Tafuta

Shuhuda za maandishi ya kale nje ya Biblia juu ya maisha, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu. Shuhuda za maandishi ya kale nje ya Biblia juu ya maisha, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu. 

Shuhuda Za Kale Kuhusu Mateso, Kifo Na Ufufuko Wa Kristo Yesu.

Mara nyingi katika ulimwengu mamboleo kuna kelele nyingi kutoka upande wa pili wakitushutumu kwa yale tunayoyahadhimisha kuwa siyo kweli. Bila shaka katika akili zao wanatudharau sana na wanatuona kama mazuzu yasiyojua nini yanafanya. Huwa najiuliza ni Wakristo wangapi wameyumbishwa kwa kelele zao na kupoteza ladha na maana nzima ya kuadhimisha mafumbo haya!

Na Padre Cletus C. Mzeru, - Roma.

UTANGULIZI: Sherehe ya Pasaka ni kipindi cha kuhadhimisha mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo, huwa kunakuwa na kelele nyingi kutoka upande wa pili wakitushutumu kwa yale tunayoyahadhimisha kuwa siyo kweli. Bila shaka katika akili zao wanatudharau sana na wanatuona kama mazuzu yasiyojua nini yanafanya. Huwa najiuliza ni Wakristo wangapi wameyumbishwa kwa kelele zao na kupoteza ladha na maana nzima ya kuadhimisha mafumbo haya! Hivyo kama mchango wangu katika Pasaka ya mwaka huu 2022 nimefanya utafiti wa kina wa maandishi ya kale mbali na Biblia yaliyoongelea juu ya maisha, kifo na ufufuko wa Kristo. Kwa nini maandishi ya kale nje ya Biblia? Hii ni kwa sababu katika Biblia suala la mateso, kifo na ufufuko wa Kristo lipo wazi na halina shaka yoyote. Natumia vyanzo vingine vya kihistoria ili kutanua wigo wa ushawishi hata kwa wale wanaojitambulisha kuwa hawana dini, au hawaviamini Vitabu Vitakatifu vya Dini. Lengo la andiko hili hasa ni kuimarisha imani ya ndugu zangu katika Kristo Yesu, ili kuweza kushiriki kikamilifu katika Liturujia na maadhimisho mbalimbali la Kiturujia kwa ibada na uchaji wa Mungu unaostahili mafumbo haya muhimu ya imani yetu.

MWANZO WA TATIZO Nimejiridhisha kuwa hakuna andiko lolote nje ya dini kuu duniani linaloweza kuthibitisha kuwa Kristo Yesu hakusulibiwa. Ni wazi sasa kuwa matatizo yote juu ya fundisho la kupinga mateso, kifo na ufufuko wa Kristo ni ubunifu kamili uliomo kwenye baadhi ya Vitabu vitakatifu vya baadhi ya dini ulimwenguni. Mwanafalsafa nguli wa kiyunani, Aristoto (384-322 K.K) ametufundisha katika kitabu chake cha Metafizikia juu ya “Kanuni ya kutokuwepo ukinzani” (The Principle of non - contradiction). (Cf., Aristoto, Metafizikia, IV, 4, 1005b 35 – 1006a 4). Kiufupi Aristoto anatufundisha kuwa haiwezekani kwa kitu kuwa na kutokuwa kwa wakati mmoja. Sasa hili la kusulibiwa kwa Kristo Yesu limekaaje? Fundisho la kupinga kifo na ufufuko wa Kristo limeleta madhara makubwa katika kubomboa imani za watu. Watu walienda mbali zaidi si tu kupinga kifo na ufufuko wa Kristo bali walifikia hata kujaribu kuhoji kuwa yawezekana Yesu mwenyewe hajawahi kuishi ulimwenguni bali ni masimulizi ya kubuni tu. Hapana, lazima kulitafutia ufumbuzi.

Kristo Yesu aliteswa, akafa na kufufuka kwa wafu
Kristo Yesu aliteswa, akafa na kufufuka kwa wafu

Mtakatifu Thomasi wa Akwino (c. 1225 – 1274 B.K) ametufundisha njia bora ya kutatua matatizo kama haya. Katika mwanga wa Mithali 8:7, Mt. Thomasi anatufundisha juu ya kazi ya mtu mwenye hekima. Anatufundisha kuwa kazi mbili za mtu mwenye hekima ni kuuelewa ukweli na kukataa makosa. (Cf., Thomasi wa Akwino, Summa Contra Gentiles (SCG), I. c.1). Katika kuuelewa ukweli Mt. Thomaso anatupatia njia kuu mbili: Kwanza ukweli tunaoupata kutumia uwezo wa akili zetu wenyewe na ukweli unaopita uwezo wa akili zetu wenyewe. (Cf., SCG, I.3). Katika kukataa makosa tunaweza tumia njia ya akili zetu wenyewe ili kukataa makosa hata ya wale wasioamini vitabu vyetu. Utumiaji wa akili zetu wenyewe ndiko kunatupeleka katika ulimwengu wa Falsafa. Hivyo basi, katika mwanga wa somo la Falsafa ya Historia kama moja wapo la somo katika kitivo cha Filosofia tutapitia baadhi ya maandiko ya kale ili kutatua changamoto hii. Katika maandiko hayo kutajikita kuangalia maisha, kifo na ufufuko wa Kristo.

MAISHA Ni dhaili kuwa Kristo aliishi duniani. Kuna ushahidi wa kutosha wa maandishi ya kale yanayodhihilisha kuishi kwake duniani. Hapa tuwaangalie walau wanahistoria wawili.  Flavius Josephus (27 – C. 100 B.K) Huyu alikuwa mwanahistoria wa kiyahudi. Alizaliwa katika ukoo wa kikuhani, mwana wa kuhani. Jina lake la kiyahudi ni Joseph ben Matthias (Yosefu, mwana wa Mathiasi). Alipofikisha umri wa miaka kumi na tisa alijiunga rasmi na Mafarisayo. Alipata elimu bora na alikuwa akiheshimika sana miongoni mwa wayahudi. Baada ya uvamizi wa Warumi na kuharibiwa kwa jiji la Jerusalemu mwaka 70 B.K alihamia Roma ambapo alifanya kazi kama mhistoria wa ikulu ya utawala wa Kaisari aitwaye Vespasian. Hapa alipewa hadhi ya uraia wa kirumi na haki zake, na kupewa jina la kifamilia toka familia ya kaisari, Flavius. Josephus alifanikiwa kuandika historia ya wayahudi kuanzia utawala wa Antiokusi Epifanesi (17 – 63 K.K) mpaka kuanguka kwa Masada 73 B.K wakati wa mapambano ya Wayahudi na Warumi.

Katika maandishi yake tunapata habari juu ya Yesu Kristo wa historia. Katika kitabu chake, The Antiquities of the Jews kinachosadikiwa kuandikwa kati ya mwaka 90 -95 B.K anamtaja na kumtambua Yesu kama mtu aliyeishi katika historia ya wayahudi. Kwanza anamtaja Yesu kama mtu mwenye busara, mtenda miujiza na mwalimu aliyewavuta kwake wayahudi kwa wayunani. Huyu anamtambua Yesu kuwa ni Kristo. (cf., Josephus, Antiquities, 18.3.3). Vilevile katika kitabu hikohiko Yesu anahusishwa na Mtume Yakobo (Yakobo Mdogo) ambaye anatajwa kuwa ndugu wa Yesu, aliyepelekwa pamoja na wenzake katika Baraza la Kiyahudi (Sanhedrin) kuhukumiwa. (cf., Josephus, Antiquities, 20.9.1).

Biblia Inashuhudi kuhusu mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu.
Biblia Inashuhudi kuhusu mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu.

Gaius Suetonius Tranquillus (c. 69 – c. 122 B.K) Huyu alikuwa mwanahistoria wa kirumi. Alifahamika zaidi kwa jina la Suetonius. Rafiki yake, Plini Mdogo (Pliny the Younger) anamuelezea kama mtu mpole, msomi na mpenda kuandika. Suetonius alikuwa Katibu Kiongozi wa mtawala wa kirumi Hadrian (117 -138 B.K) kabla ya baadaye 121 B.K kutimuliwa kwa kuhisiwa kuwa na ukaribu na mke wa mtawala huyo, aitwaye Sabina. Suetonius anafahamika zaidi kwa kitabu chake cha De vita Caesarum, kinachozungumzia maisha ya watawala kumi na wawili wa kirumi (The Twelve Caesars) kuanzia Kaisari Juliasi mpaka Kaisari Domisiani. Kitabu hiki kilikuwa na umuhimu mkubwa kiasi kwamba kilikuwa miongoni mwa vitabu vya mwanzomwanzo kuchapwa kwa wingi baada ya ugunduzi wa mashine ya uchapishaji mwaka 1500 B.K. Hii ilipelekea kitabu hiki kufahamika sana na kutafsiriwa katika lugha nyingi za bara la ulaya. Katika maandishi yake kumuhusu mtawala Klaudio (41 – 51 B.K), anazungumzia tukio la wayahudi waliofukuzwa jijini Roma mwaka 49 B.K wakihusishwa na vurugu za kidini zilizomhusisha mtu aitwaye Kristo. (Cf., Suetonius, Claudius, 25). Tukio hili la kihistoria linasimuliwa pia katika kitabu cha Matendo ya Mitume.  (Cf., Mdo 18:2). Vurugu hizi zilihusu maelewano mabaya baina ya wahahudi walioshikilia dini yao na wayahudi waliojiunga na uKristo. Kwa ushahidi huu wa wanahistoria wawili wa kiyahudi na kirumi itoshe kuthibitisha kuwa Bwana wetu Yesu Kristo aliishi kweli na anafahamika katika vitabu vya historia ya wakati wake na wala siyo mhusika wa kubuni na masimulizi yanayomhusu wala siyo kisasili.

KIFO: Upo pia ushuhuda wa kutosha wa maandiko ya kale juu ya namna kifo cha Yesu Kristo kilivyotokea. Hila kwa hapa tutaangalia maandishi ya mashahidi wawili tu ambao shuhuda zao hazina shaka yoyote ya uhalali wake. Cornelius Tacitus (c. 56 – 120 B.K) Huyu alikuwa mwanahistoria na mwanasiasa katika utawala wa kirumi. Alishika pia nyadhifa mbalimbali za utendaji katika serikali ya Rumi na makoloni yake. Wasomi wanamheshimu Tacitus kama mmoja wa wahistoria wakubwa wa Roma ya Kale. Umaarufu wake kama mhistoria mkubwa unajionesha zaidi katika vitabu vyake vikuu viwili vya historia, The Annals na The Histories. Vitabu hivi wiwili kwa pamoja vinazungumzia historia ya warumi kuanzia kifo cha Kaisari Augusto 14 B.K mpaka utawala wa Kaisari Domisiani 96 B.K. Katika kitabu chake cha mwisho kuandika, The Annals, kinachosadikiwa kuchapishwa mwaka 118 B.K, miaka michache kabla ya kifo chake, Tacitus anaelezea juu ya moto mkubwa uliozuka katika jiji la Roma wakati wa utawala wa Nero (54 – 68 B.K). Ni katika habari hii ndiyo anasimulia kuwa (1). Mtawala Nero aliwashutumu Wakristo, waliokuwa wakichukiwa kwa ibada zao, kuwa ndiyo chanzo cha moto huo. (2). Wakristo hawa walipata jina lao toka kwa Kristo aliyehukumiwa kifo kwa amri ya Ponsio Pilato aliyekuwa liwali (Praefectus) wa Yudea (27 – 37 B.K). (3). Pia ulikuwa ni wakati wa utawala wa Kaisari Tiberio (14 – 37 B.K). (Cf., Tacitus, Annals, 15. 44.3).  

Talmud: Historia ya Wayahudi ni ndefu sana iliyopitia milima na mabonde. Kuishi utumwani, kupelekwa uhamishoni na hata kuharibiwa kwa hekalu ni baadhi ya magumu waliyopitia yaliyoweza kusababisha kupoteza baadhi ya kumbukumbu zao muhimu kuhusu dini yao. Si ajabu tunasoma katika maandiko matakatifu mara kadhaa wakishutumiwa na manabii kwa kuacha misingi ya dini yao na kukumbatia ya kigeni. Hivyo kupitia shule zilizosimamiwa na “Marrebi” waliona umuhimu wa kutunza kumbukumbu zao. Kwanza waliamua kuziweka katika maandishi tamaduni zao ambazo walikuwa wakirithishana kwa njia ya mdomo toka kizazi kimoja kwenda kingine. Uratibu wa kazi hii ulifanywa vizuri ukiongozwa na Rebbi Aqiba ambaye aliyaweka maandishi hayo kulingana na mada. Alifanya kazi nzuri kabla ya kifo chake mwaka 135. Wanafunzi wake walihariri na kuboresha kazi hiyo iliyokamilika rasmi kati ya mwaka 200 B.K. Kitabu hiko kikaitwa Mishnah. Tahakiki na fafanuzi mbalimbali zilitolewa na wasomi wa kiyahudi kuhusu kitabu hicho. Nazo zikakusanywa katika kitabu kimoja kilichohitwa Gemara, ambacho kilikamilika kati ya mwaka 500 B.K. Vitabu hivi viwili viliunganishwa pamoja na kufanya kitabu kinachojulikana kwa jina la Talmud (maana yake Fundisho). Kitabu hiki sasa ndicho kinachobeba misingi ya utamaduni na maisha ya kila siku ya myahudi hadi leo.

Kitabu hiki kina mambo mengi yanayomhusu Yesu Kristo na wafuasi wake. Katika simulizi zake kuhusu Sanhedrin inasimulia jinsi baraza hilo lilivyomhukumu Yesu kuwa ni mchawi aliyewapotosha wayahudi wenzake kwa mafundisho potofu. Tangazo lilitolewa kwa siku arobaini juu ya hukumu yake ya kupigwa kwa mawe na watu waliokuwa tayari kumtetea waliombwa kujitokeza. Hakuna aliyejitokeza. Hivyo kabla ya Pasaka (ya wayahudi) aliuliwa kwa kutundikwa msalabani. (Cf., Sanhedrin, 43a). Licha ya hila zilizotumika kusimulia kisa hiki, bado katika uchanganuzi makini, tunaweza kuchota ukweli fulani wa kihistoria.

Waamini wanaitwa kusimama kidete kutangaza na kushuhudia imani yao
Waamini wanaitwa kusimama kidete kutangaza na kushuhudia imani yao

UFUFUKO: Ukweli juu ya ufufuko wa Kristo Yesu umeelezwa wazi pia na maandishi ya kale. Kwanza, kwa ushuhuda toka kwa mwanahistoria wa kiyahudi, Josephus anayetuambia kuwa Yesu, ambaye ni Kristo alihukumiwa kifo cha msalaba na Ponsio Pilato. Lakini alionekana tena siku tatu baada ya kifo chake akiwa hai kama manabii wa Mungu walivyotabiri. (Cf., Josephus, Antiquities, 18.3.3).  Vilevile mwanahistoria mkubwa wa Roma ya Kale, Tacitus, katika simulizi lake juu ya moto mkubwa uliozuka jijini Roma kipindi cha Kaisari Nero anasimulia kuwa tukio la kuuawa kwa Kristo lilituliza kwa muda “ushirikina mbaya” uliokuwa ukifanywa na wakristo. Lakini baada ya muda ukaibuka tena siyo tu Yudea ulipoanzia bali hata jijini Roma. (Cf., Tacitus, Annals, 15. 44.3). Kuibuka tena kwa wakristo kunaelezewa kuwa ni ushuhuda wa ufufuko wa Kristo. Tukio la kufufuka kwa Kristo lililorudisha tena matumaini ya wafuasi na hatimaye kutumwa rasmi na Kristo kuendeleza utume huo duniani pote. Hivyo walisambaa toka Yudea na hata kufika Roma. TAMATI: Nimalizie na maneno ya Mtume Paulo akisema... na kama Kristo hakukufufuka imani yenu ni ya bure... (Soma 1 Kor 15: 12 – 19). Na hapo uone umuhimu wa tukio la kifo na ufufuko wa Kristo. Kifo na Ufufuko wa Kristo ndiyo ilikuwa kilele cha kazi yake ya ukombozi wa mwanadamu. Ndiyo kilele cha maana ya yeye kuja ulimwenguni kwa umbo la mwanadamu. Hivyo tegemea kuwa Mpinga Kristo wa uzito wa juu hawezi kufanikisha kazi yake bila kupinga tukio la kifo na ufufuko wa Kristo.  Niwatakie nyote Pasaka Njema!! SURREXIT DOMINUS VERE, ALELUYA, ALELUYA! BWANA AMEFUFUKA KWELI, ALELUYA, ALELUYA! “... Na mtatambua yaliyo kweli na ukweli utawaweka huru. (Yn 8:31)

16 April 2022, 17:48