaifu wa mwanadamu. Na yeyote anayeikimbilia kwa toba ya kweli na moyo wa kujibandua kutoa maisha ya dhambi, ataikuta wazi daima milango ya Huruma na ataikuwa wazi kama mikono ya Baba mwenye Huruma tayari kumpokea na kumkaribisha ndani kama katika mfano wa Mwana Mpotevu (Lk. 15). Adhimisho la sherehe hii huruma ya Mungu liwe kwetu kichocheo cha kukuza imani na kutufanya wenyewe kuwa vyombo vya Huruma ya Mungu kati ya wenzetu.