Tafuta

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya V Ya Kipindi Cha Pasaka: Kristo Yesu ni: Dira, Kielelezo na Utimilifu wa Upendo wa Mungu ambao umetundikwa juu ya Msalaba Mtakatifu. Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya V Ya Kipindi Cha Pasaka: Kristo Yesu ni: Dira, Kielelezo na Utimilifu wa Upendo wa Mungu ambao umetundikwa juu ya Msalaba Mtakatifu. 

Dominika ya V ya Pasaka: Yesu Kielelezo Na Ukamilifu Wa Upendo

Kipimo cha upendo ni Kristo Yesu: “kama mimi nilivyowapenda ninyi." Kipimo cha mwanadamu daima si kamili. Kipimo cha mwanadamu daima kinapwaya na hakiendi zaidi ya udhaifu wake. Ndiyo maana anataka kipimo cha kupendana kisiwe kile cha ubinadamu bali kipimo kiwe ni upendo wa Kristo Yesu: pendaneni kama vile nilivowapenda ninyi.. Upendo uliotundikwa Msalabani.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Dominika ya V ya Kipindi cha Pasaka. Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika kipindi hiki cha Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu. Tupo bado katika kipindi cha Pasaka. Kwa siku 50 tangu dominika ya Pasaka hadi dominika ya Pentekoste tunaendelea kuadhimisha ufufuko wa Kristo tukisindikizwa kila dominika na dhamira mbalimbali kutoka Maandiko Matakatifu. Katika dominika hii ya 5 dhamira tunayopewa ni upendo wa Kristo. Kristo anatoa amri mpya ya upendo na anawaambia wanafunzi wake "mpendane kama nilivyowapenda ninyi." MASOMO KWA UFUPI: Tuyapitie sasa masomo yote matatu ya dominika hii tukianza na somo lenyewe la Injili kama ilivyoandikwa na Yohane (Yoh. 13:21-33a, 34-35). Somo linaturejesha Siku ile ya Alhamisi Kuu ambapo Yesu anakula Karamu ya mwisho akiwa na wanafunzi wake. Baada tu ya Yuda Iskarioti kuondoka, Yesu anasema saa yake ya kutukuzwa imefika. Na saa hii ya kutukuzwa ni wakati wa yeye kusulubishwa. Yesu hazungumzii mateso na kifo chake kama saa, tukio au tendo la kudhalilishwa. Kwake ni saa ya kutukuzwa na ni saa ya kumpa Mwenyezi Mungu utukufu. Baada ya maneno hayo ndio anawapa sasa kama wosia amri mpya ya mapendo.

Amri ya Upendo unaomwilishwa katika huduma makini kwa watu wa Mungu
Amri ya Upendo unaomwilishwa katika huduma makini kwa watu wa Mungu

Kusema kuwa amri anayowapa ni mpya inamaanisha kuwa ilikuwapo amri ya zamani. Amri hiyo ya zamani ni ile ambayo Mungu aliitoa kwa kinywa cha Musa katika Agano la Kale. Nayo ni “mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote na kwa nguvu zako zote” (Kum 6:4-5) na “mpende jirani yako kama nafsi yako” (Walawi 19:18). Amri hii mpya haiondoi amri ya zamani bali inakuja kuikamilisha. Tunachoona ni kuwa Yesu haigusi ile amri ya kumpenda Mungu, anajikita katika sehemu ya pili yaani amri ya kumpenda jirani. Upya wake uko wapi? Kwanza katika amri hii, Yesu anaondoa neno jirani: anasema tu pendaneni. Kwa Wayahudi, neno jirani lilileta daima tafsiri ya mtu aliye na mahusiano naye: mahusiano ya udugu wa damu, ya ukoo, ya urafiki au utaifa. Kwa misingi hiyo mtu aliye nje ya mipaka hiyo hakumuwajibisha kumuonesha upendo. Katika amri hii mpya Yesu anaposema “pendaneni” bila kuongeza neno la nani apendwe anaalika kuishi upendo usio na mipaka. Na hii inaendana kabisa na mafundisho yake ya tangu awali aliposema “mkiwatendea mema wale tu wanaowatendea mema mnapata thawabu gani? Kwa maana hata waovu hufanya vivyo hivyo.”

Upya wa amri hii upo pia katika kipimo. Kipimo cha upendo ni Kristo Yesu na wala sio tena “kama unavyojipenda mwenyewe”, bali kipimo cha upendo ni “kama mimi nilivyowapenda ninyi”, yaani kama Kristo anavyompenda kila mmoja wetu. Kipimo cha mwanadamu daima si kamili. Kipimo cha mwanadamu daima kinapwaya na hakiendi zaidi ya udhaifu wake. Ndiyo maana anataka kipimo cha kupendana kisiwe kile cha ubinadamu bali kipimo kiwe ni upendo wa Kristo: pendaneni kama vile nilivowapenda ninyi. Baada ya kuliangalia somo hilo la Injili, turudi katika somo la pili, somo linalotoka katika kitabu cha Ufunuo (Ufu 21:1-5a). Katika somo hili tunasikia juu ya mbingu mpya na nchi mpya. Yohane anauona, katika maono, mji mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka mbinguni. Katika injili Yesu amezungumzia amri mpya, hapa Yohane anaona mbingu mpya na nchi mpya. Hii inamaanisha nini? Biblia inapozungumzia upya: mfano: kuuvaa utu mpya, kuwa kiumbe kipya, kutembea katika upya wa maisha n.k haina maana ya kuonesha kitu kitu kipya kwa maana ya kitu ambacho hapo awali hakikuwepo.

Kristo Yesu ni dira, kielelezo na utimilifu wa upendo
Kristo Yesu ni dira, kielelezo na utimilifu wa upendo

Upya katika Biblia humaanisha ukamilifu, utimilifu na ukomo wake. Kile kilichokuwapo kinafikia ukamilifu wake, kile kilichokuwapo kinafikia lengo lake. Sasa Yohane anatoa maono haya kwa dunia na kwa watu wa Mungu wanaopitia kipindi kigumu katika maisha yao. Ni watu ambao wanapoangalia hali hiyo waliyomo hawaoni mwisho wao kuwa mzuri. Hawauoni mwisho kuwa mzuri kwa sababu nguvu inayopambana dhidi yao inaonekana kuwa ni kubwa mno kuliko utashi wao mwema, kuliko imani yao na kuliko hata matumaini yao. Maono haya ya Yohane yanakuja kuamsha upya imani na matumaini ya watu kuwa ni Mungu mwenyewe anayetangaza kuingilia kati na kubadilisha mkondo wa mambo. Ni yeye asemaye “tazama, nayafanya yote kuwa mapya”. Kwamba ulimwengu na hatima ya watu wanaomwamini haitaharibika wala kupotea milele bali Mungu mwenyewe ataiongoza kufikia ukamilifu wake na kulifikia lengo la kuumbwa kwake.

Dhamira hii ya upya inatusaidia pia kuielewa zaidi amri mpya ya upendo ambayo Kristo ametupatia. Kwa sababu kama yalivyokuwa magumu mazingira ya watu aliowazungumzia Yohane katika kitabu cha Ufunuo, ndivyo yalivyo pia magumu mazingira ya kuuishi upendo ule aliotuagiza Kristo. Mwaliko wa Yohane, hata hapa, unakuja kutuambia inawezekana: tukimtanguliza Mungu inawezekana. Tuliangalie sasa somo lililobakia, somo la kwanza, ambalo linatoka katika kitabu cha Matendo ya Mitume (Mdo14:21b-27). Somo hili linatupa hitimisho la safari ya kwanza ya kitume ya Paulo akiwa na msaidizi wake Barnaba. Tunasikia miji aliyotembelea na habari Njema aliyoihubiri kwa ari na msukumo mkubwa. Tunaweza kusema kuwa somo hili linakuja kutupatia ushuhuda kwa njia ya vitendo wa mojawapo ya namna ya kuuishi upendo wa Kristo. Na Mtume Paulo ndiye anayetupa ushuhuda huo kwa namna yake ya kujitoa bila kujibakiza kwa ajili ya kuwafikishia watu Habari Njema.

TAFAKARI : Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, Neno la Mungu dominika hii limetuzungumzia juu ya amri mpya ya mapendo. Kristo ametuagiza “pendaneni kama vile mimi nilivyowapenda.” Tunapoiangalia amri hii na kuyatazama maisha yetu katika familia zetu, jumuiya zetu mbalimbali, makazini na katika maisha kwa ujumla tunaona bado kuna vikwazo vingi katika kuufikia upendo huo aliotuagiza Kristo tuuishi. Ndiyo maana katika tafakari hii, ninawaalika tuvitupie macho vikwazo vitatu kati ya vingi vilivyopo. Kikwazo cha kwanza ni maslahi: Tunashindwa kuuishi upendo wa Kristo kwa wenzetu kwa sababu tu upendo haulipi, upendo hauwezi kukufanya ufikie maslahi yako binafsi. Maslahi haya yanaweza kuwa ni maendeleo ya kifedha au mali, yanaweza kuwa ni kupata nafasi za kiungozi n.k. Kwa mtu anayetafuta maslahi kama haya njia ya upendo ni njia ndefu mno na isiyo na uhakika. Badala yake mtu anajikuta anachagua kutumia njia fupi: njia ya usaliti, njia ya kujitenga wakati mwingine hadi kutelekeza familia, ndugu au marafiki ili kuyapa nafasi ya kwanza maslahi yake,. Katika Biblia, hii ndiyo njia aliyoichagua Kaini akaishia kumuangamiza Abeli ndugu yake. Tunakumbuka swali Mungu alilomuuliza “Yuko wapi Abeli ndugu yako?” kumkumbusha kuwa anao wajibu kwa ndugu yake, na wajibu huo ni upendo. Ustawi, maendeleo na maslahi ya kweli ni yale yasiyomwacha mtu nyuma.

Majeraha ya upendo ni ubinafsi, masilahi na changamoto za upendo wenyewe.
Majeraha ya upendo ni ubinafsi, masilahi na changamoto za upendo wenyewe.

Kikwazo cha pili ni majeraha ya upendo wenyewe. Wapo ambao kwa sababu ya upendo wa Kristo wamejeruhiwa na sasa wamekosa imani na yeyote. Hawawezi kuuishi upendo wa Kristo kwa sababu wanamshuku kila aliye karibu nao, hawawezi kuuishi upendo wa Kristo kwa sababu wanajiona daima wahanga wanaonewa, wanabaguliwa, thamani yao haitambulikani n.k. Kristo anapotuambia leo “pendaneni kama vile mimi nilivyowapenda” anawakumbusha wote walio na majeraha ya upendo kuwa kipimo cha upendo ni Yeye mwenyewe kwa upendo ule aliowapenda na anaoendelea kuwapenda. Kama tulivyopata nafasi ya kulifafanua somo la Injili, upendo ulio na kipimo chake kwa mwanadamu lazima unakuwa hautoshi. Ni Kristo na si mwanadamu anayeponya majeraha ya ndani, ni Kristo anayetambua thamani ya kila mmoja wetu na ni Kristo ambaye pamoja na yote hayo anatuagiza bado tupendane.

Kikwazo cha tatu ni asili jumuishi ya upendo wenyewe. Kristo amegaiza “pendaneni”. Agizo hili linatuwajibisha sote. Sote tunawajibishwa kutoa upendo na sote tunaalikwa kuupokea upendo. Kumbe katika familia, katika jumuiya au mahala pengine popote pale akitokea mmoja anayetaka kupokea tu upendo bila yeye kutoa upendo anauhatarisha upendo wenyewe, anakuwa kikwazo cha kuufikia ukamilifu wa upendo wenyewe. Na Yesu mwenyewe anasema “watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi.” Kukivuka kiwazo hiki ni kuwasaidia walegevu kutambua thamani ya upendo wa Kristo. Upendo wa Kristo unahitaji malezi na familia zetu, jumuiya zetu na jamii kwa ujumla inahitaji kulelewa ili wajibu huu jumuishi wa mapendo uwe ni wajibu wa wote.

Liturujia D5
09 May 2022, 11:37