Tafuta

Mama Kanisa katika mizunguko yote mitatu ya miaka ya Kiliturujia anatualika kutakafari ile Sura ya 10 ya Injili ya Yohane ambapo Yesu anajitambulisha kama Mchungaji mwema (mzuri). Mama Kanisa katika mizunguko yote mitatu ya miaka ya Kiliturujia anatualika kutakafari ile Sura ya 10 ya Injili ya Yohane ambapo Yesu anajitambulisha kama Mchungaji mwema (mzuri). 

Dominika IV Kipindi Cha Pasaka: Yesu Mchungaji Mwema: Dominika Ya Kuombea Miito Mitakatifu

Mama Kanisa ameitenga Dominika hii ya Mchungaji mwema/mzuri kuwa ni ya kuombea miito mitakatifu yaani: wito mama wa ndoa, upadre na utawa katika Kanisa. Nawaalika tunapotafakari Neno la Mungu pia kutenga muda kusali kwa ajili ya miito yote mitakatifu na kuwaombea wale walioitika miito hiyo neema ya uvumilivu na udumifu. Ni Mungu anayetuita katika miito mbalimbali

Na Padre Gaston George Mkude, - Rome

Amani na Salama! Dominika ya Nne ya Kipindi cha Pasaka inajulikana pia ni Dominika ya Mchungaji Mwema. Mama Kanisa katika mizunguko yote mitatu ya miaka ya Kiliturujia anatualika kutakafari ile Sura ya 10 ya Injili ya Yohane ambapo Yesu anajitambulisha kama Mchungaji mwema (mzuri). Mwinjili hatumii neno mwema kama tafsiri nyingi zinavyoiweka na badala yake anatumia neno mzuri. Ni kivumishi chenye maana ya mzuri, na hivyo ni katika uzuri ule si tu wa nje bali hasa wa ndani na ndio unaakisi wema wake. Ni katika uzuri wake unabubujika wema wake, si tu uzuri wa nje bali ni mzuri nje na ndani. Neno linalotumika la Kigiriki ni καλος (kalos) yaani mzuri na sio αγαθος (agathos) likiwa na maana ya mwema. (Εγω ειμι ο ποιμην ο καλος – Ego eimi o poimen o kalos) Ndio kusema Yesu anasema; Mimi ni mchungaji mzuri! Mama Kanisa ameitenga Dominika hii ya Mchungaji mwema/mzuri kuwa ni ya kuombea miito mitakatifu yaani: wito mama wa ndoa, upadre na utawa katika Kanisa. Nawaalika tunapotafakari Neno la Mungu pia kutenga muda kusali kwa ajili ya miito yote mitakatifu na kuwaombea wale walioitika miito hiyo neema ya uvumilivu na udumifu.

Ni Mwenyezi Mungu anayetuita katika miito hii mbali mbali kwa ajili ya kulijenga Kanisa lake, kila wito kimsingi ni utumishi iwe ule wa familia, wa kikuhani na wa kitawa. Kila mmoja wetu akumbuke tunaitwa kuwa watumishi, kuwa wadogo kwa ajili ya kuwaonjesha wengine upendo na huruma ya Mungu. Tuwaombee vijana wa kike na kiume kuwa na ujasiri wa kuitikia miito hiyo kwa upendo na sadaka kubwa. Tuwaombee pia wale wote wanaopitia nyakati ngumu na za majaribu katika maisha yao ya kuitikia miito hiyo ili wasikate tamaa hata mara moja wakitambua kudumu katika muunganiko na yule anayetuita katika miito mbalimbali katika Kanisa lake yaani Kristo Yesu, Bwana na Mwalimu. Mchungaji katika nyakati za Yesu tofauti sana na mazingira yetu ya leo ilikuwa ni aina ya maisha, ulikuwa ni aina ya wito, na hivyo mchungaji alikuwa sio tu mfugaji na mwangalizi wa mifugo yake bali zaidi sana aliyefanya mahusiano ya karibu kabisa na mifugo yake. Wachungaji walitengeneza zizi kubwa na kulizungushia ua mkubwa wa mawe, na jioni kila mmoja aliwaongoza kundi lake katika zizi hilo, na wao walibaki kwa zamu nyakati za usiku katika kulinda mifugo yao dhidi ya wezi na wanyama wakali wa mwituni.

Kristo Yesu ni Mchungaji mwema walio wake wanaisikia sauti yake.
Kristo Yesu ni Mchungaji mwema walio wake wanaisikia sauti yake.

Na kila asubuhi kila mchungaji alifika na kuwaita kwa majina kondoo au mifugo yake, nao waliijua sauti ya mchungaji wao na kumfuata. Hivyo tunaweza kuona jinsi mchungaji alivyoingia katika mahusiano ya ndani kabisa na kundi lake, na mifugo yake kiasi cha kuwajua kwa majina nao pia kumjua mchungaji kwa sauti na labda hata harufu yake. Na ndio tunasikia mara nyingi Baba Mtakatifu Francisko anawasihi wachungaji wa leo, yaani, maaskofu, mapadre na mashemasi kuwa na harufu ya kondoo, ndio kusema kuwa karibu na kuingia katika mahusiano mema na ya ndani na kondoo, ni kuwajua na kuwatambua, hali zao mbali mbali; na kuwapa nafasi nao kuweza kuijua na kuitambua sauti ya mchungaji wao. Mchungaji mzuri ni yule anayeingia katika mahusiano ya ndani na kundi lake, anayekubali kusafiri pamoja nao katika hali zote iwe za furaha na hata za huzuni na ngumu. Mchungaji mwema anakuwa tayari hata kuhatarisha na kuutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo wake, ni kuwa na upendo upeo kwa kondoo wa kundi lake.

Wachungaji pia walikuwa ni kundi la watu wa hadhi ya chini, watu waliohesabika na kuonekana kuwa na tabia na hulka kama za wanyama. Na ndio tunaona hata ushahidi wao usingekubaliwa mahakamani, ni watu najisi na hivyo wasingeweza hata kuingia hekaluni. Lakini leo Yesu anajitambulisha kuwa mmoja wa kundi lile lenye hadhi ya chini kijamii na hata kidini lakini anatumia kivumishi kuwa yeye ni mchungaji mzuri(καλος). Wachungaji ndio wanakuwa wa kwanza kupata Habari Njema ya kuzaliwa kwake katika usiku ule wa Noeli, na ndio leo tunaona anajitambulisha kama mchungaji mwema. Ndio kusema hakuna kundi lolote katika jamii ambalo Yesu analitenga na kuwa mbali nalo. Yesu anakuja ili ulimwengu mzima, ili kila mmoja wetu asipotee bali tujaliwe uzima wa milele. Muktadha wa Injili ya Dominika ya IV ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa Yn 10: 27-30. Yesu yupo hekaluni wakati wa sherehe za Kiyahudi za Hanukah (sherehe za mwanga), sikukuu ambayo ilisherehekewa kwa siku 8 kukumbuka kulitakatifuza tena hekalu baada ya kunajisiwa na utawala wa kipagani.

Mchungaji Mwema anawatambua Kondoo wake
Mchungaji Mwema anawatambua Kondoo wake

Ni katika mazingira ya hapo hekaluni wanafika Mafarisayo kwa Yesu na kumuuliza kwa hila kama yeye ndiye Masiha au la, na ndio tunaona Yesu anaanza kujitambulisha kwao kuwa yeye ni mchungaji mzuri na mwema. Yeye ni tofauti na ile taswira waliyokuwa nayo vichwani mwao, anawaalika nao kubadili vichwa vyao na ndio kukata vichwa, kuivaa mantiki mpya ndio ya Mungu mwenyewe. Yesu anawaalika kubadili vichwa vyao mintarafu sura ya Mungu waliyokuwa nayo, na badala yake kuwa na sura ya uzuri, yaani upendo na huruma ya Mungu. Na ndio hata nasi leo tunapoisoma na kuitafakari sehemu ya Injili ya leo, ni mwaliko kwetu kujifunza sura ile ya Mungu anayoifunua Yesu kwetu, ndio sura ya upendo na huruma kwa ulimwengu mzima na si kinyume chake. Nikiri mara nyingi na hasa sisi wahubiri tumekuwa tunawafundisha waamini sura isiyo sahihi ya Mungu. Leo Yesu anatugeukia sisi sote na kutuonesha sura halisi ya Mungu ni uzuri, ndio wema na upendo na huruma yake ya milele kwa watu wake wote.

Katika sehemu ya Injili ya leo ili kuitafakari vyema nawaalika japo tuangalie vitenzi vinavyotumika: Kusikiliza, kujua, kumfuasa, kutoa uzima wa milele, kutowapoteza na kutonyang’anywa. Kusikia katika Maandiko Matakatifu lina maana pana na ya kina kwani sio kitendo cha kutega sikio tu bali hasa kujishikimanisha na kumtii Mungu, ni kujenga mahusiano na kuruhusu kuongozwa naye katika yote. Hivyo anayemsikiliza Mungu ni yule anayeongozwa naye, ndiye yule anayeongozwa na Neno lake kama taa ya njia na miguu yake. Neno sikia kwa Kiebrania ndio “Shema” kutoka Kitabu cha Kumbukumbu la Torati sura ya 6, hivyo walipaswa kuisali kila siku na zaidi sana kuirithisha kwa vizazi vingine, ni mwaliko wa kumsikiliza Mungu, ni mwaliko wa kuchagua maisha badala ya kifo. Hivyo, sikia ni kufungua moyo kumpenda na kumtii Mungu, ni kuingia katika mahusiano ya ndani naye kama wana na watu wake. Shema ni kitenzi cha mwaliko wa kuingia katika mahusiano na Mungu awali ya yote.

Kujua ni kitenzi kingine ambacho nacho hakina maana ile ya kujua kwa kutumia akili zetu au milango ile ya fahamu inayotupelekea kupata maarifa kama wanadamu, bali ni mahusiano ya ndani kabisa kati yetu na Muumba wetu. Kumjua Mungu ni kuwa na mahusiano ya ndani kabisa naye, hivyo inahusisha akili, moyo, matendo na nafsi zetu katika mahusiano hayo. Ni kujua kwa maana ya γιγνοσκο (gignosko) na si οιδα (oida), hivyo ni kuingia katika mahusiano na urafiki wa ndani na si kujua kwa maana ya maarifa tu, haitoshi kujua kwa akili zetu tu, bali ni kuingia katika mahusiano ya ndani na Kristo Mfufuka na hapo ndio tunaweza kusema tunamjua, ni kwa kumpenda kweli bila masharti wala kujibakisha. (Rejea Yohane 15:9-10) Yesu anatuhakikishia sisi wafuasi wake kuwa anatupenda sisi kama vile Baba anavyompenda Yeye mfufuka. Ni kuingia na kushiriki katika Upendo mkamilifu wa Utatu Mtakatifu. Taalimungu kama sayansi ya ufahamu wa Mungu ni tofauti na sayansi au elimu nyingine kama Falsafa ambayo mtafiti anapaswa kujibidisha kwa akili zake mwenyewe tu, bali katika sayansi Mungu (Taalimungu) ni Mungu kwanza anayejifunua na kutaka kuingia katika mahusiano na mwanadamu. Kumjua Mungu kwa kweli ni Mungu kwanza anayemchagua mwanadamu kabla ya sisi hatujapiga hatua ya kumwelekea Yeye.

Hivyo upendo wa Kristo kwa Mungu na upendo wake kwa wanadamu vinaungana na kufanana, anavyokubali kufanyika mwanadamu na kufa pale juu msalabani ni kwa kumpenda Baba na sisi wanadamu. Ni upendo usiogawanyika kwa Mungu Baba na kwetu sisi wanadamu, ni upendo wa ajabu tusioweza hata kuuleza wala kuulewa kikamilifu kwa akili zetu na hata vionjo vyetu vya kibinadamu. Ni upendo unaobaki kuwa fumbo linalozidi akili na ufahamu wetu wa kibinadamu! Yule anayeingia katika mahusiano hayo ya ndani kabisa basi anamfuata huyo Mchungaji mzuri/mwema. Ni upendo huu wa ajabu unaoonesha uzuri wake wa ndani na nje, kupenda kwa namna ya Kristo ndio upendo mkamilifu ambao sisi sote tunaalikwa kufuata mfano wake katika maisha yetu. Tunaalikwa kumpenda Mungu kwa kuwapenda wengine, kwani hatuwezi kusema sisi tunampenda Mungu wakati hatuwapendi wengine, kupenda hata wanaokuwa maadui na kinyume chetu, kupenda bila masharti wala kusubiri malipo au faida kwa upande wetu. Anayemsikiliza na kumjua hatimaye anamfuasa huyo Mchungaji mzuri. Ndio kufanya maamuzi au uchaguzi wa maisha mapya, kukubali kuongozwa na mantiki ya huyo Mchungaji mzuri badala ya ile ya ulimwengu huu.

Dominika ya Mchungaji Mwema ni Siku ya kuombea Miito Mitakatifu
Dominika ya Mchungaji Mwema ni Siku ya kuombea Miito Mitakatifu

Ni kujishikamanisha naye na kukubali kuongozwa naye daima, kwa kuitii sauti yake yaani kuongozwa na Neno lake. Ni kujitoa sadaka wazimawazima kwa kufuata mfano wake, kama Yeye alivyojitoa sadaka basi nasi tunaalikwa kufanya vivyo hivyo. Tukimjua hakika tutampenda kwani kwake unabubujika upendo wote na hivyo nasi kutekwa na upendo wake wa Kimungu. Kukutana na Yesu ni kumpenda na si kinyume chake! Upendo wake una nguvu kiasi cha kututeka na kutualika nasi kutoka na kuwa mashahidi wa uzuri na wema wake wa Kimungu. Yesu pia anatoa ahadi kwa kila anayemsikiliza na kuijua sauti yake na kumfuata: Uzima wa milele. Sio uzima wa kibailojia yaani βιος (bios) bali ni ζωην αιωνιον (zoen aionion) ndio muunganiko na Mungu, ni maisha yasio na mwisho pale tunapokubali kuongozwa naye nasi tukafanya uchaguzi wa kuongozwa na mantiki yake ya Kimungu. Na uzima wa milele sio maisha baada ya kifo bali tunaanza kuyaishi pale tunapochagua maisha ya kweli yaani kuunganika na Yesu mwenyewe na hivyo kuanza kuishi maisha ya furaha ya kweli. Maisha ya milele ni furaha ya kweli, ni maisha yatokanayo na kuunganika na Mungu, ni kuishi kadiri ya mapenzi yake iwe katika maisha ya sasa na kubaki kuunganika naye hata baada ya maisha ya hapa ulimwenguni. Maisha ya uzima wa milele ni muunganiko wa daima na Mungu.

Kila anayefanya uchaguzi huo basi kwa hakika hatapotea wala kunyang’anywa kutoka mkono wenye nguvu wa Kristo Mfufuka. Na ndio hakika yetu ya kubaki wenye furaha na matumaini kwani hata kama tutapitia magumu katika maisha ya sasa daima tunabaki salama kama tunachagua kumsikiliza na kumjua na kumfuata Yesu. Ni hakika anayotupa sote kila mmoja wetu katika wito wake kuwa Yeye anatualika kuunganika naye kwani Yeye na Baba ni mmoja. Ni kutokana na umoja wao hivyo nasi tunaalikwa kushiriki umoja huo, na ndio upendo, kwani ni umoja unaotokana na upendo. Nje ya upendo huo hatuwezi kuwa na uzima wa milele, hatuwezi kupata furaha ya kweli, yaani nje yake sisi tunabaki kupotea na hivyo kupatwa na uharibifu. Uzima wa milele ni wito wetu sote iwe ni Wayahudi au watu wa mataifa na ndio tunaona mitume Paulo na Barnaba wanageukia watu wa mataifa baada ya Wayahudi kuukataa wito huo wa msingi. Utakatifu ni wito wetu sote bila ubaguzi iwe katika maisha ya ndoa, ukasisi au utawa, sote tunaalikwa kuwa watakatifu, kuunganika na Mungu na ndio kuishi maisha ya neema. Miito yote ipo ili kutusaidia kuufikia wito ule wa juu na wa milele ndio utakatifu.

Na ndio wito wa kumfuata mwanakondoo iwe katika ulimwengu huu upitao na ule wa milele mbinguni. Utakatifu ndio kilele cha kila miito tunayoitwa nayo tungali hapa ulimwenguni. Ni wito wa maisha ya sasa na yale ya milele baada ya maisha ya hapa ulimwenguni. Ni wito wa kila mwamini, wa kila mbatizwa, ni wito wa ulimwengu mzima, ndio kuwa watakatifu kama Baba yetu wa mbinguni alivyo mtakatifu. Nawatakia Dominika njema ya Kristo Mchungaji mzuri/mwema. Na tuzidi kusali kwa ajili ya miito mitakatifu na bila kuwasahau kuwaombea walioitikia miito hiyo kumsikiliza daima Kristo na kufanya uchaguzi wa kubaki daima katika muungano naye aliye mchungaji wetu mzuri. Miito yote katika Kanisa inapata maana na thamani yake katika kuunganika kwanza na Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo na katika ushirika wa Mungu Roho Mtakatifu. Kila mmoja anayetaka kuitikia wito wake basi daima aone namna ya kuunganika na huyu aliye Mchungaji wetu mzuri na mwema.

Dominika 4 Pasaka
04 May 2022, 10:51