Dominika VI ya Pasaka: Ujenzi wa Kanisa La Kisinodi: Umoja, Ushiriki Na Utume
Na Padre Efrem Msigala, OSA, - Roma.
Karibu mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican na msomaji wa Vatican News katika tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya VI ya Kipindi cha Pasaka ya Mwaka C wa Kanisa. Liturujia ya Neno la Mungu inatualika kutafakari juu ya utaratibu wa kutatua matatizo kwa njia ya mazungumzano, kwa lengo la kudumisha: Umoja, Ushiriki, Utume na Amani katika jamii mambo msingi yanayopewa kipaumbele cha pekee katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Amani ni zawadi kubwa ambayo Kristo aliwaachia Mitume wake. Wakati huo Mungu akipewa nafasi ya kwanza ndiyo amri ya upendo kumpenda Mungu na kushika amri zake. Na pia kuwa na umoja na mshikamano wa dhati kati ya wafuasi wake. Katika somo la kwanza (Mdo15:1-2.22-29), Jumuiya ya Wakristo wa kwanza inatambua matokeo ya migongano katika mafundisho na hivyo wanatafuta suluhisho katika migongano hiyo. Kuna baadhi walikuwa wanafundisha kuwa watu wa mataifa bila kutahiriwa hawawezi kuokolewa. Hivyo kukatokea mgongano na wale waliosema si lazima kwa watu wa mataifa wanaomwongokea Mungu kufanyiwa tohara. Kutokana na mgongano huo waliona muhimu baadhi ya wazee wakiongozwa na Paulo pia Barnaba kwenda kuonana na Mitume kueleza mgongano huo nao watoe mwongozo, ndivyo walivyofanya na Mitume wakaitisha Mtaguso wa Kwanza Yerusalemu. Uliotoa mwelekeo wa mafundisho ya imani iweje. Hivyo wakaandika barua rasmi au hati rasmi kuelezea ni yapi wafuate na yapi waachane nayo.
Kwa msaada na mwongozo wa Roho Mtakatifu, suala hilo lilitatuliwa kwa ufanisi na umoja wa Kanisa ulihifadhiwa. Huu ni mfano wa kwanza wa jinsi Roho wa Mungu anavyokaa katika jumuiya ya waamini, mwanzo wa mchakato wa Maadhimisho ya Mitaguso na sasa Sinodi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Kristo! Katika somo la pili (Ufu.21:10-14) bado linatokana na maono ya Mtakatifu Yohane kama tulivyosikia katika Dominika ya V ya Kipindi cha Pasaka, Mwaka C wa Kanisa: Kuhusu mbinguni, mji mtakatifu. Mtakatifu Yohane aliona kwamba jiji hilo takatifu halina hekalu tena, anasema: “kwa maana hekalu lake ni Bwana Mungu Mwenyezi na Mwana-Kondoo.” Tena, hiki ni kielelezo cha umoja wa Kanisa. Watu wote wa ulimwengu hatimaye watamwabudu Mungu katika roho na kweli. Kwa hiyo kilicho muhimu ni Mungu ambaye ataabudiwa na watu wote wa ulimwengu katika enzi zote. Katika Injili, Yohane 14:23-29 Yesu anawahakikishia wanafunzi wake kwamba atawatumia Mwalimu ambaye ni Roho Mtakatifu lakini pia akiwatia moyo kujiandaa kwa ajili ya kuondoka kwake.
Yesu anawaahidi wanafunzi wake kwamba Baba atatuma Wakili, Roho Mtakatifu, Mfariji atakayefundisha na kuwakumbusha yote ambayo Kristo alifundisha. Sehemu hii ya Injili ya Yohane inayosomwa Dominika hii ya sita ni moja kati sehemu ya mwisho sura ya 14 ambayo ni ya sura nne zenye hotuba ndefu za Yesu ya kuaga kwenye ile Karamu ya Mwisho. Sehemu hii ya sura ya 14 hii ni baada ya ile sehemu ya hotuba ndefu na ya kina ya Yesu kuhusu Karamu ya Mwisho. Katika sehemu hii, anazungumza kuhusu umoja wa wafuasi wake wote. Umoja huu unaweza kupatikana iwapo vipengele vifuatavyo vitakuwepo: Mungu anayeishi kati yetu; hii hutokea tu ikiwa tunampenda Yesu kikweli na kuzishika amri zake; na hili linawezekana kwa njia ya Roho Mtakatifu pekee. Vipengele hivi vyote vinapokuwapo, kuna umoja wa kweli katika Kanisa na katika ulimwengu mzima, na kutakuwa na amani.
Uhusiano wa Yesu na Baba na uhusiano wa wanafunzi na Yesu unawaunganisha wanafunzi na Baba pia. Yesu anaahidi kutuma Wakili, Mfariji, Roho Mtakatifu ambaye atawakumbusha wanafunzi kila kitu ambacho Yesu aliwafundisha na kuwaletea amani. Yesu anawatayarisha wanafunzi wake mapema kwa ajili ya kutokuwepo kwake ili waendelee kumwamini na wasijisikie yatima au peke yao baada ya kurudi kwake kwa Baba. Baada ya kuonekana kwake baada ya Pasaka, Yesu ataendelea kuwa pamoja na wafuasi wake kwa njia tofauti kabisa kwa karne nyingi. Katika Neno lake, Sakramenti za Kanisa, lakini kwa namna ya pekee kabisa katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu. Maadhimisho yetu Kipindi cha Pasaka yaani Siku 50 baada ya Ufufuko wa Kristo Yesu yanaelekea pia ukingoni, Liturujia inatukumbusha kwamba Yesu ataendelea kubaki nasi kwa njia ya Roho Mtakatifu, ambaye anatufundisha yote tunayopaswa kujua, anatukumbusha yote ambayo Yesu alifundisha, na anatuletea amani, lakini pia anatuimarisha. Kila mkristo amempokea Roho Mtakatifu kwa mara ya kwanza katika Sakramenti ya Ubatizo na baadaye katika Sakramenti ya Kipaimara.
Mpendwa msikilizaji mambo haya pia ni muhimu katika tafakari yetu leo: Mamlaka katika Kanisa. Mungu ametupa Neno la mamlaka katika ulimwengu ili kufanya hukumu za makusudi na kutatua migogoro. Kama walivyofanya wakristo wa kanisa la mwanzo kwa ajili ya kupambanua hali halisi ya wakati na kutoa mwelekeo wa Kanisa lifanye nini katika uinjilishaji wake. Wafanye nini pia kuondokana na migongano. Basi waliona vizuri wenye mamlaka ambayo ni mitume kuitisha Mtaguso wa kwanza wa Yerusalemu ili kuzungumza na kufikia mwafaka nini kifanyika. Na hilo lilifanyika wakatoa mwongo. Hilo lilifanyika chini ya uongozi wa Petro. Hivyo basi Petro, mwamba ambao Kanisa limejengwa juu yake ambalo milango ya kuzimu haitaushinda. Yeye na waandamizi wake, Mapapa, wanashikilia funguo za Ufalme wa Mungu. Wanachokifunga duniani kimefungwa mbinguni (Mt 16:18-19). Yesu aliombea Kanisa na hasa uongozi wake (Yohane 17).
Umuhimu wa Roho Mtakatifu: kama inavyosema Katekisimu ya Kanisa Katoliki namba 688 inaoanisha mambo kadhaa yanadhihirisha umuhimu wa Roho Mtakatifu. Kanisa ambao ni ushirika unaoishi katika imani ya mitume ambayo hupitisha au ni mahali ambapo tunamjua Roho Mtakatifu katika Maandiko Matakatifu aliyovuvia, katika mapokeo ambayo mababa wa kanisa daima ni mashahidi kwa wakati unaofaa, lakini pia katika Mamlaka fundishi ya Kanisa yaani “Magisterium” ambayo anaangazia kazi hiyo, katika Liturujia ya Sakramenti, katika karama na huduma ambazo kwazo Kanisa linajengwa; katika ishara za maisha ya kitume na kimisionari; katika ushuhuda wa watakatifu ambao kupitia kwao anadhihirisha utakatifu wake na kuendeleza kazi ya wokovu. Jambo jingine ni upendo: Dominika ya V Kristo Yesu alisistiza kuhusu upendo, kwa kujionesha kuwa ni dira, kielelezo na ukamilifu wa upendo wenyewe ambao umetundikwa juu ya Msalaba. leo anasistiza upendo wa kumpenda Mungu na kushika amri zake.
Mtakatifu Augustino akitafakari injili ya Yohane hasa sura ya 13-14 kuhusu upendo anafananisha na noti au sarafu ya fedha kuwa inasura mbili. Hivyo hivyo upendo kwa Mungu na jirani. Anasema kila sehemu ina umuhimu. Upande mmoja ukikosekana hiyo noti au sarafu si fedha tena. Ndivyo pia hata upendo. Anasema tunampenda Mungu kupitia binadamu wenzetu kwani wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Kwa hiyo amri ya kumpenda Mungu na jirani hazitenganishwi bali zinakamilishana. Pamoja na hayo anawapo waaga anawaachia amani. Amani yangu nawaachieni amani yangu na wapa. Tuombee amani kwa ulimwengu mzima. Terehe 22 Mei ni siku ambayo Mtakatifu Rita wa Cascia anakumbukwa kwa namna ya pekee. Tuombe kwa maombezi yake ambaye ni mwombezi wa mambo yaliyoshindikana, Mungu atuepushe na changamoto zinazotusumbua kipindi hiki: uviko 19, ugumu wa maisha, lakini pia kujaliwa amani ndani ya mioyo yetu, amani katika familia, amani maeneo ya kazi na amani kwa ulimwengu mzima.