Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga wa jimbo katoliki Mbeya Tanzania. Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga wa jimbo katoliki Mbeya Tanzania. 

Tanzania,Askofu Mkuu Nyaisonga:Tuifanye karamu si chachu ya kale,iwe mpya

Fumbo la Pasaka linatafsiriwa kwa maneno mepesi ya Nabii Isaya:“Alijeruhiwa kwa makosa yetu,Alichubuliwa kwa maovu yetu;Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake,Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona”(Is 53,5).Ndivyo anatoa ujumbe wa Pasaka kwa waamini na watu wote wa Tanzania kutoka kwa Askofu Mkuu G.Nyaisonga,Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania(TEC)alioutoa kupitia mtandaoni.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

“Pasaka ni siku kuu kubwa ya kwanza kati ya siku kuu zote za imani yetu Kikristo.  Katika siku kuu hii tunatafakari kwa undani zaidi mafumbo ya wokovu wetu. Hata kuzaliwa Yesu Kristo kunapata maana kutokana na tukio hili”. Ndivyo alivyoanza ujumbe wake wa Pasaka 2022 kwa njia ya mtandao, Askofu Mkuu Gervas  J. M. Nyaisonga, Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya, Tanzania. Askofu Mkuu akiendelea, ametoa Heri na Baraka za Pasaka kwa watazamaji na wasikilizaji kupitia mitandao yote ya kijamii na kwamba: “Katika siku kuu ya Pasaka Bwana amefufuka kweli kweli, Aleluya…”. Lakini pamoja na salamu hizo amesisitizia juu ya maana ya fumbo lenyewe la Pasaka kwamba: “Linatafsiriwa kwa maneno mepesi ya Nabii Isaya yasemayo: “Alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona”(Is 53, 5). “Maneno hayo yanabeba ujumbe mkubwa wa Pasaka” amesisitiza. Katika tukio la Pasaka, Yesu anapata adhabu iliyo stahili wadhambi na wakati Yeye si mdhambi. Kwa maana hiyo yote yaliyotafakariwa katika  siku ya alhamisi Kuu, Ijumaa Kuu na kufikia ufukuko wa Bwana na kuendelea yanafichwa ndani ya maneno hayo ya Nabii Isaya”, amesisitiza Askofu Mkuu Nyaisonga. Kwa njia hiyo “Pasaka ni kufungua Agano Jipya kwa sababu Agano la kale imevurugwa na dhambi, na sasa linafunguliwa agano jipya kwa njia ya umwagaji damu ya Yesu Kristo”. 

Pasaka na ubatizo wetu, mwaliko kwa kila mbatiza na asiye batizwa

Askofu Mkuu Nyaisonga amesema tafakari ya Pasaka pia ni tafakari juu ya ubatizo wetu sisi, kwa sababu ya ubatizo, mwaamini anashiriki moja kwa moja ufufuko wake Yesu na pia kuwa mtu mpya! Hivyo Pasaka inatoa fursa ya kuzaliwa kwa upya. Pasaka ni mwaliko wa kila mtu, awe mkristo na asiye mkristo. Askofu Mkuu aliongeza kusema kuwa:“Kitu kipya kina sifa nyingi lakini sifa mojawapo ni nguvu na ubora zaidi na ndiyo ilivyo hata Pasaka kwa sababu ni kuanza kwa upya, (chachu ya kale na mpya...) Sisi tunapewa utu upya na thawabu”. Sifa za ukale ni ule wa kutawaliwa na kushambuliwa mabaya, maradhi ya kuwa na uovu wa kila namna ambayo yanamuudhi mwenyezi Mungu.  

Matendo ya upendo, huruma, kiroho na kimwili

Kwa maana hiyo "tunapoingia Pasaka, Yesu anashinda ubaya na anataka tuishi katika utu mpya ambao ni wa matendo ya upendo, ya huruma, ya kiroho na kimwili. Na ndiyo huo wito wa kuwa wapya ambapo Askofu Mkuu amesisitiza huku akiwageukia waamini wote, hasa Watazania wote kwamba wajitazame kwani hawawezi kubaki kuishi ukale, wa kugombana, kutukanana, kutegeana mitego na mambo mengine  mengi yasiyo na maana; kutokuwa na shukrani, kutokujali, kulalamika, hata kwa vile vitu vinavyoeleweka, kwani hivyo ndivyo vinavyofanya kubaki na utu wa kale. Hayo yakiendelea, kama vile ghadhabu, hasira na kiburi yanajenga mazingira mazuri ya kutenda uovu!" amebainisha. 

Anayeishi ukale hupenda kuongea mabaya wengine

Mwaliko wa Pasaka kwa maana hiyo wa utu upya ni kuwa na roho ya kujali, roho ya utu, ya huruma na ya ubinadamu. Kila binadamu anaweza kukosea, lakini anayeshi Roho ya Pasaka, anaouelewa wa kutambua mambo mazuri ya mwingine afanyayo”. Askofu Mkuu Nyaisonga amesisitiza kwamba anayeishi kwenye ukale, mara nyingi hupenda kuongea mabaya ya wengine,  hivyo inabidi kujiangalia sana. Kinyume chake anayeishi roho ya Pasaka, anapenda kila mara kujipyaisha japokuwa ataona sana mabaya, kwani hata Yesu angeona mabaya yote hayo, angeyazuia hata Kalvari isingetimia, maana angesitisha mapema, lakini yeye mwenyewe akiwa msalabani alisema hao hawajuhi walitendalo”. Kwa hiyo utu upya ni kusemehe na kushukuru”, amesisitiza Askofu Mkuu.

Chachu ya kale  

Kwa kuhitimisha, ujumbe wake wa Pasaka kwa njia ya Mtandao,  Askofu Mkuu Nyaisonga, amesisitiza kwamba: “Pasaka itusaidie kuwa wapya, tuwe na mioyo mikunjufu, tuwe watu wasamehevu, watu ambao wanajali na ikiwa nitaumia, niumie kwa kumpendeza Mungu na sio kwa kuwapendeza watu". Akinuu kifungu cha Barua ya Mtakatifu Paulo Mtume wa Watu: “basi na tuifanye karamu, si kwa chachu ya kale, wala kwa chachu ya uovu na ubaya, bali kwa yasiyochachika, ndio weupe wa moyo na kweli” (1Kor  5,8) ndiyo yalikuwa matashi yake mwema kwa wote na ametoa baraka yake ili yote hayo wayatendayo yaweze kuwa kweli ya kumpendeza mwenyezi Mungu. 

UJUMBE WA PASAKA WA ASKOFU MKUU GERVAS NYAISONGA,RAIS WA BARAZA LA MAASKOFU TANZANIA
17 April 2022, 15:44