Katika maadhimisho ya Jubilei Kuu ya Miaka 2000 ya Ukristo, Dominika ya Pili ya Pasaka ilipewa jina la “Dominika ya Huruma ya Mungu.” Katika maadhimisho ya Jubilei Kuu ya Miaka 2000 ya Ukristo, Dominika ya Pili ya Pasaka ilipewa jina la “Dominika ya Huruma ya Mungu.”  

Sherehe Ya Huruma ya Mungu: Ushiriki, Matumaini Na Utume

Masomo ya Sherehe ya Huruma ya Mungu, Mwaka C wa Kanisa yanatufahamisha jinsi nguvu ya imani ilivyojidhihirisha katika jumuiya ya kwanza ya wakristo, kiri kuu ya imani ya Mtume Thomaso kuwa Yesu ni mtu kweli na Mungu kweli, kuwekwa kwa Sakramenti ya kitubio, vyanzo vya mafundisho ya Kanisa na njia zinazodhihirisha uwepo wa Kristo katika maisha yetu ya kila siku. Huruma!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, dominika ya 2 ya Pasaka. Katika maadhimisho ya Jubilei Kuu ya Miaka 2000 ya Ukristo, dominika ya Pili ya Pasaka ilipewa jina la “Dominika ya huruma ya Mungu.” Mtakatifu Faustina ndiye aliyeaminishwa kuidhihirisha huruma ya Mungu kwa maono aliyoyaona ya miali ya mwanga ya rangi nyekundu ikiwakilisha damu ya Kristo na rangi ya bluu hafifu ikiwakilisha maji ya Ubatizo. Masomo ya dominika hii yanatufahamisha jinsi nguvu ya imani ilivyojidhihirisha katika jumuiya ya kwanza ya wakristo, kiri kuu ya imani ya Mtume Thomaso kuwa Yesu ni mtu kweli na Mungu kweli, kuwekwa kwa Sakramenti ya Kitubio, vyanzo vya mafundisho ya Kanisa na njia zinazodhihirisha uwepo wa Kristo katika maisha yetu ya kila siku. Somo la kwanza kutoka Matendo ya Mitume (Mdo 5:12-16); linasimulia jinsi Kristo mfufuka alivyojidhihisha kwa ishara na maajabu aliyoyafanya kwa mikono ya Mitume (Mdo 5:12). Ni kwa nguvu ya Roho Mtakatifu Kanisa la kwanza lilianza kukua na kustawi na ni kwa nguvu hiyo hiyo wakristo wa kwanza walionyesha moyo wa mapendo na ushirikiano hata watu waliwatukuza wakawa mfano wa kuigwa katika maisha ya kijumuiya. Imani yao iliwawezesha kumwona Kristo Mfufuka hata katika vivuli vya mitume (Mdo 5:15), ndiyo maana waliwaweka wagonjwa njiani ili kivuli cha mitume kikiwapitia waweze kupona.

Sherehe ya Huruma ya Mungu: Sakramenti, Toba Na Ushuhuda
Sherehe ya Huruma ya Mungu: Sakramenti, Toba Na Ushuhuda

Hii ni imani kubwa mno, imani isiyo na shaka kuwa Kristo Yesu baada ya kufufuka ameendelea kuwepo katika maisha yetu kwa njia ya Mitume na katika nyakati zetu anaendelea kufanya kazi ya ukombozi katika nafsi ya mapadre. Imani tu yaelewa mambo haya. Waamini wenye imani juu ya uwepo wa Kristo katika nafsi ya Padre na kuwa ndiye anayeadhimisha Sakramenti katika nafsi ya Padre kama alivyofanya kwa Mitume ndio wanaonufaika na kupata baraka zake. Somo hili linatufundisha kuwa Kristo mfufuka anaendelea kuwepo katika kila Jumuiya ya Kikristo kama alivyokuwa katikati ya Jumuiya ya Waumini na wafuasi wa Kanisa la kwanza waliokusanyika kuwazunguka Mitume huko Yerusalemu. Kristo yuko akitenda kazi katika jumuiya zetu za Kikristo kila wakati. Hivyo hatuna sababu ya kuogopa au kuwa na wasiwasi kwani Kristo yuko katikati yetu akitenda kazi. 

Somo la pili la Kitabu cha Ufunuo (Uf 1:9-13,17-19); linasimulia maono ya Mtume Yohane akiwa uhamishoni katika kisiwa cha Patmo siku ya Bwana yaani Jumapili, ndiyo Dominika, siku ya ufufuko (Ufu 1:13). Yesu anajifunua kwa Yohane akisema, Usiogope, Mimi ni wa kwanza na wa mwisho na aliye hai; nami nalikuwa nimekufa, na tazama, ni hai hata milele na milele. Nami ninazo funguo za mauti, na za kuzimu. Yesu anajidhihirisha kuwa ni Kuhani kwa ishara ya kanzu aliyovaa, Mfalme kwa mshipi wa dhahabu aliojifunga na hakimu kwa ishara ya vinara 7 vya moto. Kristo ni kweli Kuhani, mfalme na hakimu mwenye haki. Ufunuo huu wa Yohane ni wa kuwaimarisha wakristo waliokuwa wanateswa na utawala wa warumi na kutokana na mafundisho ya walimu wa uongo. Yohani, alipata ufunuo huu kutoka kwa Yesu mwenyewe mfufuka akimwamuru aandike kitabu hiki cha ufunuo, ili kuwapa matumaini mapya na kuwatia moyo waamini ili waweze kuvumilia mateso kwa ajili ya imani yao kwa Kristo. Kumbe mapambano katika maisha ya Imani ni muhimu hatupaswi kukata tamaa kwani Kristo yuko pamoja nasi akitutegemeza.

Ushuhuda wa Kanisa la Mwanzo katika maisha na utume wa Kanisa
Ushuhuda wa Kanisa la Mwanzo katika maisha na utume wa Kanisa

Injili ilivyoandikwa na Yohane (Yn 20:19-31) tunayoisoma katika dominika ya pili ya Pasaka imegawanyika sehemu kuu tatu: Sehemu ya kwanza (20:19-25) - Yesu mfufuka anawatokea wanafunzi wake wakati Thomasi hayupo na kuweka sakramenti ya kitubio; sehemu ya pili (20:26-29) – Yesu Mfufuka anawatokea wanafunzi wake na Thomasi akiwepo; na sehemu ya mwisho ni 20:30-31 inayodokeza vyanzo vingine vya mafundisho ya Kanisa nje na Maandiko Matakatifu – Biblia. Yesu Mfufuka ni mjumbe wa Amani ndiyo maana maneno yake ya kwanza kila alipowatokea wanafunzi wake ni “Amani iwe kwenu”. Kisha kuwasilimu anawatuma kwa kuwaambia; “Kama Baba alivyonituma mimi, mimi nami nawapeleka ninyi”. Mwinjili Mathayo anasema; “Enendeni ulimwenguni mwote mkayafanye mataifa yote kuwa wanafunzi wangu mkiwabatiza kwa jina la Baba na la mwana na la Roho Mtakatifu” (Mt. 28:18-20). Marko anasisitiza; “Fundisheni kuyashika yote niliyowaamuru ninyi aaminiye na kubatizwa ataokolewa, asiyeamini atahukumiwa” (Mk. 16:15-16). Yohane anaendelea kusisitiza; “Naye akiisha kusema hayo, akawavuvia, akawaambia, Pokeeni Roho Mtakatifu. Wowote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wowote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa” (Yn.20:22-23). Huu ni udhibitisho wa kuwekwa kwa Sakramenti ya Upatanisho, Sakramenti ya Kitubio au ondoleo la dhambi na mamlaka waliyopewa mitume ya kuotuondolea dhambi nao wakawaridhisha mapadre. Hivyo hatuna shaka juu ya mamlaka haya. Mwenye mashaka na asiyeamini atahukumiwa, bali aaminiye ataokolewa.

“Bwana wangu na Mungu wangu” (Yn. 20:28) ni Kiri Kuu Imani ya Mtume Thomasi aitwaye pacha kuwa Kristo mfufuka ni mtu kweli na ni Mungu kweli. Thomasi mwanzoni aliyeshindwa kuamini kuwa Kristo amefufuka na amewatokea wenzake akisema; “Mimi nisipoziona mikononi mwake kovu za misumari, na kutia kidole changu katika mahali pa misumari, na kutia mkono wangu katika ubavu wake, mimi sisadiki hata kidogo” (Yn.20:25). Yesu alipowatokea mara ya pili naye akiwapo alimwambia; “Thomasi, Lete hapa kidole chako, uitazama mikono yangu; ulete na mkono wako uutie ubavuni mwangu; wala usiwe asiyeamini, bali aaminiye” (Yn. 20:27). Thomasi akajibu, akamwambia; “Bwana wangu na Mungu wangu”! Yesu akamwambia, “Wewe, kwa kuwa umeniona, umesadiki; wa heri wale wasioona, wakasadiki” (Yn. 20:29). Kumbe tunaona kuwa Imani haipatikani katika kile mtu anachoona kwa macho. Mtu hawezi kuthibitisha yale tunayoaamini kwa kutuletea vithibitisho vya kisayansi. Mtu anayetaka kuona kugusa, kuonja na kuhisi hawezi kuwa mtu wa imani. Yesu anasema, wamebarikiwa wale wasioona lakini wakaamini kwa sababu imani yao ni ya kweli, safi – isiyo na mashaka, tena ni ya kudumu.

Katika sehemu ya kwanza na ya pili katika Injili ya Dominika hii ya Huruma ya Mungu na katika somo la kwanza linalohusu jumuiya ya kwanza ya Wakristo tunaona kuwa ni katika jumuiya tunakutana na Yesu mfufuka. Thomasi alipokuwa nje ya jumuiya hakumwona Yesu, na aliporudi ndani ya jumuiya akamuona na kukiri wazi “Bwana wangu na Mungu wangu” na ni katika jumuiya ya waamini wa Kanisa la kwanza nguvu za Yesu mfufuka zilijidhihirisha kwa njia ya mitume. Ni katika maadhimisho ya kilitrujia ndipo tunapokutana na Yesu kwa njia ya sakramenti na neno la Mungu. Sakramenti na Neno la Mungu ni mali ya Kanisa – mwili wa Kristo. Hivyo tunalihitaji Kanisa ili tukutane na Yesu. Paulo anauliza: “Wataliitiaje jina lake yeye ambaye hawamwamini? Na watamwaminije yeye ambaye hawajawahi kumsikia? Na watasikiaje kama hakuna mhubiri?” (Rom 10:14).

Roho Mtakatifu katika maisha na utume wa Kanisa
Roho Mtakatifu katika maisha na utume wa Kanisa

Tunahitaji jumuiya ili kusikiliza mahubiri na mafundisho ya imani. Katika jumuiya tunaombeana, tunapata mifano kutoka kwa wengine jinsi ya kuishi imani yetu katika matendo, tunapata faida ya kuonywa na kurekebisha pale tunapokuwa tumekosea. Katika jumuiya tunapata nafasi ya kupendwa na kupenda. Tunakutana na upendo wa Mungu kwa kupitia wenzetu na sisi wenyewe tunakuwa vyombo ambavyo Mungu anapitishia upendo wake uwafikie wengine. Ni katika jumuiya Kristo anakutana nasi. Jumuiya ya Wakristo wa Kwanza ni mfano wa kuigwa kwa jumuiya zetu. Wajibu wetu ni kuzifanya jumuiya zetu ziwe kweli ishara ya uwepo wa Kristo ulimwenguni. Watu wamtambue Kristo katika jumuiya zetu. Kama kuna shida yoyote katika jumuiya suluhisho si kujitenga na jumuiya bali ni kutatua matatizo hayo. Je, upo ndani ya jumuiya? Kama haupo ingia sasa, jiunge na jumuiya, jiunge na vyama vya kitume, shiriki katika shughuli za Kanisa ili ukutane na Yesu Mfufuka upate neema na baraka tele.

Sehemu ya mwisho ya Injili ya dominika hii (Yn. 20:30-31) inatujulisha kuwa kuna vyanzo vingine vya mafundisho ya Kanisa. Kanisa Katoliki lina vyanzo vikuu vinne vya mafundisho yake ambavyo ni Bibilia Takatifu, Mapokeo kutoka kwa Mitume, Mababa wa imani na Mitaguso ya Kanisa. Bibilia sio chanzo pekee cha mafundisho ya Kanisa maana sio yote aliyoyafanya Kristo yameandikwa katika Biblia – “Basi kuna ishara nyingine nyingi alizozifanya Yesu mbele ya wanafunzi wake, zisizoandikwa katika kitabu hiki. Lakini hizi zimeandikwa; ili mpate kuamini ya kwamba Yesu ndiye Kristo, Mwana wa Mungu; na kwa kuamini mwe na uzima kwa jina lake” (Yn. 20:30-31). Habari ambazo Yohane anasema hazijaandikwa katika Bibilia ni mafundisho mengine ya Kanisa ambayo tunayapata katika mapokeo kutoka kwa mitume, mababa wa Imani na mitakuso ya Kanisa. Hivyo hatupaswi kuwa na mashaka juu ya mafundisho msingi ya Kanisa ambayo hayajaandikwa katika Bibilia Takatifu kwani hayo tunayapata katika vyanzo hivyo vingine.

Yesu mfufuka sasa anaishi nasi katika maisha yetu kwa namna ambayo mifumo yetu ya fahamu haiwezi kudhihirisha. Namna ambayo haiwezi kuguswa kwa mikono au kuonekana kwa macho yetu ya kawaida. Imani pekee ndiyo yaweza kuelewa mambo haya, haonekani kwa macho lakini nguvu na neema zake bado zipo nasi daima (Mdo 1:8). Sisi tunakutana na Yesu katika sakramenti, katika Neno lake na katika makasisi wake, katika wahitaji na wenye shida kama vile maskini, wenye njaa, wanye kiu, wafungwa, walio uchi na wagonjwa kwani yeye mwenyewe anasema lolote mliowatendea miongoni mwa wadogo hawa mlinitendea mimi. Tuombe neema na Baraka za Mungu ili tuweze kweli kumtambua Kristo Mfufuka katika maisha yetu ili tupate Amani tele. Tumsifu Yesu Kristo.

Huruma na Ushuhuda
21 April 2022, 15:31