Tafuta

Siku ya 59 ya Kuombea Miito Mitakatifu Ndani ya Kanisa Siku ya 59 ya Kuombea Miito Mitakatifu Ndani ya Kanisa 

Dominika ya Mchungaji Mwema: Siku ya 59 Ya Kuombea Miito Mitakatatifu

Siku ya 59 ya Kuombea Miito Duniani kwa mwaka 2022 , waamini wanaalikwa kutafakari kwa pamoja maana pana ya “wito” ndani ya muktadha wa Kanisa la Sinodi, Kanisa linalomsikiliza Mungu na ulimwengu. Huu ni mwaliko wa kukuza moyo wa kusikiliza, kushiriki na kushirikishana, ili kujenga familia ya kibinadamu, kuponya majeraha yake na kuiongoza kwenye maisha bora zaidi.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Dominika ya Nne ya Kipindi cha Pasaka. Dominika hii hufahamika kama dominika ya Mchungaji Mwema kwa sababu Injili inayotangazwa katika dominika hii ni ile ambayo Kristo mwenyewe anajitambulisha hivyo; kuwa yeye ndiye mchungaji mwema wa kondoo wake. Katika dominika hii, Kanisa huadhimisha pia siku ya sala kwa ajili ya kuombea miito mitakatifu. Na kwa sababu hii, dominika hii hujulikana pia kama dominika ya miito. Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya 59 ya Kuombea Miito Duniani kwa mwaka 2022 anawaalika waamini kutafakari kwa pamoja maana pana ya “wito” ndani ya muktadha wa Kanisa la Sinodi, Kanisa linalomsikiliza Mwenyezi Mungu na ulimwengu. Huu ni mwaliko wa kukuza moyo wa kusikiliza, kushiriki na kushirikishana, ili kujenga familia ya kibinadamu, kuponya majeraha yake na kuiongoza kwenye maisha bora zaidi.

MASOMO KWA UFUPI: Kama kawaida ya kipindi hiki, sehemu ya kwanza tunaitumia kuyapitia masomo ya dominika na kujaribu kuyafafanua ili kuelewa zaidi kile kinachozungumzwa. Tunaanza na somo la kwanza ambalo linatoka katika kitabu cha Matendo ya Mitume (Mdo. 13:14, 43-52). Katika somo hili Mtume Paulo anaeleza azma yake ya kuwageukia Mataifa, yaani kupeleka Injili nje ya uyahudi. Anafanya hivyo kwa sababu ndani ya uyahudi mwitikio haukuwa mzuri: Wayahudi walilisukumia mbali Neno la Mungu: hawakuwa tayari kumpokea Kristo wakiamini kuwa Torati ya Musa inatosha kuwapa wokovu bila Kristo. Lakini sio sababu hiyo tu, Paulo na wenzake wanaipeleka Injili nje ya uyahudi kwa sababu huo ndio uliokuwa mpango wa Mungu tangu awali, kwamba mataifa yote yapate nuru ya wokovu kuanzia uyahudi wenyewe. Ananukuu utabiri wa nabii Isaya kuonesha kwamba yale maneno ambayo nabii aliyatabiri sasa umefika wakati wa maneno hayo kutimia. Ni maneno yaliyosema “nimekuweka uwe nuru ya mataifa, upate kuwa wokovu hata mwisho wa dunia.” Tangu wakati huu, Paulo anaupokea wito huo wa kuwa mtume wa Mataifa na anaanza safari ya kuzunguka kote alikoweza kupeleka Habari Njema.

Siku ya 59 ya Kuombea Miito Mitakatifu Ndani ya Kanisa
Siku ya 59 ya Kuombea Miito Mitakatifu Ndani ya Kanisa

Somo la Pili linatoka katika Kitabu cha Ufunuo (Ufu 7:9. 14-17). Ni somo ambalo huwa tunalisikia siku ile ya Sikukuu ya Watakatifu Wote ambapo unatajwa umati mkubwa wa watu wasiohesabika kutoka kila kabila, taifa na jamaa wakisifu mbele ya mwanakondoo aliyeshinda, yaani Kristo mfufuka. Hawa ni watu waliokombolewa na nguvu ya damu ya Kristo. Katika dominika hii ya miito, tunaona kuwa somo la kwanza kuhusu Paulo kwenda kuwahubiria mataifa na somo hili kuhusu mataifa kuokolewa, ni masomo yanayoungana kuonesha kuwa tunda la kuitikia wito wa kuhubiri injili ni wokovu wa watu wa Mungu. Na wale wanaoipokea Injili ya Kristo katika maisha yao wanahakikishiwa kuwa sehemu ya watu waliokombolewa. Katika Injili (Yn 10:27-30) Kristo anajipambanua kuwa ndiye Mchungaji Mwema na anaongeza kusema “kondoo wangu waisikia sauti yangu, nami nawajua, nao wanifuata.” Tuingie ndani kidogo ya Injili hii ili tuone ni nini Yesu anamaanisha anapotumia lugha hii ya picha. Maneno haya Yesu anayatoa kwa wayahudi ambao kwa mara nyingine tena walianza kumhoji ili awaambie kama yeye ndiye Kristo au la! Hilo ni swali ambalo hata kwa Pilato Yesu hatalijibu. Atamwambia tu “wewe wasema”. Yesu halijibu hilo swali kwa sababu kusema kwamba Yesu ni Kristo, ni kuungama imani.

Na ungamo hili la imani ni mtu mwenyewe anapaswa kulifanya. Yesu halijibu swali hilo kwa sababu anataka mtu mwenyewe baada ya kukutana na Yesu akiri kwa kinywa chake na kukiri huko kuambatane na njia mpya ya maisha, maisha ya kikristo. Kumbe, Yesu hawapi wayahudi jibu wanalolitegemea ili wamkamate kwa maneno yake mwenyewe kuwa amejifanya Kristo. Badala yake anawaambia wao hawamtambui kwa sababu sio kondoo katika zizi lake. Kondoo walio katika zizi lake wanaisikia sauti yake, naye anawajua nao wamfuata. Kutoka hapo sasa ndio anaanza kueleza hao walio kondoo wake wana hali gani. Na anaonesha walio kondoo wake wanaishi katika uhusiano wa karibu na Yesu mwenyewe pamoja na Baba yake. Walio kondoo wake wana uzima wa milele na kuwa na uzima wa milele maana yake hawatapotea kamwe na hakuna atakayewapokonya kutoka mikononi mwake wala kutoka mikononi mwa Baba. Yesu anapowaambia wayahudi kuwa wao hawamo kati ya kondoo wake, hawafukuzii mbali bali anawaalika watoke huko nje waliko waingie ili nao wawe mojawapo wa kondoo.

Malezi na majiundo makini ni muhimu kwa miito mbalimbali ndani ya Kanisa
Malezi na majiundo makini ni muhimu kwa miito mbalimbali ndani ya Kanisa

Kwa kutambua kuwa Wayahudi hao walibaki katika kulishikilia  Agano la Kale peke yake, Yesu anatumia hilo hilo Agano la Kale ili kuwaonesha kuwa kile wanachokishikilia wakikizingatia vizuri wataona kuwa kinawaongoza kufika kwake. Anapowaambia “walio kondoo wangu wana uzima wa milele na hawatapotea kamwe” anadokeza Zaburi ya 31 inayosema “nimekukimbilia wewe Bwana nisiaibike milele”.  Kutokuaibika milele ndiko kutokupotea kamwe na ndiko kuupata uzima wa milele ambao Yesu anawapa walio kondoo wake. Tena anapowaambia hakuna anayeweza kuwapokonya kondoo wake anadokeza maneno ya Kitabu cha Hekima 3:1 “roho zao wenye haki zimo mikononi mwa Mungu” na ya Isaya 43:13 kuwa “hakuna awezaye kuokoa kutoka katika mkono wangu.” Kumbe lugha hii ya picha ya Yesu mchungaji mwema anayewaalika watu kuingia kuwa kondoo wake, mwinjili Yohane anaitumia kumaanisha kitu kile kile ambacho wainjili wengine walikimaanisha walipozungumzia ufalme wa Mungu, ufalme ambao Yesu alikuja kuuanzisha na kuwaalika watu wauingie.

TAFAKARI: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, katika dominika hii ya Mchungaji Mwema ambayo pia ni siku ya sala kwa ajili ya kuombea miito yote. Tunaielekeza tafakari yetu katika miito ya upadre na utawa, miito ambayo ndani yake mtu anajitoa kwa huduma ya kanisa katika nafsi ya Kristo na kwa namna alivyofanya Kristo mwenyewe na tena anayejitoa anajiweka tayari kuyafananisha maisha yake na maisha ya Kristo mtii, fukara na mseja. Tunaitafakari miito hii katika kipindi ambacho jamii ambamo mapadre na watawa wanaishi na kutoa huduma ni jamii zinazoishi katika kipindi cha mabadiliko, tena mabadiliko makubwa na yanayokwenda kasi mno. Yapo mabadiliko ya kifikra, yapo ya kiutendaji, ya namna ya kuishi n.k na athari za mabadiliko haya zinagusa nyanja zote. Athari hizi zinaugusa pia upadre na utawa kutoka nje na kutoka ndani. Kutoka nje, jamii yenyewe inaanza kuunda picha ya mapadre na watawa inaowataka. 

Familia ni chimbuko la miito yote ndani ya Kanisa
Familia ni chimbuko la miito yote ndani ya Kanisa

Kutoka ndani, Padre au mtawa mwenyewe anaanza kujiona hatoshi; kama haendani na kasi ya mabadiliko ya jamii aliyomo. Na haya yote tunayaita kusoma alama za nyakati. Dominika ya leo inapotualika kusali kwa ajili ya kuombea miito inatukumbusha kuwa pamoja na kusoma alama za nyakati, miito ya upadre na utawa huzaliwa katika sala na ni katika maisha ya sala hupata utambulisho wake. Bila kipengele hiki muhimu miito hii haitakuwa tena na ule utambulisho wake wa kuwa ushuhuda wa Kristo mfufuka bali itakuwa ni kama huduma nyingine yoyote ile ya kijamii, ya kisiasa au ya kimaendeleo ambayo mtu anaweza akaifanya vizuri tu bila hata kuwa padre au mtawa. Sala tunayoipaza leo kwa Mungu Baba kwa ajili ya kuombea miito ikoleze chachu ya ushuhuda wa utakatifu wa maisha ambao ni msingi usioyumba katika wimbi la mabadiliko linalozikumba jamii zetu. Tunahitaji pia wongofu wa kichungaji.

Liturujia D4 Miito

 

06 May 2022, 11:32